Kristo, Mwana mpendwa wa Mungu, aliongo- zwa kutoka nje na kukabidhiwa kwa watu ili apate kusulubiwa. Wafuasi pamoja na waumini kutoka katika maeneo yaliyozunguka walijiunga na umati uliomfuata Yesu kwenda Kalvari. Mama yake Yesu pia alikuwapo pale, akisaidiwa na Yohana, mwanafunzi mpendwa. Moyo wake ulijazwa na uchungu usioweza kutamkika, lakini bado pamoja na wanafunzi, alitumaini kuwa tukio hili lenye kuumiza lingeweza kubadilika, na Yesu angeweza kuthibitisha uweza wake na kutokea mbele ya maadui zake kama Mwana wa Mungu. Na hapo ndipo tena moyo wa mama ulipozama alipokumbuka maneno ambayo kwayo kwa kifupi hapo awali [Yesu] alieleza juu ya mambo ambayo yalikuwa yakitendwa siku ile kama vile maigizo. PLK 80.3
Mara tu Yesu alipopita mlango wa nyumba ya Pilato msalaba ambao ulikuwa umetengenezwa kwa ajili ya Baraba uliletwa na kuwekwa juu ya mabega yake yaliyokuwa yamechubuliwa na kuvuja damu. Misalaba pia iliwekwa juu ya wenzi wa Baraba, ambao ilikuwa wafe wakati mmoja na Yesu. Mwokozi alikuwa ameubeba mzigo wake mwendo mfupi tu, ambapo kutokana na upotevu wa damu nyingi na uchovu mwingi na maumivu makali, alianguka chini na kuzimia. PLK 81.1
Yesu alipoamka, walimbebesha tena msalaba mabegani mwake na kusukumwa kwenda mbele kwa nguvu. Alipepesuka kwa hatua chache, akiwa amebeba mzigo wake mzito, kisha akaanguka chini kama mtu mfu. Kwanza walimtangaza kuwa alikuwa amekufa, lakini hatimaye aliamka. Makuhani na watawala hawakuhisi huruma yo yote kwa ajili ya mhanga wao atesekaye, bali waliona kuwa isingewezekana tena kwake kubeba zana hii ya mateso. Wakati bado wanawaza lipi la kufanya, Simoni, Mkirene, akitokea upande mkabala alikutana na umati ule. Kwa uchochezi wa makuhani alikamatwa na kulazimishwa kuubeba msalaba wa Kristo. Wana wa kiume wa Simoni walikuwa wafuasi wa Yesu, bali yeye mwenyewe alikuwa hajawahi kamwe kuungana naye. PLK 81.2
Kundi kubwa lilimfuata Mwokozi hadi Kalvari. Wengi walikuwa wakidhihaki na kukejeli, lakini baadhi yao walikuwa wakiomboleza na kusimulia sifa zake. Wale ambao alikuwa amewaponya magonjwa mbalimbali na wale ambao aliwafufua kutoka katika wafu kwa bidii walitangaza kazi zake za ajabu na kudai waambiwe ni kitu gani kibaya Yesu alikuwa ametenda kiasi cha kutendewa kama mhalifu. Siku chache tu zilizopita, walikuwa wakimfuata na kuimba hosana kwa furaha huku wakipepea matawi ya mitende alipoingia Yerusalemu kwa shangwe. Lakini wengi ambao wakati ule waliimba sifa zake kwa kuwa ilikuwa ikipendeza kufanya hivyo wakati ule sasa walipaza sauti “Asulubiwe! Asulubiwe!” PLK 81.3
Apigiliwa Misumari Msalabani-Walipofika pale mahali pa mauaji, waliohukumiwa kifo walifungwa katika zana za mateso. Wakati ambapo wevi wale wawili walipopambana mikononi mwa wale waliokuwa wakiwanyoosha katika misalaba yao, Yesu hakutoa upinzani wo wote. Mama wa Yesu aliangalia kwa wasiwasi wenye maumivi makali, akitumaini kuwa huenda angetenda muujiza wa kujiokoa mwenyewe. Aliona mikono yake ikiwa imenyoshwa katika msalaba-mikono ile yenye upendo ambayo siku zote ilikuwa ikitoa mibaraka na ilinyoshwa mara nyingi ili kuwaponya wenye kuteseka. Sasa nyundo na misumari vililetwa, na misumari ilipigiliwa kwenye nyama laini na kufungamanishwa na msalaba, wanafunzi waliovunjwa moyo waliubeba kutoka kwenye tukio lile la kikatili mwili uliozimia wa mama yake Kristo. PLK 82.1
Yesu hakulalamika hata kidogo. Uso wake ulibaki kuwa umefifia rangi na kuwa mtulivu, lakini matone ya jasho yalitua juu ya uso wake. Hakukuwapo na mkono wa huruma wa kufuta matone haya ya kifo kutoka katika uso wake, wala maneno ya huruma na uaminifu usiobadilika ili kuchangamsha moyo wake wa kibinadamu. Alikuwa akikanyaga shinikizo la mvinyo peke yake kabisa; na miongoni mwa watu wote hakuna hata mmoja aliyekuwa pamoja naye. Wakati ambapo askari walikuwa wakitenda kazi yao ya kutisha na yeye alikuwa akistahimili maumivu makali mno, Yesu aliomba kwa ajili ya maadui zake: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Luka 23:34. Ombi lile la Yesu kwa ajili ya maadui zake ni la ulimwengu wote likimjumuisha kila mwenye dhambi atakayewahi kuishi tangu mwanzo hadi mwisho wa wakati. PLK 82.2
Baada ya Yesu kuwa amepigiliwa msalabani, uliinuliwa na wanaume kadhaa wenye nguvu na kutumbukizwa kwa nguvu kwenye shimo lake lililotayarishwa huku ukisababisha maumivu makali sana kwa Mwana wa Mungu. Na sasa tukio la kutisha lilionekana. Makuhani, watawala, na waandishi walisahau heshima ya nafasi zao takatifu na kujiunga na umati wenye zogo katika kumdhihaki na kumkejeli Mwana wa Mungu aliyeko kifoni, wakisema, “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.” Luka 23:37. Na wengine wakasemezana miongoni mwao kwa dhihaka, “Aliponya wengine, hawezi kujiponya mwenyewe.” Marko 15:31. Wakuu wa hekalu, askari wenye moyo mgumu, mwivi mwovu juu ya msalaba, na wale waliokuwa waovu na katili miongoni mwa umati ule-wote walijiunga katika kumwonea Kristo. PLK 83.1
Wevi wale waliosulubiwa pamoja na Yesu walipitia mateso yale yale ya kimwili aliyopitia yeye: ila mmoja alishupazwa moyo na kufanywa kukosa matumaini na kuwa fidhul i kwa sababu ya maumi vu. Alitoa mwangwi wa dhihaka za makuhani na shutuma dhidi ya Yesu, akisema, “Je! wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Luka 23:39. Mtu yule mwingine aliyehukumiwa kifo hakuwa mhalifu sugu, aliposikia maneno ya kejeli ya mwenzake katika uhalifu, “alimkemea, akisema, ‘wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa’” Luka 23:40, 41. Ndipo, moyo wake ulipomwelekea Yesu, mnururisho wa kimbingu ulifurika akilini mwake. Katika Yesu, akiwa amechubuliwa, amedhihakiwa, na kuning’inia msalabani alimwona Mkombozi wake, tumaini lake pekee, na alimwomba kwa imani na unyenyekevu: “‘Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.’ Yesu akamwambia, ‘Amin, nakuambia leo, *Kwa kuweka mkato baada ya neno “leo” badala ya baada ya neno “nakuambia” kama ilivyo katika matoleo ya kawaida, maana halisi ya aya hii inakuwa wazi zaidi. Yesu mwenyewe alisema Jumapili iliyofuata asubuhi kwamba alikuwa bado hajapanda kwenda kwa Baba yake. Yohana 20:17. hivi utakuwa pamoja nami peponi.’ ” Luka 23:42, 43. PLK 83.2
Kwa mshangao malaika waliuona upendo wa Yesu usio na kikomo ambaye, huku akiwa anateseka kwa maumivu makali kuliko yote ya akili na mwili, bado aliwafikiria wengine tu na kumtia moyo yule mwenye dhambi aliyetubu kuamini. Huku akimimina uhai wake mautini, alionesha upendo kwa wanadamu waliopotea upendo wenye nguvu kuzidi mauti. Wengi walioshuhudia matukio yale juu ya Kalvari baadaye waligundua kuwa matukio haya yaliwathibitisha katika imani ya Kristo. PLK 84.1
