Sura hii imejengwa katika Mwanzo 3:15, 21-24.
Huzuni iliijaza mbingu, pale wote walipotambua kuwa wanadamu walikuwa wamepotea na dunia ambayo Mungu alikuwa ameiumba ilikuwa ijazwe na wanadamu wapatikanao na mauti wanaopitia maisha ya taabu, maradhi, na mauti, pasipo na njia ya kuokoka kwa mkosaji. Familia yote ya Adamu ni lazima wafe. PLK 26.1
Ndipo Yesu akawafahamisha jeshi la malaika kwamba njia ya kuokoka ilikwisha kupatikana kwa ajili ya wanadamu waliopotea. Aliwaambia kuwa alikuwa amemsihi Baba yake kwamba Yesu ajitolee maisha yake kuwa fidia ya kuwakomboa. Angetumikia adhabu ya kifo juu yake mwenyewe, ili kwa kupitia kwake wanadamu waweze kupata msamaha. Kupitia katika ustahili wa damu yake, na utii kwa sheria ya Mungu, wangeweza kukubaliwa na Mungu na kurejeshwa katika ile bustani nzuri na kula matunda ya mti wa uzima. PLK 26.2
Yesu alifunua mbele yao mpango ule wa wokovu. Aliwaambia kuwa angesimama baina ya ghadhabu ya Baba yake na wanadamu wenye hatia, ili apate kubeba uovu na dhihaka, na kwamba ni wachache tu wangempokea kama Mwana wa Mungu. Karibu kila mtu angemchukia na kumkataa. Angeacha utukufu wake wote mbinguni, na kutokea duniani kama mwanadamu, kujinyenyekesha kama mwanadamu, kupitia uzoefu wake mwenyewe ajue majaribu mbalimbali ambayo yangewapata wanadamu, ili apate kujua jinsi ya kuwasaidia wale ambao wangejaribiwa. Hatimaye, baada ya kazi yake kama mwalimu kukamilishwa, angekabidhiwa katika mikono ya watu waovu na kustahimili karibu kila aina ya ukatili na maumivu ambayo Shetani pamoja na malaika zake wangeweza kuwachochea watu waovu kutenda. Afe mauti ya kikatili kuliko zote, kutundikwa kati ya mbingu na dunia kama mwenye dhambi mhalifu na kupitia wasaa wa maumivu ya kutisha, ambayo hata malaika wasingeweza kutazama, bali wangeficha nyuso zao kutoka katika tukio lile. Siyo tu kuwa angeteseka kwa maumivu makali ya kimwili, bali maumivu ya kiakili ambayo yale ya kimwili yasingeweza kulinganishwa nayo. Uzito wa dhambi za dunia yote ungekuwa juu yake. Aliwaambia kuwa angekufa na kufufuka tena katika siku ya tatu, na angepaa kwenda kwa Baba yake ili apate kuwaombea wanadamu waliotanga mbali, wenye hatia. PLK 26.3
Njia Moja Pekee Inayowezekana ya Wokovu- Malaika walisujudu mbele zake. Walijitolea maisha yao. Yesu aliwaambia kuwa kwa kifo chake angeokoa wengi, ambao maisha ya malaika yasingeweza kulipia deni. Maisha yake peke yake ndio yangekubaliwa na Baba yake kama fidia kwa ajili ya wanadamu. Baadaye, wale ambao angewakomboa wangekuwa pamoja naye, na kwa kifo chake angetoa fidia kwa watu wengi na kumwangamiza Shetani, ambaye alikuwa na nguvu za mauti. Na Baba yake angemkabidhi ufalme na ukuu wa ufalme chini ya mbingu yote, na angeimiliki milele na milele. Shetani na wenye dhambi wangeangamizwa, kamwe wasiweze kuisumbua mbingu au dunia mpya iliyotakaswa. PLK 27.1
