Sura hii imejengwa katika Isaya 14:12-14; Ezekieli 28:12-17; Ufunuo 12:7-9.
Kabla ya uasi wake mbinguni, Lusifa alikuwa malaika mkuu na aliyetukuka, ambaye kwa heshima, alikuwa akimfuatia Mwana wa Mungu. Uso wake, kama zilivyokuwa za malaika wengine, ulikuwa ni wa upole ulioangaza furaha. Kipaji cha uso wake kilikuwa kimeinuka na kipana, kikionesha uwezo mkubwa wa kiakili. Umbo lake la kimwili lilikuwa kamilifu, na mwonekano wake ulikuwa adili na wa utukufu. Nuru ya pekee ilimulika kutoka katika uso wake ikiangaza kumzunguka kwa uangavu na uzuri kuliko ilivyokuwa kwa malaika wengine; lakini Kristo Mwana wa Mungu, alikuwa juu ya kusanyiko lote la malaika. Alikuwa pamoja na Baba kabla malaika hawajaumbwa. Lusifa alimwonea wivu Kristo, na pole pole alijitwalia madaraka ambayo yalikuwa ni kwa ajili ya Kristo peke yake. PLK 5.1
Malaika walimkubali Kristo kama mtawala wa mbingu, uwezo na mamlaka yake kuwa sawa na yale ya Mungu mwenyewe. Lusifa alijidhania kuwa ndiye kipenzi cha mbinguni miongoni mwa malaika. Mungu alikuwa amempa cheo cha juu, lakini hilo halikumfanya arejeshe shukrani na sifa kwa Muumba wake. Alitamani kufikia kimo cha Mungu mwenyewe. Aliona fahari kwa sababu ya hadhi yake iliyotukuka. Alijua kuwa alikuwa anaheshimiwa na malaika. Alikuwa na kazi maalumu ya kutimiza. Alikuwa amepata fursa ya kuwa karibu na Muumbaji mkuu, na miale ya daima ya nuru tukufu iliyomzunguka Mungu wa milele kwa namna ya pekee iliangaza juu yake. Alifikiria jinsi ambavyo malaika walitii amri zake kwa haraka na furaha. Je mavazi yake hayakuwa nuru na ya kupendeza? Kwa nini Knsto aheshimiwe kiasi kile badala yake? PLK 5.2
Alitoka katika uwapo wa karibu na Baba, kwa kutoridhika na akiwa amejazwa na wivu dhidi ya Kristo. Huku akificha kusudi lake halisi, aliwakusanya malaika kumzunguka. Aliingiza mada yake, ambayo ilikuwa ni yeye mwenyewe. Kama aliyekuwa ametendewa vibaya, aliongelea jinsi ambavyo Mungu alimtelekeza na kutoa upendeleo kwa Yesu. Aliwaambia kuwa kuanzia wakati ule na kuendelea, uhuru ule mzuri ambao malaika walikuwa wakiufaidi ulikoma. Kwani je hakuwa amechaguliwa kiongozi juu yao, ambaye iliwapasa kujisalimisha kwake kwa heshima kama ya mtumwa? PLK 6.1
Aliwaambia kwamba alikuwa amewaita pamoja ili kuwahakikishia kuwa hatakubali tena kujiweka chini ya uingiliaji huu wa haki zake na zao; kuwa kamwe tena hatamsujudia Kristo. Badala yake, atajichukulia heshima juu yake ile ambayo Mungu alipaswa kumkabidhi, na atakuwa kiongozi wa wote ambao watajiweka chini yake kumfuata na kuitii sauti yake. PLK 6.2
Kulikuwako na kupishana mno miongoni mwa malaika. Lusifa na wafuasi wake walikuwa wakijaribu kuiunda upya serikali ya Mungu. Waliasi dhidi ya mamlaka ya Mwana. Malaika wale waliokuwa watiifu na wakweli walijaribu kumshawishi, malaika huyu mwasi kurudi katika kutenda mapenzi ya Muumba wake. Walibainisha wazi kuwa Kristo alikuwa ni Mwana wa Mungu, akiwa pamoja naye kabla malaika hawajaumbwa. Daima alisimama katika mkono wa kuume wa Mungu. Mamlaka yake ya upole, na upendo kamwe yalikuwa hayajawahi kutiliwa shaka, na hakutoa maagizo isipokuwa yale ambayo majeshi ya mbinguni yalifurahia kuyatekeleza. PLK 6.3
