Kisha kutoka katika jiji lile malaika wengi sana walileta taji zinazong’aa sana-taji kwa ajili ya kila mtakatifu, jina lake likiwa limeandikwa juu yake. Yesu alipozihitaji taji zile, malaika walimkabidhi, na kwa mkono wake mwenyewe wa kuume Yesu aliweka taji zile juu ya vichwa vya watakatifu. Kwa jinsi iyo hiyo malaika walileta vinubi, na Yesu alivikabidhi pia kwa watakatifu. Malaika waongozaji kwanza walipiga noti, na kisha kila sauti iliinuliwa kwa sifa za furaha na shukurani, na kila mkono kwa ustadi kabisa ulipita juu ya nyuzi za vinubi, na kutoa muziki mtamu katika sauti zilizo kamili na tamu sana. PLK 133.3
Kisha Yesu akaliongoza jeshi la waliokombolewa katika malango ya jiji lile. Aliushika mlango, na kuurudisha nyuma katika bawaba zake zinazometameta, na kuwakaribisha mataifa walioutunza ukweli waingie. Ndani yajiji kulikuwako na kila kitu chenye kufurahisha macho. Waliona utukufu tele kila mahali. Kisha Yesu aliwaangalia watakatifu wake waliokombolewa, nyuso zao zikiwa angavu kwa utukufu. Alisema, kwa sauti yake tamu, kama ya muziki, “Ninaona mazao ya taabu ya roho yangu, na nimeridhika. Utukufu huu wa fahari ni kwa ajili yenu kuufurahia milele zote. Huzuni zenu zimekoma. Hapatakuwapo na mauti tena, wala huzuni, wala kilio, wala hakutakuwapo na maumivu tena.” Waliokombolewa walisujudu na kuweka taji zao zinazong’aa miguuni pa Yesu, na kisha, mikono yake ya kupendeza ilipowainua, walivigusa vinubi vyao vya dhahabu na kuijaza mbingu yote kwa muziki mtamu sana na nyimbo kwa Mwana-Kondoo. PLK 134.1
Kisha Yesu aliwaongoza watu wake kwenda kwenye mti wa uzima, na tena waliisikia sauti yake nzuri, tamu kuliko muziki wo wote uliowahi kusikika katika sikio la mwanadamu, ikisema, “Majani ya mti huu ni kwa ajili ya kuyaponya mataifa. Kuleni nyote.” Katika mti wa uzima kulikuwako na matunda mazuri kuliko yote ambayo watakatifu wangeweza kuyala kwa uhuru. Katika jiji hili kulikuwako na kiti cha enzi kitukufu kuliko vyote, na kutoka katikati yake kulikuwako na mto safi wenye maji ya uzima, safi kama kioo. Katika kila upande wa mto ule kulikuwa na mti wa uzima, na katika kingo za mto huu kulikuwako na miti mingine mizuri iliyozaa matunda yaliyofaa kwa chakula. PLK 134.2
Lugha kwa ujumla ni dhaifu mno kujaribu kutoa maelezo ya mbinguni. Tunaweza tu kusema kwa mshangao, “Lo, ni upendo ulioje! Upendo wa ajabu kiasi gani!” Lugha iliyo bora kuliko zote inashindwa kuelezea utukufu wa mbinguni au vina visivyo na kifani vya upendo wa Mwokozi. PLK 135.1