Shetani alimdanganya Yuda na kumwongoza kufikiri kuwa alikuwa mmoja wa wanafunzi wa kweli wa Kristo, lakini moyo wake daima ulikuwa umejawa na mambo ya kimwili. Alikuwa ameona matendo makuu ya Yesu, alikuwa pamoja naye katika huduma yake, na aliukubali ushahidi mkubwa kuwa alikuwa ndiye Masihi, lakini Yuda alikuwa ni mchoyo na mwenye tamaa. Alipenda fedha. Alilalamika kwa hasira kuhusu kibweta cha thamani cha marhamu ambacho Mariamu alimimina juu ya Yesu. PLK 70.1
Mariamu alimpenda Bwana. Alikuwa amemsa- mehe dhambi zake, zilizokuwa nyingi, na alikuwa amemfufua kutoka wafu ndugu yake mpendwa mno, na alijisikia kuwa hakukuwa na kitu kilicho-kuwa cha thamani sana cha kuweza kumpa Yesu. Kadiri thamani kubwa iliyokuwa nayo ile marhamu, ndivyo ambavyo ingempendeza zaidi kuonesha shukrani zake kwa Mwokozi wake kwa kuitoa kwake. PLK 70.2
Kama udhuru kwa uroho wake, Yuda alisisitiza kuwa mafuta yale yangeuzwa na kutolewa kwa maskini. Lakini haikuwa ni kwa sababu alikuwa anawajali maskini kwa namna yo yote ile. Alikuwa ni mbinafsi, na mara nyingi alichukua kwa ajili ya matumizi yake binafsi fedha zilizowekwa chini ya ulinzi wake ili zipate kutolewa kwa maskini. Yuda hakujali kuhusu hali njema ya Yesu na hata mahitaji yake, na ili kutoa udhuru kwa tamaa zake mara kwa mara alirejea kwa maskini. Tendo la Mariamu la ukarimu lilikuwa ni karipio kali mno kwa tabia yake ya tamaa. Hali hii iliandaa njia kwa ajili ya jaribu la Shetani kupata ukaribisho wa moja kwa moja moyoni mwa Yuda. PLK 70.3
Makuhani na wakuu wa Wayahudi walimchukia Yesu, lakini makusanyiko makubwa yalisongamana ili kusikiliza maneno yake ya hekima na kushuhudia kazi zake kuu. Watu walisisimka kwa mvuto mkubwa na kwa shauku walimfuata Yesu ili kusikia mafundisho ya Mwalimu huyu wa ajabu. Wengi wa wakuu walimwamini, lakini hawakuthubutu kukiri imani yao kwa hofu ya kutengwa na sinagogi. Makuhani na wazee waliamua kuwa jambo fulani lazima lifanyike ili kutoa usikivu wa watu kutoka kwa Yesu. Walihofu kuwa kila mtu angemwamini. Hawakuweza kuona usalama wo wote kwa ajili yao wenyewe. Ni kwamba lazima wapoteze nafasi yao au wamwue Yesu. Na kwamba hata baada ya kumwua, bado kutakuwapo na wale ambao ni kumbusho hai la uweza wake. PLK 71.1
Yesu alimfufua Lazaro kutoka mautini, na walihofu kuwa ikiwa wangelazimika kumwua Yesu, Lazaro angetoa ushahidi wa uweza wake mkuu. Watu walikuwa wanakusanyika kwa wingi ili kumwona mtu huyu aliyefufuliwa kutoka mautini, na watawala walidhamiria kumwua Lazaro pia na kukomesha msisimko ule. Ndipo wangeweza kuwageuza watu kuangalia mapokeo na mafiindisho ya kibinadamu, kulipa zaka za mnanaa na bizari na jira, na hivyo kuwa tena na mamlaka juu yao. Walikubaliana kumkamata Yesu akiwa peke yake, kwa sababu iwapo wangejaribu kumchukua kutoka katika umati wakati ambapo akili za watu wote zilimfurahia, wangeweza kupigwa kwa mawe. PLK 71.2
Yuda alifahamu jinsi walivyokuwa na shauku ya kumpata Yesu, na alijitoa kumsaliti kwa kuhani mkuu na wazee kwa kulipwa vipande vichache vya fedha. Mapenzi yake kwa fedha yalimwongoza kukubali kumsaliti Bwana wake katika mikono ya maadui zake wenye uchungu naye kuliko wote. Shetani alikuwa akifanya kazi moja kwa moja kupitia kwa Yuda, na katikati ya mandhari ya kuvutia ajabu ya chakula cha mwisho msaliti huyu alikuwa akifanya mipango ya kumsaliti Bwana wake. Yesu kwa huzuni aliwaambia wanafunzi wake kuwa wote wangechukizwa katika usiku ule kwa sababu yake. Lakini Petro alithibitisha kwa nguvu kwamba hata kama wengine wote wangechukizwa kwa sababu yake [Yesu], yeye asingechukizwa. Yesu akamwambia Petro, “Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” Luka 22:31,32. PLK 71.3
Katika Bustani -Yesu alikuwa katika bustani ya Gethsemane pamoja na wanafunzi wake. Kwa huzuni kuu aliwaambia kukesha na kuomba, ili wasije wakaingia majaribuni. Alifahamu kuwa imani yao ingejaribiwa na matumaini yao kukatishwa tamaa, na kwamba wangehitaji nguvu zote ambazo wangezipata kwa kukesha kwa bidii na maombi ya dhati. Kwa kulia na kuomboleza kwa nguvu, Yesu aliomba, “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Luka 22:42. Mwana wa Mungu aliomba kwa uchungu mkuu. Matone makubwa ya damu yalijikusanya katika uso wake na kuanguka ardhini. Malaika walikuwa wakirukaruka juu ya mahali hapa, wakilitazama tukio lile, lakini ni mmoja tu aliagizwa kwenda kumtia nguvu Mwana wa Mungu katika maumivu yake makubwa. PLK 72.1
Baada ya Yesu kuomba alikuja kwa wanafunzi wake, lakini walikuwa wamelala. Katika saa ile ya kutisha hakupata huruma na maombi hata ya wanafunzi wake. Petro, ambaye katika muda mfupi tu uliopita alikuwa na moyo sana, sasa alikuwa katika usingizi mzito. Yesu alimkumbusha kuhusu matamko yake yaliyokuwa chanya na kumwambia, “Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?” Mathayo 26:40. Mara tatu Mwana wa Mungu aliomba kwa uchungu. PLK 72.2
Yuda Amsaliti Yesu-Ndipo Yuda alipofika pamoja na kundi la watu wenye silaha. Alimsogelea Bwana wake kama kawaida, ili kumsalimu. Kundi lile lenye silaha kikamzunguka Yesu, lakini pale alionesha uweza wake wa kiungu, aliposema, “Ni nani mnayemtafuta?” “Ni mimi.” Walirudi nyuma na kuanguka chini. Yesu aliuliza swali hili ili wapate kushuhudia uweza wake na kuwa na ushahidi kuwa angeweza kujiokoa yeye mwenyewe kutoka katika mikono yao kama angependa. PLK 73.1
Wanafunzi walianza kuwa na matumaini walipo waona umati ule kwa haraka wakianguka chini wakiwa na marungu na mapanga yao. Walipoamka na kumzunguka tena Mwana wa Mungu, Petro alivuta upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, na kuondoa sikio lake. Yesu alimwamuru kuweka panga lake pembeni, akisema, “Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?” Mathayo 26:53. Aliponena maneno haya, nyuso za malaika zilichangamshwa kwa matumaini. Walitaka kumzunguka Jemadari wao mara moja mahali pale na kuutawanya umati ule wenye hasira. Lakini tena huzuni ilitua juu yao, pale Yesu alipoongeza kwa kusema, “Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?” Mathayo 26:54. Mioyo ya wanafunzi pia ilizama kwa kukata tamaa na masikitiko ya uchungu pale Yesu mwenyewe aliporuhusu aongozwe na maadui zake kwenda zao. PLK 73.2
Wanafunzi walihofia maisha yao wenyewe, na wote walimwacha na kukimbia. Yesu aliachwa peke yake katika mikono ya umati wa watu katili. Ni ushindi ulioje kwa Shetani! Na ni sikitiko la jinsi gani miongoni mwa malaika wa Mungu! Makundi mengi ya malaika watakatifu, kila kundi likiwa na malaika mmoja mrefu mwenye kuwaamrisha kama kiongozi wao, walitumwa kushuhudia tukio lile. Walitakiwa kuandika kila tusi na ukatili uliowekwa juu ya Mwana wa Mungu, na kuorodhesha kila uchungu wa maumivu makali ambayo Yesu angeyapitia, kwa kuwa watu wale wale waliojiunga katika tukio hili la kutisha wataliona tena katika onesho kama la maisha halisi. PLK 73.3