Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Tumaini Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Kuufunua Wakati Ujao

    Kabla ya dhambi kuingia, Adamu alikuwa na fursa ya kuwasiliana moja kwa moja na Mwumbaji wake; lakini tangu mwanadamu alipojitenga na Mungu kwa kukosa, jamii ya wanadamu iliondolewa katika fursa hii kubwa. Hata hivyo, njia imefunguliwa kwa wakazi wa dunia kuwa na uhusiano na mbingu. Mungu amekuwa akiwasiliana na watu kwa njia ya Roho wake, na nuru ya mbingu imekuwa ikitolewa kwa ulimwengu kwa mafunuo yatolewayo kwa watumishi wake. “Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” 2 Pet. 1:21.TK 13.1

    Katika miaka 2500 ya kwanza ya historia ya mwanadamu, hakukuwa na mafunuo yaliyoandikwa. Wale waliokuwa wamefundishwa na Mungu waliwasilisha ujuzi wao kwa wengine, na ujuzi huo ulikuwa unakabidhiwa toka kwa baba kwenda kwa mtoto, kwa vizazi vingi. Maandalizi ya neno lililoandikwa yalianza wakati wa Musa. Mafunuo yenye uvuvio yaliwekwa katika kitabu kilichovuviwa. Kazi hii iliendelea kwa kipindi kirefu cha miaka 1600—kuanzia kwa Musa, mwana historia wa uumbaji na sheria, hadi kwa Yohana, mwandishi wa ukweli nyeti wa Injili.TK 13.2

    Biblia inamtaja Mungu kuwa mtunzi wake; lakini iliandikwa kwa mikono ya wanadamu; na katika mitindo tofauti ya vitabu vyake mbalimbali, inaonesha sifa bainifu za waandishi wake wengi. Ukweli wote uliofunuliwa, ulitolewa kwa “pumzi ya Mungu” (2 Tim.3:16); japo umeelezwa kwa maneno ya watu. Yeye asiye na ukomo aliangaza nuru katika akili na mioyo ya watumishi wake kwa njia ya Roho wake Mtakatifu. Aliwapa ndoto na njozi, vielelezo na mifano; na wale waliooneshwa ukweli huo waliyatafsiri mawazo hayo katika lugha za wanadamu.TK 13.3

    Vikiwa vimeandikwa katika kame tofauti, na watu waliokuwa wanatofautiana sana katika nyadhifa na katika kazi, kiakili na kiroho, vitabu vya Biblia wanaonesha tofauti kubwa katika mitindo, na pia tofauti katika aina ya mada zinazoelezewa. Aina mbalimbali za usemi zimetumia na waandishi tofauti; mara nyingi ukweli ule ule umeelezewa kwa namna ya kuvutia zaidi na mwandishi mmoja kuliko ulivyoelezewa na mwingine. Na kwa vile waandishi mbalimbali huwasilisha mada wakizingatia vipengele tofauti na maelezo ya aina mbalimbali, mambo hayo yanaweza kuonekana kuwa ni tofauti au yanakinzana kwa msomaji wa juu juu, asiye makini au mwenye mtazamo wa kupinga, wakati msomaji makini mwenye utauwa, akiwa na ufahamu wa kina, ataona upatanifu uliomo.TK 13.4

    Kama ulivyowasilishwa na watu mbalimbali, ukweli unakuja katika vipengele vyake vinavyotofautiana. Mwandishi mmoja anaguswa zaidi na sehemu moja ya suala fulani; anayashika mambo yanayokwenda sambamba na hali yake au uweza wake wa kutambua; mwingine hushika sehemu nyingine; na kila mmoja, kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, anawasilisha kile kilichogusa zaidi akili yake—kila mmoja akiwa na upande tofauti wa ukweli, lakini kukiwa na mwafaka mkamilifu kote. Na ukweli uliooneshwa kwa njia hiyo huungana kuunda kitu kizima kikamilifu, kinachofaa kukidhi mahitaji ya wanadamu katika hali zote na matukio yote katika maisha.TK 14.1

    Mungu aliona vyema kuwasilisha ukweli wake duniani kwa kutumia wanadamu, na yeye mwenyewe, kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, aliwapa watu uweza na kuwawezesha kufanya kazi hiyo. Aliongoza akili zao katika kuchagua mambo ya kusema na ya kuandika. Hazina ilikabidhiwa kwa vyombo vya udongo, lakini iliendelea kuwa ya mbinguni. Ushuhuda unatolewa kwa misemo dhaifu ya yenye upungufii wa lugha za wanadamu, lakini ni ushuhuda wa Mungu; na mtoto wa Mungu ambaye ni mtiifu na anayeamini ataona ndani yake utukufu wa uwezo wa Mungu, uliojaa neema na kweli.TK 14.2

