Sura hii imejengwa katika Matendo ya Mitume 2
Yesu alipofungua ufahamu wa wanafunzi kuhusu unabii uliomhusu yeye mwenyewe, aliwahakikishia kuwa mamlaka yote mbinguni na duniani alipewa yeye, na aliwaambia waende kuihubiri injili kwa kila kiumbe. Ghafla wakikumbuka tumaini lao la zamani kwamba Yesu angechukua nafasi yake katika kiti cha enzi cha Daudi katika Yerusalemu, wanafunzi walimwuliza, “Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” Matendo 1:6. Mwokozi aliwaacha bila uhakika kuhusu jambo hili kwa kujibu kuwa haikuwa kazi yao kujua, “nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.” Matendo 1:7. PLK 100.1
Wanafunzi wakaanza kutumaini kuwa kushuka kwa jinsi ya ajabu kwa Roho Mtakatifu kungewashawishi Wayahudi kumpokea Yesu. Mwokozi alikataa kuendelea kufafanua zaidi, kwa kuwa alifahamu kuwa wakati Roho Mtakatifu atakapokuja juu yao katika nguvu yote, akili zao zingetiwa nuru. Wangefahamu kikamilifu kazi iliyoko mbele yao na kuiendeleza kuanzia pale alipoiacha. PLK 100.2
Wanafunzi walikusanyika katika chumba cha ghorofani, wakijiunga katika maombi pamoja na wanawake waumini, pamoja na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake. Ndugu hawa, ambao walikuwa hawaamini, sasa walikuwa wamethibitika kikamilifu katika imani yao kutokana na matukio yaliyoambatana na kusulubiwa na ufufuko na kupaa kwa Bwana. Idadi iliyokusanyika ilikuwa ni kama watu mia moja na ishirini. PLK 100.3
Kushuka kwa Roho Mtakatifu -“Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Roho Mtakatifu, akiwa katika umbile la ndimi za moto zilizogawanyika kwenye ncha zake na kutua juu ya kundi lililokusanyika, alikuwa ni ishara ya karama kutolewa kwao ya kuzungumza lugha kadhaa mbalimbali kwa ufasaha ambao hawakuwa nao kabla ya hapo. Na kutokea kwa moto kulimaanisha ari kubwa ambayo wangefanyia kazi na uwezo ambao ungeandamana na maneno yao. PLK 101.1
Katika kutiwa nuru huku kutoka mbinguni, Maandiko ambayo Yesu alikuwa amefafanua kwao yalijitokeza katika akili zao kwa mng’ao wa wazi na uzuri wa ukweli dhahiri na wenye nguvu. Pazia ambalo lilikuwa linawazuia wasione kile ambacho Kristo alikikomesha sasa lilikuwa limeondolewa, na walifahamu kusudi la utume wa Kristo na asili ya ufalme wake kwa uwazi mkamilifu. PLK 101.2
Katika Nguvu ya Pentekoste-Wayahudi walikuwa wametawanyika karibu katika kila taifa, na walikuwa wakiongea lugha mbalimbali. Walikuwa wamesafiri kutoka mbali kuja Yerusalemu na walikuwa wanakaa pale kwa kitambo kwa ajili ya siku kuu za kidini zilizokuwa zinaendelea wakati ule ili kutimiza masharti yake. Watu waliokuja kuabudu waliokusanyika pale walikuwa ni wa kila lugha iliyofahamika. Utofauti huu wa lugha mbalimbali ulikuwa ni kikwazo kikuu kwa kazi ya watumishi wa Mungu katika kueneza mafundisho ya Kristo kokote duniani. Lakini Mungu alikidhi hitaji la mitume kwa namna ya kimiujiza, na kwa watu, hii ilithibitisha kikamilifu mno ushuhuda wa mashahidi hawa wa Kristo. Roho Mtakatifu aliwatendea kile ambacho wasingeweza kukikamilisha wenyewe katika maisha yao yote. Sasa wangeweza kutawanya ukweli wa injili hata sehemu za mbali, huku wakiongea kwa usahihi lugha za wale ambao waliwahudumia. Karama hii ya kimuujiza ilikuwa ni ushahidi wa juu kabisa ambao wangeliweza kuutolea ulimwengu kwamba utume wao ulikuwa na kibali cha Mbingu. PLK 101.3
“Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa ku wa ki la mmoj a ali wasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?” PLK 102.1
Makuhani na watawala walikasirishwa mno na tukio hili la kustajaabisha, ambalo liliripotiwa katika Yerusalemu nzima na jirani zake. Lakini hawakuthubutu kuchukua hatua yo yote katika kutimiza makusudi yao maovu kwa hofu ya kujianika wenyewe kwa chuki ya watu. Walikuwa wamemwua Bwana, lakini sasa hapa walikuwapo watumishi wake, watu wasio na elimu kutoka Galilaya, wakieleza utimizwaji wa kushangaza wa unabii na kufundisha fundisho juu ya Yesu kwa lugha zote zilizozungumzwa wakati ule. Walizungumza kwa uwezo kuhusu matendo ya ajabu ya Mwokozi na kufungua kwa wasikilizaji wao mpango wa wokovu katika rehema na kafara ya Mwana wa Mungu. Maneno yao yaliwasadikisha na kuwaongoa maelfu waliosikiliza. Mafundisho ya mapokeo na ushirikina ambayo yalifundishwa na makuhani yalifagiliwa mbali kutoka katika akili zao, na walikubali mafundisho safi ya Neno la Mungu. PLK 102.2
Hubiri la Petro-Petro aliwaonesha kuwa kile walichokuwa wanakishuhudia ni utimizwaji wa moja kwa moja wa unabii wa Yoeli, ambaye alitabiri kuwa nguvu kama hii ingekuja juu ya watu wa Mungu ili kuwaandaa kwa ajili ya kazi maalumu. PLK 103.1
Petro alifuatilia uzao wa Kristo katika msitari wa moja kwa moja hadi katika nyumba iliyoheshimiwa ya Daudi. Hakutumia hata moja ya mafundisho ya Yesu ili kuthibitisha nafasi yake halisi, kwa sababu alifahamu kuwa chuki zao zilikuwa kubwa mno kiasi kwamba isingeleta matokeo yo yote. Lakini aliwaelekeza kwa Daudi, ambaye Wayahudi walimchukulia kuwa ni mzee mheshimiwa sana katika taifa lao. Petro alisema: “Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu.” PLK 103.2
Hapa Petro anaonesha kuwa Daudi asingekuwa anaongea kuhusu yeye mwenyewe, bali kwa hakika kuhusu Yesu Kristo. Daudi alikufa kifo cha kawaida kama watu wengine. Kaburi lake, pamoja na vumbi lenye kuheshimiwa lililokuwa limeibeba, lilikuwa limetunzwa kwa uangalifu mkuu hadi wakati ule. Kama mfalme wa Israeli na pia kama nabii, Daudi aliheshimiwa kwa namna ya pekee na Mungu. Katika njozi ya kinabii Mungu alimwonesha maisha ya baadaye na huduma ya Kristo. Aliona kukataliwa kwake, kuhukumiwa kwake, kusulubiwa, kuzikwa, kufufuka, na kupaa kwake. PLK 103.3
Daudi alishuhudia kuwa roho ya Kristo isingeachwa kaburini, wala mwili wake kuona uharibifu. Petro alionesha kuwa Yesu wa Nazareti alitimiza unabii huu. Mungu kwa hakika alimfufua kutoka kaburini kabla mwili wake haujaoza. Sasa alikuwa ndiye aliyekwezwa katika mbingu za juu kabisa. PLK 103.4
Katika tukio lile la kukumbukwa, idadi kubwa ambao hadi wakati ule walichukia wazo la mtu wa kawaida kama Yesu kuweza kuwa Mwana wa Mungu sasa walishawishika kabisa na ukweli na walimkubali kama Mwokozi. Watu elfu tatu waliongezeka katika kanisa. Mitume waliongea kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, na hakuna hata mtu mmoja aliweza kuhoji maneno yao. Ujumbe wao ulithibitishwa kwa miujiza yenye nguvu, waliyoitenda kwa kumwagwa kwa Roho wa Mungu. Wapafunzi wenyewe walishangazwa kwa matokeo ya udhihirisho huu wa uweza wa Mungu na mavuno makubwa na ya haraka ya waumini. Watu wote walijazwa na mshangao. Wale ambao hawakuachia chuki na imani zao kali waliogopa mno kiasi kwamba hawakudiriki kuizuia kazi hii yenye nguvu, iwe ni kwa sauti au kwa vurugu, na upinzani wao ulikoma kwa kipindi hiki. PLK 104.1
