Wakati Yesu alipofunua kwa wanafunzi wake hatima ya Yerusalemu na matukio ya kuja kwake mara ya pili, pia alitabiri uzoefu wa watu wake tangu wakati ambapo angechukuliwa kutoka kwao hadi kurudi kwake katika uweza na utukufu kwa ajili ya ukombozi wao. Kutoka katika Mlima wa Mizeituni, Mwokozi aliona dhoruba zilizokuwa karibu kuanguka juu ya kanisa ambalo mitume wangelianzisha, na, akiangalia kwa kina zaidi katika siku za usoni, jicho lake liliona tufani kali, yenye nguvu ya uharibifu ambayo ilikuwa iwapige waftiasi wake katika zama zilizokuwa zinakuja za giza na mateso. Katika kauli chache fupi, zilizo muhimu kwa namna ya kutisha, alitabiri taabu ambazo kwazo watawala wa dunia hii wangelitesa kanisa la Mungu. Wafuasi wa Kristo ni lazima waipite njia ile ile ya fedheha, shutuma, na mateso ambayo Bwana wao aliipita. Chuki iliyolipuka juu ya Mkombozi wa dunia ingedhihirishwa dhidi ya wote ambao wangeliamini jina lake. PLK 107.1
Historia ya kanisa la awali ilithibitisha usahihi wa maneno ya Mwokozi. Nguvu za dunia na kuzimu zilijipanga kupambana na Kristo kupitia kwa wafuasi wake. Upagani uliona mbele kuwa iwapo injili ingefaulu, hekalu zake na madhabahu yangefagiliwa mbali. Hivyo ulipanga majeshi yake ili kuuangamiza Ukristo. Mioto ya mateso iliwashwa. Wakristo walinyang’anywa mali zao na kufukuzwa kutoka katika makazi yao. Walistahimili “mashindano makubwa ya maumivu.” “Walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; ” Waebrania 10:32; 11:36. Idadi yao kubwa walipiga muhuri ushuhuda wao kwa damu yao. Watu wakuu pamoja na watumwa, matajiri na maskini, wasomi na wasio na elimu, waliuawa kwa jinsi hiyo bila huruma. PLK 107.2
Juhudi ya Shetani ya kutaka kuliangamiza kanisa la Kristo kwa vurugu zilikuwa ni za bure. Pambano kuu ambalo ndani yake wanafunzi wa Yesu walitoa maisha yao halikukoma pale hawa wabeba bendera waaminifu walipoanguka katika vituo vyao vya ulinzi. Kwa kuangamizwa walishinda. Watendakazi wa Mungu waliuawa, lakini kazi yake ilisonga mbele kwa uthabiti. Injili iliendelea kuenea, na idadi ya waongofu wake iliendelea kuongezeka. Ilipenya katika maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki, hata kwa majeshi ya Kirumi. Mkristo mmoja alisema, akiwashawishi watawala wapagani waliokuwa wakiendelea na mateso: Alisema, “Mnaweza kutuua, kututesa, kutuhukumu kifo. ... Udhalimu wenu ni uthibitisho kuwa sisi hatuna hatia. ... Wala ukatili wenu ... hauwasaidii.” Huu ulikuwa ni mwito wenye nguvu wa kuwaleta wengine katika imani kwa Kristo. “Kwa kadiri mnavyotufyeka, ndivyo idadi yetu inavyoongezeka; damu ya Kristo ni mbegu.” PLK 108.1
Maelfu walifungwa jela na kuuawa, lakini wengine walijitokeza kuchukua nafasi zao. Na wale waliouawa kwa ajili ya imani zao walihifadhiwa salama kwa Kristo. Walipigana vita vilivyo vizuri na wanapaswa kupokea taji ya utukufu pale Kristo atakapokuja. Mateso waliyoyavumilia yaliwasogeza Wakristo kila mtu karibu na mwenzake na karibu na mkombozi wao. Kielelezo cha maisha yao na ushuhuda wa vifo vyao vilikuwa ni ushuhuda wa ukweli daima; na, pale ambapo hapakutegemewa kabisa wafuasi wa Shetani walikuwa wakiacha utumishi wake na kujiunga chini ya bendera ya Kristo. PLK 108.2
