Baada ya Shetani kukoma majaribu yake, alimwacha Yesu kwa kitambo. Malaika walimtayarishia chakula huko nyikani na kumtia nguvu, na baraka za Baba yake zilikuwa juu yake. Majaribu makali kabisa ya Shetani yalishindwa, na bado alikuwa akiangalia mbele katika wakati wa huduma ya Yesu, ambapo kwa nyakati mbalimbali angejaribu njama zake dhidi yake. Bado alitumaini kumshinda kwa kuwachochea wale ambao wangekataa kumpokea Yesu wamchukie na kujaribu kumwangamiza. PLK 64.2
Shetani na malaika zake walikuwa wakishughulika mno wakati wa huduma ya Yesu, wakiwashawishi watu kwa kutokuamini, chuki, na dhihaka. Mara kadhaa wakati Yesu alipoongea ukweli unaochoma moyo, ukielekeza katika dhambi zao, watu wangekasirika. Shetani na malaika zake waliwashawishi wapate kuyaondoa maisha ya Mwana wa Mungu. Zaidi ya mara moja waliokota mawe ili wamtupie, lakini malaika walimlinda na kumchukua kutoka katika umati wenye hasira kwenda mahali pa salama. Tena, wakati ukweli wa wazi ukitoka katika midomo yake mitakatifu, watu walimkamata na kumwongoza katika ukingo wa mlima, wakikusudia kumtupa chini. Ubishani ulitokea miongoni mwao kuhusu kitu gani walichopaswa kumtendea, wakati ambapo malaika tena walimficha kutoka katika macho ya umati ule, na alipita katikati yao alipokuwa akienda zake. PLK 65.1
Shetani bado alikuwa na tumaini kwamba ule mpango mkuu wa wokovu ungeshindwa. Aliweka nguvu zake zote ili kufanya mioyo ya watu kuwa migumu na hisia zao kuwa chungu dhidi ya Yesu. Alitumaini kuwa ni watu wachache tu wangempokea kama Mwana wa Mungu kiasi kwamba angetafakari kuwa mateso yake na kafara kuwa makubwa mno kuweza kutolewa kwa ajili ya kundi dogo tu kama lile. Lakini iwapo wangekuwapo watu wawili tu ambao wangempokea Yesu kama Mwana wa Mungu na kumwamini kwa ajili ya wokovu, bado angetekeleza mpango ule. PLK 65.2
Kuwafariji Wanaoteseka - Yesu alianza kazi yake kwa kuivunja nguvu ya Shetani juu ya mateso. Aliwarejesha wagonjwa katika afya njema, akawapa vipofu kuona, na kuwaponya vilema, akiwasababisha kurukaruka kwa furaha wakimsifu Mungu. alirejesha afya njema kwa wale ambao waliugua sana, wakiwa wameshikwa katika nguvu katili za Shetani kwa miaka mingi. Kwa maneno yenye neema aliwafariji waliokuwa dhaifu, waliotetemeka, na waliokuwa wanakata tamaa. Wanyonge, wenye kuteseka ambao Shetani alikuwa amewashika kwa ushindi, Yesu aliwang’oa kwa nguvu kutoka katika mshiko wake, akiwarejeshea afya ya kimwili na furaha kuu pamoja na kuridhika. Aliwahuisha wafu, na walimtukuza Mungu kwa ajili ya maonesho makuu ya uweza wake. Alitenda kwa nguvu sana kwa wale wote waliomwamini. PLK 65.3