    Katika Neno lake, Mungu amekabidhi watu ujuzi ulio muhimu kwa ajili ya wokovu. Maandiko Matakatifu yanapaswa kukubaliwa kama ufunuo wa mapenzi ya Mungu ulio na mamlaka, usiokosea. Maandiko ndiyo kiwango cha tabia, chanzo cha mafundisho, na kipimo cha mwenendo. “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” 2 Tim. 3:16, 17.TK 14.3

    Hata hivyo, kitendo cha Mungu kufunua mapenzi yake kwa watu kwa kutumia Neno lake hakipunguzi umuhimu wa uwepo wa uongozi endelevu wa Roho Mtakatifu. Kinyume chake, Mwokozi wetu aliahidi uwepo wa Roho, ili kufunua Neno kwa watumishi wake, kuangazia na kuyafanyia kazi mafundisho yake. Na kwa kuwa Roho wa Mungu ndiye aliyeivuvia Biblia, haiwezekani kwa mafundisho ya Roho kupingana na Neno.TK 14.4

    Roho hakutolewa—na hawezi kutolewa—ili achukue nafasi ya Biblia; kwani Maandiko yanasema wazi kabisa kwamba Neno la Mungu ndiyo kipimo cha mafundisho na mwenendo wote. Mtume Yohana anasema, “msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” 1 Yoh. 4:1. Isaya naye anasema, “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Isa. 8:20.TK 15.1

    Fedheha kubwa imeletwa katika kazi ya Roho Mtakatifu na makosa ya kundi la watu ambao, wakati wanadai kuwa wamepata maarifa katika katika Neno la Mungu, wanasema kuwa hawahitaji uongozi zaidi wa Neno la Mungu. Wanatawaliwa na hisia ambazo wanadhani ni sauti ya Mungu ndani ya moyo. Lakini roho inayowatawala si yule Roho wa Mungu. Tabia hii ya kufuata hisia na kupuuza Maandiko, inaweza kuleta machafuko, udanganyifu na uharibifu. Inasaidia tu kuendeleza makusudi ya yule mwovu. Kwa kuwa kazi ya Roho Mtakatifu ni ya muhimu kwa kanisa la Kristo, moja ya malengo ya Shetani ni kuifedhehesha kazi ya Roho kwa njia ya makosa ya watu wenye itikadi kali, na kuwafanya watu wakipuuze chanzo hiki cha nguvu ambacho Bwana wetu ametupatia.TK 15.2

    Sambamba na Neno la Mungu, Roho wa Mungu alikuwa aendelee kufanya kazi yake katika kipindi chote cha Injili. Wakati Maandiko ya Agano la Kale na Jipya yakitolewa, Roho Mtakatifu hakukoma kuwasilisha nuru katika akili za kila mtu, kando ya mafunuo ambayo yangeingizwa katika Maandiko. Biblia yenyewe inaeleza jinsi watu walipokea, kwa njia ya Roho Mtakatifu, maonyo, makaripio, ushauri na maelekezo katika masuala ambayo hayakuhusika na utoaji wa Maandiko. Na wanatajwa manabii ambao maneno yao hayajaandikwa. Vivyo hivyo, baada ya kumalizika kazi ya kuandika Maandiko, Roho Mtakatifu alikuwa aendelee na kazi yake ya kuelimisha, kuonya, na kuwafariji watoto wa Mungu. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia..”TK 15.3

    “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote: ... na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yn. 14:26; 16:13. Maandiko yanafundisha wazi kabisa kuwa, ahadi hizi hazikuwa zimekusudiwa kwa ajili ya kanisa la mitume tu, bali zilikuwa zinaendelea katika kanisa la Kristo katika vizazi vyote. Mwokozi aliwahakikishia wafuasi wake, “mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt. 28:20. Paulo pia anasema kuwa karama na kazi za Roho ziliwekwa kanisani “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili Wakristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu Wakristo.” Efe. 4:12, 13.TK 16.1

    Mtume Paulo aliwaombea waumini wa Efeso, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mmwito wake jinsi lilivyo; ... na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo.” Efe. 1:17-19. Kazi ya Roho wa Mungu katika kuelimisha akili na kuzionesha mambo ya kina ya Neno Takatifu la Mungu ni baraka ambayo Paulo alikuwa akiitafuta kwa ajili ya kanisa la Efeso.TK 16.2