Hoja za mitume peke yake, wazi na zenye kusha- wishi kama zilivyokuwa zisingeweza kuondoa chuki za Wayahudi ambao walikuwa wamehimili ushahidi mwingi kiasi kile. Bali Roho Mtakatifu alisindikiza hoja zile mioyoni mwao kwa nguvu za kimbingu. Zilikuwa kama mishale yenye ncha kali ya Mwenyezi, zikiwasadikisha kuhusu hatia yao ya kutisha katika kumkataa na kumsulubisha Bwana wa utukufu. “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, ‘Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.’ ” PLK 104.2
Petro aliwasihi watu waliosadikishwa kuwa ukweli kwamba walimkataa Kristo ni kwa sababu walikuwa wamedanganywa na makuhani na viongozi. Iwapo wangeendelea kuwategemea kwa ajili ya ushauri na kusubiri viongozi wale kumkubali Kristo ati ndipo nao wadiriki kufanya hivyo, kamwe wasingeweza kumpokea. Ingawa watu wale wenye nguvu walikiri kuwa watauwa, walikuwa ni watu wenye tamaa na bidii ya kutafuta utajiri na utukufu wa kidunia. Kamwe wasingekuja kwa Kristo ili wapate nuru. Yesu alitabiri adhabu ya kutisha ambayo ingekuja juu ya watu kwa sababu ya ukaidi wao wa kutokuamini, bila kujali ushahidi wenye nguvu waliopewa kwamba Yesu alikuwa ni Mwana wa Mungu. PLK 104.3
Tangu wakati huu na kuendelea, lugha ya wanafunzi ilikuwa safi, sahili, na sahihi kwa maneno na matamshi, iwe wanaongea lugha ya mama yao au lugha ya kigeni. Watu hawa wa kawaida, ambao kamwe hawakuwa wamesoma katika shule yo yote ya manabii, waliwasilisha ukweli wa juu na safi kiasi cha kuwashangaza waliosikia. Wasingeweza kwenda kwa nafsi zao sehemu zote za dunia, bali walikuwapo watu katika sikukuu hizi kutoka katika kila sehemu ya dunia, nao walibeba kweli walizozipata kwenda nazo katika makazi yao mbalimbali na kuzieneza miongoni mwa watu wao, na kuwaleta waongofu kwa Kristo. PLK 105.1
Fundisho kwa Ajili ya Siku Zetu-Tunao ushuhuda huu kuhusu uanzishaji wa kanisa la Kikristo si tu kama sehemu muhimu ya historia takatifu bali pia kama fundisho. Wote wanaolikiri jina la Kristo wanapaswa kusubiri, kukesha, na kuomba kwa moyo mmoja. Tunapaswa kuweka kando tofauti zote na kuruhusu umoja na upendo wa dhati kati yetu kuwa juu ya vyote. Ndipo maombi yetu yanapoweza kwenda juu kwa pamoja kwa Baba yetu wa mbinguni kwa imani thabiti isiyochoka. Ndipo tunaweza kusubiri kwa ajili ya utimizwaji wa ahadi kwa saburi na matumaini. PLK 105.2
Jibu linaweza kuja kwa kasi ya ghafla na nguvu kubwa mno, au inaweza kucheleweshwa kwa siku au majuma kadhaa, na imani yetu kujaribiwa. Lakini Mungu anajua jinsi gani na lini atajibu maombi yetu. Ni sehemu yetu ya kazi kujiunganisha wenyewe na njia ya Mungu. Mungu anawajibika kwa sehemu yake ya kazi. Yeye aliyeahidi ni mwaminifu. Jambo kubwa na la muhimu kwa upande wetu ni kuwa wenye moyo na akili moja tukiweka kando husuda na hila, na kama watu wanyenyekevu wa maombi, kukesha na kungoja. Yesu, Mwakilishi wetu na aliye Kichwa chetu yuko tayari kutenda kwa ajili yetu kile alichokitenda kwa wale waliokuwa wakiomba na kukesha katika siku ya Pentekoste. PLK 105.3