Walisisitiza kuwa heshima ya pekee ya Kristo haikuwa inapunguza ile heshima ambayo tayari Lusifa alikuwa ameipokea. Malaika wale walilia machozi. Walijaribu kwa bidii kumbembeleza aache njama zake ovu na kujisalimisha chini ya Muumbaji wao. Hadi wakati ule, walisisitiza, mambo yote yalikuwa ni amani na upatanifu. Je kungekuwapo na sababu yo yote ipi kwa ajili ya sauti hii ya mfarakano na uasi? PLK 6.4
Lusifa alikataa kusikiliza. Na kisha akageuka kutoka kwa malaika watiifu na wakweli, akiwashutumu kuwa watumwa. Malaika hawa, watiifu kwa Mungu, walisimama kwa mshangao walipoona kuwa Lusifa alikuwa akiendelea na juhudi yake ya kuchochea uasi. Aliwaahidi serikali mpya na nzuri kuliko ile waliyokuwa nayo, ambayo ndani yake kungekuwa na uhuru kamili. Idadi kubwa walionesha nia yao ya kumkubali kama kiongozi wao na amiri jeshi wao. Alipoona kuwa juhudi zake zilipokelewa kwa mafanikio, alijidanganya kuwa punde tu angeweza kuwa na malaika wote upande wake, na kwamba hapo angekuwa sawa na Mungu mwenyewe. Kisha wote wangesikia sauti yake ya mamlaka ikiamrisha jeshi lote la mbinguni. PLK 7.1
Kwa mara nyingine tena malaika watiifu walimwo- nya, wakimhakikishia juu ya kile ambacho lazima kitakuwa matokeo iwapo atang’ang’ania. Yeye aliyeweza kuwaumba malaika anaweza kupindua mamlaka yao yote kwa uwezo wake na kwa uamuzi thabiti kuadhibu ushupavu na uasi wao wa kutisha. Kudhani kwamba malaika anaweza kupinga sheria ya Mungu, ambayo ni takatifu kama Mungu mwenyewe! Waliwaonya wale malaika waasi kufunga masikio yao kwa hoja za kudanganya za Lusifa, na walimshauri yeye pamoja na wote ambao alikuwa amewavuta kwake kwenda kwa Mungu na kukiri kwamba walikuwa wametenda kosa hata kwa kule tu kuruhusu wazo la kuhoji mamlaka yake. PLK 7.2
Wengi wa wafuasi wa Lusifa walitaka kufuata ushauri huu wa malaika watiifu na kutubia kutokuridhika kwao na hivyo kukaribishwa tena katika kuaminiwa na Baba pamoj a na Mwana wake. Ndipo mwasi mkuu al ipotangaza kuwa aliijua sheria ya Mungu, na kwamba iwapo angekubali kujisalimisha na kuonesha utii wa kitumwa, heshima yake ingeondolewa kwake. Asingeweza tena kuaminiwa kupewa madaraka yake ya juu. Aliwaambia kuwa yeye na wao walikuwa wamekwenda mbali mno kiasi cha kutoweza kurudi nyuma, na alikuwa tayari kukabiliana na matokeo, kwa sababu kamwe asingeweza kuinama kwa ibada ya kitumwa kwa Mwana wa Mungu. Alidai kuwa Mungu asingeweza kusamehe, na sasa ni lazima watetee uhuru wao na kuchukua kwa mabavu nafasi ile ambayo hawakupewa kwa hiari. Kwa njia hii Lusifa, “mbeba nuru,” ambaye alishiriki utukufu wa Mungu, aliyesimama kando ya kiti chake cha enzi, kwa kutenda dhambi akawa Shetani, “adui.” PLK 7.3
Malaika wale watiifu walifanya haraka kwenda kwa Mwana wa Mungu ili kumwambia kile kilichokuwa kinaendelea miongoni mwa malaika. Walimkuta Baba akiwa anaongea na Mwana wake, ili kuamua ni jinsi gani, kwa faida ya malaika wale watiifu, wangeweza kuyaangusha milele mamlaka yale ambayo Shetani amejitwalia mwenyewe. Mungu mkuu angeweza kumtupa mara moja huyu mdanganyifu mkuu kutoka mbinguni, lakini hili halikuwa kusudi lake. Angependa kuwapa waasi hawa nafasi sawa ili wapate kupima uwezo na nguvu zao dhidi ya Mwana wake mwenyewe na malaika watiifu. PLK 8.1
