Sura ya 9—Ushindi
Ufufuo
Wanafunzi walipumzika siku ya Sabato, wakiomboleza kifo cha Bwana wao, wakati ambapo Yesu, mfalme wa utukufu, alilala kaburini. Usiku ulipokuwa unajongea, askari waliwekwa ili kulinda mahali pa pumziko la Mwokozi, wakati ambapo malaika waliruka bila kuonekana juu ya mahali hapa patakatifu. Usiku uliendelea kuisha taratibu, na wakati kungali giza malaika waliokuwa wakilinda walijua kuwa wakati ulikuwa umekaribia wa kufunguliwa kwa Mwana wa Mungu, Amiri jeshi wao mpendwa. Walipokuwa wakisubiri kwa shauku kubwa saa ile ya ushindi wake, malaika mwenye nguvu alikuja akiruka kwa kasi kutoka mbinguni. Uso wake ulikuwa kama radi, na mavazi yake meupe kama theluji. Nuru yake ilifukuza giza katika njia yake na kusababisha malaika waovu, ambao walikuwa wamedai kwa ushindi kuumiliki mwili wa Yesu, wakimbie kwa hofu kutoka katika mng’ao na utukufu wake. Mmoja wa malaika kutoka mbinguni ambaye alishuhudia tukio la kunyanyaswa kwa Kristo na alikuwa akiangalia mahali pale pa pumziko alijiunga na malaika kutoka mbinguni, na kwa pamoja walishuka chini hadi kwenye kaburi. Nchi ilitetemeka na kutikisika waliposogea karibu, na palitokea tetemeko kuu.PLK 91.1
Hofu iliwaingia walinzi wa Kirumi. U wapi sasa uwezo wao wa kuulinda mwili wa Yesu? Hawakufikiri juu ya wajibu wao au juu ya wanafunzi kuuiba mwili wake. Wakati nuru ya malaika ilipomulika kuwazunguka, angavu kuliko jua, kundi lile la ulinzi la Kirumi walianguka chini ardhini kama wafu. Malaika mmoja alilishika lile jiwe kubwa na kuliviringisha mbali kutoka katika mlango wa kaburi, na akakaa juu yake. Mwingine yule aliingia ndani ya kaburi na kufungua sanda kutoka katika kichwa cha Yesu.PLK 91.2
“Baba Yako Anakuita”-Ndipo kwa sauti iliyosababisha nchi kutetemeka, malaika yule aliyetoka mbinguni alilia kwa sauti kuu, “Ee Mwana wa Mungu, Baba yako anakuita! Toka nje!” Mauti hayakuweza kutawala juu yake tena. Yesu aliinuka kutoka katika wafu, akiwa mshindi. Kwa kicho makini malaika waliokusanyika waliangalia tukio lile. Na wakati Yesu alipokuwa akitoka nje ya kaburi, wale malaika wanaong’aa waliinama hadi nchi kwa ibada na kumsalimu kwa nyimbo za ushindi na shangwe.PLK 92.1
Taarifa ya Walinzi wa Kirumi-Jeshi la malaika wa mbinguni lilipoondoka kaburini na nuru pamoja na utukufu kutoweka, walinzi wa Kirumi walijaribu kuinua vichwa vyao na kuangalia-angalia. Walijazwa na mshangao walipoona kuwa lile jiwe kubwa lilikuwa limeviringishwa mbali kutoka katika mlango wa kaburi na kwamba mwili wa Yesu ulikuwa umeondoka. Walifanya haraka kuingia mjini ili kuwajulisha makuhani na wazee yale waliyoyaona. Wale wauaji waliposikia kisa cha kustaajabisha, nyuso zao wote zilibadilika. Hofu iliwapata kuhusu kile walichokuwa wamekitenda. Iwapo taarifa hii ni sahihi, basi wamekwisha. Kwa kitambo walikaa kimya, wakiangaliana, wasijue la kufanya au kusema. Kuikubali taarifa hii ingekuwa kujihukumu wao wenyewe. Walienda pembeni ili kushauriana kitu gani cha kufanya. Waliwaza kuwa iwapo taarifa ya askari hawa itaenea miongoni mwa watu, wale waliomwua Yesu watauawa kama wenye hatia ya mauaji.PLK 92.2
