Mbingu yote ilikuwa ikisubiri saa ya ushindi ambayo Yesu angepanda kwenda kwa Baba yake. Malaika walikuja ili kumpokea Mfalme wa utukufu na kumsindikiza kwa shangwe kwenda mbinguni. Baada ya Yesu kuwabariki wanafunzi wake, alijitenga kutoka kwao na akainuliwa juu. Na alipoanza safari ya kwenda juu, mateka wengi waliofufuliwa wakati wa kufufuka kwake walimfuata. Kusanyiko kuu la malaika wa mbinguni walisubiri ujio wake. PLK 98.1
Kisha jeshi lote la mbinguni walimzunguka Amiri jeshi wao mkuu na kuinama mbele yake kwa kicho kikuu mno, wakiweka taji zao zinazometameta miguuni pake. Na kisha wakashika vinubi vyao vya dhahabu, na kwa sauti tamu zilizopangika vizuri wakaijaza mbingu yote na muziki mtamu na nyimbo za Mwana-kondoo aliyechinjwa, ambaye yu hai tena katika ukuu na utukufu. PLK 98.2
Ahadi ya Kurudi-Wanafunzi walipokuwa wakita- zama juu kuelekea mbinguni kwa huzuni ili wapate kumwona kwa mara ya mwisho Mwokozi wao anayepaa, malaika wawili wakiwa katika mavazi meupe walisimama kando yao na kuwaambia, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” Matendo 1:11. Wanafunzi walinena juu ya matendo yake ya ajabu na matukio ya kushangaza na yenye utukufu yaliyotendeka katika kipindi cha muda mfupi. PLK 98.3
Hasira ya Shetani-Shetani tena alishauriana na malaika zake, na kwa chuki kali dhidi ya serikali ya Mungu aliwaambia kuwa wakati ambapo akingali ana uwezo na mamlaka yake duniani, juhudi zao lazima zizidishwe mara kumi zaidi dhidi ya wafuasi wa Yesu. Walikuwa hawajashinda katika shambulio lo lote dhidi ya Kristo lakini lazima wawashinde wafuasi wake, ikiwezekana. Katika kila kizazi ni lazima wajitahidi kuwanasa wale ambao wanamwamini Yesu. Ndipo malaika wa Shetani wakaenda nje kama simba aungurumaye, wakitafuta kuwaangamiza wafuasi wa Yesu. PLK 99.1