Maisha ya Kristo yalijazwa kwa maneno na matendo ya wema, huruma, na upendo. Kila wakati alikuwa tayari kusikiliza na kutuliza matatizo ya wale waliokuja kwake. Miili iliyoponywa ya watu wengi ilikuwa imebeba ushahidi wa uweza wake wa kiungu. Lakini bado, hata baada ya kuwatendea makubwa kiasi hicho, wengi walikuwa wanamwonea haya huyu Mhubiri mkuu na mnyenyekevu. Kwa sababu watawala hawakumwamini, watu hawakuwa tayari kumpokea Yesu. Alikuwa ni mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko. Hawakuweza kuvumilia kutawaliwa na maisha yake matulivu na ya kujikana nafsi. Walitaka kufurahia heshima inayotolewa na ulimwengu. Hata hivyo, wengi walimfuata Mwana wa Mungu na kusikiliza maelekezo yake, wakifurahia maneno ambayo yalitoka katika midomo yake kwa neema sana. Maneno yake yalikuwa yamejaa maana, na bado yalikuwa dhahiri kiasi kwamba mtu dhaifu kuliko wote angeweza kuyaelewa. PLK 66.1
Upinzani Usio na Nguvu -Shetani na malaika zake walipofusha macho na kutia giza ufahamu wa Wayahudi, na kuwachochea wakuu wa watu na watawala ili wayaangamize maisha ya Mwokozi. Watawala waliwatuma watu wapate kumleta Yesu kwao, lakini hawa waliotumwa walipofika karibu na alipokuwapo walishangaa sana. Walimwona akiwa amejaa utu wema na huruma pale alipoyashuhudia mateso ya mwanadamu. Walimsikia akisema kwa upendo na upole akiwatia moyo waliokuwa dhaifu na wenye kuteseka. Walisikiliza maneno yake ya hekima, na wakapendezewa mno. Hawakuweza kumkamata. Walirudi kwa makuhani na wazee pasipokuwa na Yesu. PLK 66.2
Walipoulizwa, “Mbona hamkumleta?” walisema kile walichokiona kuhusu miujiza yake, na maneno matakatifu ya hekima, upendo, na maarifa waliyoyasikia. Waliishia kusema, “Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena!” Yohana 7:45, 46. Kuhani mkuu aliwalaumu kuwa wao pia walidanganyika, na baadhi ya askari waliona aibu kwa nini hawakumchukua kifungoni. Makuhani waliuliza kwa dharau iwapo yupo mtawala ye yote aliyemwamini. Wengi wa mahakimu na wazee walimwamini Yesu, lakini Shetani aliwazuia kulikubali jambo hilo. Waliogopa dharau za watu kuliko walivyomwogopa Mungu. PLK 67.1
Hadi hapo njama na chuki za Shetani hazikuwa zimevunja mpango wa wokovu. Muda ulikuwa unasogea karibu kwa ajili ya Yesu kutimiza kusudi lililomfanya aje duniani. Shetani na malaika zake walishauriana na kuamua kuwachochea taifa la Yesu mwenyewe kudai kwa bidii damu yake na kulundika ukatili na dharau juu yake. Walitarajia kuwa Yesu angekasirikia kutendewa vile na kushindwa kudumisha unyenyekevu na upole wake. PLK 67.2
Wakati ambapo Shetani alikuwa akiweka mipango yake, Yesu kwa uangalifu alikuwa akifungua kwa wanafunzi wake mateso ambayo alipaswa kuyapitia- kwamba angesulubiwa na kwamba angefufuka tena katika siku ya tatu. Lakini ufahamu wao ulielekea kuwa dhaifu, na hawakuweza kufahamu kile alichowaambia. PLK 67.3
Kubadilika Sura -Imani ya wanafunzi wale iliimarishwa sana wakati wa kubadilika sura, waliporuhusiwa kuona utukufu wa Kristo na kusikia sauti kutoka mbinguni ikishuhudia kuhusu sifa yake ya kiungu (Angalia Mathayo 17:1-8.) Mungu aliamua kuwapa wanafunzi wa Yesu uthibitisho imara kuwa yeye ndiye aliyekuwa Masihi, ili kwamba katika huzuni yao kuu na kukata tamaa wakati wa kusulubiwa kwake, wasingepoteza kabisa imani. Wakati wa kubadilika sura Bwana aliwatuma Musa na Eliya kuzungumza na Yesu kuhusu mateso na kifo chake. Badala ya kuwachagua malaika kuzungumza na Mwana wake, Mungu aliwachagua wale ambao wenyewe walipitia uzoefu wa majaribu ya dunia. PLK 68.1
Eliya alitembea pamoja na Mungu. Kazi yake ilikuwa ya maumivu na yenye majaribu, kwa sababu kupitia kwake Bwana aliweka wazi dhambi za Israeli. Eliya alikuwa ni nabii wa Mungu, hata hivyo ilibidi akimbie kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kuokoa maisha yake. Taifa lake mwenyewe lilimwinda kama mnyama wa porini ili wapate kumwangamiza. Lakini Mungu alimhamisha Eliya. Malaika walimbeba katika utukufu na ushindi hadi mbinguni, bila ya kuonja kifo. PLK 68.2
Musa alikuwa ni mkuu kuliko ye yote aliyewahi kuishi kabla yake. Mungu alimheshimu sana. Alikuwa amependelewa kuweza kusema na Mungu uso kwa uso, kama vile mtu anavyosema na rafiki yake. Aliruhusiwa kuona nuru angavu na utukufu bora unaomfunika Baba. Kupitia kwa Musa Bwana aliwaokoa Waisraeli kutoka katika utumwa wa Misri. Musa alikuwa ni mpatanishi kwa ajili ya watu wake, mara kwa mara akisimama kati yao na ghadhabu ya Mungu. Wakati hasira ya Bwana ilikuwa kubwa dhidi ya Israeli kwa sababu ya kutokuamini kwao, kulalamika kwao, na dhambi zao za kuchukiza, upendo wa Musa kwao ulijaribiwa. Mungu alipendekeza kuwaangamiza watu na kisha kutengeneza taifa lenye nguvu kutoka kwake. Musa alionesha upendo wake kwa Israeli kwa kukusihi kwa bidii kwa niaba yao. Katika dhiki yake alimwomba Mungu kuacha hasira yake kali na kumsamehe Israeli, au afute jina lake kutoka katika kitabu chake. PLK 68.3
Musa alipitia kifo, lakini Mikaeli alishuka chini na kumpa uhai kabla mwili wake haujaanza kuoza. Shetani alijaribu kuuzuia ule mwili, kwa kudai kuwa ulikuwa wake, lakini Mikaeli alimfufua Musa na kumchukua kwenda mbinguni. Shetani alimshutumu Mungu vikali, akimsuta kuwa si mwenye haki kwa kuruhusu windo lake kuchukuliwa kutoka kwake. Lakini Kristo hakumkaripia adui yake, ingawa ilikuwa ni kupitia kwa majaribu ya Shetani ndipo mtumishi wa Bwana alianguka. Kwa upole alimwelekeza kwa Baba yake, akisema, “Bwana na akukemee!” Yuda 9. PLK 69.1
Yesu alikuwa amewaambia wanafunzi wake kwamba kulikuwako na wengine ambao walikuwa wamesimama pamoja naye ambao wasingeonja mauti hadi pale ambapo wangeuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu. Wakati wa kubadilika sura ahadi hii ilitimizwa. Uso wa Yesu ulibadilishwa pale, uking’aa kama jua. Mavazi yake yalikuwa meupe na yenye kumeremeta. Musa alikuwapo pale kuwawakilisha wale ambao watafufuliwa kutoka katika wafu wakati wa ujio wa pili wa Yesu. Na Eliya, ambaye alihamishwa kwenda mbinguni bila kuona kifo, aliwawakilisha wale ambao watabadilishwa kwenda katika hali ya kutokufa wakati wa kurudi kwa Yesu nao watahamishwa kwenda mbinguni pasipo kuona kifo. Kwa mshangao na hofu wanafunzi wale waliona ukuu wa ajabu wa Yesu na wingu lile lililowafunika, nao walisikia sauti ya Mungu kwa utukufu wa kutisha, ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu. Msikieni yeye!” PLK 69.2