Maridhiano na Upagani-Kwa hiyo Shetani aliweka mipango yake ili kupambana kwa mafanikio zaidi dhidi ya serikali ya Mungu, kwa kuinua bendera yake ndani ya kanisa la Kikristo. Iwapo wafuasi wa Kristo wangeweza kudanganywa na kufanywa wamchukize Mungu, nguvu zao, ustahamilivu, na uthabiti vingeshindwa, na wangekuwa windo rahisi kwa Shetani. PLK 108.3
Adui mkuu sasa alijaribu kupata kwa njia ya udanganyifu kile ambacho alishindwa kukipata kwa matumizi ya nguvu. Mateso yalikoma, na katika nafasi yake aliweka vivutio vya hatari zaidi vya ustawi upitao heshima ya kidunia. Waabudu sanamu waliongozwa kupokea sehemu ya imani ya Kikristo, huku wakikataa kweli zingine za lazima. Walikiri kumpokea Yesu kama Mwana wa Mungu na kuamini kuhusu kifo chake na ufufuo, lakini hawakusadikishwa kuhusu dhambi na hawakujisikia kuhitaji toba au badiliko la moyo. Kwa maridhiano fulani kwa upande wao, walipendekeza kwamba Wakristo pia walipaswa kufanya maridhiano, ili kwamba wote waweze kuungana katika jukwaa la imani kwa Kristo. PLK 109.1
Sasa kanisa lilikuwa katika hatari ya kuogofya. Jela, mateso, moto, na upanga vilikuwa ni mibaraka ukilinganisha na vitu hivi. Baadhi ya Wakristo walisimama imara, wakitangaza kuwa wasingeweza kufanya maridhiano. Wengine waliwaza kuwa iwapo wangekubali au kurekebisha baadhi ya vipengele vya imani yao na kuungana na wale waliopokea sehemu ya Ukristo, ingeweza kuwa njia ya uongofu wao kamili. Huu ulikuwa ni wakati wa uchungu mkuu kwa wafuasi waaminifu wa Kristo. Chini ya kificho cha Ukristo wa kujifanya, Shetani kwa werevu alikuwa akitumia mbinu za kuingia yeye mwenyewe katika kanisa, ili kupotosha imani zao na kugeuza akili zao kutoka katika neno la ukweli. PLK 109.2
Hatimaye sehemu kubwa ya Wakristo walishusha viwango na kutengeneza muungano baina ya Ukristo na upagani. Ingawa waabudu sanamu walidai kuwa wameongoka, na walijiunga na kanisa, bado waling’ang’ania ibada zao za sanamu, walichofanya ni kubadilisha sanamu zao za ibada kuwa sanamu za Yesu, hata za Mariamu na za watakatifii. Chachu mbaya ya ibada ya sanamu iliyoingizwa kwa njia hii katika kanisa, iliendeleza kazi yake ya uharibufu. Mafundisho ya imani yasiyoridhisha, kaida za kishirikina, na taratibu za ibada za sanamu zilijumuishwa katika imani na ibada za kanisa. Wafuasi wa Kristo walipojiunga na waabudu sanamu, dini ya Ukristo iliharibiwa na kanisa likapoteza usafi na uwezo wake. Hata hivyo, kulikuwako na baadhi, ambao hawakupotoshwa na madanganyo haya. Bado walidumisha uaminifu wao kwa Muasisi wa ukweli na kumwabudu Mungu peke yake. PLK 109.3
Siku zote kumekuwako na makundi mawili miongoni mwa wale wanaokiri kuwa wafuasi wa Kristo. Wakati ambapo watu walioko katika kundi moja wanajifunza maisha ya Mwokozi na kujitahidi kurekebisha makosa yao na kutafuta kufanana na Kielelezo chake, wale walioko katika kundi lingine wanakataa kweli za wazi, na za kivitendo zinazoanika wazi makosa yao. Hata katika wakati wake uliokuwa bora kuliko nyakati zote, kanisa halikuwa limeundwa kabisa na watu ambao ni wakweli, wasafi, na waaminifu peke yao. Mwokozi wetu alifundisha kwamba wale ambao kwa makusudi wanajiingiza katika dhambi wasipokelewe kanisani. Lakini bado aliwaunganisha kwake watu ambao walikuwa na tabia zenye dosari, na aliwapa manufaa ya mafundisho na Kielelezo chake, ili kuwapa fursa ya kuona na kurekebisha makosa yao. PLK 110.1
Lakini hakuna muungano baina ya Mfalme wa nuru na mfalme wa giza, na haiwezekani kuwapo muungano kati ya wafuasi wao. Pale Wakristo walipokubali kuungana na wale ambao waliongoka nusu nusu tu kutoka katika upagani, walianza kusafiri katika njia iliyoelekea mbali zaidi na ukweli. Shetani alishangilia kuwa alikuwa amefaulu katika kuwadanganya wengi miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Ndipo alipoleta uwezo wake juu yao ili kuwaathiri zaidi, akiwachochea kuwatesa wale waliobaki kuwa waaminifu kwa Mungu. Hakuna mtu anayeweza kufahamu jinsi ya kuipinga imani ya kweli ya Kikristo zaidi ya wale ambao hapo mwanzo walikuwa watetezi wake. Hawa Wakristo walioikana imani, wakijiunga na wenzi wao waliokuwa nusu wapagani, walielekeza vita vyao dhidi ya vipengele muhimu kuliko vyote vya mafundisho makuu ya Kristo. PLK 110.2
Wale waliotaka kuwa waaminifu waligundua kuwa ilihitaji mapambano makali sana ili kuweza kusimama thabiti dhidi ya udanganyifu na machukizo yaliyofichwa katika mavazi ya kikasisi na kuingizwa kanisani. Biblia haikukubaliwa tena kama kiwango cha imani. Fundisho la uhuru wa kidini liliitwa uzushi, na waliolishikilia walichukiwa na kushutumiwa. PLK 111.1
Utengano wa Lazima-Baada ya mapambano makali na yaliyodumu kwa muda mrefu wale waaminifu wachache waliamua kuvunja uhusiano wote na kanisa lililokuwa limeasi iwapo bado lingekataa kujiondoa katika ubaya wote na ibada ya sanamu. Waliona kuwa utengano ulikuwa ni wa lazima kabisa ili waweze kulitii Neno la Mungu. Hawakuthubutu kuvumilia makosa yaliyokuwa ni ya kufisha roho zao wenyewe na hivyo kuweka mfano ambao ungehatarisha imani ya watoto wao na watoto wa watoto wao. Ili kupata amani na umoja, walikuwa tayari kufanya mapatano yo yote yanayokubaliana na kuwa wakweli kwa Mungu, bali walijisikia kuwa hata amani ingekuwa ni ghali mno iwapo ingemaanisha kutoa kafara ya kanuni. Iwapo amani ingekuja kwa kulegeza msimamo wa ukweli na haki, basi acha pawepo na tofauti, na hata vita. Lingekuwa jambo la manufaa kwa kanisa na dunia iwapo kanuni zile zilizowashawishi wale waumini thabiti zingeamshwa katika mioyo ya watu waliokiri kuwa wa Mungu. PLK 111.2
Mtume Paulo anatangaza kuwa “wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.” 2Timotheo 3:12. Kwa nini basi kwa sehemu kubwa inaonekana kuwa mateso yamelala? Sababu pekee ni kwamba kanisa limepatana na kawaida ya dunia, na kwa sababu hiyo haiwezi kuamsha upinzani wo wote. Dini iliyoko katika wakati wetu huu si dini yenye sifa safi na takatifu ambayo ilikuwa ni sifa za imani ya Kikristo katika siku za Kristo na mitume wake. Ni kwa sababu pekee ya roho ya maridhiano na dhambi, kwamba kweli kuu za Neno la Mungu hazizingariwi, kwa sababu kuna utauwa kidogo mno katika kanisa, ndio maana Ukristo kwa hakika unapendwa kiasi hicho na dunia. Hebu na pawepo na uamsho wa imani na nguvu ya kanisa la kwanza, na roho ya mateso itahuishwa na mioto ya mateso itawashwa tena. PLK 112.1