    Baada ya udhihirisho wa ajabu wa Roho Mtakatifu katika Siku ya Pentekoste, Petro aliwasihi watu watubu na kubatizwa katika jina la Kristo, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao; akisema: “nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.” Mdo. 2:38, 39.TK 16.3

    Kwa njia ya nabii Yoeli, Bwana alikuwa ameahidi udhihirisho maalum wa Roho wake sambamba na matukio ya siku kuu ya Mungu. Yoe. 2:28. Unabii huu ilitimia kwa sehemu katika kumwagwa kwa Roho Siku ya Pentekoste; lakini utatimia kikamilifu zaidi katika udhihirisho wa neema ya Mungu itakayoongoza kazi ya mwisho ya Injili. Pambano kuu kati ya wema na uovu litazidi kuwa kali hadi mwisho wa wakati. Katika kame zote hasira ya Shetani imekuwa ikidhihirishwa dhidi ya kanisa la Kristo; na Mungu amewapa watu wake neema na Roho, ili kuwaimarisha wasimame dhidi ya nguvu za yule mwovu. Wakati mitume Wakristo walipotakiwa kupeleka Injili yake kwa ulimwengu na kuiandika kwa ajili ya vizazi vya baadaye, walikuwa wanaangaziwa na Roho kwa namna ya pekee. Lakini kanisa linavyokaribia ukombozi wake wa mwisho, Shetani atafanya kazi kwa nguvu zaidi. Atakuja akiwa “mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” Ufu. 12:12. Atafanya kazi, “kwa uwezo wote, na ishara, na ajabu za uongo.” 2 Thes. 2:9. Kwa miaka 6,000 kiumbe huyu mwenye akili nyingi aliyewahi kuwa juu zaidi miongoni mwa malaika wa Mungu amekuwa akifanya kwa bidii kazi ya kudanganya na uharibifu. Na undani wote na ujuzi wa kishetani uliopatikana, ukatili wote aliobuniwa katika wakati wa mapambano haya ya enzi, utatumika dhidi ya watu wa Mungu katika pambano la mwisho. Na wakati huo wa hatari, wafuasi Wakristo watapeleka onyo la ujio wa Bwana; na jamii ya watu itaandaliwa kwa ajili ya kusimama mbele yake wakati wa kuja kwake, wakiwa hawana “mawaa wala aibu mbele yake.” 2 Pet. 3:14. Wakati huu, kipawa maalum cha neema ya Mungu na uwezo hakitahitajika kidogo kwa kanisa kuliko kilivyokuwa kinahitajika wakati wa mitume.TK 16.4

    Kwa kuangaziwa na Roho Mtakatifu, matukio ya pambano kati wema na uovu, ambalo limedumu kwa muda mrefu yamekuwa yakifunuliwa kwa mwandishi wa kitabu hiki. Mara nyingi nimeruhusiwa kuona mambo ya pambano kuu kati ya Kristo, Mfalme wa uzima, Mwanzilishi wa wokovu, na Shetani, mfalme wa uovu, mwanzilishi wa dhambi, mvunjaji wa kwanza wa sheria takatifu ya Mungu. Uadui wa Shetani dhidi ya Kristo umedhihirishwa dhidi ya wafuasi Wakristo. Chuki ile ile dhidi ya kanuni za sheria ya Mungu, sera ile ile ya udanganyifu, inayofanya uongo uonekane kama ukweli, inayofanya sheria za wanadamu zishikwe badala ya sheria ya Mungu, na watu wamefanywa waabudu kiumbe badala ya Mwumbaji, inaweza kuonekana katika historia yote iliyopita. Juhudi za Shetani za kuwasilisha vibaya tabia ya Mungu, ili kuwafanya watu wang’ang’anie dhana potovu juu ya Mwumbaji, na hivyo kumtazama kwa hofu na chuki badala ya upendo; juhudi zake za kuweka kando sheria ya Mungu, kuwafanya watu wajione kuwa hawafungwi na sheria hiyo; na mateso yake kwa wale wanaothubutuu kuupinga udanganyifu wake, yameonekana katika hisitoria ya wazee, manabii na mitume, hisitoria ya wafia dini na wanamatengeneo.TK 17.1

