Sura imejengwa katika Kutoka 5-15.
Mungu siku zote ana watu wake, hata wanapozidiwa 1VI idadi kwa mbali na wale wanaomwasi. Kwa mfano, watu wanane peke yake-Nuhu na familia yake- waliingia ndani ya safina ambayo Mungu alimwagiza Nuhu kuijenga kama kimbilio kutoka katika Gharika. Henoko alitembea na Mungu katika kipindi ambacho sehemu kubwa ya watu walikuwa waovu. Mungu alimwita Ibrahimu kuacha nchi yake ya asili na kwenda Kanaani. Uzao wake uliokuja kujulikana kama Waisraeli, waliishi pale hadi njaa ilipowapeleka Misri, ambapo baadaye walifanywa kuwa watumwa. Hapa kuna kisa cha ajabu juu ya jinsi Mungu alivyowaokoa wale waliokuwa wanaishi chiniya utumwa wa Wamisri zaidi ya miaka elfu moja kabla ya Kristo . PLK 32.1
Kwa miaka mingi wana wa Israeli walikuwa chini ya utumwa wa Wamisri. Ni familia chache tu waliingia Misri, lakini waliongezeka na kuwa umati mkubwa. Na huku wakiwa wamezungukwa na ibada za sanamu, wengi wao walipoteza ufahamu wa Mungu wa kweli na walisahau sheria yake. Na walijiunga na Wamisri katika ibada zao za jua, mwezi, na nyota, na za wanyama na sanamu, kazi za mikono ya wanadamu. PLK 32.2
Lakini bado miongoni mwa Waebrania walikuwapo baadhi waliohifadhi ufahamu wa Mungu wa kweli, Muumbaji wa mbingu na wa dunia. Wale waaminifu walihuzunika, na katika dhiki zao walimlilia Bwana kwa ajili ya ukombozi kutoka katika utumwa wa Wamisri, ili apate kuwatoa kutoka Misri, ambapo wangeachana na ibada ya sanamu na mivuto inayoshawishi kutenda mabaya iliyokuwa ikiwazunguka kila upande. PLK 32.3
Ingawa wengi wa Waisraeli walikuwa wamekwisha kupotoshwa na ibada ya sanamu, wale waliokuwa waaminifu walisimama imara. Hawakuwa wameficha imani yao, bali kwa uwazi waliwathibitishia Wamisri kuwa walikuwa wanamtumikia Mungu pekee wa kweli na aliye hai. Walirudiarudia ushahidi wa kuwapo kwa Mungu na uwezo wake tangu uumbaji na kuendelea mbele. Wamisri walikuwa na fursa ya kuijua imani ya Waebrania pamoja na Mungu wao. Walikuwa wamejaribu kudhoofisha imani ya wale waliomwabudu Mungu wa kweli kwa uaminifu, na waliudhika kwa vile hawakufanikiwa kwa kutumia vitisho, ahadi ya zawadi, au kwa kuwatendea ukatili. PLK 33.1
Wafalme wawili wa mwisho ambao walikalia kiti cha enzi cha Misri walikuwa ni wakatili ambao waliwatendea Waebrania kwa ukatili. Wazee wa Israeli walijaribu kuinua imani iliyokuwa ikididimia ya Waisraeli kwa kuwakumbusha kuhusu ahadi ya Mungu aliyoitoa kwa Ibrahimu na maneno ya Yusufu ya kiunabii mara tu kabla hajafa, yakitabiri kukombolewa kwao kutoka Misri. Baadhi walisikiliza na kuamini. Wengine waliangalia hali zao binafsi za kusikitisha, na hawakuweza kuwa na tumaini. PLK 33.2
Farao alijivuna kwamba angetaka kuona huyo Mungu wao akiwaokoa kutoka katika mikono yake. Maneno haya yalivunja kabisa matumaini ya Waisraeli wengi. Hali ilielekea kuwa kama vile mfalme pamoja na washauri wao walivyosema. Walijua kuwa walikuwa wanatendewa kama watumwa na kwamba lazima wastahimili kila kiwango cha uonevu ambao wasimamizi na watawala wao wangeweka juu yao. Watoto wao wa kiume waliwindwa na kuuawa. Maisha yao wenyewe yalikuwa ni mzigo, na wakati huo wakimwamini, na kumwabudu, Mungu wa mbinguni. PLK 33.3
Ndipo wakalinganisha hali yao na ile ya Wamisri ambao hawakumwamini kabisa Mungu aliye hai mwenye uwezo wa kuokoa au kuangamiza. Baadhi yao waliabudu sanamu, sanamu zilizotengenezwa kwa mbao na mawe, wakati ambapo wengine walichagua kuabudu jua, mwezi, na nyota. Lakini bado walikuwa wamestawi na kuwa matajiri. Na baadhi ya Waebrania waliwaza kwamba iwapo Mungu alikuwa juu ya miungu yote asingewaacha jinsi hii wakiwa kama watumwa kwa taifa la waabudu sanamu. PLK 33.4
Muda ulikuwa umewadia wa Mungu kujibu maombi ya watu wake walioonewa na kuwatoa Misri kwa udhihirisho mkuu wa nguvu zake ili kwamba Wamisri wakiri kwamba Mungu wa Waebrania, ambaye walimdharau alikuwa juu ya miungu yote. Mungu angelitukuza jina lake mwenyewe, ili mataifa mengine wapate kusikia kuhusu uwezo wake na kutetemeka kwa ajili ya matendo yake makuu, na ili kwamba watu wake, kwa kushuhudia kazi zake za kimiujiza, wageuke kikamilifu kutoka katika ibada zao za sanamu na kumfanyia ibada safi. PLK 34.1
Katika kuwakomboa Waisraeli kutoka Misri, Mungu aliwaonesha wazi Wamisri wote rehema zake maalumu kwa ajili ya watu wake. Maadamu Farao asingeweza kuthibitishiwa kwa njia nyingine yo yote ile, Mungu aliona kuwa ni sawa kutekeleza hukumu zake juu yake, ili apate kufahamu kupitia uzoefu wa kuhuzunisha kuwa uwezo wa Mungu ulikuwa ni bora juu ya yote. Angetoa uthibitisho wa wazi usiopingika kwa mataifa yote kuhusu uwezo na haki yake takatifu, ili jina lake lipate kutangazwa katika dunia yote. Mungu alikusudia kuwa udhihirisho huu wa nguvu ungeimarisha imani za watu wake, na kwamba uzao wao wangemwabudu kwa uaminifu yeye peke yake aliyefanya matendo ya rehema kiasi hicho kwa ajili yao. PLK 34.2
Baada ya amri ya Farao iliyowataka watu kutengeneza matofali bila kupewa majani, Musa alimwambia kuwa Mungu, ambaye alijifanya kutokumfahamu, angemlazimisha kusalimu amri kwa madai yake na kukiri mamlaka yake kama Mtawala mkuu kuliko wote. PLK 34.3
Mapigo-Miujiza ya kuigeuza fimbo kuwa nyoka na mto kuwa damu haikubadilisha moyo mgumu wa Farao kumfanya aruhusu Israeli kuondoka, bali ulizidisha tu chuki yake kwa Waisraeli. Kazi za waganga wake zilimfanya aamini kuwa Musa alikuwa ametenda miujiza hii kwa kutumia uganga. Hata hivyo, wakati pigo la vyura lilipotolewa, alikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba mambo hayakuwa hivyo. Mungu angeweza kuwasababisha watoweke na kurudi kwenye mavumbi katika muda mfupi sana, lakini hakufanya hili, ili kwamba watakapoondolewa, mfalme na Wamisri wasiweza kusema kuwa ilikuwa ni matokeo ya uchawi, kama vile kazi ya waganga. Vyura walikufa, na kisha watu wakawakusanya pamoja katika malundo. Waliona miili ya vyura iliyokuwa ikioza mbele yao, ambayo ilikuwa inachafua hewa. Hapa mfalme yule pamoja na Misri yote walipata ushahidi ambao falsafa yao isiyo na maana isingeweza kuelezea, kwamba kazi hii haikuwa ya kichawi bali ni hukumu ya Mungu wa mbinguni. PLK 35.1
Waganga wale wasingeweza kutengeneza chawa, ambao walitumika kama pigo lililofuata. Mungu asingeruhusu wafanye ionekane hata kwao au kwa watu wa Misri kwamba wangeweza kusababisha pigo la chawa. Aliondoa kila udhuru ambao Farao angeweza kuwa nao kama sababu ya kutokuamini kwake. Aliwalazimisha hata waganga wenyewe kutamka, “Jambo hili ni chanda cha Mungu.” PLK 35.2
Baadaye lilifuatia pigo la makundi ya inzi. Hawakuwa inzi kama hawa ambao bila kudhuru wanatusumbua wakati wa majira fulani ya mwaka. Kwa usahihi zaidi, mainzi ambao Mungu aliwaleta juu ya Misri walikuwa wakubwa na wenye sumu. Kuuma kwao kulikuwa kunaleta maumivu makali kwa wanadamu na wanyama pia. Mungu aliwatenga watu wake kutoka kwa Wamisri na hakuruhusu inzi hata mmoja kutokea katika maeneo yao yote. PLK 35.3
Kisha Bwana akatuma pigo la ugonjwa kwa wanyama wao, wakati huo huo akiwahifadhi wanyama wa Waebrania, kiasi kwamba hakufa hata mmoja wao. Lilifuatia pigo la majipu kwa watu na wanyama pia, na waganga hawakuweza hata kujikinga wao wenyewe dhidi yake. Kisha Bwana akatuma juu ya Misri pigo la mvua ya mawe iliyochanganyika na moto, pamoja na radinangurumo. Mudawakilapigoulitolewakablapigo halijaja, ili kwamba mtu ye yote asije akasema kwamba lilitokea kwa bahati tu. Bwana alidhihirisha kwa Wamisri kwamba dunia yote ilikuwa chini ya utawala wa Mungu wa Waebrania-kwamba radi, mvua ya mawe, na tufani vyote vinatii sauti yake. Farao, mfalme mwenye kiburi ambaye hapo awali aliuliza, “Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake?” alijinyenyekesha na kusema, “Mimi nimekosa ... Bwana ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu.” Alimwomba Musa kuwa mpatanishi wake na Mungu, ili asimamishe ile ngurumo na radi ya kutisha. Kisha Bwana alituma pigo la kuogofya la nzige. Mfalme aliamua ni heri kupokea mapigo kuliko kumtii Mungu na kuruhusu Waisraeli kuondoka Misri. Bila kujuta aliuongoza ufalme wake wote kupitia miujiza ya hukumu hizi za kutisha. Ndipo Bwana akatuma giza juu ya Misri. Sio tu kwamba watu walinyang’anywa nuru, bali angahewa ilikuwa ni nzito sana, kiasi kwamba upumuaji ulikuwa mgumu. Waebrania, hata hivyo, walikuwa na angahewa safi na nuru katika maskani yao. PLK 36.1
Mungu alileta pigo moja zaidi la kutisha juu ya Misri, kali kuliko lo lote lililotangulia kabla yake. Ilikuwa ni mfalme pamoja na makuhani wa ibada za sanamu waliokataa hadi mwisho ombi la Musa. PLK 36.2
Watu walitaka Waebrania waruhusiwe kuondoka Misri. Musa alimwonya Farao na watu wa Misri, na Waisraeli pia, kuhusu namna na matokeo ya pigo la mwisho-mzaliwa wa kwanza wa kila nyumba angekufa. Katika usiku ule, wa kutisha mno kwa Wamisri na wa kufurahisha sana kwa watu wa Mungu, sikukuu ya ibada ya pasaka ilianzishwa. PLK 36.3
Ilikuwa ni vigumu sana kwa mfalme wa Misri na watu wenye kiburi na waabudu sanamu kukubali masharti ya Mungu wa mbinguni. Pigo baada ya pigo lilikuja juu ya Misri, na mfalme hakukubali kushindwa hadi alipolazimishwa kwa kuadhibiwa na ghadhabu ya Mungu ya kutisha. PLK 37.1
Kila pigo lilikuja kwa karibu sana na kila moja likiwa kali zaidi kuliko lililopita, na sasa hili lingekuwa la kutisha kuliko lo lote lililotangulia kabla yake. Lakini mfalme mwenye kiburi alikasirika mno, na kukataa kujinyenyekesha. Na Wamisri walipoona matayarisho makuu yakifanywa miongoni mwa Waisraeli kwa ajili ya usiku ule wa kutisha, walidhihaki ile ishara ya damu iliyonyunyizwa kwenye miimo ya milango ya Waisraeli. PLK 37.2
Waisraeli walifuata maelekezo ambayo Mungu aliwapa, na wakati malaika wa mauti alipokuwa akipita kutoka nyumba hadi nyumba miongoni mwa Wamisri, wote walikuwa tayari kwa kuanza safari yao na walikuwa wakingoja tu yule mfalme mkaidi pamoja na watu wake kuwaambia waondoke. PLK 37.3
“Hata ikawa usiku wa manane Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu.” PLK 37.4
“Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, ‘Ondo- keni, tokeni katika watu wangu, ninyi wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni Bwana kama mlivyosema. Twaeni kondoo zenu na ng’ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia.’ Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, ‘Tumekwisha kufa sote.’ PLK 37.5
“Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. Bwana akawajalia kukubaliwa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara.” PLK 38.1
Bwana alidhihirisha hili kwa Ibrahimu karibu miaka mia nne kabla halijatimizwa: “Bwana akamwambia Abramu, ‘Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.’ ” Mwanzo 15:13, 14. PLK 38.2
“Na kundi kubwa la watu waliochangamana nao wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng’ombe, wanyama wengi sana.” Wana wa Israeli walitoka Misri wakiwa na mali zao, ambazo hazikuwa za Farao, kwa kuwa kamwe hawakuwa wameziuza kwake. Yakobo na wana wake waliingia Misri wakiwa na kondoo na ng’ombe wao. Waisraeli walikuwa wameongezeka mno kwa idadi, na kondoo na ng’ombe wao waliongezeka sana. Mungu aliwahukumu Wamisri kwa kupeleka mapigo juu yao, na aliwafanya wawaharakishe watu wake watoke nje ya Misri wakiwa na mali yote waliyomiliki. PLK 38.3
Nguzo ya Moto-“Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa. Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.” PLK 38.4
Baada ya siku kadhaa tangu Waisraeli wameondoka Misri, Wamisri walimwambia Farao kuwa walikuwa wamekimbia na kamwe wasingerudi tena kumtumikia. Na walisikitika kwa kuwa waliwaruhusu kuondoka Misri. Ilikuwa ni hasara kubwa mno kwa kuondolewa huduma ya Waisraeli, na walijuta kuwa walikubali kuwaruhusu waende. Bila kujali maumivu yote waliyoyapata katika hukumu za Mungu, walishupazwa mioyo mno kutokana na ukaidi wao wa kudumu kiasi kwamba waliamua kuwafuatilia Waisraeli ili kuwarejesha Misri kwa nguvu. Mfalme alichukua jeshi kubwa sana na magari ya vita mia sita, na kuwafuatilia, na kuwafikia walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari. PLK 39.1
“Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. Wakamwambia Musa, ‘Je! kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, “Tuache tuwatumikie Wamisri?” Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani’ “Musa akawaambia watu, ‘Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.’” PLK 39.2
Wokovu katika bahari ya Shamu-“Bwana aka- mwambia Musa, ‘Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya, nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.’” Mungu alitaka Musa aelewe kuwa yeye Mungu angefanya kazi kwa ajili ya watu wake-kwamba hitaji lao kwake lingekuwa ni fursa. Walipokuwa wamekwenda mbali kiasi walichoweza, Musa bado analazimika kuwaambia wasonge mbele. Inabidi atumie fimbo ambayo Mungu alimpa kupasua maji. PLK 39.3
“Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.” “Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli; akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; ikafika kati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha.” PLK 40.1
Wamisri hawakuweza kuwaona Waebrania, kwa sababu wingu la giza nene lilikuwa mbele yao-wingu ambalo kwa Waisraeli lilikuwa ni nuru tele. Kwa jinsi hii Mungu alionesha uwezo wake wa kuwajaribu watu wake, iwapo wangeweza kumwamini baada ya kuwa amewapa ushahidi wa jinsi ile wa uangalizi na upendo wake kwao, na kukemea kutokuamini na kulalamika kwao. “Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto.” Maji yaliinuka na kusimama katika pande zote mbili kama kuta zilizogandishwa, wakati Israeli alipotembea katika ardhi kavu katikati ya bahari. PLK 40.2
Jeshi la Misri lilikuwa likisheherekea usiku ule kuwa Waisraeli tena walikuwa katika mamlaka yao. Walidhani kuwa hakukuwa na uwezekano wo wote wa kuponyoka, kwa kuwa mbele ya Waisraeli Bahari ya Shamu ilitanda, na jeshi kubwa la Misri lilikuwa karibu nyuma yao. Asubuhi, walipokuja baharini na kuangalia, tazama kulikuwako na njia kavu, maji yalikuwa yamegawanyika, yakisimama kama ukuta pande zote mbili, na watu wa Israeli walikuwa nusu mwendo kuvuka bahari, huku wakitembea kwenye ardhi kavu. Wamisri walingoja kidogo wakisubiri kuamua kitu gani cha kufanya baada ya hapo. Walikatishwa tamaa na kukasirishwa kwamba wakati ambapo walikuwa karibu kuwarejesha Waisraeli chini ya mamlaka yao, wakiwa na uhakika wa kuwateka, njia ambayo haikutegemewa inafunguka kwa ajili yao katika bahari. Waliamua kuwafuatilia. PLK 41.1
“Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, ‘Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, dhidi ya Wamisri.’” PLK 41.2
Wamisri walithubutu kupita katika njia ambayo Mungu aliitayarisha kwa ajili ya watu wake, na malaika wa Mungu walipita katikati ya jeshi lao na kuondoa magurudumu ya magari yao. Walisumbuka. Kusonga kwao kulikuwa taratibu mno, nao wakaanza kuwa na wasiwasi. Wakakumbuka hukumu ambazo Mungu wa Waebrania alikuwa ameleta juu yao kule Misri kuwalazimisha wamruhusu Israeli aende zake, na walifikiri kwamba Mungu angeweza kuwaweka wote katika mikono ya Waisraeli. Walitambua kuwa Mungu alikuwa akiwapigania Waisraeli, na wakaogopa mno na kuanza kugeuka nyuma ili kuwakimbia, wakati ambapo “Bwana akamwambia Musa, ‘Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao.’” PLK 41.3
“Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana akawafutilia mbali hao Wamisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja. Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.” PLK 42.1
“Ndivyo Bwana alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni mwa bahari wamekufa.” PLK 42.2
Waisraeli waliposhuhudia kazi ya ajabu ya Mungu katika maangamizo ya Wamisri, walijiunga katika wimbo wa shangwe wenye maneno ya kushawishi mno na sifa za shukrani. PLK 42.3