Waliamua kuwanunua askari hawa ili walifiche jambo hili kuwa siri. Makuhani na wazee waliwapa fedha nyingi, wakisema, “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.” Mathayo 28:13. Na pale askari hawa walipohoji vipi kitakachowatokea itakapogundulika kuwa walilala wakiwa kwenye lindo, maafisa wa Kiyahudi waliwaahidi kuwa watamsihi gavana na kuhakikisha usalama wao. Kwa ajili ya fedha askari wa Kirumi waliuza heshima yao na kukubali kufuata ushauri wa makuhani na wazee.PLK 92.3
Malimbuko ya Ukombozi-Wakati Yesu akiwa amening’inia msalabani, alisema kwa sauti kuu, “Imekwisha,” miamba ilipasuka, nchi ilitikisika, na baadhi ya makaburi yalifunguka. Alipoinuka kama mshindi juu ya mauti na kaburi, wakati dunia ilipokuwa ikisukwasukwa na utukufu wa mbinguni kumulika kuzunguka mahali pale patakatifu, wengi wa watakatifu waliokuwa wamekufa, kwa kuitii sauti yake, walitoka nje kutoka katika makaburi yao kama mashahidi kuwa alikuwa amefufuka. Watakatifu hawa waliofadhiliwa na kufufuliwa walifufuka katika hali ya utukufu. Walikuwa ni wateule kutoka katika kila kizazi, tangu uumbaji hata siku za Kristo. Hivyo wakati viongozi wa Kiyahudi walipokuwa wanatafuta kuficha ukweli kuhusu kufufuka kwa Kristo, Mungu aliamua kuwaleta jeshi kutoka makaburini ili kushuhudia kuwa Yesu alikuwa amefufuka, na kutangaza utukufu wake.PLK 93.1
Wale waliohuishwa baada ya kufufuka kwa Kristo waliwatokea watu wengi, wakiwaambia kuwa kafara kwa ajili ya wanadamu ilikamilishwa, kwamba Yesu, ambaye Wayahudi walimsulubisha, alikuwa amefufuka kutoka katika wafu. Ili kuthibitisha maneno yao walitangaza, “Tumefufuka pamoja naye.” Walishuhudia kuwa ilikuwa ni kwa sababu ya uweza wake mkuu wao waliitwa kutoka katika makaburi yao. Bila kujali ripoti ya uongo iliyokuwa inazunguka, kufufuka kwa Kristo kusingeweza kufichwa na Shetani, malaika zake, au makuhani wakuu, kwa sababu jeshi hili la watakatifu, waliotolewa kutoka katika makaburi yao, walieneza habari za ajabu na za furaha. Yesu pia alijionesha mwenyewe kwa wanafunzi wake wenye huzuni, na waliovunjika moyo, akifukuzilia mbali hofu zao na kuwasababishia furaha na shangwe.PLK 93.2
Wanawake Kaburini-Asubuhi na mapema ya siku ya kwanza ya juma, kabla hakujapambazuka, wanawake wacha Mungu walikuja kaburini wakileta manukato mazuri ili kuupaka mwili wa Yesu. Walikuta lile jiwe kubwa limeviringishwa kutoka katika mlango wa kaburi, na mwili wa Yesu haukuwamo mle. Mioyo yao ilisononeka, wakihofia kuwa maadui zao walikuwa wameuchukua mwili ule kutoka mle. Ghafla waliwaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, nyuso zao zikiwa changamfu na za kung’aa. Hawa viumbe wa mbinguni walifahamu kile ambacho wanawake hawa walikuja kutenda, na mara moja waliwaambia kuwa Yesu hakuwamo kaburini. Alikuwa amefufuka, lakini wangeweza kupaona pale alipokuwa amelala. Waliwaambia kuwa waende wakawaambie wanafunzi wake kuwa angewatangulia kwenda Galilaya. Kwa hofu na furaha kuu, wanawake wale waliharakisha kurudi kwa wanafunzi wenye huzuni na kuwaeleza mambo waliyoyaona na kusikia.PLK 94.1
Wanafunzi hawakuweza kuamini kuwa Yesu alikuwa amefufuka, lakini walikimbia haraka kwenda kaburini, pamoja na wanawake wale walioleta habari hii. Walikuta kuwa Yesu hakuwamo mle. Waliona sanda yake ya kitani lakini hawakuweza kuiamini habari ile njema kwamba alikuwa amefufuka kutoka katika wafu. Walirudi nyumbani, wakishangaa juu ya kile walichokiona, na pia juu ya taarifa waliyoileta wanawake wale kwao.PLK 94.2
Lakini Mariamu aliamua.......... kubaki akizunguka zunguka pale kaburini, akitafakari kuhusu kile ambacho amekiona na kukisikia, akihuzunishwa na wazo kuwa inawezekana amedanganyika. Alihisi kuwa bado majaribio mengine yalikuwa yakimsubiria. Huzuni yake iliamshwa, na akaangua kilio kwa uchungu mno. Aliinama chini ili kuangalia tena ndani ya kaburi, na mle aliwaona malaika wawili wakiwa katika mavazi meupe. Mmoja alikaa mahali ambapo kichwa cha Yesu kilikuwa kimelazwa, na mwingine mahali ambapo miguu yake ilikuwa. Walizungumza naye kwa upole na kumwuliza kwa nini alikuwa analia. Alijibu, “Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.” Yohana 2:13.PLK 94.3
“Usining’ang’anie”-Alipogeuka kutoka kwenye kaburi alimwona Yesu amesimama karibu naye, lakini hakuweza kumtambua. Aliongea naye kwa upole, na kumwuliza kwa nini alikuwa na huzuni na kumwuliza ni nani alikuwa akimtafuta. Huku akidhani kuwa alikuwa akiongea na mtunza bustani, alimwuliza iwapo alikuwa amemchukua Bwana wake na kumpeleka kwingine, basi amwambie ni wapi alipomlaza ili apate kwenda kumchukua. Yesu aliongea naye kwa sauti yake ya kimbingu, akisema, “Mariamu!” Alifahamu toni ya sauti hii ya upendo na kwa haraka akajibu, “Bwana!” katika fiiraha yake alikaribia kumkumbatia, lakini Yesu alisema, “Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” Yohana 20:17. Kwa furaha aliharakisha kwenda kwa wanafunzi akiwa na habari njema. Yesu kwa haraka alipaa kwenda kwa Baba yake ili asikie kutoka katika kinywa chake kuwa alikuwa ameikubali kafara ile na kupokea mamlaka yote mbinguni na duniani.PLK 95.1
Wakati Yesu akiwa mbele ya Mungu na kuzungukwa na utukufu wake, hakuwasahau wanafunzi wake waliokuwa duniani. Alipokea mamlaka kutoka kwa Baba yake ili apate kurudi duniani na kuwapa mamlaka. Siku ile ile alirudi na kujionesha kwa wanafunzi wake. Ndipo alipowaruhusu kumshika, kwa kuwa alikuwa amekwisha kwenda kwa Baba yake na kupokea mamlaka.PLK 95.2
Tomaso Mwenye Mashaka -Wakati huu Tomaso hakuwako. Hakuweza kupokea taarifa ya wanafunzi wa Yesu kwa unyenyekevu, bali kwa uthabiti na kwa kujiamini alithibitisha kuwa asingeamini hadi aweke vidole vyake katika alama za misumari na mkono wake katika mbavu zake pale ambapo mkuki wa ukatili ulipenyezwa. Kwa jinsi hii alionesha upungufu wa imani kwa ndugu zake. Iwapo kila mmoja angehitaji ushahidi kama ule, hakungekuwako mtu leo wa kumpokea Yesu na kuamini kuhusu kufufuka kwake. Lakini ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kuwa wale ambao wasingeweza kwa wenyewe kumwona na kumsikia Mwokozi aliyefufuka wangeweza kupokea taarifa za wanafunzi wake.PLK 96.1
Mungu hakupendezwa na kutokuamini kwa Tomaso. Yesu alipokutana tena na wanafunzi wake, Tomaso alikuwa pamoja nao, na alipomwona Yesu, aliamini. Lakini alikuwa ametangaza kuwa asingeridhika pasipo ushahidi wa hisia kujumlishwa juu ya ule wa kuona, naye Yesu alimpatia ushahidi ule aliouhitaji. Tomaso alilia kwa sauti, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Lakini Yesu alimkemea kwa kutokuamini kwake, akisema, “Wewe kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.” Yohana 2:28, 29.PLK 96.2
Anguko la Wauaji wa Kristo-Habari zilipoenea kutoka mji mmoja hadi mwingine kutoka kijiji hadi kijiji kingine, viongozi wa Wayahudi walihofia maisha yao na hivyo kuficha chuki yao dhidi ya wanafunzi wa Yesu. Tegemeo pekee walilokuwa nalo ni kueneza taarifa yao ya uongo. Na wale waliodhani kuwa uongo huu ulikuwa ni kweli waliupokea. Pilato alitetemeka aliposikia kuwa Kristo alikuwa amefufuka. Hakuweza kutilia mashaka shuhuda zilizotolewa, na kuanzia pale amani ilimtoweka milele. Kwa sababu ya heshima ya kidunia, kwa hofu ya kupoteza mamlaka na maisha yake, alimhukumu Yesu kifo. Sasa alithibitishiwa kikamilifu kuwa hakuwa tu na hatia ya damu ya mtu asiye na makosa, bali ya Mwana wa Mungu. Maisha ya taabu na unyonge ndiyo yalikuwa ya Pilato hadi mwisho wake. Kukata tamaa na uchungu viliangamiza kila hisia ya tumaini na furaha. Alikataa kufarijiwa, na alikufa kifo cha shida kuliko vingine vyote.PLK 96.3
Siku Arubaini Pamoja na Wanafunzi-Alibaki pamoja na wanafunzi wake kwa siku arubaini, akiwajaza furaha na shangwe kadiri alivyowafunulia kwa ukamilifu zaidi uhalisi wa ufalme wa Mungu. Aliwaagiza kutoa ushuhuda juu ya mambo waliyoyaona na ^uyasikia kuhusu mateso, kifo, na ufufuo wake. Ilibidi waeleze kuwa alikuwa ametoa kafara kwa ajili ya dhambi, na kwamba wote wanaotaka wanaweza kuja kwake na kupata uzima. Kwa upole wa dhati aliwaambia kuwa wangeteswa na kupata dhiki, lakini wangepata msaada kwa kukumbu0ka uzoefu wao na maneno aliyowaambia. Aliwaambia kuwa aliyashinda majaribu ya Shetani na kwamba alipata ushindi kupitia katika mashitaka na mateso. Shetani asingekuwa na uwezo zaidi juu yake, bali kwamba atazidisha majaribu yake juu yao na juu ya wale watakaoliamini jina lake. Lakini wangeshinda kama yeye alivyoshinda. Yesu aliwapa uwezo wanafunzi wake wa kutenda miujiza, na aliwaambia kuwa ijapokuwa watateswa na watu waovu, mara kwa mara angewatuma malaika wake kuwaokoa; maisha yao yasingeondolewa hadi pale utume wao utakapokamilika. Ndipo wanaweza kuhitajika kutia muhuri kwa damu yao ushuhuda ule walioutoa.PLK 97.1
Wafuasi wake wenye dukuduku walisikiliza mafundisho yake kwa furaha, kwa shauku wakijilisha kwa kila neno lililotoka katika kinywa chake kitakatifu. Sasa walifahamu kwa hakika kuwa alikuwa ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Maneno yake yalizama katika mioyo yao, na walihuzunika kuwa ni ndani ya muda mfupi tu watalazimika kutengana na Mwalimu wao wa kimbingu na wasiweze tena kusikia maneno yake yenye kufariji na yenye neema. Lakini tena mioyo yao ilichangamshwa kwa upendo na furaha kuu, pale Yesu alipowaambia kuwa angeenda kuandaa makao kwa ajili yao na kuja tena kuwachukua, ili wapate kuwa pamoja naye siku zote. Pia aliahidi kumtuma Mfariji, Roho Mtakatifu, kuwaongoza katika ukweli wote. “Akainua mikono yake akawabariki.” Luka 24:50.PLK 97.2