Shetani alichukua umbile la nyoka na kuingia Edeni. Alijiweka juu ya mti wa ujuzi na kuanza kula matunda yake taratibu. PLK 18.2
Bila kutambua mwanzoni, Hawa alijitenga kutoka kwa mume wake alipokuwa akihudumia bustani. Alipotambua kile kilichotokea, alihisi kuwa kungeweza kutokea hatari, lakini tena alifikiri kuwa alikuwa salama, hata kama hakudumu kuwa karibu pembeni mwa mume wake. Alikuwa na hekima ya kuweza kutambua pale ambapo hatari ingekuja, na nguvu ya kuweza kukabiliana nayo. Malaika walikwisha kumwonya kutokutenda hili. Hawa alijikuta akikaza macho yake kuangalia tunda la mti uliokatazwa akiwa na mchanganyiko wa shauku ya udadisi na kuvutiwa. PLK 18.3
Aliona kuwa lilikuwa la kupendeza mno, na kuwaza moyoni mwake kwa nini Mungu aliwazuia vikali kiasi kile wasilile. Sasa ilikuwa fursa ya Shetani. Alisema naye kana kwamba alikuwa na uwezo wa kusoma mawazo yake: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?” Kwa maneno laini na ya kupendeza, na kwa sauti ya kimuziki, aliongea na Hawa aliyestajabishwa. Alishangazwa kusikia nyoka akiongea, kwa vile alifahamu kuwa Mungu hakuwa amempa nyoka uwezo wa kunena. PLK 18.4
Udadisi wa Hawa uliamshwa. Badala ya kuondoka pale kwa haraka, alitega masikio kumsikiliza nyoka akiongea. Haikufahamika moyoni mwake kuwa huyu angekuwa ndiye yule adui aliyeanguka, akimtumia nyoka kama chombo. Ni Shetani aliyekuwa akiongea, wala si nyoka. Hawa alivutiwa, akadanganyika, na kupumbazwa. Iwapo angekutana na mtu mwenye staha, mwenye umbile kama la malaika na anayefanana na wao, angeweza kujihadhari. PLK 18.5
Sauti hii ya ajabu ingetosha kumkimbiza kwa mume wake na kumwuliza kwa nini mtu mwingine aongee naye kwa uhuru jinsi ile. Bali aliingia katika mapambano na nyoka. Alilijibu swali lake: “matunda ya miti ya bustani twaweza kula lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani, Mungu amesema, ‘msiyale, wala msiyaguse, msije mkafa.’” Shetani alijibu, “Hakika hamtakufa. Kwa maana Mungu anajua ya kuwa siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” PLK 19.1
Shetani alitaka wadhani kwamba kwa kula matunda ya mti uliokatazwa wangepokea maarifa mapya ya kigeni na yaliyo bora zaidi ya yale ambayo tayari walikuwa nayo. Hii imekuwa ni kazi yake maalumu, yenye mafanikio makubwa, tangu alipoanguka-kuwaongoza watu kudadisi siri za Mwenyezi na wala kutoridhika na kile ambacho Mungu amedhihirisha, na wala wasiwe waangalifu kutii kile alichokiagiza. Anataka awafanye wasitii amri za Mungu na kisha kuwafanya waamini kuwa wanaingia katika uwanja wa ajabu wa maarifa. Hii ni dhana tupu, na ni udanganyifu wa kutisha. PLK 19.2
Wanashindwa kufahamu kile ambacho Mungu amefunua, na wanadharau amri zake za wazi na kuitamani hekima isiyomtegemea Mungu, wakitafuta kufahamu kile ambacho amechagua kuwaficha wenye miili ya kufa. Wanafurahishwa na mawazo yao ya kuendelea na kuvutiwa na falsafa zao wenyewe zilizo tupu, lakini wanapapasa-papasa katika giza la usiku wa manane kuhusiana na maarifa ya kweli. PLK 19.3
Hayakuwa mapenzi ya Mungu kwamba wana ndoa hawa wasiokuwa na dhambi wapate ufahamu wo wote wa mabaya. Kwa hiari aliwapa mema tele lakini alizuia kwao mabaya. Hawa alidhani kuwa maneno ya nyoka yalikuwa ya hekima, na alilikubali dai lake thabiti, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” huku kulikuwa ni kumfanya Mungu kuwa Mwongo. Shetani kwa ushupavu alidokeza kuwa Mungu alikuwa amewadanganya ili kuwazuia wasipate maarifa ambayo yangewafanya wao kuwa sawa na yeye [Mungu] mwenyewe. Mungu alisema, Mkila mtakufa hakika. Nyoka alisema, mkila “Hakika hamtakufa.” PLK 20.1
Mjaribu alimhakikishia Hawa kuwa mara tu baada ya kula tunda lile angepokea ujuzi bora ambao ungemfanya kuwa sawa na Mungu. Alielekeza fikra za Hawa kwake yeye mwenyewe. Alisema kwamba sababu iliyomfanya apate uwezo wa kusema ni kwa vile alikuwa amekula matunda ya mti uliokatazwa kwao. Alidokeza kwamba Mungu asingeweza kutekeleza neno lake. Ilikuwa ni tishio tu ili kuwaogopesha na kuwazuia kupata kilicho bora. Pia aliwaambia kuwa wasingeweza kufa. Je hawakuwa wamekula kutoka katika mti wa uzima ambao unadumisha kutokufa? Aliwaambia kuwa Mungu alikuwa anawadanganya ili kuwazuia kufikia hali ya juu zaidi ya maisha na furaha kubwa zaidi. PLK 20.2
Mjaribu alichuma tunda na kumpa Hawa. Alilichukua mkononi mwake. Sasa, alisema mjaribu, mlikatazwa hata kuligusa msije mkafa. Alimwambia kuwa asingepata hisia yo yote ya uovu na kifo kwa kulila tofauti na huko kuligusa au kulibeba tunda hilo. Hawa alitiwa ujasiri kwa sababu hakuhisi mara moja ishara za Mungu kutopendezwa. Alidhani kuwa maneno yote ya mjaribu lazima ni ya hekima na sahihi. Alikula, na alifurahishwa na tunda lile. Iilielekea kuwa tamu sana kwake kwa ladha, na alidhani kuwa alihisi ndani yake matokeo ya ajabu ya tunda lile. PLK 20.3
Hawa Anakuwa Mjaribu-Ndipo alipochuma yeye mwenyewe matunda na kuyala, akiwaza kuwa alikuwa akihisi uwezo utiao nguvu wa maisha mapya na ya hali ya juu zaidi kutokana na matokeo ya kufurahisha ya tunda lililokatazwa. Alikuwa katika msisimko wa ajabu na usio wa kawaida alipokuwa anakwenda kumtafuta mume wake mikono yake ikiwa imejaa matunda yaliyokatazwa. Alimwambia mambo ya hekima ambayo nyoka aliyasema, na alitaka mara moja kumchukua kwenda kwenye mti wa ujuzi. Alimwambia kuwa alikuwa amekula baadhi ya matunda yake, na badala ya kuhisi hali yo yote ya kifo, alipata uzoefu wa hisia ya kupendeza na ya kufurahisha. Mara tu baada ya Hawa kutokutii, aligeuka kuwa chombo chenye nguvu ambacho kupitia kwake Shetani angesababisha anguko la mume wake. PLK 21.1
Adamu alifahamu vyema kabisa kuwa mwenzi wake hakulitii katazo pekee ambalo Mungu aliwapa ili kupima uaminifu na upendo wao. Hawa alitoa wazo kuwa nyoka alisema kwamba hakika hawatakufa, na maneno yake lazima yatakuwa kweli, kwa kuwa hakuhisi ishara yo yote ya Mungu kuchukizwa, bali hisia ya kupendeza, kama vile wanavyojisikia malaika, alidhani. PLK 21.2
Adamu alijuta kuwa Hawa alitoka kando yake, lakini sasa tendo limekwisha kutendeka. Ni lazima atenganishwe kutoka kwa mtu ambaye alimpenda sana na kumfurahia kama mwenzi wake. Angewezaje kuruhusu hilo litokee? Upendo wake kwa Hawa ulikuwa na nguvu. Na kwa kukata tamaa kabisa aliamua kushiriki msiba wake. Aliwaza kuwa Hawa alikuwa ni sehemu yake mwenyewe, na kama itabidi afe, basi atakufa pamoja naye, kwa vile hataweza kuvumilia wazo la kutengana naye. PLK 21.3
Alikosa imani kwa Muumba wake mwenye rehema na aliye mwema. Hakufikiria kuwa Mungu, ambaye aliyemfanya kutoka katika mavumbi ya ardhi kuwa kiumbe hai, kilicho kizuri, na kumwumba Hawa kuwa mwenzi wake, angeweza kujaza nafasi yake. Hata hivyo, je maneno ya nyoka huyu mwerevu hayawezi kuwa sahihi? Hawa alikuwa amesimama mbele yake, akiwa ni wa kupendeza na mzuri na dhahiri bila hatia kama vile alivyokuwa kabla hajakosa kutii. Alikuwa akidhihirisha upendo mkuu, na wa hali ya juu kwake kuliko ilivyokuwa hapo kabla ya kutokutii kwake, akidai kuwa haya yalitokana na yeye kula tunda lile. Hakuona dalili zo zote za kifo ndani yake. PLK 22.1
Aliamua kujaribu bahati zake. Alinyakua tunda na haraka akalila, na kama alivyokuwa Hawa, hakuhisi matokeo yake mabaya mara moja. PLK 22.2
Uhuru wa Mwanadamu wa Kuchagua-Mungu aliwaelekeza wazazi wetu wa kwanza kuhusu mti wa ujuzi, na walikuwa na taarifa kamili kuhusu anguko la Shetani na hatari ya kusikiliza mapendekezo yake. Mungu hakuwanyima uwezo wa kula tunda lililokatazwa. Aliwaacha kama mawakala huru wa kuamini neno lake, kutii amri zake, na kuishi, au kumwamini mjaribu, kutokutii, na kuangamia. PLK 22.3
Upendo wa kuvutia na amani na furaha kamili ya kuridhisha, ilionekana kuondolewa kutoka kwao, na badala yake kukosekana kwa kitu fulani kulikuja juu yao ambako kamwe walikuwa hawajapata kuhisi hapo kabla. Ndipo kwa mara ya kwanza waligeuza fikra na macho yao kuelekea kwa vitu vya nje. Hawakuwa wamevaa nguo bali walikuwa wamefunikwa na nuru kama malaika wa mbinguni walivyokuwa. Nuru hii iliyowafunika kabisa sasa ilikuwa imeondoka. Ili kusaidia hisia zao za uhitaji na uchi waliokuwa wamehisi, walitafuta namna fulani ya vazi kwa ajili ya miili yao, kwani ni vipi wangeweza kukutana na macho ya Mungu na malaika wakiwa uchi? PLK 22.4
Shetani alifurahishwa mno na mafanikio yake. Sasa alikuwa amemjaribu mwanamke kutomwamini Mungu, kuhoji hekima yake, na kujaribu kujipenyeza katika mipango yake isiyochunguzika. Na kupitia kwake pia alimwangusha Adamu, ambaye, kwa sababu ya upendo wake kwa Hawa, aliacha kuitii amri ya Mungu na hivyo kuanguka pamoja naye. PLK 23.1
Bwana alimtembelea Adamu na Hawa na kuwaambia matokeo ya kutokutii kwao. Waliposikia mjongeo wa Mungu wa kifahari, walijaribu kujificha wasionwe na yeye ambaye walifurahia kukutana naye pale walipokuwa katika hali yao ya kutokuwa na hatia na ya utakatifu. “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, ‘Uko wapi?’ Akasema, ‘Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.’Akasema, ‘Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?’ ” PLK 23.2
Bwana aliuliza swali hili si kwa sababu alihitaji taarifa, bali ni kwa sababu ya kuwasadikisha wale wanandoa juu ya hatia yao. Uliwezaje kuwa na aibu na kuogopa? Adamu alikiri dhambi yake, si kwa sababu alitubu kwa ajili ya kutokutii kwake kukuu, bali ili kulaumu dhambi yake juu ya Mungu. “Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Kisha Mungu alisema na mwanamke: “Nini hili ulilolifanya?” Hawa akajibu, “Nyoka alinidanganya, nikala..” PLK 23.3
Laana -Ndipo Bwana akasema na nyoka: “Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako.” Kama vile nyoka alivyokuwa ametukuka juu ya wanyama wote wa mwituni, angeshushwa hadhi chini ya wote na kuchukiwa na watu, kwa sababu alikuwa ndiye chombo ambacho kwake Shetani alitenda kazi yake. Kisha “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” PLK 23.4
Mungu aliilaani ardhi kwa sababu ya dhambi yao ya kula kutoka katika mti wa ujuzi, na kutangaza, “kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako.” Alikuwa amewapa mema na kuzuia mabaya. Sasa anatangaza kuwa watakula mazao yake, yaani, wangepata uzoefu wa mabaya siku zote za maisha yao. PLK 24.1
Kuanzia wakati ule na kuendelea, jamii ya wanadamu wangesumbuliwa na majaribu ya Shetani. Adamu alipewa maisha ya kudumu ya kazi ngumu na wasiwasi badala ya kazi ya kufurahisha, na ya kupendeza aliyokuwa akiifurahia hadi kufikia hapo. Wangepata uzoefu wa kuvunjika moyo, huzuni, na maumivu, na hatimaye kufikia uharibifu. Walitengenezwa kwa mavumbi ya ardhi, na katika mavumbi wangerudi. PLK 24.2
Waliarifiwa kuwa iliwabidi kupoteza makazi ya Edeni. Walikubali kushindwa na udanganyifu wa Shetani na kuamini neno la Shetani, kwamba Mungu angeweza kusema uongo. Kwa kutokutii kwao walikuwa wamefungua njia kwa ajili ya Shetani kupata nafasi ya kuwafikia kirahisi, na hivyo haikuwa salama kwao kubakia katika Bustani ya Edeni, katika hali yao ya dhambi na kupata nafasi ya kuufikia mti uzima na hivyo kudumisha maisha ya dhambi. Waliomba waruhusiwe kubaki bustanini, ingawa walikiri kuwa walikuwa wamepoteza haki zote za kuwapo katika Edeni yenye furaha kamili. Waliahidi kwamba katika siku za baadaye wangempa Mungu utii thabiti. Waliambiwa kuwa katika anguko lao kutoka katika kutokuwa na hatia hadi kufikia kuwa na hatia hawakupata nguvu yo yote, bali udhaifu mkuu. Hawakuhifadhi uaminifu wao pale walipokuwa katika hali ya utakatifu, furaha isiyo na hatia, na sasa wangekuwa na nguvu pungufu zaidi ya kuweza kudumu kuwa wakweli na waaminifu katika hali hii ya hatia iliyo dhahiri. Walikuwa wamejazwa na maumivu ya kina mno pamoja na majuto. Sasa walitambua kuwa adhabu ya dhambi ni mauti. PLK 24.3
Malaika waliagizwa mara moja kuilinda njia ya kuelekea katika mti wa uzima. Ulikuwa ni mpango uliodhamiriwa wa Shetani kwamba Adamu na Hawa wasimtii Mungu, wachukiwe naye, na kula matunda ya mti wa uzima, ili kwamba wapate kudumisha maisha ya dhambi. Lakini malaika watakatifu walitumwa ili kuzuia njia yao kuelekea katika mti wa uzima. Kuwazunguka malaika hawa kulimulika mionzi ya nuru kila upande, iliyoonekana kama mapanga yanayomeremeta. PLK 25.1