Matengenezo ya Waprotestanti yaliinuka ili kushughulikia makosa mengiya Rumi. Wanamate- ngenezo hao walichukua pia masuala mengine amhayo waliyapata katika Maandiko Matakatifu, lakiniyalikuwa yamepuuzwa kwa muda mrefu. Mnamo karne ya 19, mvuto kuhusu kuja kwa Kristo mara ya pili ulikuwa ukiongezeka miongoni mwa wanafunzi wa Biblia wa madhehebu na nchi mbalimbali. Wengi walitarajia tukio hilo kuonekana katika nusu ya kwanza ya karne hiyo. Vuguvugu hili lilikuwa na nguvu zaidi hasa nchini Marekani, ambapo wafuasi wake walikuja kufahamika kama ‘Waadventista. ” Kulingana na unabii wa wakati wa Danieli 8:14 kuhusu kutakaswa kwa patakatifu, walitarajia kuwa Yesu angekuja na kuitakasa dunia mnamo mwaka 1844. Wakati jambo hili lilipokosa kutokea, baadhi yao waliichunguza Biblia ili kujua ni kwa nini haikuwa hivyo. PLK 121.1
Patakatifu pa Mbinguni na pa Duniani-Katika uchunguzi wao wanafunzi hawa wa Biblia wenye bidii walijifunza kuwa patakatifu pa duniani, ambapo Musa alipajenga kwa agizo la Mungu kulingana na mfano aliooneshwa juu ya Mlima Sinai, palikuwa “ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa.” Waebrania 9:9. Walijifunza kuwa sehemu zake mbili takatifu zilikuwa ni “nakala za mambo yaliyo mbinguni”; ambapo Kristo Kuhani Mkuu wetu, ni “mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu”; na kwamba “Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu;” Waebrania 9:23; 8:2; Waebrania 9:24. PLK 121.2
Patakatifu pa mbinguni, ambapo Kristo anahudumu kwa niaba yetu, ndio patakatifu pa kwanza ambapo patakatifu palipojengwa na Musa palikuwa ni nakala yake. Kama patakatifu pa duniani palivyokuwa na vyumba viwili, patakatifu na patakatifu mno, ndivyo ambavyo pana vyumba viwili katika patakatifu pa mbinguni. Na sanduku la agano linalobeba sheria ya Mungu, madhabahu ya kufukizia uvumba, na vifaa vingine vya huduma vilivyokuwa vinapatikana katika patakatifu pa duniani, pia vina nakala katika patakatifu pa mbinguni. Katika njozi takatifu mtume Yohana aliruhusiwa kuingia mbinguni, na pale aliona kinara cha taa, na madhabahu ya kufikizia uvumba, na kisha “Hekalu la Mungu lililoko mbinguni” lilipofunguliwa, aliona pia “sanduku la agano lake.” Ufunuo 4:5; 8:3; Ufunuo 11:19. PLK 122.1
Wale waliokuwa wakitafuta ukweli walipata uthibitisho usiopingika kwamba kuna patakatifu huko mbinguni. Musa alijenga patakatifu pa duniani kulingana na mfano aliooneshwa. Paulo alitangaza kuwa mfano ule ulikuwa ni hema ya kweli, ambayo ipo mbinguni (Waebrania 8:2, 5). Yohana alishuhudia kuwa aliiona mbinguni. PLK 122.2
Mwishoni mwa siku 2,300, mnamo mwa 1844, hapakuwa na patakatifu duniani kwa kame nyingi. Kwa hiyo, ni lazima patakatifu pa mbinguni ndipo palipooneshwa katika tangazo husika, “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” (Danieli 8:14). Lakini ingewezekanaje patakatifu pa mbinguni kutakaswa? Wakigeukia tena Maandiko, wanafunzi wa unabii walijifunza kuwa utakasaji huu haukuwa wa uondoaji wa uchafu halisi, kwa kuwa ulikuwa ukamilishwe kwa damu, kwa hiyo ni lazima kuwe ni kutakaswa kutokana na dhambi. Mtume anasema: “Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo [damu za wanyama], lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo [yaani, damu ya thamani ya Kristo].” Waebrania 9:23. PLK 122.3
Ili kupata ufahamu zaidi kuhusu utakasaji ambao unabii unauelezea, walihitaji kuelewa huduma za patakatifu pa mbinguni. Wangeweza tu kujifunza hili kwa kuangalia huduma za patakatifu pa duniani, kwa sababu Paulo anasema kuwa makuhani waliohudumu pale walitumika kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni,” Waebrania 8:5. PLK 123.1
Kutakaswa kwa Patakatifu-Kama ambavyo dhambi za watu zilihamishwa, kimfano, hadi patakatifu pa duniani kwa njia ya damu ya sadaka ya dhambi, ndivyo ambavyo kwa kweli, dhambi zetu zinahamishiwa katika patakatifu pa mbinguni kupitia kwa damu ya Kristo. Na kama utakaso wa mfano wa duniani ulivyokamilishwa kwa kuondolewa kwa dhambi zilizopachafua patakatifu, ndivyo ambavyo utakasaji halisi wa patakatifu pa mbinguni unapaswa kutimilizwa kwa uondoaji, au ufutaji wa dhambi ambazo kumbukumbu zake zimeandikwa pale. Hii inahitaji kuchunguzwa kwa vitabu vya kumbukumbu ili kuthibitisha ni nani, ambao kupitia toba ya dhambi na imani katika Kristo, wanastahili kupata manufaa ya upatanisho wake. Kwa hiyo utakasaji wa patakatifu unahusisha kazi ya hukumu ya upelelezi. Kazi hii ni lazima ifanyike kabla ya kuja kwa Kristo ili kuwakomboa watu wake, kwa sababu pale atakapokuja, ujira wake utakuwa pamoja naye ili kumpa kila mmoja sawasawa na kazi zake. (Ufunuo 22:12). PLK 123.2
Hivyo, wale walioifuata nuru inayozidi kung’aa ya neno la unabii waliona kuwa badala ya kuja duniani mwishoni mwa siku 2,300 mnamo mwaka 1844, Kristo aliingia katika patakatifu pa patakatifu pa hekalu la mbinguni, mbele za Mungu, ili kutekeleza kazi ya mwisho ya upatanisho, katika kujiandaa na ujio wake. PLK 123.3
Ujumbe Makini-Wakati Kristo alipoingia katika patakatifu pa patakatifu pa hekalu la mbinguni ili kutekeleza kazi ya mwisho ya upatanisho, aliwakabidhi watumishi wake ujumbe wa mwisho wa rehema unaopasa kutolewa kwa ulimwengu. Huu ni ujumbe wa onyo wa malaika wa tatu wa Ufunuo 14. Nabii anaona kuwa mara tu baada ya kutangazwa kwake, Mwana wa Adamu atakuja kwa utukufu ili kuvuna mavuno ya ulimwengu. PLK 124.1
Onyo la kuogofya kuliko yote yaliyowahi kutolewa kwa wanadamu linapatikana katika ujumbe wa malaika wa tatu (Ufunuo 14:9-12). Ni lazima iwe ni dhambi ya kutisha ambayo inasababisha kumwagwa kwa ghadhabu ya Mungu isiyochanganywa na rehema. Watu hawapaswi kuachwa gizani kuhusu jambo hili muhimu. Onyo dhidi ya dhambi hili halina budi kutolewa kwa ulimwengu kabla ya kuja kwa hukumu za Mungu, ili wote wajue ni kwa nini hukumu hizi ni lazima zitolewe na waweze kuwa na fursa ya kuziepuka. PLK 124.2
Katika suala la pambano kuu, makundi mawili yaliyo dhahiri, na yanayotofautiana yanajitokeza. Katika kundi moja kuna kila mtu ambaye atamsujudu “huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,” na hivyo wanajiletea juu yao hukumu za kutisha zilizotangazwa na malaika wa tatu. Kundi lingine, likiwa kinyume kabisa na dunia, ni la wale “wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Ufunuo 14:9, 12. PLK 124.3