Maadui wa Yesu sasa walisubiri kifo chake kwa shauku kubwa. Walifikiri kuwa kifo chake kingenyamazisha milele uvumi wa uweza wake wa kiungu na maajabu ya miujiza yake. Walijiambia wenyewe kuwa hapo ndipo ambapo wasingeendelea tena kutetemeka kwa ajili ya mvuto wake. Wale askari katili wasio na huruma ambao waliunyosha mwili wa Yesu juu ya msalaba waligawana mavazi yake, wakibishana juu ya vazi moja, lililofumwa bila kuwa na upindo. Hatimaye waliliamua jambo hili kwa kupiga kura juu yake. Maandiko Matakatifu miaka mia kadhaa iliyopita yalikuwa yamekwisha kuelezea tukio hili kwa usahihi kabisa kabla halijatokea: “Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu limenisonga; Wamenizuia mikono na miguu. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.” Zaburi 22:16, 18. PLK 84.2
Somo la Upendo kwa Wazazi-Macho ya Yesu yalizunguka-zunguka katika umati uliokusanyika ili kushuhudia kifo chake, na chini ya msalaba alimwona Yohana akimtegemeza Mariamu, mama wa Kristo. Alikuwa amerejea kwenye tukio hili la kutisha, kwa kushindwa kuendelea kukaa mbali na Mwanawe. Somo la mwisho la Yesu lilihusu upendo wa mtu kwa wazazi. Aliutazama uso wa mama yake uliojaa huzuni, na pia Yohana. Akimwangalia tena mama yake alisema, “Mama, tazama, mwanao” Kisha kwa wanafunzi “Tazama, mama yako” Yohana 19:26, 27. Yohana alielewa vizuri kabisa maneno ya Yesu na jukumu lile takatifu alilokuwa anamkabidhi. Mara moja alimwondoa mama wa Kristo kutoka katika tukio la kutisha la Kalvari. Kuanzia muda ule alimjali kama ambavyo mwana ye yote mwenye kuwajibika angefanya, alimchukua nyumbani kwake. Mfano mkamilifu wa upendo wa Yesu kwa wazazi unang’aa bila kuhafifishwa na ukungu wa miaka mingi. Wakati akistahimili mateso makali kuliko yote, hakumsahau mama yake, bali alifanya kila kilichokuwa muhimu kwa ajili ya mustakabali wake. PLK 84.3
Utume wa maisha ya Yesu ya kidunia sasa ulikaribia kutimizwa. Ulimi wake ulikuwa umekauka, naye alisema, “Naona kiu!” Wakajaza sifongo kwa siki na nyongo na kumpa ili anywe; na alipoionja, akaikataa. Na sasa Bwana wa uzima na utukufu alikuwa anakufa, akiwa fidia kwa ajili ya jamii ya wanadamu. Ilikuwa ni hisia ya dhambi, iliyoleta juu yake hasira ya Baba juu yake kama mbadala wetu, iliyofanya kikombe alichokinywea kuwa kichungu mno, na kuuvunja moyo wa Mwana wa Mungu. PLK 85.1
Uovu wa jamii ya wanadamu uliwekwa juu ya Kristo kama mbadala wetu. Alihesabiwa kuwa mwenye dhambi ili apate kuwakomboa wenye dhambi kutoka katika laana ya sheria. Hatia ya kila mzao wa Adamu katika kila kizazi ilikandamiza katika moyo wake. Ghadhabu ya Mungu na maonesho ya kutisha ya chuki yake kwa sababu ya uovu yaliujaza moyo wa Mwanawe kwa mshangao. Kuondolewa kwa uso wa Baba kutoka kwa Mwokozi katika saa hii ya maumivu makali kuliko yote kuliuchoma moyo wake kwa huzuni ambayo wanadamu kamwe hawawezi kuielewa. Kila mchomo wa maumivu makali ambao Mwana wa Mungu alistahamili katika msalaba, matone ya damu yaliyotiririka kutoka kichwani, mikononi, na katika miguu yake, misukosuko ya maumivu yaliyoutikisa mwili wake, na uchungu usiotamkika ulioijaza roho yake wakati ambapo Baba alikuwa ameuficha uso wake kutoka kwake, husema kwetu na kutuambia, ni kwa sababu ya upendo kwenu ndio maana Mwana wa Mungu anakubali kuruhusu uhalifu wote huu wa kutisha kuwekwa juu yake. Kwa ajili yenu anauteka ufalme wa mauti na kufungua malango ya Paradiso na maisha yasiyo na kifo. Yeye aliyetuliza mawimbi makali kwa neno lake na kutembea juu ya mawimbi yanayofoka povu, aliyefanya mapepo kutetema na maradhi kukimbia kutokana na mguso wake, aliyewafufua wafu na kuwarejeshea uhai na kufungua macho ya vipofu, anajitoa mwenyewe juu ya msalaba kama kafara ya mwisho kwa ajili ya wenye dhambi. Yeye, mbeba dhambi, anastahimili adhabu ya kisheria kwa ajili ya dhambi na kuwa dhambi yenyewe kwa ajili yetu. PLK 85.2
Shetani aliusonga moyo wa Yesu kwa majaribu yake makali kuliko yote. Dhambi, kitu kilichochukiza sana machoni mwake, ililundikwa juu yake hadi akagumia kwa sababu ya uzito wake. Haishangazi kwamba ubinadamu wake ulitikisika katika saa ile ya kuogofya. Malaika walishuhudia kwa mshangao uchungu wa kukatisha tamaa wa Mwana wa Mungu, mkubwa kuliko uchungu ule wa kimwili kiasi kwamba hata hakuweza kuuhisi huu wa kimwili. Majeshi ya mbinguni walifunika nyuso zao kutoka katika tukio hili la kutisha. PLK 86.1
Viumbe vya asili visivyo na uhai vilionesha huruma kwa Mwasisi wao aliyetukanwa na anayekufa. Jua lilikataa kuangalia tukio lile la kutisha. Mionzi yake angavu ilikuwa ikiiangaza nchi hadi kufikia adhuhuri, ambapo ghafla ilionekana kana kwamba ilizimwa. Giza totoro liliuzunguka msalaba na maeneo ya karibu nayo, kama vile kitambaa kizito cheusi cha mazishi. Giza hili lilidumu kwa saa tatu. Ilipotimu saa tisa giza lile nene la kutisha liliinuka kutoka kwa watu, lakini bado lilimfunika Mwokozi kama vile joho. Radi zenye hasira zilionekana kana kwamba zinarushwa kwake pale msalabani. “Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? ” Marko 15:34. PLK 87.1
Imekwisha-Kimya kimya watu walisubiri kuona mwisho wa tukio hili la kutisha. Hatimaye tena jua linawaka, bali msalaba umefunikwa na giza. Ghafla utusitusi unatoweka kutoka katika msalaba, na kwa sauti y a wazi kama tarumbeta inayosikika kana kwamba inatoa mwangwi kwa ulimwengu wote wa vilivyoumbwa, Yesu anasema kwa sauti kuu, “Imekwisha!” “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Luka 23:46. Nuru iliizunguka msalaba na uso wa Mwokozi uling’aa kwa utukufu kama jua. Ndipo alipoinamisha kichwa chake kifuani mwake na kufa. PLK 87.2
Katika muda ule Kristo alipokufa, kulikuwapo na makuhani wakihudumu hekaluni mbele ya pazia lililotenganisha patakatifu na patakatifu pa patakatifu. Ghafla walihisi ardhi ikitetemeka chini yao, na pazia la hekalu, kitambaa imara na kizuri, kilipasuliwa vipande viwili kuanzia juu hadi chini na mkono ule ule ulioandika maneno ya hukumu katika kuta za ikulu ya Belshaza. PLK 87.3
Yesu hakuachia uhai wake hadi pale alipokamilisha kazi aliyokuja kuifanya, na ndipo alipotamka kwa pumzi yake ya mwisho, “Imekwisha!” Malaika walishangilia kwa kusikia maneno yale, kwa kuwa mpango mkuu wa ukombozi ulikuwa ukitekelezwa kwa ushindi. Kulikuwako na furaha mbinguni kwamba sasa, kwa kupitia maisha ya utii, watoto wa Adamu wangeweza hatimaye kuinuliwa hadi katika uwapo wa Mungu. Shetani alikuwa ameshindwa. Alijua kuwa ufalme wake ulipotea. PLK 87.4
Maziko-Yohana alikanganyikiwa asijue la kufanya na mwili wa Bwana wake mpendwa. Alitetemeka kwa hofu ya wazo kuwa angeshughulikiwa na askari wale wenye vurugu na wasio na huruma na kuwekwa katika makaburi yasiyo ya heshima. Alifahamu kuwa asingepata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Wayahudi, na alikuwa na matumaini kidogo sana ya kuweza kupata kitu cho chote kutoka kwa Pilato. Lakini Yusufu na Nikodemo walijitokeza katika dharura hii. Wote wawili walikuwa ni wajumbe wa Sanhedrini na walikuwa na mazoea na Pilato. Wote wawili walikuwa na mali pamoja na umashuhuri. Walikuwa wamedhamiria kuwa mwili wa Yesu ulipaswa kupewa maziko ya heshima. PLK 88.1
Yusufu alikwenda kwa ujasiri kwa Pilato na kumwomba apewe mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko. Pilato aliwapa agizo la kiserikali lililotaka Yusufu apewe mwili wa Yesu. Wakati ambapo mwanafunzi Yohana alikuwa na wasiwasi na kusumbuliwa kuhusu mabaki matakatifu ya Bwana wake mpendwa, Yusufu wa Arimathaya alirudi akiwa na agizo kutoka kwa gavana, na Nikodemu akitarajia matokeo ya mahojiano ya Yusufu na Pilato alikuja akiwa na mchanganyiko wenye gharama kubwa wa manemane na udi wenye uzito karibu ratili mia moja. Mtu mheshimiwa kuliko wote katika Yerusalemu asingeweza kuoneshwa heshima kubwa kuliko hii katika kifo chake. PLK 88.2
Taratibu na kwa kicho, kwa mikono yao wenyewe waliuondoa mwili wa Yesu kutoka katika chombo kile cha mateso, machozi yao ya huruma yakimiminika walipokuwa wakiuangalia mwili wake uliochubuliwa na kukwaruzwa, ambao kwa uangalifu waliuosha na kuutakasa kutokana na matone ya damu. Yusufu alimiliki kaburi jipya, lililochongwa kwenye mwamba, ambalo alikuwa akilitunza kwa ajili yake yeye mwenyewe. Lilikuwa karibu na Kalvari, na sasa alikuwa ameliandaa kaburi hili kwa ajili ya Yesu. Mwili, pamoja na manukato yaliyoletwa na Nikodemu, yalifungwa kwa uangalifu katika sanda ya kitani, na wanafunzi wale watatu wakaubeba mzigo wao kwenda katika kaburi hili jipya, ambalo kamwe hakuna mtu aliwahi kulazwa mle kabla. Pale waliinyosha miguu ile iliyoraruliwa na kuikunja mikono ile iliyochubuliwa juu ya kifua kisichokuwa na mapigo ya moyo. Wanawake wa Galilaya walikuja karibu, kuona kuwa mambo yote yamefanyika yaliyotakiwa kufanywa kwa ajili ya mwili huu usio na uhai wa Mwalimu wao mpendwa. Kisha waliona jiwe kubwa likiviringishwa katika maingilio ya kaburi, na Mwana wa Mungu aliachwa kupumzika. Wanawake wale walikuwa wa mwisho kutoka pale msalabani, na wa mwisho kutoka katika kaburi la Kristo. PLK 88.3
Ijapokuwa viongozi wa Kiyahudi walitimiza mpango wao wa kishetani kwa kumwua Mwana wa Mungu, wasiwasi wao haukuwaacha wala wivu wao juu ya Kristo aliyekufa. Ikiwa imechanganyika na furaha ya ulipizaji kisasi uliotimizwa, walikuwa na hofu isiyozimika kwamba mwili wake uliokufa ambao ulikuwa umelala katika kaburi la Yusufu ungeweza kufufuka na kuwa hai tena. Kwa hiyo “wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, ‘Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.” Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, “Amefufuka katika wafu;” na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.’ ” Mathayo 27:62-64. Pilato kama Vile Wayahudi hakuwa tayari kuruhusu Yesu aamke akiwa na uweza na kuwaadhibu wenye hatia, wale ambao walimwangamiza, kwa hiyo aliweka kikosi cha askari wa Kirumi chini ya amri ya makuhani. PLK 89.1
Wayahudi walitambua faida ya kuwa na walinzi kama wale kuzunguka kaburi la Yesu. Waliweka muhuri juu ya jiwe lililofunika kaburi ili kwamba lisiweze kusogezwa bila ukweli huo kujulikana, wakichukua kila tahadhari kuwa wanafunzi wasije wakadanganya kuhusu mwili wa Yesu. Lakini mipango yao yote ilitumika tu kufanya ushindi wa kufufuka kuwa mkamilifu na kuthibitisha ukweli wake kikamilifu zaidi. PLK 90.1