Sura hii imejengwa katika Mwanzo 1.
Baba na Mwana waliianza kazi ile kuu, na ya ajabu waliyokuwa wameipanga-kuiumba dunia. Dunia ilitokea katika mkono wa Muumbaji ikiwa ni nzuri ajabu. Kulikuwako na milima na vilima na tambarare, vilivyotenganishwa na mito na maumbile mengine ya maji. Dunia haikuwa tambarare moja pana, bali usawa ule wa mandhari uliingiliwa kati na vilima na milima, si mirefu na yenye mawemawe kama ilivyo kwa sasa, bali ilikuwa na maumbo yaliyo linganifu na mazuri. Miamba iliyo wazi, na kutokeza juu haikuonekana kamwe juu yao, bali ilikuwa chini ya uso wake, ikiwa kama mifupa ya dunia. PLK 11.1
Maji yalitawanywa kwa usawa. Vilima, milima, na tambarare zilizokuwa nzuri sana zilivishwa kwa mimea na maua na miti mirefu ya fahari ya kila aina, ambayo ilikuwa mikubwa na mizuri mara nyingi mno kuliko miti ya leo. Hewa ilikuwa safi na yenye kuleta afya, na nchi ilionekana kama ikulu bora. Malaika waliona hili na kufurahi kwa ajili ya kazi za Mungu zilizo za ajabu na nzuri. PLK 11.2
Walipokwisha kuiumba dunia na wanyama juu yake, Baba na Mwana walitekeleza kusudi lao, lililopangwa kabla ya kuanguka kwa Shetani, kuwafanya wanadamu kwa mfano wao wenyewe. Walikuwa wamefanya kazi pamoja katika uumbaji wa dunia na kila kiumbe hai kilichokuwa juu yake. Na sasa Mungu alisema kwa Mwana wake, “Na tufanye mtu kwa mfano wetu.” PLK 11.3
Adamu alipotoka katika mkono wa Mwumbaji wake, alikuwa na urefu bora na ulinganifu mzuri. Sura yake ilikuwa kamilifu na nzuri. Rangi yake ya mwili haikuwa nyeupe wala kijivujivu, bali nyekundu iking’ara kwa rangi ya afya bora. Hawa hakuwa mrefu kama Adamu. Kichwa chake kilifikia juu kidogo ya mabega yake. Yeye, pia, alikuwa bora, mwenye ulinganifu mzuri, na mrembo sana. PLK 11.4
Ingawa Mungu alikuwa amefanya kila kitu katika ukamilifu wa uzuri, na dunia ilionekana kutokosa kitu cho chote cha kumfanya Adamu na Hawa kuwa na furaha, lakini Mungu alionesha upendo wake mkuu kwao kwa kupanda bustani mahususi kwa ajili yao. PLK 12.1
Ilikuwa watumie sehemu ya muda wao katika kufanya kazi ya kupendeza ya kuitunza bustani hiyo, na sehemu nyingine kuongea na malaika, kusikiliza maelekezo yao, na katika tafakari za furaha. Kazi yao haikuwa ya kuchosha bali ya kufurahisha na yenye kutia nguvu. Bustani hii nzuri ndio ilikuwa iwe maskani yao. PLK 12.2
Katika bustani hii Bwana aliweka miti ya kila aina kwa ajili ya matumizi na uzuri. Kulikuwa na miti iliyosheheni matunda tele, yaliyojaa harufu nzuri, na yenye ladha ya kupendeza, ambayo Mungu alipanga yawe chakula kwa ajili ya wana ndoa hawa watakatifu. Palikuwapo na mizabibu ya kupendeza iliyokuwa wima kwenda juu, ikiwa imejazwa na mizigo ya matunda yake. Ilikuwa ni kazi ya kufurahisha ya Adamu na Hawa kutengeneza matao mazuri ya kivuli kutokana na matawi ya mizabibu na kuyaelekeza, yakitengeneza makazi ya asili kuwa mazuri, miti iliyo hai na majani, yakiwa yamebeba matunda yao yenye kunukia. PLK 12.3
Dunia ilikuwa imefunikwa kwa kijani hai, wakati ambapo maelfu ya maua yenye harufu nzuri ya kila aina na kila rangi yaliinuka juu kuwazunguka Adamu na Hawa kwa wingi tele. Kila kitu kilipangwa kwa namna ya kupendeza na tukufu. Katikati ya bustani ulisimama mti wa uzima, utukufu wake ukiwa ni zaidi ya miti mingine yote. Matunda yake yangewahifadhi hai milele. Majani yake yalikuwa na sifa za uponyaji. PLK 12.4
Adamu na Hawa katika Edeni- Wana ndoa hawa watakatifu walikuwa na furaha sana wakiwa katika Edeni. Mungu aliwapa utawala usio na mpaka juu ya kila kitu chenye uhai. Simba na mwana kondoo walicheza pamoja kando yao kwa amani na bila kudhuriana au walilala miguuni pao. Ndege wa kila rangi na kila aina ya manyoya walirukaruka miongoni mwa miti na maua na kuwazunguka Adamu na Hawa, wakati ambapo sauti zao nyororo za kimuziki zilitoa mwangwi miongoni mwa miti kwa mpatano mzuri wa sauti huku wakiimba sifa kwa Muumba wao. PLK 13.1
Adamu na Hawa walipendezwa na uzuri wa maskani yao ya Edeni. Walifurahishwa na chiriku wadogo waliowazunguka, wakiwa wamevikwa manyoya mazuri, na huku wakiimba muziki wao wa furaha na uchangamfu. Wana ndoa hawa watakatifu walijiunga nao na kuinua sauti zao kwa nyimbo zenye sauti za kupatana za upendo, sifa, na za ibada kwa Baba na Mwana wake kwa ajili ya ushahidi wa upendo uliowazunguka kila upande. Walitambua utaratibu na upatanifu wa uumbaji, ambao ulionesha hekima na maarifa ambavyo havikuwa na kikomo. PLK 13.2
Siku zote walikuwa wakivumbua uzuri mpya na utukufu wa ziada wa maskani yao ya Edeni, ambavyo vilijaza mioyo yao kwa upendo wa kina zaidi na kutoa katika vinywa vyao misemo ya sifa na kicho kwa Muumba wao. PLK 13.3