Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Kutawazwa kwa Kristo

    Kisha Kristo anaonekana tena kwa maadui zake. Juu kabisa ya jiji lile, juu ya msingi wa dhahabu safi, kuna kiti cha enzi, kikiwa juu na kuinuliwa sana. Juu ya kiti hiki cha enzi ameketi Mwana wa Mungu, na kumzunguka ni raia wa ufalme wake. Hakuna lugha inayoweza kueleza uweza na ukuu wa Kristo; hakuna kalamu inayoweza kuandika ukuu wake. Utukufu wa Baba wa Milele unamfunika Mwana wake. Uangavu wa kuwapo kwake unalijaza jiji la Mungu na kuvuka hadi nje ya malango, ukiijaza dunia yote kwa mwangaza wake.PLK 140.2

    Karibu kabisa na kiti cha enzi wameketi wale ambao hapo awali walikuwa na bidii katika njia ya Shetani, lakini, ambao, walitolewa kama kinga kutoka katika moto, na kumfuata Mwokozi wao kwa upendo mkuu na wa kina. Waliofuatia ni wale waliokamilisha tabia ya Kikristo wakiwa katikati ya uongo na kutokuamini, wale walioiheshimu sheria ya Mungu wakati ulimwengu wa Kikristo ukisema kuwa ilikuwa imebatilika, pamoja na mamilioni wa zama zote, ambao waliuawa kwa ajili ya imani yao. Na nyuma yao kuna “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu; watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufunuo 7:9. Vita vyao vimekwisha, ushindi wao umepatikana. Wamepiga mbio na kuifikia mede. Tawi la mtende mikononi mwao ni alama ya ushindi wao, na vazi jeupe ni nembo au ishara ya haki isiyo na waa ya Kristo, ambayo kwa sasa ni yao.PLK 140.3

    Waliokombolewa wanapaza sauti kwa wimbo wa sifa ambao unatoa mwangwi tena na tena kupita katika anga: “Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.” Na malaika wanaunganisha sauti zao katika sifa. Kama ambavyo waliokombolewa walivyoshuhudia uwezo na nia mbaya ya Shetani, walikuwa wameona, kuliko wakati mwingine wo wote uliopita, kuwa hakuna uwezo mwingine isipokuwa tu ule wa Kristo ndio ambao ungeweza kuwafanya kuwa washindi. Katika jeshi lile lote ling’aalo hakuna hata mmoja wa kujichukulia sifa ya wokovu juu yao wenyewe, kana kwamba walishinda kwa uwezo na wema wao binafsi. Hawana cho chote cha kusema kuhusu kile walichokifanya au mateso waliyopata, bali mzigo wa kila wimbo, noti kuu ya kila wimbo, ni, “Wokovu una Mungu wetu ... na Mwana-Kondoo.” Ufunuo 7:10.PLK 141.1

    Mbele ya kusanyiko la wakazi wa duniani na mbinguni, kutawazwa kwa mwisho kwa Mwana wa Mungu kunafanyika. Na sasa, akiwa amevikwa kwa uweza mkuu na mamlaka, Mfalme wa wafalme anatamka hukumu juu ya waasi wa serikali yake na kutenda haki juu ya wale walioihalifu sheria yake na kuwaonea watu wake. Nabii wa Mungu anasema: “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” Ufunuo 20:11, 12.PLK 141.2

    Mara tu vitabu vya kumbukumbu vilipofunguliwa, na jicho la Kristo kuwatazama waovu, walitambua kila dhambi waliyowahi kuitenda. Wanaona hasa pale ambapo miguu yao iliteleza na kuiacha njia ya usafi na utakatifu, jinsi ambavyo kiburi na uasi viliwapeleka mbali katika kuihalifu sheria ya Mungu. Majaribu yenye ushawishi ambayo waliyaimarisha kwa kuendekeza dhambi, mibaraka waliyoipotosha, na mawimbi ya rehema yaliyorudishwa nyuma kwa moyo mkaidi usiotubu-vyote hivi vinajitokeza kama kwamba vimeandikwa kwa herufi za moto.PLK 142.1

    Onesho Kamili la Pambano Kuu-Juu ya kiti cha enzi wanaona msalaba, na matukio ya jaribu na anguko la Adamu na hatua zilizofuata katika mpango mkuu wa ukombozi vinaonekana kama vile kutazama mfululizo wa mambo mbalimbali. Kuzaliwa kwa Mwokozi katika hali duni, maisha yake ya awali ya kawaida na utii, ubatizo wake katika Yordani, kuflinga na kujaribiwa kwake jangwani, huduma yake ya hadhara iliyowapatia wanaume na wanawake baraka za mbingu zilizo bora kabisa, siku zilizojawa na matendo ya upendo na rehema, nyakati za usiku za maombi na kukesha katika sehemu za faragha milimani, njama za husuda, chuki, na uovu uliolipiza fadhila zake, maumivu ya ajabu na ya kutisha pale Gethsemane chini ya uzito unaoseta wa dhambi za dunia yote, kusalitiwa kwake mikononi mwa wauaji, matukio ya kutisha ya usiku ule wa kuogofya: mfungwa asiyetoa upinzani, aliyeachwa na wanafunzi wake aliowapenda sana, akiharakishwa kwa jeuri kupita katika mitaa ya Yerusalemu, Mwana wa Mungu kwa kushangiliwa akioneshwa mbele ya Anasi, akishitakiwa katika ikulu ya kuhani mkuu, katika ukumbi wa hukumu wa Pilato, akiwa mbele ya Herode mwoga na katili, akidhihakiwa, kutukanwa, kuteswa na kuhukumiwa kufavyote hivi vinaoneshwa dhahiri.PLK 142.2

    Na sasa mbele ya umati huu mkubwa matukio ya mwisho yanadhihirishwa: Mtesekaji mstahimilivu akiitembea njia ya kuelekea Kalvari, Mfalme wa mbingu akiwa ameangikwa msalabani, makuhani wenye majivuno na umati wenye zogo wakizomea na kudhihaki maumivu yake ya kufa, giza lisilo la kawaida, dunia inayosukwasukwa, mawe yaliyopasuliwa, makaburi yaliyofunguliwa, yakiashiria wakati ule Mkombozi wa ulimwengu alipokata roho.PLK 143.1

    Onesho la kutisha linaonekana kama ilivyokuwa hasa. Shetani, malaika zake, na wafuasi wake hawana uwezo wa kugeuka na kutoiangalia picha hii ya matendo yao wenyewe. Kila mhusika anakumbuka nafasi yake aliyotekeleza. Herode, ambaye aliwaua watoto wa Bethlehemu wasio na hatia katika juhudi za kutaka kumwangamiza Mfalme wa Israeli; Herodia mwovu, ambaye katika roho yake yenye hatia inakaa damu ya Yohana Mbatizaji; Pilato mdhaifu na mnafiki; askari wenye dhihaka; makuhani na viongozi na watu waliokasirika ambao walipaza sauti wakisema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu” - wote wanafahamu jinsi gani hatia yao ilivyo kubwa sana. Wanajaribu bila mafanikio kujificha kutoka katika utukufu wa Uungu wa uso wake unaong’aa kuliko utukufu wa jua, wakati ambapo waliokombolewa wanaweka taji zao miguuni pa Mwokozi, wakisema, “Alikufa kwa ajili yangu!”PLK 143.2

    Miongoni mwa waliokombolewa wapo mitume wa Kristo, Paulo shujaa, Petro mwenye bidii, Yohana mpendwa na apendaye, na ndugu zao wenye mioyo ya kweli, na pamoja nao jeshi kubwa la wafia dini, wakati ambapo nje ya kuta za jiji, pakiwa na kila kitu kiovu na chenye kuchukiza, wapo wale waliowatesa, kuwafunga, na kuwaua. Yupo Nero, lile jitu la kutisha kwa ukatili na uovu, akiangalia furaha na heshima ya watu ambao aliwahi kuwatesa, na ambao katika maumivu yao makali mno alipata furaha yake ya Kishetani. Mama yake yuko pale ili kushuhudia matokeo ya kazi yake mwenyewe, kuona jinsi ambavyo mhuri mwovu wa tabia aliyoiambukiza kwa mwanae, hisia kali zilizotiwa moyo na kukuzwa kwa ushawishi na mfano wake, vimezaa matunda ya uhalifu ulioufanya ulimwengu kutetemeka.PLK 143.3

    Wapo makasisi na maaskofu ambao walidai kuwa wawakilishi wa Kristo, na huku wakitumia kitanda cha kutesea, jela, na nguzo za kuchomea watu moto ili kudhibiti dhamiri za watu wake. Wapo mapapa wenye kiburi waliojiinua wenyewe juu ya Mungu na kuthubutu kubadili sheria yake Yeye Aliye Juu. Wale waliojifanya kuwa mababa wa kanisa wana hesabu ya kutoa mbele za Mungu, ambayo kutokana na hiyo wangefurahi kusamehewa. Wataona wakiwa wamechelewa sana kuwa yeye Mwenye kufahamu yote ana wivu na sheria yake, na kwamba hatamsamehe mwenye hatia. Sasa wanatambua kuwa Kristo anajibainisha na watu wake wanaoteseka, na wanahisi nguvu ya maneno yake mwenyewe, “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Mathayo 25:40.PLK 144.1

    Katika Kizimba cha Hukumu-Ulimwengu wote wa waovu unasimama wakiwa wameshitakiwa katika kizimba cha hukumu cha Mungu, wakiwa wanashitakiwa kwa uhaini mkuu dhidi ya serikali ya mbinguni. Waliopotea hawana mtu hata mmoja wa kuwatetea katika kesi yao. Hawana udhuru wo wote, na hukumu ya mauti ya milele inatamkwa dhidi yao.PLK 144.2

    Sasa ni dhahiri kwa wote kuwa mshahara wa dhambi si uhuru bora na uzima wa milele, bali ni utumwa, uharibifu, na mauti. Waovu wanaona kile ambacho wamekipoteza kwa sababu ya maisha yao ya kuasi. Walidharau “utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana” pale walipopewa, lakini sasa unaonekana kuwa ni wa kutamanika kiasi gani. “Vyote hivi,” roho iliyopotea inalia, “Ningeliweza kuvipata, lakini nilichagua kuviweka vitu hivi mbali nami. Lo, shauku kubwa ajabu kiasi gani! Nimebadilisha amani, furaha, na heshima kwa umaskini, aibu, na kuvunjika moyo.” Wote wanaona kwamba kutengwa kwao kutoka mbinguni ni haki. Katika maisha yao walitangaza, Kamwe hatutaruhusu huyu Yesu kutawala juu yetu.PLK 144.3

    Wakiwa kama wamepumbazwa, waovu waliangalia kutawazwa kwa Mwana wa Mungu. Wanaona katika mikono yake mbao za sheria takatifii, amri ambazo walizidharau na kuzivunja. Wanashuhudia kwa mshangao mlipuko wa furaha, na sifa kutoka kwa waliokombolewa, na kadiri mwangwi wa sauti tamu unavyosambaa hadi kwa majeshi yaliyoko nje ya jiji, wote kwa pamoja wanasema, “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu, Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa.” (Ufunuo 15:3), na huku wakianguka kifudifudi, wanamwabudu Mfalme wa uzima.PLK 145.1

    Mauti ya Pili-Shetani anaonekana kama vile amepooza pale anapoona utukufu na ukuu wa Kristo. Yeye ambaye hapo mwanzo alikuwa ni kerubi afunikaye anakumbuka ni wapi alipoanguka. Malaika mwenye kung’ara, “mwana wa asubuhi”-amebadilika kiasi gani, ameshushwa cheo kiasi gani!PLK 145.2

    Shetani anaona kuwa uasi wake wa hiari umemfanya asifae kwa ajili ya mbingu. Alielekeza nguvu zake kupambana dhidi ya Mungu, hivyo usafi, amani na upatanifu wa mbinguni kwake vingekuwa ni mateso makuu. Shutuma zake dhidi ya rehema na haki za Mungu sasa zimenyamazishwa. Lawama ambayo amejaribu kuitoa kwa Yehova inamkalia kabisa juu yake mwenyewe. Na sasa Shetani anainama chini na kukiri haki ya hukumu yake.PLK 145.3

    Kila hoja ya ukweli na uongo katika pambano kuu lililodumu kwa muda mrefu imewekwa wazi. Haki ya Mungu imethibitishwa kikamilifu. Ulimwengu wote umeona uwasilishaji dhahiri wa kafara kuu ambayo Baba na Mwana waliitoa kwa niaba ya wanadamu. Saa imewadia ambapo Kristo anachukua nafasi yake anayostahili na anatukuzwa juu ya falme na mamlaka na kila jina linalotamkwa.PLK 146.1

    Ingawa Shetani amelazimishwa kukiri haki ya Mungu na kusujudu kwa ukuu wa Kristo, tabia yake inabaki bila kubadilika. Roho ya uasi, kama vile mto mkubwa, inalipuka tena. Akiwa amejawa na wazimu, anadhamiria kutojitoa katika pambano kuu hili. Wakati umefika kwa ajili ya pambano kuu la mwisho kabisa dhidi ya Mfalme wa mbingu. Anafanya haraka kupita miongoni mwa wafuasi wake na kujaribu kuwachochea kwa hasira yake mwenyewe na kuwaamsha kwa ajili ya vita vya papo hapo. Lakini katika mamilioni wasiohesabika wote aliowashawishi kwenye uasi, hakuna hata mmoja sasa wa kukubali mamlaka yake ya juu. Uwezo wake unafikia mwisho wake. Waovu wamejawa na chuki ileile kwa Mungu inayomchochea Shetani, lakini wanaona kuwa suala lao halina matumaini yo yote, kwamba hawawezi kumshinda Yehova. Wanamkasirikia Shetani na wale ambao walikuwa mawakala wake katika udanganyifu. Kwa hasira ya mapepo wanawageukia, na pale linafuatia tukio la vita ya kiulimwengu.PLK 146.2

    Ndipo yanapotimia maneno ya nabii: “Maana Bwana ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa.” Isaya 34:2. “Awanyeshee wasio haki mitego, Moto na kiberiti na upepo wa hari, Na viwe fungu la kikombe chao.” Zaburi 11:6. Moto unashuka chini kutoka kwa Mungu kutoka mbinguni. Dunia inavunjika. Silaha za asili zilizofichwa katika vina vyake zinatolewa. Mioto ilayo inalipuka kutoka katika nyufa zenye midomo wazi. Siku imekuja ambayo “inawaka kama tanuru.” Malaki 4:1. Viumbe vya asili vinayeyuka kwa joto kali, na dunia pamoja na kazi zilizomo ndani yake zinateketea. (2Petro 3:10). Uso wa dunia unaonekana kama bonge moja lililoyeyuka-ziwa kubwa sana linalochemka la moto. Ni wakati wa hukumu na maangamizo ya wasiomcha Mungu - “Maana ni siku ya kisasi cha Bwana, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni.” Isaya 34:8.PLK 146.3

    Waovu wanapokea malipo yao ya haki hapa duniani. ‘“Watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza,’ asema Bwana wa majeshi.” Malaki 4:1. Baadhi wanaangamizwa mara moja, wakati wengine wanateseka siku kadhaa. Wote wanaadhibiwa kulingana na matendo yao. Shetani anateswa, si tu kwa sababu ya uasi wake mwenyewe, bali kwa ajili ya dhambi zote alizowasababisha watu wa Mungu kuzitenda. Adhabu yake itakuwa kubwa mno kupita ile ya watu aliowadanganya. Baada ya wote walioanguka kwa madanganyo yake kuangamia, yeye bado atapaswa kuishi na kuteseka zaidi. Katika moto utakasao, hatimaye waovu wanaangamizwa, mizizi na matawi - Shetani ndiye mzizi, na wafuasi wake ni matawi. Haki ya Mungu inaridhishwa, na watakatifu na malaika wote wanasema kwa sauti kuu, Amina.PLK 147.1

    Wakati dunia imefunikwa kwa moto wa kisasi cha Mungu, watakatifu wako salama ndani ya Jiji Takatifu. Juu ya wale waliokuwa na sehemu katika ufufuo wa kwanza, mauti ya pili haina nguvu. (Ufunuo 20:6.) Wakati ambapo Mungu kwa waovu anakuwa ni moto ulao, kwa watu wake yeye ni jua pamoja na ngao (Zaburi 84:11).PLK 147.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents