Shetani na malaika zake walikuwa wakishughulika mno katika ukumbi wa hukumu, wakiharibu hisia na huruma za wanadamu. Angahewa ile ilikuwa nzito na kuchafuliwa kwa sababu ya mvuto wao. Waliwachochea kuhani mkuu pamoja na wazee kumfedhehesha na kumwonea Yesu kwa jinsi iliyo ngumu zaidi kwa asili ya ubinadamu kuweza kustahimili. Shetani alidhani kuwa dhihaka na fujo za jinsi ile zingeamsha malalamiko au manung’uniko fulani kutoka kwa Mwana wa Mungu, au kwamba angeonesha uweza wake wa kiungu na kujing’oa kwa nguvu kutoka katika mshiko wa umati ule, ili kwamba kwa jinsi hii mpango wa wokovu hatimaye ungeshindwa. PLK 74.1
Kukana kwa Petro-Petro alimfuatilia Bwana wake baada ya kusalitiwa kwake. Alikuwa na shauku ya kuona ni kitu gani kingemtokea Yesu. Lakini aliposhitakiwa kuwa mmoja wa wanafunzi wake, hofu kuhusu usalama wake binafsi ilimwongoza kutamka kwamba alikuwa hamjui mtu yule. Wanafunzi wa Yesu walitambulika kwa usafi wa lugha yao, na Petro, ili kuwasadikisha washitaki wake kuwa hakuwa mmoja wa wanafunzi wa Kristo, alilikana shitaka lile mara ya tatu kwa kulaani na kuapa. Yesu ambaye alikuwa mbali kidogo kutoka kwa Petro, Aligeuka akimtazama kwa uso wenye huzuni na wa kukaripia. Ndipo mwanafunzi yule alipokumbuka maneno ambayo Yesu alimwambia kule orofani, na pia dai lake mwenyewe lililokuwa thabiti, “Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.” Mathayo 26:33. Alikuwa amemkana Bwana wake, hata kwa kulaani na kuapa, lakini kutazama kule kwa Yesu kuliyeyusha moyo wa Petro na kumwokoa. Alilia kwa uchungu na kutubu dhambi yake kuu, na aliongoka, na ndipo alipokuwa tayari kuwaimarisha ndugu zake. PLK 74.2
Katika Chumba cha Hukumu-Watu walipiga kelele wakidai damu ya Yesu. Askari walimpiga mijeledi kikatili, wakamvika vazi kuu kuu la kifalme la rangi ya zambarau, na kuzungushia kichwa chake kitakatifu kwa taji ya miiba. Wakaweka fimbo ya utete mkononi mwake na kumwinamia, huku wakimsalimu kwa dhihaka, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” Yohana 19:3. Kisha wakachukua fimbo ile ya utete kutoka mkononi mwake na kumpiga nayo kichwani mwake, na kusababisha miiba kuchoma paji la uso wake, na kufanya damu ichuruzike katika uso wake hadi kwenye kidevu. PLK 75.1
Yesu alijua kuwa malaika walikuwa wakishu-hudia tukio lile la kufedheheshwa kwake. Malaika mwenye nguvu kidogo kuliko wote angeweza kumwokoa Yesu, na kusababisha umati ule wenye kudhihaki kuanguka bila kuwa na uwezo wa kufanya kitu cho chote. Yesu alijua kuwa iwapo angemwomba Baba yake, malaika wangeweza kumfungua mara moja. Lakini ilikuwa ni lazima ateseke kwa vurugu za watu waovu, ili kutekeleza mpango wa wokovu. PLK 75.2
Yesu alisimama akiwa mpole na mnyenyekevu mbele ya umati wenye hasira wakati walipokuwa wakimtendea maonevu maovu kuliko yote. Walimtemea mate usoni- uso ule ambao siku moja inayokuja watatamani kujificha wasiuone, uso ambao utatoa nuru katika mji wa Mungu na utaangaza kwa mwanga mkali kuliko wa jua. Kristo hakuonesha uso wa hasira kwa wakosaji wale. Walifunika kichwa chake kwa vazi kuu kuu, na kufunika macho yake asiweze kuona, na kisha wakampiga usoni na kudai, “Tabiri, ni nani aliyekupiga?” Luka 22:64. PLK 75.3
Baadhi ya wanafunzi wake walipata ujasiri hata wakaweza kuingia pale ambapo Yesu alikuwapo na hivyo kuweza kushuhudia kuhukumiwa kwake. Walitarajia kuwa angelionesha uweza wake wa kiungu, ajiokoe kutoka katika mikono ya maadui zake, na kuwaadhibu kwa ajili ya ukatili wao juu yake. Matumaini yao yalipanda na kushuka kadiri matukio tofauti tofauti yalivyoj ifunua. Wakati mwingine walikuwa na mashaka, wakidhani kuwa huenda walikuwa wamedanganyika. Lakini sauti ile ambayo waliisikia katika ule mlima wa kubadilika sura, na utukufu waliouona pale uliimarisha imani yao kuwa alikuwa ni Mwana wa Mungu. Walivuta akilini mwao matukio mbalimbali ambayo walikuwa wameyashuhudia, miujiza waliyomwona Yesu akiitenda katika kuwaponya wagonjwa, kufungua macho ya vipofu, kuzibua masikio ya viziwi, kukemea na kufukuza mapepo, kuwahuisha wafu, na hata kutuliza upepo na bahari. PLK 76.1
Wasingeweza kusadiki kuwa angeweza kufa. Walitumaini kuwa bado angeweza kuinuka kwa uweza, na kwa sauti ya kuamrisha kuutawanya umati huu wenye kiu ya damu, kama vile alivyoingia hekaluni na kuwafukuza wabadilishaji wa fedha ambao walikuwa wanafanya nyumba ya Mungu kuwa mahali pa biashara, walipokimbia kutoka kwake kana kwamba walikuwa wanafukuzwa na jeshi la askari wenye silaha. Wanafunzi walitumaini kuwa Yesu angedhihirisha uweza wake na kuwathibitishia wote kuwa yeye ndiye alikuwa Mfalme wa Israeli. PLK 76.2
Ungamo la Yuda-Yuda alijazwa na majuto ya uchungu na aibu kwa tendo lake la kukosa uaminifu kwa kumsaliti Yesu. Na pale aliposhuhudia maonevu ambayo Mwokozi aliyavumilia, alijawa na huzuni. Alimpenda Yesu, lakini alipenda fedha zaidi. Hakudhania kamwe kuwa Yesu mwenyewe angeweza kuruhusu achukuliwe na watu wale aliowaongoza. Alitarajia kuwa angetenda muujiza na kujiokoa kutoka kwao. Lakini alipoona watu wale wenye hasira katika jumba la hukumu, wakiwa na kiu ya damu, alihisi hatia yake kwa kina. Wakati ambapo watu wengi walikuwa wakimshitaki na kumlaumu Yesu kwa ukali, Yuda alikimbia kutoka katika umati huu, akikiri kuwa alikuwa ametenda dhambi kwa kuisaliti damu isiyo na hatia. Aliwarudishia makuhani ile fedha waliyomlipa, na kuwaomba wamwachie Yesu, akitangaza kuwa hakuwa na hatia kabisa. PLK 76.3
Kwa kitambo kidogo, hasira na ghasia ziliwafanya makuhani kunyamaza kimya. Hawakutaka watu wajue kuwa walikuwa wamemwajiri mmoja wa wafuasi bayana wa Yesu ili kumsaliti mikononi mwao. Lakini ungamo la Yuda pamoja na mwonekano wake dhaifu na wenye hatia uliwafunua makuhani mbele ya watu, ukionesha kuwa ilikuwa ni chuki ndio ilisababisha wamkamate Yesu. Wakati Yuda alipotangaza wazi kwa nguvu kwamba Yesu hakuwa na hatia, makuhani walijibu, “Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.” Mathayo 27:4. Walikuwa na Yesu chini ya mamlaka yao na walidhamiria kutekeleza mipango yao. Yuda akizidiwa na huzuni, alizitupa fedha zile ambazo kwa sasa alizidharau miguuni pa wale waliokuwa wamemwajiri, na, kwa uchungu na hofu, aliondoka na kwenda kujinyonga. PLK 77.1
Yesu alikuwa na wafuasi wengi sana katika kusanyiko lile, na kule kukaa kwake kimya bila kujibu lo lote kwa maswali mengi aliyoulizwa kuliwashangaza watu wale. Katika dhihaka na vurugu zote za watu wale, umbile lake halikuonesha, mkunjo wa uso au hali yo yote ya kufadhaika. Alikuwa ni mwenye kuheshimika na mtulivu. Watazamaji walimwangalia kwa mshangao. Walilinganisha umbile lake kamilifu na mwenendo wake thabiti wa heshima na mwonekano wa wale waliokaa katika hukumu dhidi yake, na wakasemezana kuwa alionekana kufaa zaidi kuwa mfalme kuliko ye yote miongoni mwa watawala wale. Hakuwa na ishara yo yote ya kuwa mhalifu. Macho yake yalikuwa ya upole, maangavu na yasiyoonesha hofu yo yote, uso wake ulikuwa mpana na ulioinuliwa juu. Kila sehemu ya uso kwa nguvu ilidhihirishwa kwa wema na kanuni iliyo bora. Ustahamilivu wake na kujizuia ulikuwa tofauti sana na wa wanadamu wa kawaida kiasi kwamba wengi walitetemeka. Hata Herode na Pilato walisumbuliwa sana na mwonekano wake bora wa kiungu. PLK 77.2
Yesu mbele ya Pilato-Tangu mwanzo, Pilato aliridhika kuwa Yesu hakuwa mwanadamu wa kawaida. Alisadiki kuwa alikuwa ni wa tabia bora na kutokuwa na hatia kabisa juu ya mashitaka yote yaliyokuwa dhidi yake. Malaika waliokuwa wakishuhudia tukio lile walitambua kusadiki kwa mtawala huyu wa Kirumi, na ili kumwokoa kwa tendo la kutisha la kumkabidhi Yesu ili apate kusulubiwa, malaika alitumwa kwa mke wa Pilato, ambaye alimpa taarifa kupitia katika ndoto kuwa alikuwa ni Mwana wa Mungu ambaye mume wake alikuwa akiendesha kesi yake, na kwamba alikuwa ni mtesekaji asiye na hatia. Mara moja [mkewe Pilato] alipeleka habari kwa Pilato, ikieleza kuwa alisumbuliwa sana katika ndoto kwa ajili ya Yesu na kumwonya asimtendee neno lo lote huyo Mtakatifu. Mjumbe aliyetumwa akijisukuma kwa haraka katika umati, aliiweka barua mikononi mwa Pilato. Alipoisoma, alitetemeka na kubadilika rangi, na kuamua mara moja kuwa hatafanya cho chote cha kumhukumu Yesu kifo. Iwapo Wayahudi walitaka damu ya Yesu, asingeweka uwezo wake katika hilo, bali angeshughulika apate kumwokoa. PLK 78.1
Atumwa kwa Herode-Pilato aliposikia kuwa Herode alikuwa Yerusalemu, alifarijika sana, kwa sababu alitumaini kujiondoa katika wajibu wote wa mashitaka na hukumu ya kifo cha Yesu. Mara moja alimpeleka yeye, pamoja na washitaki wake, kwa Herode. Muuaji wa Yohana Mbatizaji alikuwa ameacha katika dhamiri yake doa ambalo asingeweza kujisafisha mwenyewe. AliposikiahabarizaYesunamatendomakuuyaliyotendwa naye, aliogopa na kutetemeka, akiamini kuwa alikuwa ni Yohana Mbatizaji aliyefufuka kutoka kwa wafu. Pilato alipompeleka Yesu kwake, Herode alilichukulia tendo hili kama ishara ya kukubaliwa kwa uwezo, mamlaka, na hukumu zake. Hili likuwa na matokeo ya kuleta urafiki baina ya watawala hawa wawili, ambao kabla ya hapa walikuwa ni maadui. Herode alifurahishwa kwa kumwona Yesu, akitegemea kwamba angetenda miujiza mikuu kwa ajili ya kuridhishwa kwake. Lakini haikuwa kazi ya Yesu kukidhi shauku au kutafuta usalama wake binafsi. Angeweza kutumia uweza wake wa kiungu na wa kimiujiza katika wokovu wa wengine, na wala si kwa ajili yake mwenyewe. PLK 78.2
Yesu hakujibu cho chote kwa maswali mengi sana aliyoulizwa na Herode, na wala hakuwajibu maadui zake. Herode alikasirika kwa vile Yesu hakuonekana kuyagopa mamlaka yake, na kwa kutumia askari zake alimkejeli, kumdhihaki, na kumwonea Mwana wa Mungu. Lakini bado alishangazwa na mwonekano bora ulio kama mfano wa Mungu, Yesu aliouonesha wakati alipofedheheshwa kwa kuonewa, na huku akiogopa kumhukumu kifo, alimrudisha tena kwa Pilato. PLK 79.1
Shetani na malaika zake walikuwa wanamjaribu Pilato na kujaribu kumwongoza kufikia uangamivu wake mwenyewe. Walimpendekezea kuwa iwapo asingehusika katika kumhukumu Yesu kifo, wengine wangefanya hi vyo. Watu walikuwa na kiu ya damu yake na iwapo Pilato asingemtoa ili apate kusulubiwa, yeye Pilato angepoteza uwezo na heshima yake ya kidunia na angeshutumiwa kuwa muumini wa mtu laghai. Kwa sababu ya hofu ya kupoteza uwezo na mamlaka yake, Pilato aliridhia juu ya juu ya washitaki wake, umati ule walilipokea jambo hili, wakisema kwa sauti, “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu” (Mathayo 27:25), hata hivyo Pilato hakuwa amejitoa katika kuwajibika na hili; alikuwa na hatia ya damu ya Kristo. Kwa ajili ya faida yake binafsi, upendo wake wa kuheshimiwa na watu wakuu wa dunia, alimtoa mtu asiye na hatia ili apate kufa. Iwapo Pilato angefuata msimamo wake mwenyewe, asingejihusisha na kitu cho chote cha kumhukumu Yesu kifo. PLK 79.2
Mwonekano pamoja na maneno ya Yesu wakati wa kuendeshwa kwa kesi yake uliacha alama kubwa sana katika akili za watu waliokuwapo pale. Matokeo ya mvuto huu yalikuwa wazi baada ya kufufuka kwake. Miongoni mwa wale walioongezeka katika kanisa wakati ule, walikuwapo wengi ambao imani zao zilianzia wakati wa hukumu ya Yesu. PLK 80.1
Hasira ya Shetani ilikuwa kubwa alipoona kuwa ukatili wote aliowaongoza Wayahudi kumtendea Yesu haukusababisha kutoka kwake lalamiko hata lililo dogo kabisa. Ingawa alikuwa ameichukua asili ya ubinadamu juu yake, alihimiliwa na ustahamilivu kama wa Mungu. PLK 80.2