    Katika pambano kuu la mwisho, Shetani atatumia sera hiyo hiyo, atadhihirisha roho hiyo hiyo, na atafanya kazi zake kwa makusudi yale yale aliyokuwa nayo katika kame zilizopita. Kile ambacho kimekuwepo kabla, kitakuwepo, isipokuwa pambano linalokuja litakuwa kali na la kutisha kuliko lo Iote ambalo dunia imewahi kulishuhudia. Udanganyifu wa Shetani utakuwa wa hila zaidi na mashambulizi yake yatakuwa ya ushupavu zaidi. Kama yumkini, atawapotosha wateule. Mk. 13:22.TK 17.2

    Kwa kuwa, Roho wa Mungu ameufunua katika akili zangu, ukweli mkuu wa Neno lake na matukio yaliyopita na yajayo, nimeagizwa kuwajulisha wengine mambo niliyooneshwa—kuielezea historia ya pambano katika enzi zilizopita, na hasa kuiwakilisha katika namna ambayo itaangazia pambano lijalo ambalo linakuja upesi. Ili kutimiza lengo hilo nimejitahidi kuchagua na kuweka pamoja matukio katika historia ya kanisa katika njia ambayo itaonesha kufunuliwa kwa ukwei upimao ambao katika vipindi fulani umekuwa ukitolewa kwa ulimwengu, ukawasha hasira ya Shetani na chuki ya kanisa lipendalo ulimwengu, na ambao umeendelea kudumishwa kwa ushuhuda wa wale “ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Katika maandishi haya tunaweza kupata picha ya pambano lililo mbele yetu. Tukiyaangalia kwa kuzingatia Neno la Mungu, na kwa kuangaziwa na Roho wake, tunaweza kuona hila za yule mwovu zikiwekwa wazi pamoja na hatari ambazo inawapasa kuziepuka wale watakaoonekana “hawana mawaa” mbele ya Bwana siku atakapokuja.TK 18.1

    Matukio makubwa yaliyotukia katika maendeleo ya matengenezo katika siku za nyuma ni mambo yaliyotokea kihistoria, yanajulikana vizuri na yanatambuliwa ulimwenguni kote na Waprotestanti; ni ukweli ambao hakuna anayeweza kuupinga. Historia hii nimeielezea kwa ufupi, kulingana na upeo wa kitabu hiki na ufupisho ambao ni lazima uzingatiwe. Ukweli umefupishwa katika nafasi ndogo kama ilivyoonekana inafaa katika kuyaelewa matumizi yake. Wakati mwingine, mahali ambapo mwanahistoria fulani ameyakusanya matukio ili kuwezesha kuwe na mwonekano mpana wa suala zima kwa muhtasari, au kama ameweka muhtasari wa vipengele katika njia inayofaa, maneno yake yamenukuliwa; lakini katika sehemu zingine hakuna nukuu yo yote iliyotajwa, kwa kuwa madondoo yenyewe hayakutolewa kwa ajili ya kumtambua mwandishi husika kama bingwa, lakini kwa sababu usemi wake unatoa maelezo yaliyo tayari na yenye nguvu katika kuelezea suala husika. Katika kusimulia mambo na maoni ya wale wanaoendeleza kazi ya matengenezo katika siku zetu, kazi zilizokwisha kuchapwa zimetumika kwa njia hiyo hiyo.TK 18.2

    Si kusudi la kitabu hiki kuelezea ukweli mpya juu ya misukosuko ya siku za nyuma, bali ni kuelezea mambo na kanuni ambazo zinahusiana na matukio yajayo. Lakini yakitazamwa kama sehemu ya pambano kati ya nguvu za nuru na zile za giza, maandishi yote haya yanayohusu siku za nyuma yanaonekana kuwa na maana mpya; na kwa njia ya maandhishi hayo nuru inayaangazia mambo yajayo, ikiiangazia njia ya wale ambao watatakiwa kushuhudia “kwa ajili ya Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo, ” hata kwa hatari ya kukosa mema yote ya nchi, kama ilivyokuwa kwa wanamatengenezoTK 19.1

    Lengo la kitabu hiki ni kuelezea matukio ya pambano kuu kati ya ukweli na uongo; kufichua hila za Shetani na mbinu za kuzipinga kwa ufanisi; kuwasilisha ufumbuzi wa kuridhisha wa tatizo kubwa la uovu, kuangazia chanzo cha dhambi na kuondolewa kwa dhambi ili kufanya haki na fadhila za Mungu katika kushughulikia viumbe vyake zidhihirike, na kuonesha hali isiyobadilika ya sheria yake takatifu.TK 19.2

    E.G.W.

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents