Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 18—Mwanamatengenezo wa Kimarekani

    Mkulima mwadilifu na mwaminifu, ambaye alikuwa ameshawishika kutilia mashaka mamlaka ya Kiungu ya Maandiko, lakini ambaye alitamani kwa dhati kuujua ukweli, alikuwa mtu mahsusi ambaye Mungu alimchagua kuongoza utangazaji wa ujio wa pili wa Kristo. Kama wanamatengenezo wengine wengi, William Miller katika siku zake za awali alipambana na umaskini na hivyo alijifunza masomo makuu ya nguvu na kujikana nafsi. Watu waliozaliwa katika familia aliyozaliwa walikuwa na sifa ya kupenda kujitegemea, roho ya kupenda uhuru, uwezo wa kuvumilia, na uzalendo wa hali ya juu—sifa ambazo zilijulikana kama sehemu ya maisha yake. Baba yake alikuwa kapteni katika jeshi la Mapinduzi, na mazingira ya maisha ya Miller ya awali yalimwandaa kutoa maisha yake kafara katika mapambano na mateso ya kipindi cha dhoruba.PKSw 242.1

    Alikuwa na mwili wenye afya njema, na hata katika utoto wake kulikuwa na ushahidi wa uwezo wa akili usiokuwa wa kawaida. Alivyoendelea kukua na kuwa mtu mzima, jambo hili lilizidi kuwa dhahiri. Akili yake ilikuwa kazini saa zote na ilikuwa na uwezo mkubwa, na alikuwa na kiu kubwa ya kupata maarifa. Ingawa hakubahatika kupata elimu ya chuo kikuu, shauku yake ya masomo na tabia yake ya kutafakari kwa makini na kufanya uchambuzi wa mambo kwa kina vilimfanya kuwa mtu mwenye busara na mawazo mapana. Alikuwa na tabia ya uadilifu usiokuwa na dosari na alikuwa na sifa njema isiyokuwa na doa, kwa jumla akitambuliwa kwa uaminifu, matumizi mazuri ya fedha, na ukarimu. Kwa sababu ya nguvu na kufanya kazi alijenga umahiri mapema, ingawa tabia zake za kujifunza bado ziliendelea kudumishwa. Alifanya kazi mbalimbali zikiwemo za kiraia na za kijeshi kwa mafanikio makubwa, na njia za kupata mali na heshima zilionekana kuwa wazi mbele yake.PKSw 242.2

    Mama yake alikuwa ni mcha Mungu kweli kweli, na katika utoto wake, William Miller alipewa mafundisho ya dini na mama yake. Katika miaka ya mwanzoni ya utu uzima, hata hivyo, alitupwa katika jamii ya wakana Mungu, ambao mvuto wao ulikuwa mkubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa kwa sehemu kubwa walikuwa raia wema na watu wenye huruma na mwelekeo wa ukarimu. Kutokana na jinsi walivyo, wakana Mungu, wakiwa katikati ya taasisi za Kikristo, tabia zao kwa kiwango kikubwa zilijengwa na mazingira yao. Uzuri wao wa tabia uliowapa heshima na kuaminika vilivyotokana na mafundisho ya Biblia; na hata hivyo karama hizi nzuri ziliharibiwa sana kiasi ambacho zilikuwa na mvuto uliokuwa kinyume na neno la Mungu. Kwa kujichanganya na hawa watu, Miller alianza kuiga tabia zao. Ufafanuzi wa mafundisho ya Biblia wa wakati huo ulileta matatizo yaliyoonekana kutoweza kuvukwa; hata hivyo imani yake mpya, wakati ikiweka pembeni Biblia, haikuleta jambo lolote la kuchukua nafasi ya Biblia, na hakuweza kuridhika kabisa. Aliendelea kushikilia mawazo haya, hata hivyo, kwa karibu miaka kumi na mbili. Lakini akiwa na umri wa miaka thelathini na nne Roho Mtakatifu aligusa moyo wake na akaelewa hali yake kama mtu mwenye dhambi. Imani yake ya zamani haikumpa uhakika wa furaha ng'ambo ya kaburi. Mustakabali wake ulionekana kuwa giza na utusitusi. Akitafakari miaka ya baadaye kuhusu hisia zake za sasa alisema:PKSw 242.3

    “Kupotea milele lilikuwa wazo linaloleta unyong'onyevu na hofu, na uwajibikaji ulikuwa uharibifu kwa wote. Mbingu zilikuwa kama shaba juu ya kichwa changu, na dunia ilikuwa kama chuma chini ya nyayo zangu. Umilele—ulikuwa ni nini? Na kifo—kwa nini kilikuwepo? Kwa kadiri nilivyotafakari zaidi, ndivyo nilivyozidi kwenda mbali na uhalisia. Nilivyozidi kufikiria ndivyo mahitimisho yangu yalizidi kusambaratika. Nilijaribu kuacha kufikiri, lakini mawazo yangu hayakuweza kutawalika. Nilikuwa na hali mbaya kweli kweli, lakini sikujua chanzo chake ni nini. Nilinung'unika na kulalamika, lakini sikujua ninamnung'unikia na kumlalamikia nani. Nilijua kulikuwa na jambo ambalo siyo sahihi, lakini sikujua ni kwa jinsi gani siyo sahihi au kujua mahali pa kupata jambo lililo sahihi. Niliomboleza, lakini sikuwa na tumaini”PKSw 243.1

    Aliendelea katika hali hii kwa miezi kadhaa. “Kwa ghafla,” anasema, “tabia ya Mwokozi ilifunuliwa na kuwa wazi katika akili zangu. Ilionekana kuwa ni lazima kutakuwa na mwenye uhai aliye mwema sana na huruma nyingi ambaye anaweza kujipatanisha yeye mwenyewe kwa ajili ya makosa yetu, na hivyo kutuokoa kutoka katika mateso na adhabu ya dhambi. Kwa ghafla nilihisi jinsi mwenye uhai huyo anavyopaswa kuwa mwema sana, na niliwaza moyoni mwangu kuwa ningejitupa mikononi mwake, na kutumainia rehema za mwenye uhai huyo. Lakini swali liliibuka, itathibitishwaje kuwa kiumbe kama huyo yupo? Kando ya Biblia, sikuweza kupata ushahidi wa uwepo wa Mwokozi kama huyo, au hata uwepo wa hali njema ya wakati ujao....PKSw 243.2

    “Niliona Biblia ikichora picha ya Mwokozi niliyemhitaji; na nilitatizwa kugundua jinsi ambavyo kitabu kisichokuwa na pumzi ya Mungu kinavyoweza kujenga kanuni zinazokidhi kikamilifu mahitaji ya ulimwengu ulioanguka. Nililazimika kukiri kuwa Maandiko lazima yawe ufunuo kutoka kwa Mungu. Maandiko yakaja kuwa chanzo cha furaha yangu; na Yesu akawa rafiki yangu.PKSw 243.3

    Mwokozi alikuja kuwa mkuu miongoni mwa makumi elfu, Maandiko yaliyokuwa giza na yaliyopingana kabla, sasa yalikuwa taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu. Akili yangu ilitulia na kuridhika. Niligundua kuwa Mungu ni Mwamba katikati ya bahari ya maisha. Biblia ikawa kitabu changu kikuu cha kujifunza, na ninaweza kusema kwa hakika, nilikichunguza kwa furaha kubwa. Hatimaye niligundua kuwa nusu yake ilikuwa haijasimuliwa kwangu. Nilishangaa na kujiuliza kwa nini nilikuwa sioni uzuri na utukufu wake kabla, na nilistaajabu kuwa kwa nini hata nilijaribiwa kuitupilia mbali. Niligundua kuwa mambo yote ambayo moyo wangu uliyatamani yalipatikana katika Biblia, na tiba ya kila ugonjwa wa moyo ilikuwemo humo. Nilipoteza hamu ya kusoma vitabu vingine, na nilielekeza moyo wangu kupata hekima itokayo kwa Mungu.”—S. Bliss, Memoirs of Wm. Miller, ukurasa 65-67.PKSw 243.4

    Miller alitangaza hadharani imani yake katika dini ambayo alikuwa akiidhihaki. Lakini marafiki zake wakana Mungu hawakuchelewa kumletea hoja ambazo yeye mwenyewe alikuwa akizitumia dhidi ya mamlaka ya Kimungu ya Maandiko. Wakati huo hakuwa tayari kuzijibu; lakini alieleza kuwa ikiwa Biblia ni ufunuo kutoka kwa Mungu ni lazima isijipinge yenyewe; na kwamba kwa kuwa ilitolewa kwa ajili ya mafundisho ya mwanadamu, lazima iweze kueleweka kwake. Alidhamiria kujifunza Maandiko kwa ajili yake mwenyewe, na kujiridhisha ikiwa kila kupingana kunakodhaniwa kuwepo kunaafikiwa.PKSw 244.1

    Akijitahidi kuondoa maoni potovu yote aliyokuwa nayo kabla, na akiweka pembeni vitabu vinavyofafanua Biblia, alilinganisha maandiko kwa maandiko kwa msaada wa rejea zilizoko pembeni mwa kurasa za Biblia na kitabu chenye orodha ya maneno yaliyo mengi ya Biblia yaliyopangiliwa kialfabeti. Alipanga kujifunza Biblia kwa muda maalumu ule ule na kwa utaratibu maalumu; akianza na Kitabu cha Mwanzo, na akisoma fungu kwa fungu, hakuendelea mbele ya aya ambazo alikuwa akijifunza mpaka maana ya aya hizo ilipoeleweka kabisa na kujiridhisha kuwa hakuna tashwishi ya aina yo yote iliyobaki. Alipogundua jambo lo lote lisiloelewekwa, ilikuwa desturi yake kulilinganisha aya husika na aya zingine zote zilizogusia jambo alilokuwa akilichunguza. Kila neno liliruhusiwa kuchangia katika kufafanua jambo lililodokezwa na aya husika, na ikiwa wazo la aya hiyo liliafikiana na aya zingine, tatizo liliisha. Kwa njia hiyo, iwe alikutana na sehemu ya Maandiko ngumu kuelekweka alipata maelezo yake katika sehemu nyingine ya Maandiko. Alivyoendelea kujifunza kwa bidii kwa maombi ya dhati ili kupata kuangaziwa na Mungu, jambo lile ambalo lilionekana kuwa giza kwake mwanzoni lilieleweka vizuri. Alipata uzoefu wa ukweli wa maneno ya mwandishi wa Zaburi: “Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga” (Zaburi 119:130). Kwa shauku kubwa alijifunza vitabu vya Danieli na Ufunuo, akitumia kanuni ile ile ya kutafsiri aliyoitumia kwa maandiko mengine, na aligundua, kwa furaha kubwa, kuwa mifano ya kiunabii iliweza kueleweka. Aliona kuwa sehemu mbalimbali za unabii, ambazo zilikuwa zimetimizwa, zilitimizwa katika ulimwengu unaoonekana; kwamba vielelezo mbalimbali vyote, sitiari zote, mifano yote, tashbihi zote, nk., ziliweza kufafanuliwa kwa kulinganisha na muktadha ulio karibu, au maneno ambayo yametumika kuzielelezea yamefasiliwa katika sehemu zingine za Maandiko, na kwa kufafanuliwa hivyo, zilipaswa kueleweka moja kwa moja kama zilivyo. “Kwa njia hiyo niliridhika,“alisema,“kuwa Biblia ni mfumo wa ukweli uliofunuliwa, uliotolewa kwa uwazi na usahili kiasi kwamba msafiri, hata kama angekuwa mjinga kiasi gani, hawezi kushindwa kuelewa kile Maandiko yanachosema.”—Bliss, ukurasa 70. Kiunganishi baada ya kiunganishi cha mnyororo wa ukweli kilibariki juhudi zake, kwa kadiri jinsi alivyofuatilia matukio makubwa ya unabii. Malaika wa mbinguni waliongoza akili yake na kumfunulia Maandiko ili aweze kuelewa.PKSw 244.2

    Akichukua jinsi ambavyo sehemu mbalimbali za unabii uliokwisha kutimizwa wakati uliopita kama kigezo cha kupima jinsi unabii wa mambo yaliyokuwa bado yanakuja katika wakati ujao, aliridhika kuwa wazo lililoenea kuwa utawala wa kiroho wa Kristo—milenia ya wakati mfupi kabla ya mwisho wa dunia—halikuungwa mkono na neno la Mungu. Fundisho hili, likielekeza kwa miaka elfu moja ya haki na amani kabla ya ujio binafsi wa Bwana, liliifanya siku ya Mungu kuonekana iko mbali sana. Lakini, haidhuru lilikuwa la lilifurahisha kiasi gani, liko kinyume na mafundisho ya Kristo na mitume Wake, waliotangaza kuwa ngano na magugu vinapaswa kukua pamoja mpaka wakati wa mavuno, mwisho wa dunia; kuwa “watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu;” kuwa “siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari;” na kuwa ufalme wa giza utaendelea mpaka ujio wa Bwana na utakomeshwa kwa roho ya mdomo Wake na kuangamizwa kwa mwanga wa ujio wake. (Mathayo 13:30, 38-41; 2 Timotheo 3:13, 1; 2 Wathesalonike 2:8).PKSw 245.1

    Fundisho la kuongoka kwa ulimwengu na utawala wa kiroho wa Kristo halikufundishwa na kanisa la mitume. Kwa jumla halikukubaliwa na Wakristo mpaka karibu na mwanzoni mwa karne ya kumi na nane. Kama inavyokuwa kwa kosa lingine lo lote lile, matokeo yake yalikuwa mabaya. Liliwafundisha kutazama mbali katika wakati ujao kwa ajili ya ujio wa Bwana na liliwazuia wasiangalie dalili zilizoashiria ukaribu wa ujio Wake. Lilijenga hisia ya kujiamini na usalama ambao haukuwa na msingi mzuri na liliwafanya wengi kupuuzia maandalizi muhimu kwa ajili ya kumlaki Bwana wao.PKSw 245.2

    Miller aligundua kuwa ujio binafsi ulio sisisi wa Kristo ulifundishwa wazi wazi katika Maandiko. Paulo anasema: “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu” (1 Wathesalonike 4:16). Na Mwokozi alitangaza: “Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.” “Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:30, 27). Ataandamana na majeshi yote ya mbinguni. “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye” (Mathayo 25:31). “Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake” (Mathayo 24:31).PKSw 246.1

    Wakati wa kuja Kwake wenye haki waliokufa watafufuliwa, na wenye haki walio hai watabadilishwa. “Hatutalala sote” alisema Paulo, “lakini sote tutabadilika, “kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa” (1 Wakorintho 15:5153). Na katika barua kwa Wathesalonike, baada ya kueleza ujio wa Bwana, alisema: “Nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1 Wathesalonike 4:16, 17).PKSw 246.2

    Ni mpaka wakati wa ujio wa Kristo Mwenyewe ambapo watu Wake watapokea ufalme. Mwokozi alisema:“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu” (Mathayo 25:31-34). Tumeona kwa njia ya maandiko ambayo yametolewa hapa kuwa Mwana wa Adamu atakapokuja wafu watafufuliwa na kuwa na hali ya kutokufa na walio hai wanabadilishwa. Kwa badiliko hili kubwa wanajiandaa kupokea ufalme; kwani Paulo anasema:“Nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika” (1 Wakorintho 15:50). Mwanadamu katika hali yake ya sasa ana hali ya kufa, ana mwili unaoharibika; lakini ufalme wa Mungu utakuwa usioharibika, unaodumu milele. Kwa hiyo mwanadamu katika hali yake ya sasa hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu. Lakini Yesu atakapokuja, atawapa watu Wake hali ya kutokufa; na halafu atawaita kuurithi ufalme ambao tangu wakati huo utakuwa urithi wao.PKSw 246.3

    Maandiko haya na maandiko mengine yalithibitisha wazi kwa akili ya Miller kuwa matukio ambayo yalitarajiwa kutokea kabla ya kuja kwa Kristo, kama vile utawala wa amani ulimwenguni kote na uanzishwaji wa ufalme wa Mungu hapa duniani, yatafuata baada ya ujio wa pili wa Kristo. Hali kadhalika, ishara zote za nyakati na hali ya ulimwengu vililandana na maelezo ya kiunabii ya siku za mwisho. Alilazimishwa kufikia majumuisho, kwa kujifunza Maandiko peke yake, kuwa kipindi kilichowekwa cha kuendelea kuwepo dunia katika hali yake ya sasa, kilikuwa karibu kuisha.PKSw 247.1

    “Aina nyingine ya ushahidi ambao uliathiri kiasi kikubwa akili yangu,” alisema, “ulikuwa kufuatana kwa matukio katika muda katika Maandiko.... Nilikuta jambo hilo likiwa limetabiriwa katika unabii, likiwa limetimia katika wakati uliopita, mara nyingi likiwa limetokea katika kipindi husika cha wakati. Miaka mia moja na ishirini hadi wakati wa gharika (Mwanzo 6:3); siku saba ambazo zilitangulia kabla ya gharika, pamoja na siku arobaini za mvua iliyotabiriwa (Mwanzo 7:4); miaka mia nne ya safari ya uzao wa Ibahimu (Mwanzo 15:13); siku tatu za ndoto za mnyweshaji na mwokaji (Mwanzo 40:12-20); miaka saba ya Farao (Mwanzo 41:28-54); miaka arobaini jangwani (Hesabu 14:34); miaka mitatu na nusu ya njaa (1 Wafalme 17:1) [tazama Luka 4:25;] ... miaka sabini ya utumwani (Yeremia 25:11); Nyakati saba za Nebukadneza (Danieli 4:13-16); na majuma saba, majuma sitini na mbili, na juma moja, ambayo jumla yake ni majuma sabini, yaliyoamriwa juu ya Wayahudi (Danieli 9:24-27),—matukio ambayo yalihusisha nyakati hizi yalikuwa mwanzoni ni unabii tu, na yalitimizwa kulingana na utabiri husika.”—Bliss, pages 74, 75.PKSw 247.2

    Wakati ambapo, kwa hiyo, alikuta, katika kujifunza Kwake Biblia, vipindi mbalimbali vyenye matukio yanayofuatana, kwa uelewa wake, yaliendelea mpaka wakati wa kuja mara ya pili kwa Kristo, hakuchukulia vipindi hivyo kama “nyakati zilizoteuliwa,” ambazo Bwana alizifunua kwa watumishi Wake. “Mambo ya siri,” alisema Musa, “ni ya Bwana Mungu wetu: lakini mambo yale yaliyofunuliwa kwetu ni yetu sisi na watoto wetu milele;” na Bwana alisema kwa njia ya nabii Amosi, kuwa Yeye “hatafanya jambo lo lote, bila kuwafunulia siri watumishi Wake” (Kumbukumbu 29:29; Amosi 3:7). Wanafunzi wa neno la Mungu wanaweza, hivyo basi, kutarajia kwa uhakika kuona tukio la kutisha sana lililotajwa kwa uwazi katika Maandiko ya ukweli likitokea katika historia ya mwanadamu.PKSw 247.3

    “Kwa kuwa nilikuwa nimeamini,” alisema Miller, “kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho” (2Timotheo 3:16); kuwa halikuletwa wakati wo wote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali liliandikwa na watu watakatifu wakiongozwa na Roho Mtakatifu (2 Petro 1:21), na liliandikwa ‘kwa ajili ya mafundisho yetu, kuwa sisi kwa uvumilivu na faraja ya Maandiko tuweze kuwa na tumaini’ (Warumi 15:4), nililazimika kuchukulia sehemu za Biblia zinazotaja nyakati zinazofuatana kuwa sehemu ya Biblia kama sehemu zingine za neno la Mungu zilivyo, na kuwa zilistahili kutiliwa maanani, kama sehemu zingine zozote za Maandiko. Hivyo basi nilihisi kuwa katika kujaribu kuelewa kile ambacho Mungu katika rehema Yake aliona vema kutufunulia, sikuwa na haki kuruka vipindi vya kiunabii.”—Bliss, uk. 75.PKSw 247.4

    Unabii ulioonekana kuwa wazi zaidi katika kufunua wakati wa ujio wa pili ni ule wa Danieli 8:14: “Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” Akifuata kanuni yake ya kuyafanya Maandiko yajitafsiri yenyewe, Miller aligundua kuwa siku katika unabii wa mifano huwakilisha mwaka (Hesabu 14:34; Ezekieli 4:6); aliona kuwa kipindi cha siku 2300 za kiunabii, au miaka sisisi 2300, kingeenda mbele sana hadi kuvuka kufungwa kwa kipindi cha Wayahudi kuwa taifa takatifu, kwa hiyo kisingewakilisha hekalu la kipindi cha Wayahudi kama taifa takatifu la Mungu. Miller alikubaliana na mtazamo uliokuwepo mpaka wakati huo kuwa katika zama za Ukristo dunia ndiyo patakatifu, na hivyo alielewa kuwa kutakataswa kwa hekalu kulikotabiriwa katika Danieli 8:14 kuliwakilisha kutakaswa kwa dunia kwa moto wakati wa ujio wa pili wa Kristo. Kwa hiyo, ikiwa mahali sahihi pa kuanzia pangepatikana kwa ajili ya siku 2300, alijumuisha kuwa wakati wa ujio wa pili wa Kristo ungeweza kuthibitishwa kirahisi. Hivyo wakati wa mwisho wa mambo yote ungeweza kufunuliwa, wakati ambao hali ya sasa, pamoja na “kiburi na nguvu zake zote, majivuno na upuuzi, uovu na uonevu, vingekoma;” wakati laana “ingeondolewa duniani, kifo kingeangamizwa, zawadi kutolewa kwa watumishi wa Mungu, manabii na watakatifu, na wale wanaolicha jina Lake, na waangamizwe watu wanaoiharibu dunia.”—Bliss, ukurasa 76.PKSw 248.1

    Kwa bidii kubwa, Miller aliendelea kuchunguza unabii, wakati wote wa usiku na mchana ukitumiwa kujifunza kile ambacho kilionekana kuwa na umuhimu mkubwa na ambacho kiliamsha shauku kubwa ya kukifuatilia. Katika sura ya nane ya Danieli hakuweza kupata kidokezo cho chote ambacho kingemwezesha kujua mwanzo wa kipindi cha siku 2300; malaika Gabrieli, ingawa alikuwa amepewa amri ya kumfanya Danieli aelewe njozi, alimpa maelezo kidogo. Wakati mateso ya kutisha yaliyotarajia kulipata kanisa yalipofunuliwa katika njozi ya nabii, nguvu za kimwili zilimtoka. Hakuweza kustahimili zaidi, na malaika alimwacha kwa muda. Danieli “alizimia, na alikuwa mgonjwa kwa siku.” “Na nilishangazwa na njozi,” alisema, “lakini hakuna aliyeelewa.”PKSw 248.2

    Walakini Mungu alimwagiza mjumbe Wake: “mfahamishe mtu huyu maono haya.” Agizo hili lilitekelezwa. Katika kulitii agizo hilo, malaika, muda fulani baadaye, alimrudia Danieli, na kusema: “nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu;” “basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya” (Danieli 8:27, 16; 9:22, 23, 25-27). Kwa hiyo kulikuwa na jambo moja muhimu katika njozi ya sura ya 8 ambayo ilikuwa imeachwa bila kutolewa maelezo, ambalo, ni lile linalohusiana na wakati—kipindi cha siku 2300; kwa hiyo malaika, kwa kurudi na kuendelea na maelezo yake, anashughulikia zaidi mada ya wakati:PKSw 248.3

    “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu. Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu.”PKSw 249.1

    Malaika alitumwa kwa Danieli kwa ajili ya kusudi moja tu la kumwelezea jambo ambalo alikuwa ameshindwa kulielewa katika njozi ya sura ya nane, jambo ambalo lilihusiana na wakati—“Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” Baada ya kumwagiza Danieli “atafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya,” maneno ya kwanza ya malaika ni haya: “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu.” Neno lililotafsiriwa hapa “umeamriwa” linamaanisha “kukata.” Majuma sabini, yanayowakilisha miaka 490, yalitangazwa na malaika kuwa yamekatwa, hususani kuhusiana na Wayahudi. Lakini majuma hayo yalikatwa kutoka wapi? Kwa kuwa siku 2300 ndizo zilikuwa kipindi pekee cha wakati kilichotajwa katika sura ya 8, ndicho kipindi ambacho kutokana nacho majuma sabini yalikatwa; majuma sabini yanapaswa kuwa sehemu ya siku 2300, na vipindi vyote viwili vinapaswa kuanza pamoja. Majuma sabini yalitangazwa na malaika kuanza tarehe ya kutangazwa kwa amri ya kurejesha na kuujenga upya mji wa Yerusalemu. Ikiwa tarehe ya amri hii ingepatikana, tarehe ya kuanza kwa kipindi kikuu cha siku 2300 ingeweza kujulikana kwa hakika.PKSw 249.2

    Katika sura ya saba ya Ezra ndiko inakopatikana amri (Aya za 12-26). Katika ukamilifu wake wote ilitolewa na Artashasta, mfalme wa Uajemi, 457 K.K. Lakini katika Ezra 6:14 nyumba ya Bwana inasemekana kuwa ilijengwa “kulingana na amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi.” Hawa wafalme watatu, kwa kuanzisha, kukazia, na kukamilisha amri, waliifanya itekelezwe kikamilifu kama ilivyotakiwa na unabii kuonesha mwanzo wa miaka 2300. Kwa kuchukua mwaka 457 K.K., wakati amri ilipokamilishwa, kama tarehe ya kutolewa kwa amri, kila kipengele cha unabii uliohusu majuma sabini ulionekana kuwa umeshatimizwa.PKSw 249.3

    “Tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili”—yaani, majuma sitini na mbili, au miaka 483. Amri ya Artashasta ilianza kutekelezwa wakati wa vuli ya mwaka 457 K.K. Tangu tarehe hii, miaka 483 inaishia vuli ya mwaka B.K. 27. (Tazama Kiambatisho.) Wakati huu unabii huu ulitimizwa. Neno ‘Masihi’ linamaanisha “Mpakwa Mafuta” Katika vuli ya B.K. 27 Kristo alibatizwa na Yohana na kupokea upako wa Roho. Mtume Petro anashuhudia kuwa “Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu” (Matendo 10:38). Na Mwokozi Mwenyewe alisema: “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema” (Luka 4:18). Baada ya ubatizo Wake alikwenda Galilaya, “akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia” (Marko 1:14, 15).PKSw 250.1

    “Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja.” Hili “juma” linalotajwa hapa ni juma la mwisho miongoni mwa majuma sabini; ni miaka saba ya mwisho kipindi kilichopangwa mahsusi kwa ajili ya Wayahudi. Katika kipindi hiki kinachoanzia mwaka B.K. 27 hadi mwaka B.K. 34, Kristo, mwanzoni kwa njia ya nafsi Yake Mwenyewe na baadaye kwa njia ya wanafunzi Wake, alipeleka mwaliko wa injili hususani kwa Wayahudi. Mitume walipotoka na kwenda nje wakiwa na habari njema ya ufalme, maelekezo ya Mwokozi yalikuwa: “Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” (Mathayo 10:5, 6).PKSw 250.2

    “Na kwa nusu ya juma hilo ataikomesha sadaka na dhabihu.” Mwaka B.K. 31, miaka mitatu na nusu baada ya ubatizo Wake, Bwana wetu alisulubishwa. Kwa kafara kuu iliyotolewa juu ya mlima wa Kalwari, alikomesha mfumo wa sadaka ambazo kwa miaka elfu nne zilielekeza kwa Mwanakondoo wa Mungu ajaye. Mfano ulikutana na kitu halisi, na kafara zote za mfumo wa kaida zilikomea hapo.PKSw 250.3

    Majuma sabaini, au miaka 490, hususani waliyopewa Wayahudi, yaliishia, kama tulivyoona, mwaka, B.K. 34. Wakati huo, kupitia kwa tendo la Baraza Kuu la Wayahudi, Sanhedrini, taifa lilitia muhuri kukataa kwake injili kwa kumwua Stefano na kuwatesa wafuasi wa Kristo. Tangu hapo, ujumbe wa wokovu, ambao mwanzoni ulikuwa upelekwe kwanza kwa Wayahudi, ulipelekwa ulimwenguni. Wanafunzi, wakiwa wamelazimishwa na mateso kuukimbia mji wa Yerusalemu, “walienda kila mahali wakilihubiri neno.” “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.” Petro, akiongozwa na Mungu, alimfungulia injili akida wa Kaisaria, Kornelio mcha Mungu; na Paulo mwenye juhudi, akiwa ameongolewa na kuipokea imani ya Kristo, aliagizwa kupeleka habari njema “mbali kwa watu wa Mataifa” (Matendo 8:4, 5; 22:21).PKSw 250.4

    Kwa kiwango hicho kila kipengele cha unabii kilitimizwa kikamilifu, na mwanzo wa majuma sabini ukathibitika wazi kuwa ni mwaka 457 K.K., na yanaishia mwaka B.K. 34. Kutokana na maelezo hayo hakuna ugumu wa kupata mwisho wa kipindi cha siku 2300. Majuma sabini— siku 490— zikiwa zimekatwa kutoka siku 2300, kulikuwa na siku 1810 zilizobaki. Baada ya mwisho wa siku 490, siku 1810 zilikuwa bado kutimizwa. Tangu mwaka B.K. 34, miaka 1810 inaishia 1844. Kwa hiyo siku 2300 za Danieli 8:14 zinaishia mwaka 1844. Mwishoni mwa hiki kipindi kikuu cha kiunabii, kwa ushuhuda wa malaika wa Mungu, “patakatifu patatakaswa.” Hivyo wakati wa kutakaswa kwa patakatifu—ambako kuliaminiwa na karibu ulimwengu wote kuwa kungetokea wakati wa ujio wa pili wa Kristo—kulikuwa kumebainishwa kikakamilifu.PKSw 251.1

    Miller na wenzake mwanzoni waliamini kuwa siku 2300 zingeishia msimu wa masika wa mwaka 1844, ambapo unabii huelekeza kwa msimu wa vuli wa mwaka huo. (Tazama Kiambatisho.) Kutokuelewa vizuri kipengele hiki kuliwasababishia kuvunjika moyo na kuingiwa mashaka kwa wale waliokuwa wameweka tarehe ya awali kama siku ya ujio wa Bwana. Lakini jambo hili halikuathiri hata kidogo nguvu ya hoja iliyoonesha kuwa siku 2300 ziliishia mwaka 1844, na kuwa tukio kuu lililowakilishwa na utakaso wa patakatifu lazima lingetokea.PKSw 251.2

    Akianza kujifunza Maandiko kama alivyofanya, kwa lengo la kuthibitisha kuwa yalikuwa ufunuo kutoka kwa Mungu, Miller hakuwa, tangu mwanzo kabisa, na matarajio hata kidogo ya kufikia hitimisho ambalo sasa alifikia. Yeye mwenyewe hakuweza kukubali kirahisi matokeo ya utafiti wake. Lakini ushahidi wa Maandiko ulikuwa wa wazi na wenye nguvu kiasi kwamba asingeweza kuupuuza.PKSw 251.3

    Alikuwa ametumia miaka miwili kwa ajili ya kujifunza Biblia, ambapo, mwaka 1818, alifikia kushawishika kwa dhati kuwa ndani ya miaka ishirini na tano Kristo angetokea kuwakomboa watu Wake. “Sihitaji kusema,” Miller alisema, “kuhusu furaha iliyoujaza moyo wangu nikitafakari juu ya matazamio yenye furaha, na juu ya shauku kuu ya roho yangu ya kushiriki katika furaha za waliokombolewa. Biblia sasa kikawa kitabu kipya kwangu. Biblia ilikuwa chakula cha fikra; kila jambo lililoonekana kuwa giza, la siri, au lisiloeleweka kwangu katika mafundisho yake, liliyeyuka kutoka katika akili yangu mbele ya nuru angavu ambayo sasa ilipambazuka kutoka katika kurasa zake takatifu; na, ndiyo, ukweli ulikuwa na mwangaza na utukufu mwingi kiasi gani! Mambo yote yaliyokuwa yakionekana kupingana na kutopatana ambayo niliyaona katika neno la Mungu yaliyotoweka; na ingawa kulikuwa na maeneo mengi ambayo nilikuwa sijaridhika kuwa nimepata uelewa kamili, hata hivyo nuru kubwa ilitoka katika Maandiko iliangazia akili yangu ambayo kabla ya hapo ilikuwa gizani, kiasi kwamba nilifurahia kujifunza Maandiko ambayo hapo awali sikudhani kuwa ningeweza kuipata katika mafundisho yake.”—Bliss, ukurasa 76, 77.PKSw 251.4

    “Pamoja na kushawishika sana kuwa matukio makuu hayo yalitabiriwa katika Maandiko na kuwa yalitarajiwa kutimizwa katika muda mfupi sana, suala lilikuja moyoni kwa nguvu nyingi lilihusiana na wajibu wangu kwa ulimwengu, kutokana na ushahidi ambao ulikuwa umegusa akili yangu.”— Ibid., ukurasa 81. Hakuwa na njia nyingine isipokuwa kuhisi kuwa ilikuwa wajibu wake kuwaeleza wengine nuru aliyokuwa ameipokea. Alitarajia kukutana na upinzani kutoka kwa watu wasiomcha Mungu, lakini alikuwa na hakika kuwa Wakristo wote wangefurahia katika tumaini la kukutana na Mwokozi ambaye walikiri kumpenda. Hofu yake pekee ilikuwa kwamba katika furaha yao kubwa ya matarajio ya ukombozi wenye utukufu, uliokuwa tayari kukamilika, wengi wao wangepokea fundisho hilo bila kuchunguza kikamilifu Maandiko yaliyoeleza ukweli wake. Hivyo, alisita kuuwasilisha, isije ikawa pengine amekosea na yeye kuwa njia ya kuwapoteza wengine. Hivyo aliongozwa kupitia upya ushahidi uliounga mkono hitimisho alilofikia, na kufikiria kwa uangalifu kila ugumu uliojitokeza katika akili yake. Aliona kuwa kila kipingamizi kiliyeyuka mbele ya nuru ya neno la Mungu, kama ukungu unavyoyeyuka katika miale ya jua. Miaka iliyotumika kwa njia hiyo ilimwacha akiwa ameshawishika kikamilifu kuhusu usahihi wa msimamo wake.PKSw 252.1

    Na sasa wajibu wa kuhakikisha kuwa wengine wanafikishiwa kile ambacho aliamini kuwa kilifundishwa kwa uwazi katika Maandiko, ulimjia kwa nguvu mpya. “Nilipokuwa nikiendelea kufanya shughuli zangu,” alisema, “uliendelea daima kupiga kengele masikioni mwangu, ‘Nenda ukauambie ulimwengu hatari inayowakabili.’ Aya hii ilidumu kumjia akilini mwake: ‘Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako” (Ezekieli 33:8, 9). Nilihisi kuwa ikiwa watu waovu wangeonywa kikamilifu, wengi wao wangetubu; na kuwa ikiwa wasingeonywa, damu yao ingedaiwa mikononi mwangu.”—Bliss, ukurasa 92.PKSw 252.2

    Alianza kuwasilisha mawazo yake kwa mtu mmoja mmoja kwa kadiri fursa zilivyojitokeza, akiombea kuwa mchungaji fulani aguswe na nguvu ya mafundisho yake na ajitolee kuyatangaza. Lakini hakuweza kuondoa wazo kuwa alikuwa na wajibu binafsi wa kufanya katika kutoa onyo hilo. Maneno yalikuwa yakirudia akilini mwake: “Nenda kauambie ulimwengu; damu yao nitaitaka mikononi mwako.” Kwa muda wa miaka tisa alisubiri, mzigo ukiwa bado unalemea moyo wake, mpaka mwaka 1831 ambapo kwa mara ya kwanza aliwasilisha hadharani sababu za imani yake.PKSw 253.1

    Kama Elisha alivyoitwa kuacha kufuatana na ng'ombe waliokokota jembe la kulima mashambani, na kupokea joho la wakfu kwa ajili ya kazi ya kinabii, kadhalika William Miller aliitwa na kuacha plau yake na kujiweka wakfu kuwafunulia watu siri za ufalme wa Mungu. Akiwa katika hali ya kutetemeka, alianza kazi yake, akiwaongoza wasikilizaji wake pole pole, hatua kwa hatua, na kuwapitisha katika vipindi mbalimbali vya kiunabii hadi ujio wa pili wa Kristo. Kwa kila juhudi alipata nguvu na ujasiri alipoona shauku ya watu wengi ikiongezeka kutokana na maneno yake.PKSw 253.2

    Ilikuwa kwa njia ya maombi ya rafiki zake tu, ambapo katika maneno yao alisikia wito wa Mungu, akiwa mtu mzima, asiye na uzoefu wa kuongea hadharani, na akilemewa na mzigo wa hisia ya kutokufaa kwake kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yake. Lakini tangu hotuba yake ya kwanza kazi zake zilibarikiwa kwa namna ya ajabu sana kwa ajili ya wokovu wa roho. Hotuba yake ya kwanza ilifuatwa na mwamko wa kidini ambapo wanafamilia wote wa familia kumi na tatu, isipokuwa watu wawili, waliongoka. Muda mfupi baadaye aliitwa kuhubiri katika maeneo mengine, na karibu katika kila mahali kazi yake ilileta uamsho wa kazi ya Mungu. Wenye dhambi walioongolewa, Wakristo walihamasishwa kujiweka wakfu kikamilifu zaidi, na wanaoamini kuwa Mungu aliuumba ulimwengu halafu akaucha ujiendeshe wenyewe na wakana Mungu waliongozwa kukiri ukweli wa Biblia na dini ya Kikristo. Ushuhuda wa wale ambao miongoni mwao aliwafundisha ulikuwa: “Tabaka fulani la akili limefikiwa na mtu ambaye haendeshwi na mvuto wa watu wengine.”—Ibid., ukurasa 138. Mahubiri yake yalikusudiwa kuamsha akili za jamii ili zitafakari mambo makubwa ya dini na kudhibiti hali ya udunia iliyokuwa ikikua na tamaa za kizazi kile.PKSw 253.3

    Karibu katika kila mji kulikuwepo na makundi ya watu, wengine, wakiwa katika mamia, walioongoka kama matokeo ya mahubiri yake. Katika maeneo mengi makanisa ya Kiprotestanti ya karibu ya madhehebu zote yaliwekwa wazi kwa ajili yake, na miito kwa ajili ya kufanya kazi daima ilitoka kwa wachungaji wa makanisa kadhaa. Ilikuwa kanuni yake ya kudumu kutohubiri katika makansia ambayo hakuitwa, hata muda mfupi baadaye alijikuta hawezi kutimiza nusu ya maombi yaliyokuwa yamefurika kwake. Wengi wa wale ambao hawakukubali mawazo yake ya wakati mahsusi wa ujio wa pili walishawishika kuhusu uhakika na ukaribu wa ujio wa Kristo na hitaji lao la kujiandaa. Katika baadhi ya miji mikubwa kazi yake ilileta mguso mkubwa sana. Wauza pombe waliacha biashara yao na kugeuza vilabu vyao kuwa vyumba vya mikutano; vituo vya kuchezea kamari vilivunjwa; wasioamini, waumini uwepo wa Mungu asiyejishughulisha na viumbe wake, Waumini wa uwepo wa ukweli usiopingika, na hata mafisadi wa kutupwa walifanya matengenezo, ambao baadhi yao walikuwa hawajakanyaga kanisani kwa miaka mingi. Mikutano ya maombi ilianzishwa na madhehebu mbalimbali, katika maeneo mbalimbali, karibu kila saa; wafanyabiashara walikutana wakati wa mchana kwa ajili ya maombi na kumsifu Mungu. Hakukuwa na misisimko bandia, badala yake kulikuwa na kicho katika mawazo ya watu karibu wote. Kazi ya William Miller, kama ilivyokuwa ya Wanamatengenezo wa awali, ilikuwa na mwelekeo wa kushawishi ufahamu na kuamsha dhamiri kuliko kusisimua hisia peke yake.PKSw 253.4

    Mwaka 1833 Miller alipokea leseni ya kuhubiri, kutoka katika Kanisa la Kibaptisti, ambalo yeye alikuwa mshiriki wake. Idadi kubwa ya wachungaji wa madhehebu yake waliidhinisha kazi yake, na aliendelea na kazi zake kwa kibali chao rasmi. Alisafiri na kuhubiri kwa muda wote mfululizo bila kupumzika, ingawa kazi zake binafsi kimsingi zilikomea katika majimbo ya New England na Middle States. Kwa miaka kadhaa gharama zake zote zilitoka katika mfuko wake binafsi, na baadaye hakuweza kupata fedha ya kutosha kumwezesha kwenda kila mahali alikoalikwa. Kwa hiyo kazi zake za hadhara, zikiwa hazina ya lengo la kujipatia fedha, ziligeuka kuwa mzigo mzito kwake kwa kuwa hakuwa na kipato kikubwa, ambacho pole pole kiliendelea kupungua katika kipindi hiki cha maisha yake. Alikuwa baba wa familia kubwa, lakini kwa kuwa wote walikuwa wabanaji wazuri wa matumizi na wenye bidii kubwa ya kazi, shamba lake lilitosha kuwapa kipato cha kujikimu kama familia na cha kusaidia katika kazi zake za kuhubiri injili.PKSw 254.1

    Mwaka 1833, miaka miwili baada ya Miller kuanza kuwasilisha hadharani ushahidi wa ujio wa haraka wa Kristo, ishara ya mwisho miongoni mwa ishara zilizoahidiwa na Mwokozi kama dalili za ujio Wake wa pili. Yesu alisema: “Nyota zitaanguka mbinguni” (Mathayo 24:29). Na Yohana katika kitabu cha Ufunuo, alipoona katika njozi matukio ambayo yangeashiria siku ya Mungu: “Na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi” (Ufunuo 6:13). Unabii huu ulitimizwa kiajabu na kikamilifu kwa mvua ya vimondo ya Novemba 13, 1833. Hilo lilikuwa onesho lililoshuhudiwa eneo kubwa na la ajabu duniani la nyota kuanguka kwa namna ambayo haijapata kutokea na kuandikwa kabla ya hapo; “anga lote, juu ya nchi yote ya Marekani, ambalo, kwa saa kadhaa, lilikuwa katika misuko-suko ya kuwaka moto! Hakuna tukio kama lile lilowahi kutokea katika anga la nchi ya Marekani, tangu watu walipoanza kuishi katika nchi ile, ambalo lilitazamwa na tabaka moja la watu katika jamii kwa shauku kubwa, na kuangaliwa kwa hofu na taharuki kuwa na tabaka jingine.” “Fahari yake na uzuri wa ajabu ungali bado katika akili za watu walio wengi.... Hakuna mvua yo yote iliyowahi kunyesha duniani iliyokuwa nzito zaidi kuliko ile ya vimondo; mashariki, magharibi, kaskazini, na kusini, ilikuwa sawasawa, anga lote lilikuwa katika hali ya mtikisiko mkubwa.... Onesho hilo, kama lilivyoelezwa na Jarida la Profesa Silliman, lilishuhudiwa katika anga lote la Amerika ya Kaskazini.... Tangu saa nane alfajiri mpaka wakati wa mchana wote, anga likiwa katika utulivu mkamilifu na bila mawingu, mchezo endelevu wa vitu vinavyong'aa sana vilidumu kuonekana katika anga lote.”—R. M. Devens, American Progress; or, The Great Events of the Greatest Century, ch. 28, pars.1-5.PKSw 254.2

    “Hakuna lugha, kwa hakika, inayoweza kuelezea mwonekano wa mg'aro ule wa ajabu; ... hakuna mtu hata mmoja ambaye hakushuhudia anaweza kuelewa kikamilifu dhana ya utukufu wa tukio lile. Ilionekana kana kwamba mbingu zenye nyota zilikuwa zimekusanyika pamoja karibu na kilele juu yao, na wakati huo huo zilikuwa zikirusha, kwa kasi ya mwanga, kila upande wa upeo; na bado hazikuchoka—maelfu ya vipande vya nyota kwa haraka vikifuatiwa na maelfu mengine ya vipande vya nyota, kana kwamba viliumbwa kwa ajili hiyo.”—F. Reed, in the Christian Advocate and Journal, Dec. 13, 1833. “Mwonekano sahihi wa mtini unaopukutisha mapooza yake unapopulizwa na upepo wenye nguvu, ilikuwa haiwezekani kuangalia.”— “The Old Countryman,” in Portland Evening Advertiser, Novemba 26, 1833.PKSw 255.1

    Katika jarida la New York Journal of Commerce la Novemba 14, 1833, ilichapishwa makala kuhusu tukio hili la ajabu, ikiwa na kauli hii: “Hakuna mwanafalsafa au msomi aliyewahi kusimulia au kuandika kumbukumbu ya tukio, ninadhani, kama lile la jana asubuhi. Nabii miaka elfu moja na mia nane iliyopita aliwahi kusimulia vizuri, ikiwa tutapata taabu ya kuelewa nyota kuanguka kumaanisha nyota zinazoanguka,.... katika maana pekee ambayo inawezekana kuwa halisi.”PKSw 255.2

    Hivyo ndivyo ilivyoonekana ishara ya mwisho miongoni mwa dalili za ujio wa Kristo, ambazo Yesu aliwaasa wanafunzi Wake: “Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni” (Mathayo 24:33). Baada ya dalili hizi, Yohana aliona, kama tukio kuu linalotarajiwa baada ya hili, mbingu zikiondolewa kama ukurasa uliokunjwa, wakati dunia ikitetemeka, milima na visiwa vikiondolewa mahali pake, na waovu kwa hofu wakiukimbia uso wa Mwana wa Adamu (Ufunuo 6:12-17).PKSw 255.3

    Wengi wa walioshuhudia kuanguka kwa nyota, waliliona kama ujumbe wa ujio wa hukumu, “tukio la kutisha, mtangulizi wa hakika, ishara ya rehema, ya siku ile kuu ya kutisha.”—“The Old Country-man,” in Portland Evening Advertiser, Novemba 26, 1833. Hivyo mawazo na macho ya watu yalielekezwa kwa utimizo wa unabii, na wengi waliongozwa kuzingatia onyo la ujio wa pili wa Kristo.PKSw 256.1

    Mwaka 1840 utimizo mwingine wa ajabu wa unabii uliamsha shauku kubwa ya watu. Miaka miwili kabla, Josiah Litch, mmoja wa wachungaji mashuhuri akihubiri juu ya ujio wa pili, alichapisha ufafanuzi wa Ufunuo 9, akitabiri anguko la Himaya ya Otomani. Kwa mujibu wa ukokotoaji wake, utawala huu ulipaswa kupinduliwa “mwaka B.K. 1840, wakati fulani katika mwezi wa Agosti;” na siku chache kabla ya utekelezwaji wake aliandika: “Akiruhusu kipindi cha kwanza, miaka 150, kutimizwa kikamilifu kabla ya Deacozes hajapewa ufalme kwa ruhusa ya Waturuki, na kwamba miaka 391, siku kumi na tano, kilianzia mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kingeishia Agosti 11, 1840, wakati mamlaka ya Otomani juu ya Konstantinopo ilitarajiwa kufikia mwisho. Na hili, niliamini, litatokea hivyo hivyo.”—Josiah Litch, in Signs of the Times, and Expositor of Prophecy, August 1, 1840.PKSw 256.2

    Wakati mahsusi uliotajwa, Uturuki, kupitia mabalozi wake, ilikubali ulinzi wa mamlaka ya umoja wa mataifa ya Ulaya, na kwa njia hiyo ilijiweka chini ya udhibiti wa mataifa ya Kikristo. Tukio hili lilitimiza kikamilifu utabiri. (Tazama Kiambatisho.) Ilipoeleweka vizuri, watu wengi walishawishika kuamini usahihi wa kanuni za tafsiri ya unabii zilizotumiwa na Miller na wenzake, na mwamko wa ajabu uliletwa katika vuguvugu la ujio wa pili. Watu wenye elimu na cheo waliungana na Miller, katika kuhubiri na kuchapisha mafundisho yake, na tangu 1840 hadi 1844 kazi ilipanuka haraka.PKSw 256.3

    William Miller alijaliwa uwezo mkubwa wa akili; na ikiwa imenidhamishwa kwa tafakari na usomaji; aliiongezea hekima ya mbinguni kwa kujiunganisha na Chanzo cha hekima. Alikuwa mtu mwenye uadilifu wa hali ya juu, ambaye katika hali zote alipewa heshima na kutambuliwa mahali popote uadilifu wa tabia na uzuri wa msimamo bora vilithaminiwa. Akichanganya ukarimu wa kweli kutoka moyoni na unyenyekevu wa Kikristo na nguvu ya kujitawala, alikuwa msikivu na mwepesi wa kufikiwa na watu wote, alikuwa tayari kusikia maoni ya wengine na kupima hoja zao. Bila uchungu wala mihemko alizipima nadharia zote na mafundisho yote kwa neno la Mungu, na mpangilio wake wa hoja na ujuzi mkubwa wa Maandiko vilimwezesha kupinga makosa na kuanika uongo.PKSw 256.4

    Pamoja na hayo aliendesha kazi yake katikati ya upinzani mkali. Kama ilivyokuwa kwa Wanamatengenezo wa awali, ukweli aliouwasilisha haukupokelewa na walimu mashuhuri wa dini. Kwa kuwa watu hawa hawakuweza kutetea hoja zao kwa kutumia Maandiko, walilazimika kutumia misemo na mafundisho ya wanadamu, na mapokeo ya viongozi wa makanisa waliopita. Lakini neno la Mungu lilikuwa ushuhuda pekee uliokubaliwa na wahubiri wa ukweli wa marejeo. “Biblia, na Biblia pekee,” ilikuwa ndiyo kanuni kuu. Kukosekana kwa nguvu ya Maandiko kwa upande wa wapinzani wao kulijazwa na matusi na dhihaka. Muda, pesa, na talanta vilitumiwa kuwachafua watu ambao kosa lao pekee lilikuwa kutazamia kwa furaha ujio wa Bwana wao na kujaribu kuishi maisha matakatifu na kuwasihi wengine wajiandae kwa ajili ya ujio Wake.PKSw 257.1

    Juhudi kubwa zilitumiwa kuvuta akili za watu mbali na somo la ujio wa pili. Mbinu zilitumika ionekane kana kwamba ni dhambi, kana kwamba ni jambo la kuonea aibu, kujifunza unabii unaohusiana na ujio wa Kristo na mwisho wa dunia. Kwa njia hiyo huduma ya kichungaji ya wakati huo ilidhalilisha imani katika neno la Mungu. Mafundisho yao yaliwafanya watu wawe wapagani, na wengi walitiwa moyo kufuata njia zao za tamaa zinazopingana na Mungu. Waasisi wa maovu waliwasingizia Waadventista kuwa ndio waliotenda maovu waliyoyaasisi wao.PKSw 257.2

    Wakati alikusanya na kujaza nyumba wasikilizaji wenye akili na walio makini, jina la Miller kwa nadra sana lilitajwa katika vyombo vya habari vya kidini isipokuwa kwa kusudi la kumdhihaki au kumpinga. Wasiojali na wasiomcha Mungu wakiwa wametiwa moyo na mafundisho ya walimu wa dini, walimwita majina ya utani ya kumdhihaki, na kumdhalilisha kwa vichekesho vyenye maneno na misemo ya kufuru, katika juhudi za kurundika matusi juu yake na juu ya kazi yake. Mzee mwenye mvi aliyekuwa ameacha nyumba yake nzuri na kusafiri kwa gharama yake kutoka jiji moja hadi jingine, kutoka mji hadi mji mwingine, akifanya kazi bila kupumzika akitoa onyo zito kwa ulimwengu juu ya hukumu iliyo karibu, alikataliwa kwa kejeli kama mtu anayeshikilia sana mambo bila kutumia akili, laghai, na tapeli.PKSw 257.3

    Maneno ya dhihaka, uongo, na matusi yaliyorundikwa juu ya Miller yalialika matamko makali kutoka katika vyombo vya habari, hata visivyokuwa vya kidini, dhidi ya wapinzani wake.” Kushughulikia jambo nyeti na lenye matokeo ya kutisha kama hilo,” kwa dhihaka na kejeli kulitangazwa na kidunia kuwa “siyo tu kuumiza hisia za wahubiri na watetezi wao,” bali “kudhihaki siku ya hukumu na kumpuuza Mungu Mwenyewe, na kubeza vitisho vya hukumu Yake.”—Bliss, ukurasa wa 183.PKSw 257.4

    Mwasisi wa maovu yote alitafuta siyo tu kufuta matokeo ya ujumbe wa marejeo, bali pia kumwangamiza mjumbe nwenyewe. Miller alihubiri ukweli wa Maandiko kama ulivyo na kugusa mioyo ya wasikilizaji wake, akiwaonya makosa yao na kusumbua kuridhika kwao, na maneno yake yaliyokata moja kwa moja yalimwamsha adui yao. Upinzani uliooneshwa na washiriki wa kanisa dhidi ya ujumbe wake uliwafanya wasiomcha Mungu kwenda mbali zaidi katika uovu wao; na maadui walipanga jinsi ya kuondoa uhai wake wakati akiondoka kutoka mahali pa mkutano. Lakini malaika watakatifu walikuwa katikati ya kundi la watu, na mmoja wa malaika hawa, akiwa katika umbo la mwanadamu, aliushika mkono wa mtumishi wa Bwana na kwa kumwondoa kwa usalama kutoka katikati ya kundi la watu wenye hasira. Kazi ya Miller ilikuwa haijaisha, na Shetani na wafuasi wake walishindwa kutekeleza kusudi lao.PKSw 258.1

    Licha ya upinzani wote, shauku katika vuguvugu la ujio wa pili iliendelea kukua. Tangu makumi na mamia, makanisa yalikua na kufikia hadi kuwa maelfu mengi. Waumini wapya wengi walijiunga na makanisa, lakini baada ya muda mfupi roho ya upinzani ilidhihirishwa dhidi ya hata waongofu hawa wapya, na makanisa yalianza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wale waliokumbatia mawazo ya Miller. Hatua hii ilisababisha Miller kujibu kwa njia ya kalamu yake, akawasiliana na Wakristo wa madhehebu yote, akisisitiza kuwa ikiwa mafundisho yake yalikuwa ya uongo, aoneshwe kosa lake kutoka katika Maandiko.PKSw 258.2

    “Ni nini tunachokiamini,” alisema, “ambacho hatukuagizwa kuamini na neno la Mungu, ambalo ninyi wenyewe mnakubali kuwa ni kanuni, na kanuni pekee, ya imani na matendo yetu? Tumefanya nini kinachofanya tushambuliwe kwa maneno makali kutoka katika mimbari na vyombo vya habari, na kuwapa haki ya kutuondoa sisi (Waadventista) katika makanisa na ushirika wenu?” “Ikiwa tuna makosa, tunaomba mtuoneshe ni wapi tumekosea. Tuonesheni kutoka katika neno la Mungu mahali tulipokosea; tumetukanwa vya kutosha; hilo haliwezi kutushawishi tuamini kuwa tumekosea; neno la Mungu pekee ndilo linaweza kubadilisha mitazamo yetu. Majumuisho yetu yamepatikana kwa tafakari kubwa na maombi ya dhati, kwa kadiri tulivyoona ushahidi katika Maandiko.”—Ibid., ukurasa 250, 252.PKSw 258.3

    Tangu zama na zama maonyo ambayo Mungu aliyatuma kwa ulimwengu kwa njia ya watumishi Wake yalikutana na mashaka na kutoamini. Wakati uovu wa watu walioishi kabla ya gharika ulipomfanya Mungu alete gharika ya maji duniani, kwanza aliwaambia kusudi Lake, ili wapate fursa ya kugeuka na kuziacha njia zao. Kwa miaka mia moja na ishirini sauti ya onyo ilisikika ili watubu, ili ghadhabu ya Mungu isidhihirishwe kwa kuangamizwa kwao. Lakini ujumbe wa onyo ulionekana kama hadithi isiyokuwa na maana, na hawakuuamini. Wakipata ujasiri katika uovu wao walimdhihaki mjumbe wa Mungu, wakapuuza miito yake ya toba, na hata wakamshitaki kuwa alikuwa na kiburi. Inawezekanaje mtu mmoja kusimama dhidi ya watu wote wenye mamlaka duniani? Ikiwa ujumbe wa Nuhu ulikuwa wa kweli, kwa nini ulimwengu wote haukuuona na kuuamini? Mtu mmoja atoe hoja dhidi ya hekima ya watu maelfu! Hawakutilia maanani onyo, wala hawakutafuta hifadhi katika safina.PKSw 258.4

    Watu wenye dhihaka walionesha vitu katika maumbile ya asili,— kufuatana kusikobadilika kwa misimu, anga la bluu ambalo halijawahi kunyesha mvua, mapori ya kijani ambayo yalilowanishwa na umande laini wa usiku,—na walipiga kelele: “Si huyu anasema mifano?” Wakionesha dharau walimtangaza mhubiri wa haki kuwa mshikiliaji mkubwa wa mambo bila kutumia akili; na waliendelea, kwa shauku kubwa zaidi, kutafuta anasa, na walidhamiria kwenda katika njia za uovu zaidi, kuliko kabla ya hapo. Lakini kutokuamini kwao hakukuzuia tukio lililotabiriwa. Mungu alivumilia kwa muda mrefu uovu wao, akiwapa muda wa kutosha ili watubu; lakini kwa wakati uliopangwa hukumu Zake zilitekelezwa juu ya watu waliokataa rehema Yake.PKSw 259.1

    Kristo alisema kuwa kutakuwepo kutokuamini kama huko kuhusiana na ujio Wake wa pili. Kama vile watu wa wakati wa Nuhu ambao hawakutambua “hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo,” katika maneno ya Mwokozi wetu, ” kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:39). Wakati watu wanaodai kuwa watu wa Mungu wanapoungana na ulimwengu, wakiishi kama walivyo, na wakiungana nao katika anasa zilizokatazwa; wakati anasa za dunia zinapokuwa anasa za kanisa; wakati kengele za ndoa zinapolia, na watu wote wanatarajia kuwa na miaka ya mafanikio ya kidunia—ndipo, kwa ghafla kama vile umeme wa radi unavyomulika kutoka mbinguni, ndivyo utakavyokuja mwisho wa ndoto zao nzuri na matumaini yao ya uongo.PKSw 259.2

    Kama vile Mungu alivyomtuma mtumishi Wake kuuonya ulimwengu juu ya Gharika iliyokuwa inakuja, ndivyo alivyowatuma wajumbe waliochaguliwa ili wakatangaze ukaribu wa hukumu ya mwisho. Na kama vile watu wa wakati wa Nuhu walivyocheka na kudhihaki utabiri wa mhubiri wa haki, kadhalika katika wakati wa Miller wengi, hata miongoni mwa watu waliodai kuwa watu wa Mungu, walidhihaki maneno ya onyo.PKSw 259.3

    Na ni kwa nini mafundisho na mahubiri juu ya ujio wa pili wa Kristo hayakupokelewa na makanisa? Wakati kwa waovu ujio wa Bwana huleta kilio na uangamivu, kwa wenye haki umejaa shangwe na tumaini. Ukweli huu mkuu umekuwa faraja ya watu wa Mungu waaminifu katika zama zote; kwa nini ulikuja, kama Mwasisi wake, “jiwe likwazalo” na “mwamba uchukizao” kwa wanaodai kuwa watu Wake? Ni Bwana wetu aliyewaahidi wanafunzi Wake: “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu” (Yohana 14:3). Ni Mwokozi wetu mwenye huruma, ambaye, akitarajia upweke na huzuni ya wafuasi Wake, aliwatuma malaika wawafariji kwa kuwapa uhakikisho kuwa Yesu atarudi tena akiwa vilevile walivyomwona akienda mbinguni. Wanafunzi walipokuwa wamesimama wakitazama kwa makini juu kumwona anavyotoweka Yeye ambaye walimpenda, umakini wao ulikamatwa na maneno haya: “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo 1:11). Tumaini liliamshwa upya na ujumbe wa malaika. Wanafunzi “wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu” (Luka 24:52, 53). Walifurahia siyo kwa sababu ya Yesu kutengana nao na kuwaacha wapambane na majaribu na vishawishi vya ulimwengu, bali kwa sababu ya uhakikisho wa malaika kuwa Yesu atarudi tena.PKSw 259.4

    Utangazaji wa ujio wa Kristo unapaswa kuwa sasa, kama ulivyofanywa na malaika kwa wachungaji wa Bethlehemu, habari njema ya furaha kuu. Wanaompenda Mwokozi kwa dhati hawawezi kutulia bali wahubiri kwa furaha tangazo lililojengwa juu ya neno la Mungu kuwa Yule ambaye Kwake matumaini yao ya uzima wa milele yanapatikana anakuja tena, siyo kuja kutukanwa, kudharauliwa, na kukataliwa, kama ilivyokuwa wakati wa ujio Wake wa kwanza, bali katika nguvu na utukufu, kuwakomboa watu Wake. Ni wale wasiompenda Mwokozi wanaotamani asije, na hakuwezi kuwepo ushahidi hitimishi kuwa makanisa yamemwacha Mungu kuliko mwasho na uadui unaoamshwa na ujumbe huu uliotumwa kutoka mbiguni.PKSw 260.1

    Watu waliopokea fundisho la ujio wa pili wa Kristo waliamshwa na kuona umuhimu wa toba na unyenyekevu mbele ya Mungu. Watu wengi wamekuwa wakitanga-tanga kwa muda mrefu kati ya Kristo na ulimwengu; sasa walihisi kuwa ilikuwa wakati wa kuwa na msimamo. “Masuala ya umilele yalichukua sura ya uhalisia mpya. Mbingu ilisogezwa karibu yao, na walijisikia kuwa wenye hatia mbele ya Mungu.”—Bliss, ukurasa 146. Wakristo waliamshwa na kupata uzoefu mpya wa maisha ya kiroho. Waliongozwa kujisikia kuwa muda ulikuwa mfupi, kuwa kile walichopaswa kukifanya kwa ajili ya wanadamu wenzao ilipaswa kifanyike haraka. Dunia ilirudishwa nyuma, umilele ulionekana kufunguka mbele yao, na roho, pamoja na vyote vinavyohusiana na umilele wake, vilionekana kugubika mambo ya kidunia. Roho wa Mungu alikuwa pamoja nao na aliwapa nguvu za kutoa miito kwa ndugu zao, na kwa wenye dhambi, ili wajiandae kwa ajili ya siku ya Mungu. Ushuhuda wa kimya wa maisha yao ya kila siku ulikuwa karipio la daima dhidi ya washiriki wa makanisa wa mazoea na wasiojiweka wakfu kwa Mungu kikamilifu. Watu hawa hawakupenda kusumbuliwa katika shughuli zao za kutafuta raha, kazi zao za utafutaji wa pesa, na shauku zao za kupata heshima ya ulimwengu. Hivyo basi, uadui na upinzani viliamshwa dhidi ya imani ya ujio wa Kristo na watu waliotangaza imani hiyo.PKSw 260.2

    Kwa kadiri hoja zilizotokana na vipindi vya kiunabii zilivyoonekana kuwa zisizowezwa kupingwa, wapinzani walijaribu kuwakatisha tamaa watu wasijifunze somo hilo kwa kufundisha watu kuwa masuala ya unabii yalikuwa yametiwa muhuri. Hivyo basi, Waprotestanti walifuata nyayo za Waroma. Wakati kanisa la kipapa lilizuilia Biblia (tazama Kiambatisho) isionwe na watu, Makanisa ya kiprotestanti yalidai kuwa sehemu muhimu ya Neno Takatifu—na kwamba sehemu ambayo inaeleza ukweli, hususani, ukweli unaohusu wakati wetu—isingeweza kueleweka.PKSw 261.1

    Wachungaji na waumini walitangaza kuwa unabii wa Danieli na Ufunuo ulikuwa siri zisizoweza kueleweka. Lakini Kristo aliwaelekeza wanafunzi Wake wasome maneno ya nabii Danieli yanayohusu matukio ambayo yangetokea katika wakati wao, na alisema: “Asomaye na afahamu” (Mathayo 24:15). Na dai kuwa kitabu cha Ufunuo ni siri, na kuwa hakiwezi kueleweka, linapingwa na kitabu cha Ufunuo chenyewe: “Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi.... Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu” (Ufunuo 1:1-3).PKSw 261.2

    Nabii anasema: “Heri asomaye”—wapo ambao hawatasoma; mbaraka siyo wao. “Na wao wayasikiao”—wapo baadhi, pia, wanaokataa kusikia chochote kuhusu unabii; mbaraka siyo wa tabaka hili. “Na kuyashika yaliyoandikwa humo”—wengi wanakataa kusikia maonyo na mafundisho yaliyomo katika kitabu cha Ufunuo; hakuna hata mmoja anaweza kudai mbaraka ulioahidiwa. Wote wanaodhihaki masomo ya unabii na kufanyia mzaha mifano iliyotolewa kwa umakini mkubwa katika kitabu hiki, wote wanaokataa kufanya matengenezo ya maisha yao na kujiandaa kwa ajili ya ujio wa Mwana wa Adamu, hawatabarikiwa.PKSw 261.3

    Katika kuzingatia ushuhuda wa Uvuvio, watu wanadirikije kufundisha kuwa kitabu cha Ufunuo ni siri ambayo mwanadamu hawezi kuelewa? Kitabu cha Ufunuo ni siri ambayo imefunuliwa, ni kitabu ambacho kimefunuliwa. Mafundisho ya kitabu cha Ufunuo yanaelekeza akili kuchunguza unabii wa Danieli, na vyote viwili huwasilisha mafundisho muhimu sana, ambayo Mungu amempa mwanadamu, kuhusu matukio yanayotarajiwa kutokea wakati wa kufunga kwa historia ya ulimwengu huu.PKSw 261.4

    Yohana alifunuliwa mandhari za kina na zinazosisimua katika uzoefu wa kanisa. Aliona hali, hatari, migogoro, na ukombozi wa mwisho wa watu wa Mungu. Aliandika ujumbe wa mwisho utakaokomaza mavuno ya dunia, ama kama miganda ya nafaka kwa ajili ya ghala la mbinguni au mizigo ya kuni kwa ajili ya mioto ya maangamizi. Masomo ya muhimu sana yalifunuliwa kwake, hususani kwa ajili ya kanisa la siku za mwisho, kuwa wale ambao walitakiwa kuacha makosa na kuukumbatia ukweli walipaswa wafundishwe kuhusu hatari na migogoro iliyokuwa inakuja dhidi yao. Hakuna mtu hata mmoja ambaye anatakiwa kuwa gizani kuhusu kile kinachokuja duniani.PKSw 261.5

    Kwa nini, basi, watu wengi hawajui chochote kuhusu sehemu hii za Maandiko Matakatifu? Kwa nini watu wengi ni wazito kuchunguza mafundisho ya kitabu cha Ufunuo? Ni matokeo ya juhudi kubwa ya mfalme wa giza kuwaficha watu kile ambacho kinafunua uongo wake. Kwa sababu hiyo, Kristo Mfunuaji, akiona kabla vita ambayo ingepigwa dhidi ya mafundisho ya kitabu cha Ufunuo, alitangaza mbaraka kwa watu wote wanaosoma, kusikia, na kuchunguza maneno ya unabii wa kitabu cha Ufunuo.PKSw 262.1

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents