Duniani, waovu walikuwa wameangamizwa, na maiti zao zililala juu ya uso wa nchi. Ghadhabu ya Mungu katika mapigo yale saba ya mwisho ilikuwa imeanguka juu ya wakazi wa dunia, na kuwasababisha kutafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu na wakamlaani Mungu. Baada ya watakatifu kuokolewa kwa sauti ya Mungu, umati wa waovu waligeuza hasira zao kwao wenyewe kila mtu kwa mwenzake. Dunia ilionekana kana kwamba imegharikishwa kwa damu, na miili iliyokufa ilikuwa imetapakaa kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine. PLK 136.1
Dunia ilionekana kama jangwa lenye ukiwa. Miji na vijiji, vikiwa vimebomolewa na tetemeko la ardhi, vilikaa katika malundo. Milima ilikuwa imehamishwa kutoka mahali pake, ikiacha mashimo makubwa. Mawe yaliyochongoka, yaliyorushwa nje na bahari, au kumegwa kutoka katika ardhi yenyewe, yalitawanyika juu ya uso wake. Miti mikubwa iliyong’olewa ilitapanywa juu ya nchi. Hapa ndipo patakuwa makazi ya Shetani na malaika zake waovu kwa muda wa miaka elfu moja. Hapa ndipo atakapofungwa, ili azunguke juu na chini katika uso wa dunia uliovunjika apate kuona matokeo ya uasi wake dhidi ya sheria ya Mungu. Kwa miaka elfu moja anaweza kufurahia matunda ya laana ambayo aliisababisha. PLK 136.2
Akiwa amefungwa peke yake katika dunia hataweza kuwa na fursa ya kutembelea malimwengu mengine, ili kuwajaribu na kuwasumbua wale ambao hawakuanguka. Katika kipindi hiki Shetani anateseka vikali mno. Tangu kuanguka kwake sifa zake za uovu zimekuwa zikitenda kazi bila kukoma. Lakini katika muda huu wa miaka elfu moja atanyang’anywa uwezo wake na kuachwa kutafakari juu ya sehemu aliyotekeleza tangu kuanguka kwake, na kutazamia mbele kwa kutetemeka na hofu kwenye mustakabali wa kuogofya ambapo atalazimika kuteseka kwa ajili ya maovu yote aliyoyatenda na kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zote alizosababisha zitendwe. PLK 136.3
Kutoka kwa malaika na kwa watakatifu waliokombolewa zilikuja kelele za shangwe kama za vyombo elfu kumi vya muziki, kwa sababu Shetani asingewasumbua tena kamwe na kuwajaribu na kwa sababu wakazi wa malimwengu mengine waliwekwa huru dhidi ya kuwapo kwake na majaribu yake. PLK 137.1
Yesu pamoja na waliokombolewa waliketi juu ya viti vya enzi, na watakatifu walitawala kama wafalme na makuhani kwa Mungu. Kristo, katika umoja na watu wake, waliwahukumu waovu waliokufa, wakilinganisha matendo yao na Kitabu cha Sheria, Neno la Mungu, na kuamua kila kesi kulingana na matendo yaliyotendwa katika mwili. (Angalia Ufunuo 20:4-6.) Kisha waliwagawia waovu fungu lile ambalo ni lazima walipate, kulingana na matendo yao, na liliandikwa mbele ya majina yao katika kitabu cha mauti. Yesu pamoja na watakatifu pia walimhukumu Shetani na malaika zake. Adhabu ya Shetani ingekuwa kubwa mno kupita ile ya wale aliowadanganya. Mateso yake yangeyapita mateso yao kiasi kwamba hayawezi kulinganishwa nayo. Baada ya wote wale aliowadanganya kuangamia, Shetani ilikuwa aendelee kuishi na kuteseka kwa kipindi kirefu zaidi. PLK 137.2
Baada ya hukumu ya waovu waliokufa kumalizika, mwishoni mwa miaka elfu moja, Yesu aliondoka katika jiji lile, pamoja na watakatifu na msafara wa malaika ulimfiiata. Yesu alishuka juu ya mlima mkubwa, na mara tu miguu yake ilipougusa, ulipasuka na kuwa uwanda mpana. Ndipo lile jiji kubwa na zuri, lenye misingi kumi na miwili na milango kumi na miwili, mitatu kila upande, na malaika katika kila mlango, lilijitokeza juu. Watakatifu walipaza sauti, “Jiji! jiji kuu! Linashuka kutoka kwa Mungu kutoka mbinguni!” Na lilishuka chini pamoja na uzuri wake wote na utukufu wa kutia kiwi machoni, na kutulia juu ya uwanda ule mkuu ambao Yesu aliuandaa kwa ajili yake. PLK 137.3
Ufufuo wa Pili-Kisha Yesu na msafara wote wa malaika watakatifu na watakatifu wote waliokombolewa walitoka katika lile jiji. Malaika walimzunguka Amiri jeshi wao na kumsindikiza katika njia yake, na maandamano ya watakatifu yalifuata. Ndipo, kwa ukuu wa kutisha na kuogofya, Yesu aliwaita waovu waliokufa na kuwafufua. Waliinuka wakiwa na miili ile ile midhaifu, isiyo na afya iliyokwenda kaburini. Ni tukio la ajabu sana! Wale waliokuwa katika ufufuo wa kwanza wote walitoka wakiwa na afya ya kutokufa, lakini katika ufufuo wa pili alama za laana zinaonekana juu ya wote. Wafalme na wakuu wa dunia, maskini na watu wa hali ya chini, wasomi na wasio na elimu, wanatoka kaburini pamoja. Wote wanamwona Mwana wa Adamu. Watu wale wale waliomdharau na kumdhihaki, wale walioweka taji ya miiba katika uso wake mtakatifu na kumpiga kwa mwanzi, wanamwona sasa katika ukuu wake wote wa kifalme. Wale waliomtemea mate katika saa yake ya kujaribiwa sasa wanageuka wasione kule kukaziwa macho kunakochoma na wajiepushe na utukufu wa uso wake. Wale waliopigilia misumari katika mikono na miguu yake sasa wanatazama zile alama za kusulibiwa kwake. Wale waliochoma mkuki ubavuni mwake wanaona alama za ukatili wao katika mwili wake. Na wanafahamu kuwa ndiye yule yule waliyemsulibisha na kumdhihaki katika maumivu yake makali ya kufa. Ndipo kunainuka kilio kimoja kirefu cha huzuni, huku wakikimbia ili kujificha kutoka mbele za uso wa Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. PLK 138.1
Wote wanatafuta kujificha kwenye miamba ili kujikinga mbali na utukufu wa kutisha wake Yeye ambaye walimdharau hapo mwanzo. Na, wakiwa wamezidiwa na kutiwa uchungu kwa sababu ya ukuu na utukufu wake mkuu, wanainua sauti zao wote kwa pamoja, na kwa uwazi wa kutisha wanatamka, “Amebarikiwa Yeye ajaye kwa jina la Bwana!” PLK 139.1
Kisha Yesu na malaika watakatifu, na watakatifu wote, wanakwenda tena ndani ya jiji lile, na vilio vya uchungu na maombolezo ya waovu waliohukumiwa vinalijaza anga. Ndipo Shetani akaanza tena kazi yake. Alizunguka miongoni mwa wafuasi wake na kuwatia nguvuwalewaliokuwadhaifunawanyonge,akiwaambia kuwa yeye pamoja na malaika zake walikuwa na nguvu. Alielekeza kwa mamilioni waliofufuliwa wasioweza kuhesabiwa. Walikuwapo mashujaa wenye nguvu na wafalme waliokuwa hodari sana katika vita na ambao walikuwa wamezishinda falme nyingi. Na walikuwapo majitu yenye nguvu na mashujaa ambao hawakuweza kushindwa katika vita hata moja. Alikuwapo Napoleon mwenye kiburi na mwenye kupenda makuu, ambaye kukaribia kwake kulisababisha falme kutetemeka. Watu wenye maumbile makubwa na mwonekano wa heshima kubwa walikuwapo pale, ambao walikuwa wameanguka katika vita huku wakiwa na kiu ya kushinda. PLK 139.2
Wanapotoka katika makaburi yao wanaurudia mfululizo wa mawazo yao katika mahali palepale yaliposimamishwa na kifo. Wanakuwa na tamaa ileile ya kushinda ambayo ilikuwa ikiwatawala pale walipoanguka. Shetani anashauriana na malaika zake na kisha na wale wafalme na washindi na watu wenye nguvu. Na ndipo anapoliangalia jeshi kubwa lile na kuliambia kuwa jeshi lililoko katika jiji lile ni dogo na dhaifu, na kwamba wanaweza kwenda na kuliteka, na kuwaondoa wakazi wake nje, na kumiliki utajiri wake na kujitukuza wenyewe. PLK 139.3
Shetani anafanikiwa katika kuwadanganya, na mara moja wote wanaanza kujiandaa kwa ajili ya vita. Kuna watu wengi sana ambao ni hodari katika jeshi hili kubwa, na wanatengeneza kila aina ya vifaa vya kivita. Kisha, wakiwa na Shetani kama kiongozi wao, jeshi kubwa hili linasonga mbele. Wafalme na mashujaa wanafuatia kwa karibu baada ya Shetani, na umati unafuata nyuma yao wakiwa katika makundi makundi. Kila kundi lina kiongozi wake, na kwa utaratibu wanatembea juu ya uso wa nchi uliobomoka-bomoka kuelekea katika Jiji Takatifu. Yesu anayafunga malango ya jiji lile, na askari wa jeshi hili kubwa wanalizingira na kujipanga kwa vita, wakitarajia mapambano makali. PLK 140.1