Go to full page →

Sura Ya 25 - Nyumba ya Mkristo KN 169

KATIKA kuchagua nyumba, Mungu angependa tufikiri jambo la kwanza, mivuto ya tabia ya adili na ya dini itakayotuzunguka pamoja na jamaa zetu. Mahali pa kuiweka nyumba pakitafutwa kusudi hili halina budi kuwa jambo la kuongoza uchaguzi huo. Usitawaliwe na tamaa ya mali, mitindo, wala desturi za mtaa. Fikiri kile ambacho kitasaidia kuleta utovu wa anasa, usafi, afya na thamani halisi. KN 169.1

Badala ya kukaa mahali ambapo vitu vya kuonekana machoni na sauti zinazosikika hushawishi mawazo mabaya, mahali ambapo makelele na fujo huchosha na kutia wasiwasi, nenda mahali uwezapo kutazama kazi zake Mungu. Tafuta raha ya moyoni mahali penye uzuri na utulivu na amani ya viumbe vya asili. Hebu macho yatazame mashamba yenye neema, mahali penye miti mingi kidogo, na vilima. Angalia anga, isiyo na mavumbi wala moshi wa mjini, na kuvuta hewa safi itiayo afya na nguvu iliyojaa angani. KN 169.2

Wakati umewadia, ambao kadiri Mungu anavyofungua njia, jamaa za watu nyumbani wangehamia nje ya miji mikubwa. Watoto wangechukuliwa mashambam. Wazazi wangejipatia mahali pazuri pa kufaa kadiri wawezavyo kwa fedha zao. Ingawa makao yawe madogo, walakini pasikose kuwepo shamba linalopakana liwezalo kulimwa. KN 169.3

Baba na mama wenye kipande cha shamba na nyumba ya kupendeza ni wafalme na malkia. Ikiwezekana, nyumba lwe nje ya mji, mahali watoto wawezapo kupata udongo wa kulima shamba. Kila mmoja na awe na kipande cha shamba lake mwenyewe; na ukiwafundisha namna ya kutengeneza shamba, namna ya kuutayarisha udongo kwa ajili ya kupanda mbegu, na faida ya kupalilia shamba, wafundishe pia jinsi ilivyo muhimu kuondoa desturi mbaya na maovu maisham. Wafundishe kuzuia mazoea mabaya kama wanavyozuia magugu mashambani mwao. Itachukua muda mrefu kufundisha masomo haya, lakini italeta faida kubwa. KN 169.4

Dunia ina mibaraka iliyosetirika ndani yake kwa ajili ya wale wenye moyo na nia na ustahimilivu kuzikusanya hazina zake. Wakulima wengi wameshindwa kupata malipo ya kutosha toka mashambani mwao kwa sababu hushughulika na kazi hiyo kana kwamba ni ya aibu na yenye kuwaondolea heshima; hawaoni kuwa pana mbaraka ndani yake kwao na kwa watu wa nyumbani mwao. KN 169.5

Wazazi wana wajibu uwapasao kwa Mungu kufanya makao yao yawe na hali ipatanayo na ukweli wanaoukiri. Ndipo wanaweza kutoa mafundisho sahihi kwa watoto wao, na watoto wataweza kujifunza kufananisha makao haya hapa chini na yale makao ya juu mbinguni. Jamaa hii hapa haina budi, kama iwezekanavyo, kuwa mfano wa ile jamaa ya mbinguni. Ndipo vishawishi vinayowajia kuwavuta kujifurahisha kwa anasa za mambo hafifu na manyonge vitakosa nguvu. Yapasa watoto wafundishwe kuwa hapa duniani wao ni watu tu wanaojaribiwa kama watafaa ama sivyo, na kuelimishwa ili wawe wenyeji wa makao yale ambayo Kristo anawaandalia wale wampendao na kuzishika amri zake. Huu ndio wajibu wa kwanza kabisa uwapasao wazazi. KN 170.1

Kadiri iwezekanavyo, nyumba zote zinazokusudiwa kukaliwa na wanadamu zingejengwa mahali palipoinuka, palipokaushwa vizuri. Kufanya hivi kutahakikisha kuwa unacho kiwanja kikavu. Mara nyingi watu hawajali jambo hili. Basi, udhaifu wa daima, magonjwa mabaya, na vifo vingi ni matokeo ya unyevu na homa ya malaria inayopatikana katika nyanda za chini zisisoweza kukauka vizuri. KN 170.2

Katika kujenga nyumba, ni jambo la muhimu sana kuweka madirisha makubwa ili kuingiza hewa safi na mwanga wa jua. Hewa safi na mwangaza viwepo kwa wingi katika kila chumba nyumbani. Vyumba vya kulala na viwe mahali panapopata hewa safi mchana na usiku. Chumba cho chote kisichoweza kufunguliwa kila siku na kuingiliwa na hewa na mwangaza, hakifai kwa kulala. KN 170.3

Uwanja uliofanywa kuwa wa kupendeza kwa kupandwa miti huko na huko maua, kwa kuacha nafasi nzuri kutoka nyumba yenyewe, una mvuto mzuri kwa watu wa nyumbani, na ukitunzwa vizuri, hautaleta madhara yo vote kwa afya. Lakini miti ya kivuli na vichaka karibu na nyumba huifanya iwe ya kuleta ugonjwa, kwa kuwa huzuia hewa isiingie kwa wingi na kukinga mionzi ya nuru ya jua. Matokeo yake huwa unyevu ama uvundo unaojikusanya nyumbani, hasa siku za baridi. KN 170.4