Lakini aliwapa malaika kazi yao, kupanda na kushuka wakiwa na msaada wa kutia nguvu kutoka katika utukufu kwa ajili ya kumliwaza Mwana wa Mungu katika mateso yake na kumhudumia. Pia, ilikuwa wawalinde na kuwatunza raia wa neema kutokana na malaika waovu na giza ambalo daima Shetani angerusha kuwazunguka. Isingewezekana kwa Mungu kugeuza au kubadilisha sheria yake, ili apate kuwaokoa wenye dhambi waliopotea na wanaoangamia. Kwa hiyo, aliruhusu Mwana wake mpendwa kufa kwa ajili ya dhambi zao. PLK 27.2
Shetani kwa mara nyingine alifurahi pamoja na malaika zake kwamba kwa kusababisha anguko la wanadamu, ataweza kumshusha Mwana wa Mungu kutoka katika cheo chake kilichotukuka. Aliwaambia malaika zake kwamba Yesu atakapochukua asili ya wanadamu walioanguka, angeweza kumzidi nguvu na kuzuia kufanikiwa kwa mpango wa wokovu. PLK 28.1
Kwa unyenyekevu na huzuni isiyoweza kuelezeka Adamu na Hawa waliondoka katika bustani ya kupendeza ambamo walikuwa na furaha hadi pale walipokosa kutii agizo la Mungu. Hali ilikuwa imebadilika. Haikuwa ile isiyobadilika, kama ilivyokuwa kabla ya dhambi. Mungu aliwavisha mavazi ya ngozi ili kuwakinga kutokana na kuhisi hali ya baridi na joto ambayo sasa wanakabiliana nayo. PLK 28.2
Sheria ya Mungu Isiyobadilika-Mbingu yote iliomboleza kwa sababu ya kutokutii na anguko la Adamu na Hawa, ambako kulileta ghadhabu ya Mungu juu ya jamii yote ya wanadamu. Waliondolewa katika ushirika na Mungu na kutumbukizwa katika hali ya huzuni isiyo na matumaini. PLK 28.3
Sheria ya Yehova, ambayo ni msingi wa serikali yake mbinguni na duniani, ilikuwa takatifu kama yeye mwenyewe alivyo mtakatifu, na kwa sababu hii Mungu asingeweza kukubali maisha ya malaika kuwa kama kafara kwa ajili ya kuvunjwa kwake. Sheria yake ni muhimu zaidi machoni pake kuliko malaika watakatifu wanaokizunguka kiti chake cha enzi. Baba asingeweza kuondoa au kugeuza hata agizo moja la sheria yake ili kuwasaidia wanadamu katika hali yao ya kuanguka. Lakini Mwana wa Mungu, ambaye pamoja na Baba waliwaumba, angeweza kufanya fidia kwa ajili yao ambayo ingekubalika na Mungu, kwa kutoa maisha yake kuwa kafara na kubeba ghadhabu ya Baba yake. Malaika walimwambia Adamu kuwa, kama dhambi yake ilivyoleta mauti na umaskini, kafara ya Kristo ingeleta nuruni maisha na kutokufa. PLK 28.4
Mwonekano wa Siku za Usoni- Mungu alifunua kwa Adamu mambo muhimu ya siku za usoni, kuanzia kufukuzwa kwake Edeni hadi Gharika, na kuendelea mbele kufikia ujio wa kwanza wa Kristo duniani. Upendo wake kwa Adamu na uzao wake wote ungemfanya Mwana wa Mungu kushuka chini na kuchukua asili ya mwanadamu, na hivyo, kupitia kuaibishwa kwake yeye mwenyewe, apate kuwainua wote ambao wangemwamini. Kafara ya jinsi hiyo ilikuwa na thamani ya kutosha kuokoa dunia nzima. Lakini ni wachache tu ambao wangekubali kuupokea wokovu ulioletwa kwao kupitia kafara ya ajabu kiasi kile. Walio wengi wasingetii masharti yaliyohitajika kwao ili wapate kupokea wokovu wake mkuu. Wangependelea dhambi na uvunjaji wa sheria ya Mungu kuliko toba na utii, huku wakitegemea kwa njia ya imani katika ustahili wa kafara iliyotolewa. Kafara hii ilikuwa ni ya thamani kubwa isiyopimika ya kutosha kumfanya mtu ye yote anayeikubali kuwa wa thamani kubwa kuliko dhahabu safi. PLK 29.1
Dhabihu ya Kafara-Wakati Adamu alipotoa dhabihu ya dhambi kutokana na maelekezo maalumu ya Mungu, ilikuwa ni utaratibu wa ibada wa kuhuzunisha mno kwake. Mkono wake lazima uondoe uhai, ambao Mungu peke yake angeweza kuuweka, na kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushuhudia kifo. Alimwangalia mnyama anayechuruzika damu, akitapatapa kwa maumivu makali ya kifo, alipaswa kutazamia kwa imani Mwana wa Mungu, ambaye mnyama huyu, alimwakilisha, ambaye ilibidi afe kama kafara ya wanadamu. PLK 29.2
Dhabihu hii inayofuata utaratibu maalumu, ambayo Mungu aliianzisha, ilikuwa iwe kumbusho la daima kwa Adamu kuhusu hatia yake, na pia ukubali wa toba na dhambi yake. Tendo hili la kuondoa uhai lilimpa Adamu utambuzi wa kina na mkamilifu zaidi wa dhambi yake, ambayo hakuna kitu pungufu ya damu ya Mwana wa Mungu ingeweza kuitakasa. Alistaajabia wema usio na kikomo na pendo lisilo kifani ambalo lingeweza kutoa fidia ya jinsi hiyo ili kumwokoa mhalifu. Adamu alipokuwa anamchinja yule mnyama asiye na hatia, ilionekana kwake kama vile alikuwa akimwaga damu ya Mwana wa Mungu kwa mkono wake mwenyewe. Alifahamu kuwa iwapo angedumu kuwa mkweli kwa Mungu na kwa sheria yake takatifu, kusingekuwapo na kifo cha mnyama au mwanadamu. Lakini bado katika dhabihu ya kafara, ambayo ilikuwa ikielekeza kwa dhabihu ya Mungu 88iliyo kuu na kamilifu ya Mwana wa Mungu mwenyewe, ilionekana nyota ya matumaini ya kumulika katika siku za usoni zenye giza na za kutisha, na kuleta ahueni kwa hali yake ya kukosa matumaini kabisa na kuangamia. PLK 29.3
Hapo mwanzo kiongozi wa kila familia alichukuliwa kuwa ndiye mtawala na kuhani wa nyumba yake mwenyewe. Baadaye, jamii ya wanadamu ilipoongezeka juu ya nchi, watu walioteuliwa na Mungu walifanya ibada hii makini ya kutoa kafara kwa ajili ya watu. Akili za wenye dhambi ilibidi zihusishe damu ya wanyama na damu ya Mwana wa Mungu. Kifo cha mnyama wa kafara kilikuwa kitoe ushahidi kwa wote kuwa adhabu ya dhambi ni mauti. Kwa tendo la kafara, wenye dhambi walikubali hatia zao na kuonesha imani zao, wakiitazamia kafara iliyo kuu na kamilifu ya Mwana wa Mungu. ambaye vifo vya wanyama vilimwakilisha. Pasipo upatanisho wa Mwana wa Mungu pasingelikuwapo na utoaji wa baraka au wokovu kutoka kwa Mungu kuja kwa wenye dhambi. Mungu alikuwa makini katika kudumisha heshima ya sheria yake. Ukiukaji wa sheria ile ulisababisha utengano wa kutisha baina ya Mungu na wenye dhambi. Mungu aliruhusu Adamu katika hali yake bila dhambi kuwa na mawasiliano huru, ya moja kwa moja, na yenye kufurahisha na Muumba wake. Baada ya dhambi yake Mungu angewasiliana na wanadamu kupitia kwa Kristo na malaika. PLK 30.1