Ilikuwa ni usiku wa manane ndipo Mungu alipochagua kuwakoa watu wake. Wakati waovu walipokuwa wakiwadhihaki, ghafla jua lilitokeza, likiwaka kwa nguvu zake zote, na mwezi ulitulia kabisa. Waovu walitazama tukio hili kwa mshangao, huku watakatifu, kwa furaha adhimu waliona ishara za mwanzo za kukombolewa kwao. Ishara na maajabu vilifuatana kwa mfuatano wa haraka. Kila kitu kilionekana kwamba kinaondolewa katika njia yake ya asili. Vijito vilikoma kutiririka. Mawingu mazito, meusi yaliinuka na kugongana yenyewe kwa yenyewe. Lakini kulikuwako sehemu moja dhahiri ambapo utukufu ulitulia, na kutokea pale sauti ya Mungu ilisikika kama sauti ya maji mengi, ikitikisa mbingu na nchi. Kulikuwa na tetemeko kuu. Makaburi yalifimguka, na wale waliokuwa wamekufa katika imani katika ujumbe wa malaika wa tatu, wakitunza Sabato, walitoka katika vitanda vyao vya mavumbi wakiwa wametukuzwa, wapate kusikia agano la amani ambalo Mungu alikuwa anataka kulifanya na wale ambao walishika sheria yake. PLK 130.2
Anga lilifunguka na kufunga na lilikuwa katika hali ya msukosuko. Milima ilitikisika kama matete katika upepo na kutawanya mawe yaliyopasuka kwenda kila mahali kuizunguka. Bahari ilichemka kama chungu na kurusha mawe juu ya nchi. Na wakati Mungu alipolitoa agano la milele kwa watu wake, alitamka sentensi moja, na kutulia, wakati maneno yale yalipokuwa yakienea katika nchi. Israeli wa Mungu walisimama na macho yao yakiwa yamekazwa kuangalia juu, wakisikiliza maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa Yehova na kuenea katika nchi kama ngurumo za radi yenye sauti kubwa kuliko zote. Ilikuwa ni wakati wa kicho cha kutisha. Mwisho wa kila sentensi watakatifu walipaza sauti,“Utukufu! Haleluya!” Nyuso zao ziliangazwa kwa utukufu wa Mungu, ziking’ara kwa utukufu kama vile uso wa Musa wakati aliposhuka kutoka juu ya mlima Sinai. Waovu hawakuweza kuwaangalia kwa sababu ya utukufu ule. Na wakati Mungu alipotangaza baraka za milele juu ya wale ambao walikuwa wamemheshimu kwa kuitunza Sabato yake kwa kuitakasa, walipaza sauti za ushindi juu ya mnyama na sanamu yake. PLK 131.1
Kuja kwa Kristo Mara ya Pili-Muda si mrefu lilitokea wingu kubwa jeupe, ambalo juu yake aliketi Mwana wa Adamu. Lilipotokeza kwa mara ya kwanza kwa mbali, wingu hili lilikuwa dogo sana. Kadiri lilivyosogea karibu na dunia, kila mtu aliweza kuona utukufu na ukuu mkamilifu wa Yesu kadiri alivyokuwa akisonga mbele ili kushinda. Msafara wa malaika watakatifu wakiwa na taji angavu zenye kumetameta juu ya vichwa vyao ulimsindikiza katika njia yake. PLK 132.1
Hakuna lugha inayoweza kuelezea utukufu wa tukio lile. Wingu lile hai la ukuu na utukufu usio kifani lilishuka karibu zaidi na zaidi, juu yake alikuwapo Yesu mwenye kupendeza, pasipo taji ya miiba bali taji ya utukufu katika paji lake takatifu. Katika joho lake na paja lake jina liliandikwa, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana (Ufunuo 19:16). Uso wake uling’aa kama jua la adhuhuri, macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na miguu yake ilikuwa na mwonekano wa shaba iliyo safi sana (Ufunuo 1:15,16). Sauti yake ilisikika kama sauti ya vyombo vingi vya muziki. Dunia ilitikisika mbele ya uso wake, mbingu zilitoweka kama ukurasa unavyokunjwa pamoja, na kila mlima na kisiwa viliondolewa kutoka mahali pake. “Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?” Ufunuo 6:15-17. PLK 132.2
Wale ambao muda mfupi uliokuwa umepita walikuwa tayari kuwaangamiza watoto wa Mungu waaminifu, sasa walishuhudia utukufu wa Mungu ukiwakalia juu yao. Na katikati ya utisho wao walisikia sauti za watakatifu kwa sauti za furaha, zikisema, “Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemngoja atusaidie.” Isaya 25:9. PLK 132.3
Ufufuo wa Kwanza-Dunia ilitikisika kwa nguvu wakati sauti ya Mwana wa Mungu ilipowaita watakatifu waliolala kutoka katika makaburi yao. Waliitikia wito ule na kutoka wakiwa wamevikwa utukufu wa kutokufa, wakisema kwa sauti kuu, “Ushindi, ushindi, juu ya mauti na kaburi! Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?” (Angalia 1 Wakorintho 15:55). Ndipo watakatifu walio hai na wale waliofufuka waliinua sauti zao kwa sauti kuu za furaha ya ushindi. Miili ile iliyokwenda kaburini ikiwa imebeba alama za maradhi na mauti ilitoka ikiwa na afya na nguvu ya kutokufa. Watakatifu walio hai wanabadilishwa mara moja, katika kufumba na kufumbua, na kunyakuliwa pamoja na wale waliofufuka, na wote kwa pamoja wanakutana na Bwana wao angani. Lo, mkutano wa furaha kiasi gani! Marafiki waliotengwa na mauti waliungana, wasitengane tena kamwe. PLK 133.1
Katika kila upande wa gari la wingu kulikuwako na mabawa, na chini yake kulikuwako na magurudumu yaliyo hai. Na watakatifu waliokuwa katika wingu lile wakapaza sauti wakisema, “Utukufu! Haleluya!” Na gari lile likapaa kwenda juu katika Jiji Takatifli. Kabla ya kuingia jijini, watakatifu walipangwa katika mraba mkamilifu, Yesu akiwa katikati. Alisimama kichwa na mabega yake yakiwa juu ya watakatifu na juu ya malaika. Wote katika mraba ule wangeweza kuona umbo lake tukufu na uso wake wa kupendeza. PLK 133.2