Katika vita hivi kila malaika angechagua upande, ili wote waone. Isingeweza kuwa salama kumruhusu ye yote ambaye alijiunga na Shetani kuendelea kuwapo mbinguni. Walikuwa wamejifunza somo la uasi halisi dhidi ya sheria ya Mungu isiyobadilika, na hali hii haiwezi kutibika. Iwapo Mungu angetumia uwezo wake wa kumwadhibu mwasi huyu mkuu, malaika wale ambao hawakuridhika wasingeweza kufichuliwa. Kwa hiyo Mungu alichukua njia nyingine, kwa sababu alitaka kudhihirisha haki na hukumu zake wazi kwa viumbe wote wa mbinguni. PLK 8.2
Vita Mbinguni-Ulikuwa ni uhalifu mkuu kuliko mwingine wo wote kuasi dhidi ya serikali ya Mungu. Mbingu yote ilionekana kuwa katika ghasia. Malaika walipangwa katika vikosi, kila kundi likiwa na kamanda wake. Shetani alikuwa akipigana vita dhidi ya sheria ya Mungu, kwa sababu alikuwa na hamu ya kujitukuza mwenyewe na hakutaka kuwa chini ya mamlaka ya Mwana wa Mungu, aliye kamanda mkuu wa mbinguni. PLK 9.1
Malaika wote wa mbinguni waliitwa kuhudhuria mbele za Baba. Shetani bila aibu alitangaza kutokuridhika kwake kwamba Kristo aliheshimika zaidi yake. Alisimama juu kwa kiburi na kusisitiza kuwa alipaswa kuwa sawa na Mungu. Malaika wema walilia machozi waliposikia maneno ya Shetani na majivuno yake ya kijeuri. Mungu alitangaza kuwa waasi hawawezi kuendelea kuwapo mbinguni. Walikuwa wamedumisha kuishi kwao katika hadhi ya juu na kwa furaha kwa sharti la utii kwa sheria ambayo Mungu alikuwa ameitoa ili kuwatawala viumbe wa mbinguni. Lakini hakuna jinsi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaokoa wale waliothubutu kukiuka sheria yake. PLK 9.2
Shetani alikuwa shupavu katika uasi wake, akidhihirisha dharau yake kwa sheria ya Mwumbaji wake. Alidai kuwa malaika hawakuhitaji sheria bali walitakiwa kuachwa huru kufuata mapenzi yao wenyewe, ambayo siku zote yangewaongoza sawa. Sheria, alisema, ilikuwa ni kizuio cha uhuru wao, na kuiondoa sheria ilikuwa ni kusudi moja kubwa la yeye kuchukua msimamo wa upinzani. PLK 9.3
Furaha ya malaika ilikuwa katika utii wao mkamilifu kwa sheria. Kila mmoja wao alikuwa na kazi yake maalumu aliyopewa, na hadi Shetani alipoasi, palikuwa na utaratibu kamili na utendaji wa upatanifti kule mbinguni. PLK 9.4
Ndipo palikuwako na vita mbinguni. Mwana wa Mungu, Mfalme wa mbingu, na malaika wake waaminifu waliingia katika mgogoro na mwasi mkuu na wale walioungana naye. Mwana wa Mungu na malaika wale wakweli, na waaminifu walishinda, na Shetani na wafuasi wake walifukuzwa kutoka mbinguni. Malaika wote waliobaki walimkubali na kumwabudu Mungu wa haki. Hakuna hata doa la uasi liliachwa mbinguni. Kila kitu kilikuwa amani na upatanifu tena, kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Malaika mbinguni waliomboleza kuhusu msiba wa wale waliokuwa wenzi wao katika raha na furaha kamili. Mbingu yote ilihisi kupotea kwao. PLK 10.1
Baba alishauriana na Mwana wake kuhusu kuchukua hatua mara moja juu ya mpango wao wa kuwafanya wanadamu kuishi duniani. Angewaweka katika matazamio ili kuona uaminifu wao kabla hawajaweza kufanywa kuwa wa kudumu milele. Ilikuwa wapewe fadhila za Mungu. Wangepata fursa ya kuongea na malaika, hali kadhalika malaika nao kuongea nao. Mungu hakuona kuwa ni vema kuwaweka katika hali inayopita uwezo wa kutokutii. PLK 10.2