Muda ulifika ambapo Yesu ilibidi achukue juu yake asili ya mwanadamu, ajinyenyekeshe kama mwanadamu, na kupata majaribu ya Shetani. PLK 59.1
Alizaliwa bila fahari yo yote ya kidunia, katika zizi na kulazwa katika hori la ng’ombe. Hata hivyo kuzaliwa kwake kuliheshimiwa sana kupita kuzaliwa kwa mwanadamu mwingine ye yote. Malaika kutoka mbinguni waliwajulisha wachungaji kuhusu ujio wa Yesu, na nuru na utukufu kutoka kwa Mungu vilifuatana na ushuhuda wao. Jeshi la mbinguni lilichukua vinubi vyao na kumtukuza Mungu. Kwa shangwe walitangaza ujio wa Mwana wa Mungu katika ulimwengu ulioanguka ili kukamilisha kazi ya ukombozi, na kwa kifo chake kuleta amani, furaha, na uzima wa milele kwa wanadamu. Mungu aliutukuza ujio wa Mwana wake. Malaika walimwabudu. PLK 59.2
Ubatizo wa Yesu-Miaka thelathini baadaye, malaika wa Mungu walizunguka juu ya tukio la kubatizwa kwake. Roho Mtakatifu alishuka katika umbo la hua na kutua juu yake na huku watu wakiwa wamesimama kwa mshangao mkubwa, macho yao yakiwa yamekazwa kwake, walisikia sauti ya Baba kutoka mbinguni, ikisema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Marko 1:11. PLK 59.3
Yohana hakuwa na hakika kwamba alikuwa ni Mwokozi aliyekuja kubatizwa naye katika Mto Yordani. Lakini Mungu alikuwa amemwahidi ishara ambayo kwayo angeweza kumfahamu Mwana-kondoo wa Mungu. Yohana aliitambua ishara ile wakati hua wa mbinguni alipotua juu ya Yesu na utukufu wa Mungu kuangaza ukimzunguka. Yohana alinyosha mkono wake, akiuelekeza kwa Yesu, na kwa sauti kuu alisema, “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” Yohana 1:29. PLK 59.4
Huduma ya Yohana-Yohana aliwataarifu wanafunzi wake kuwa Yesu alikuwa ndiye Masihi aliyeahidiwa, Mwokozi wa ulimwengu. Wakati kazi ya Yohana ilipokuwa inafungwa, aliwafundisha wanafunzi wake kumwangalia Yesu na kumfuata kama Mwalimu Mkuu. Maisha ya Yohana yalikuwa ya kusikitisha na ya kujikana nafsi. Alitangaza ujio wa kwanza wa Kristo lakini hakuruhusiwa kushuhudia miujiza yake na kufurahia uwezo ambao aliudhihirisha. Yesu alipojithibitisha kama mwalimu, Yohana alifahamu kuwa yeye mwenyewe alipaswa kufa. Sauti yake ilisikika kwa nadra, isipokuwa nyikani. Maisha yake yalikuwa ya upweke. Hakuambatana na familia ya baba yake, wala kufurahia kujumuika nao, bali aliwaacha ili atimize utume wake. Umati wa watu waliacha miji yenye shughuli nyingi na vijiji, wakikusanyika nyikani ili kusikia maneno ya nabii wa ajabu. Yohana alikwenda katika kiini cha tatizo la watu. Aliikemea dhambi, bila kuhofu matokeo yake, na kuandaa njia kwa ajili ya Mwana-kondoo wa Mungu. PLK 60.1
Herode alisisimka aliposikia shuhuda za Yohana zenye nguvu na za wazi, na kwa shauku kuu alitafuta kujua afanye nini ili apate kuwa mwanafunzi wake. Yohana alifahamu kuwa Herode alikuwa anaelekea kumwoa mke wa ndugu yake wakati mume wake akiwa bado yu hai, na kwa uaminifu alimwambia Herode kuwa jambo hili halikuwa halali. Herode hakutaka kujinyima kitu cho chote kile. Alimwoa mke wa ndugu yake, na kwa ushawishi wa mke huyo, alimkamata Yohana na kumweka jela, akikusudia, hata hivyo, kumfungulia. Wakati Yohana akiwa amezuiliwa pale, kupitia kwa wanafunzi wake alisikia kuhusu matendo makuu ya Yesu. Hakuweza kwenda ili kusikia maneno yake ya neema, bali wanafunzi wake walimjulisha na kumfariji kwa yale waliyoyasikia. Muda mfupi baadaye Yohana alikatwa kichwa, kupitia kwa ushawishi wa huyo mke wa Herode. Wanafunzi wa chini kabisa waliomfuata Yesu, wakashuhudia miujiza yake na kusikia maneno ya faraja aliyoyasema, walikuwa ni wakuu kuliko Yohana Mbatizaji (angalia Mathayo 11:11); yaani, walitukuzwa na kuheshimiwa, na walikuwa na raha zaidi katika maisha yao. PLK 60.2
Yohana alikuja katika roho na uwezo wa Eliya ili kutangaza ujio wa kwanza wa Yesu. Luka 1:17. Yohana aliwawakilisha wale ambao katika siku za mwisho wangeondoka kwenda nje katika roho na uwezo wa Eliya kuitangaza siku ya ghadhabu na ujio wa pili wa Yesu. PLK 61.1
Jaribu-Baada ya ubatizo wa Yesu katika Yordani, aliongozwa na Roho kwenda nyikani, ili ajaribiwe na mwovu. Roho Mtakatifu alikuwa amemwandaa kwa ajili ya tukio lile maalumu la majaribu makali. Kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na Shetani na katika siku zile hakula cho chote. Kila kitu kilichomzunguka hakikumpendeza, hali ambayo asili ya ubinadamu ingetamani kuiepuka. Alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu pamoja na Shetani katika mahali pa ukiwa na upweke. Mwana wa Mungu alipauka na kudhoofika, kwa sababu ya kufunga na mateso. Lakini njia yake iliwekwa wazi mbele yake, na lazima atimize kazi ile aliyokuja kuifanya. PLK 61.2
Shetani alitumia nafasi ya mateso ya Mwana wa Mungu na akapanga kumsumbua kwa majaribu mengi, akitarajia kupata ushindi juu yake kwa sababu alikuwa amejinyenyekesha kama mwanadamu. Shetani alikuja na jaribu hili: “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.” Alimjaribu Yesu apate kujishusha ili ampe uthibitisho kuwa alikuwa ndiye Masihi, kwa kutumia uweza wake wa kiungu. Yesu alimjibu kwa upole “Imeandikwa ya kwamba, lmtu hataishi kwa mkate tu.’ ” Luka 4:3, 4. PLK 61.3
Shetani alitaka kushindana na Yesu kuhusu kuwa kwake Mwana wa Mungu. Alielekeza katika hali yake ya udhaifu na mateso na kwa majivuno alithibitisha kuwa alikuwa na nguvu kumpita Yesu. Lakini ushahidi wa Mungu kutoka mbinguni uliosema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” (Luka 3:32), ulitosha kumwimarisha Yesu kupitia mateso yake yote. Kristo hakuwa chini ya masharti yo yote kumshawishi Shetani kuhusu uwezo wake au kwamba yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Shetani ana ushahidi wa kutosha kuhusu cheo kilichotukuka na mamlaka ya Mwana wa Mungu. Kukataa kwake kujisalimisha chini ya mamlaka ya Kristo ndiyo kulikomfungia nje ya mbingu. PLK 62.1
Ili kuonesha uwezo wake yeye mwenyewe, Shetani alimbeba hadi Yerusalemu na kumweka juu ya kinara cha hekalu, na pale alimjaribu ili apate kutoa ushahidi kuwa alikuwa ndiye Mwana wa Mungu kwa kujirusha chini kutoka katika umbali wa kutia kizunguzungu. Shetani alikuja na maneno yaliyovuviwa ya Biblia: “Kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba, mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” Yesu akajibu akamwambia, “Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.” Luka 4:10-12. Shetani alitaka kumfanya Yesu atumie vibaya rehema za Baba yake na kuthubutu kukomesha maisha yake kabla ya kutimiza utume wake. Alitarajia kuwa mpango wa wokovu ungeshindwa, lakini mpango huu ulipangwa kwa kina mno kiasi kwamba Shetani asingeweza kuupindua au kuuharibu. PLK 62.2
Kristo ni mfano kwa Wakristo wote. Wanapo- jaribiwa au haki zao zinapopingwa, wanapaswa kubeba yote kwa uvumilivu. Hawapaswi kujisikia kuwa wana haki ya kumwita Bwana kuonesha uweza wake ili wapate ushindi dhidi ya maadui zao, isipokuwa pale ambapo Bwana ataheshimiwa moja kwa moja kwa kufanya hivyo. Iwapo Yesu angejitupa chini kutoka kwenye kinara cha hekalu, kitendo kile kisingemtukuza Baba yake, kwa kuwa hakuna mtu ye yote angeona tukio lile isipokuwa Shetani na malaika wa Mungu. Na kungekuwa ni kumjaribu Bwana ili aoneshe uwezo wake kwa adui yake mchungu kuliko wote. Huko kungekuwa ni kujishusha mbele ya yule ambaye Yesu alikuja ili apate ku mshinda. PLK 62.3
“Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, ‘Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.’ PLK 63.1
“Yesu akajibu akamwambia, ‘Imeandikwa, “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” ‘ ” Luka 4:5-8. Shetani alimwonesha Yesu falme za dunia katika nuru ya kupendeza mno. Iwapo Yesu angemwabudu pale pale, alijitolea kuacha madai yake kuhusu umiliki wa dunia. Iwapo mpango wa wokovu ungetimizwa na Yesu kufa kwa ajili ya kuwakomboa wenye dhambi, Shetani alijua kuwa uwezo wake yeye mwenyewe ungedhibitiwa na hatimaye kuondolewa kabisa, na kwamba angeangamizwa. Kwa hiyo ulikuwa ni mpango wake wa makusudi, kama ingewezekana, kumzuia Yesu kutimiza kazi ile kuu aliyokwisha kuianza. Iwapo mpango wa Mungu wa ukombozi ungeshindwa, basi Shetani angedumisha ufalme ambao wakati ule alidai kuwa wake. Alijidanganya mwenyewe kuwa hapo ndipo angetawala kwa kumpinga Mungu wa mbinguni. PLK 63.2
Mjaribu Akemewa -Shetani alifurahishwa pale Yesu alipoweka kando uwezo pamoja na utukufu wake na kuiacha mbingu. Alidhani kuwa hali hii ilikuwa inamweka Mwana wa Mungu chini ya uwezo wake yeye Shetani. Jaribu lile liliwashinda kirahisi sana ile njozi takatifu katika Edeni kiasi kwamba alitarajia kwamba kwa uwezo wake wa kishetani na hila angeweza kumshinda hata Mwana wa Mungu na hivyo kuokoa maisha yake yeye mwenyewe pamoja na ufalme wake. Kama angeweza kumjaribu Yesu kupotea kutoka katika njia ya mapenzi ya Baba yake, angeweza kutimiza lengo lake. Lakini Yesu alimkabili mjaribu huyu kwa karipio, “Nenda zako, Shetani!” Alipaswa kusujudu kwa Baba yake peke yake. PLK 63.3
Shetani alidai ufalme wa dunia kuwa wake na kupendekeza kwa Yesu kwamba angeweza kuepuka mateso yake yote, kwamba hakuwa na haja ya kufa ili ndipo aupate ufalme wa dunia hii. Iwapo tu angemwabudu, angeweza kuwa na umiliki wa dunia na utukufu wa kutawala juu yao. Lakini Yesu hakusisimka. Alijua kuwa muda bado ulikuwa haujafika ambapo, kwa gharama ya maisha yake mwenyewe, angeweza kuukomboa ufalme kutoka mikononi mwa Shetani, na kwamba, baada ya muda kitambo, wote mbinguni na duniani wangejisalimisha kwake. Alichagua maisha yake ya mateso na kifo chake cha kuogopesha kama njia ambayo Baba yake aliiagiza kwa ajili yake ili apate kuwa mrithi halali wa falme za dunia na kufanya ziwekwe mikononi mwake kama milki ya milele. Shetani pia atawekwa mikononi mwake apate kuangamizwa kwa mauti, kamwe asimsumbue tena Yesu na watu wake waliokombolewa kwa utukufu. PLK 64.1