Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 14—Wanamatengenezo wa Baadaye Uingereza

    Wakati Luther alipokuwa akiifungua Biblia iliyokuwa imefungwa kwa watu wa Ujerumani, Roho wa Mungu alimsukuma Tyndale kufanya jambo hilo hilo kwa nchi ya Uingereza. Biblia ya Wycliffe ilikuwa imetafsiriwa kutokana na Biblia ya Kilatini, ambayo ilikuwa na makosa mengi. Haikuchapishwa, na gharama ya nakala ya muswada ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba watu wachache matajiri au wenye vyeo vya juu pekee ndio wangeweza kuinunua; na, zaidi ya hapo, kwa sababu ya kanisa kuipiga marufuku, ilikuwa na nafasi finyu sana ya kusambazwa. Mwaka 1516, mwaka mmoja kabla ya hoja za Luther, Erasmus alichapisha toleo lake la Kigiriki na Kilatini la Agano Jipya. Sasa kwa mara ya kwanza neno la Mungu lilichapishwa katika lugha ya asili. Katika toleo hili makosa mengi yaliyokuwa katika matoleo ya nyuma yalisahihishwa, na maana ilitolewa kwa uwazi zaidi. Iliwaongoza wengi miongoni mwa matabaka ya wasomi kuwa na uelewa mzuri zaidi wa ukweli, na ilitolewa msukumo mpya kwa kazi ya matengenezo. Lakini watu wa kawaida bado, kwa kiwango kikubwa, walikuwa wamenyimwa neno la Mungu. Ilimpasa Tyndale amalizie kazi ya Wycliffe ya kuwapa watu wa nchi yake Biblia.PKSw 185.1

    Mwanafunzi mwenye bidii na mtafutaji wa dhati wa ukweli, alipokea injili kutokana na Agano Jipya la Kigiriki la Erasmus. Bila woga alihubiri imani yake, akikazia kuwa mafundisho yote inapaswa yapimwe kwa Maandiko. Na kwa dai la upapa kuwa kanisa ndilo lililotoa Biblia, na hivyo kanisa pekee ndilo lenye mamlaka ya kuifafanua, Tyndale alijibu: “Unamjua aliyemfundisha tai kutafuta mawindo? Ndiyo, Mungu yule yule anawafundisha watoto Wake wenye njaa kumtafuta Baba yao katika neno Lake. Mbali na kutotupatia Maandiko, ni ninyi wenyewe mlioyaficha ili tusiyaone; ni ninyi wenyewe mnaowachoma moto watu wanaoyafundisha, na kama mngeweza, mngechoma moto Maandiko yenyewe.”—D'Aubigne, History of the Reformation of the Sixteenth Century, b. 18, ch. 4.PKSw 185.2

    Mahubiri yaTyndale yaliamsha shauku kubwa; na watu wengi waliukubali ukweli. Lakini mapadri walikuwa macho, na mara tu alipoondoka eneo moja, kwa njia ya vitisho na upotoshaji, walijitahidi kuharibu kazi yake. Mara nyingi walifanikiwa. “Ni jambo gani lifanyike?” alisema. “Ninapokuwa nikipanda katika eneo moja, adui anashambulia eneo ambalo nimetoka. Siwezi kuwa kila mahali. O! ikiwa Wakristo wangekuwa na Maandiko Matakatifu katika lugha yao wenyewe, wao wenyewe wangeweza kuwakabili hawa wapotoshaji. Bila Biblia haiwezekani kuwaimarisha walei katika ukweli.”—Ibid., b. 18, ch. 4.PKSw 185.3

    Kusudi jipya lilikuja akilini.” Ilikuwa katika lugha ya Israeli“alisema,“zaburi ziliimbwa katika hekalu la Yehova; na je, agano jipya halipaswi kuongea nasi kwa Kiingereza miongoni mwetu? ... Je, kanisa si linapaswa kuwa na nuru kubwa zaidi wakati wa mchana kuliko wakati wa mapambazuko? ... Ni lazima Wakristo wasome Agano Jipya katika lugha yao wenyewe.” Wasomi na walimu wa kanisa hawakubaliani miongoni mwao wenyewe. Kwa njia ya Biblia pekee ndiyo wangeweza kuujua ukweli. “Mmoja anamfuata msomi huyu, mwingine yule.... Sasa kila mwandishi anampinga mwenzake. Tunaweza kujua ni yupi anasema ukweli na ni anasema uongo? ... Kwa njia gani? ... Kwa haki ni kwa njia ya neno la Mungu.”—Ibid., b. 18, ch. 4.PKSw 186.1

    Haikuchukua muda mrefu ambapo msomi mmoja wa Kikatoliki alisema: “Ni afadhali tusingekuwa na amri za Mungu kuliko kuwa na amri za papa” Tyndale alijibu: “Ninampinga papa na sheria zake; na ikiwa Mungu atahifadhi maisha yangu, kabla ya miaka mingi kupita nitamfanya mvulana anayelima kwa jembe la kukokotwa na ng'ombe ayajue Maandiko kuliko wewe unavyoyajua.”—Anderson, Annals of the English Bible, uk. 19.PKSw 186.2

    Kusudi ambalo alikuwa ameanza kulifikiria, la kuwagawia watu Maandiko ya Agano Jipya katika lugha yao wenyewe, sasa lilithibitika, na mara moja alianza kulitekeleza. Mateso yalipomfukuza nyumbani, alikimbilia mjini London, na pale, kwa muda fulani alifanya kazi zake bila usumbufu. Lakini tena fujo za watetezi wa upapa zilimlazimisha kukimbia. Uingereza yote ilionekana imefungwa dhidi yake, hivyo aliamua kutafuta hifadhi katika nchi ya Ujerumani. Hapa alianza kuchapa Agano Jipya la Kiingereza. Kazi ilisimamishwa mara mbili; lakini alipokatazwa kuchapisha katika jiji moja, alikwenda katika jiji jingine. Hatimaye alielekea katika jiji la Worms, ambapo, miaka michache kabla, Luther alitetea injili mbele ya Baraza Kuu la Kitaifa. Katika jiji lile la zamani walikuwepo marafiki wengi wa Matengenezo, na Tyndale pale alifanya kazi yake bila vikwazo zaidi. Nakala elfu tatu za Agano Jipya muda si mrefu zilikamilika, na toleo jingine lilifuata mwaka ule ule.PKSw 186.3

    Kwa juhudi kubwa na uvumilivu mwingi aliendelea na kazi zake. Pamoja na kwamba mamlaka za Kiingereza zililinda bandari zake kwa ulinzi makini sana, neno la Mungu, kwa njia mbalimbali, lilisafirishwa kwa siri hadi jijini London na kutokea hapo lilisambaa katika nchi nzima. Watetezi wa upapa walijaribu kuukandamiza ukweli, lakini bila mafanikio. Askofu wa Durham wakati mmoja alinunua kwa mwuzaji wa vitabu aliyekuwa rafiki wa Tyndale Biblia zote alizokuwa nazo, kwa kusudi la kuziharibu, akidhani kuwa kwa kufanya hivyo angeweza kuizuia kazi kwa kiwango kikubwa. Lakini, kinyume chake, pesa zilizopatikana kwa njia hiyo, zilitumiwa kununua karatasi za kuchapia toleo jipya na bora zaidi, ambalo, kama isingekuwa kwa njia hiyo, lisingeweza kuchapishwa. Wakati Tyndale alipofungwa gerezani, alipewa fursa ya kuachiliwa uhuru kwa sharti la kutaja majina ya watu waliomsaidia kupata fedha za kuchapishia Biblia zake. Alijibu kuwa askofu wa Durham alikuwa amemsaidia zaidi kuliko watu wengine wote; kwa kumlipa pesa nyingi kwa ajili ya vitabu vilivyokuwa vimebaki mkononi, alimwezesha kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa.PKSw 186.4

    Tyndale alisalitiwa na kuingia katika mikono ya maadui zake, na wakati mmoja alifungwa gerezani kwa miezi mingi. Hatimaye alishuhudia kwa ajili ya imani yake kwa kifo cha mfia dini; lakini silaha alizoziandaa zimewawezesha askari wengine kupigana vita katika karne zote hadi wakati wetu huu.PKSw 187.1

    Latimer alihubiri kutoka mimbarani kuwa Biblia ilipaswa kusomwa katika lugha ya watu. Mwasisi wa Maandiko Matakatifu, alisema, “ni Mungu Mwenyewe;” na Maandiko haya yanashiriki nguvu na umilele wa Mwasisi wake. “Hakuna mfalme, mkuu wa dola, hakimu, wala mtawala ... ambaye hapaswi kulitii... neno Lake” “Hebu tusitembee katika njia zetu wenyewe, bali neno la Mungu lituongoze: tusiwafuate... mababu zetu, wala tusiangalie waliyoyafanya, bali tuyaangalie yale ambayo walipaswa kuyafanya.”—Hugh Latimer, “First Sermon Preached Before King Edward VI”PKSw 187.2

    Barnes na Frith, marafiki waaminifu wa Tyndale, waliinuka kuutetea ukweli. Ridleys na Cranmer walifuata. Viongozi hawa katika Matengenezo ya Uingereza walikuwa wasomi, na wengi wao waliheshimiwa sana kwa bidii yao au uchaji wao miongoni mwa wanajumuia wa Kirumi. Upinzani wao kwa upapa ulitokana na ugunduzi wao wa makosa “kiongozi mkuu wa kanisa” Ugunduzi wao wa siri za Babeli uliwapa nguvu ya ushuhudiaji dhidi yake.PKSw 187.3

    “Sasa niulize swali la ajabu,” alisema Latimer. “Ni askofu au kasisi yupi aliye na bidii zaidi kuliko wote katika nchi nzima ya Uingereza? ... Ninakuona ukisikiliza na ukisubiri kwa hamu kubwa nimtaje .... Ninakuambia: ni Shetani.... Yeye haondoki katika jimbo lake; mwite wakati wowote unapomtaka, yuko nyumbani daima; ... yeye yuko kwenye jembe lake la kukokotwa na ng'ombe.... Huwezi kumkuta wakati wowote akijikalia kivivu, nakuhakikishia.... Mahali Shetani alipo, ... pale hakuna vitabu, badala yake kuna mishumaa; pale hakuna Biblia, badala yake kuna shanga; pale hakuna nuru ya injili, badala yake, kuna nuru ya mishumaa, ndiyo, nyakati za mchana; ... msalaba wa Kristo upo chini, uchumaji wa fedha kwa njia ya pagatori(toharani) uko juu; ... hakuna kuwavika walio uchi, maskini, wasiojiweza, badala yake kuna kuabudu sanamu na kupamba kwa uchangamfu vitu visivyokuwa na uhai; mapokeo na sheria ya mwanadamu vimeinuliwa juu, mapokeo ya Mungu na neno Lake takatifu sana vimeshushwa chini.... O! kwamba makasisi wetu wangekuwa na bidii ya kupanda mbegu ya mafundisho mazuri, kama Shetani alivyo na bidii ya kupanda kila aina ya magugu!”—Ibid., “Sermon of the Plough.”PKSw 187.4

    Kanuni kuu iliyoshikiliwa na hawa Wanamatengenezo—kanuni ile ile iliyoshikiliwa na Wawaldensia, na Wycliffe, na John Huss, na Luther, Zwingli, na wale walioungana nao—ilikuwa mamlaka isiyokosea ya Maandiko Matakatifu kama kanuni ya imani na matendo. Walitupilia mbali haki ya mapapa, mabaraza, Mababa, na wafalme, kutawala dhamiri katika masuala ya dini. Biblia ndiyo iliyokuwa mamlaka yao, walipima mafundisho na madai yote kwa mafundisho yake. Imani kwa Mungu na neno Lake viliwashikilia watu hawa watakatifu walipoachia maisha yao kwenye nguzo ya kuchomea moto watu. “Farijikeni,” alisema Latimer akiwaambia wenzake wakati ndimi za moto zilipokuwa karibu kunyamazisha sauti zao, “leo tunawasha mshumaa, kwa neema ya Mungu, katika nchi ya Uingereza, ambao ninaamini hautazimwa kamwe.”—Works of Hugh Latimer 1:8.PKSw 188.1

    Katika nchi ya Scotland mbegu za ukweli zilizotawanywa na Columba na watendakazi wenzake hazikuharibiwa kabisa. Kwa miaka mamia baada ya makanisa ya Uingereza kujisalimisha kwa utawala wa Rumi, makanisa ya Scotland walidumisha uhuru wao. Katika karne ya kumi na mbili, hata hivyo, upapa ulianzishwa hapa, na hakuna nchi ambayo utawala wa Rumi ulikuwa na nguvu zaidi kuliko iliyokuwa nayo katika nchi ya Scotland. Hakuna mahali ambako giza lilikuwa nene zaidi kuliko lililokuwepo katika nchi ya hii. Lakini bado ilikuja miale ya nuru iliyopasua giza na kutoa ahadi ya mchana unaokuja. Waloladi, waliokuja kutoka Uingereza wakiwa na Biblia na mafundisho ya Wycliffe, walifanya kazi kubwa ya kuhifadhi ukweli wa injili, na kila karne ilikuwa na mashahidi na wafia dini wake.PKSw 188.2

    Pamoja na ufunguaji wa Matengenezo Makuu yalikuja maandishi ya Luther, na halafu Agano Jipya la Kiingereza la Tyndale. Bila kuonwa na uongozi wa kanisa la Rumi, wajumbe hawa walizunguka kimya kimya katika milima na mabonde, na kuwasha upya mwenge wa ukweli ambao ulikuwa karibu kuzimika katika nchi ya Scotland, na kusahihisha makosa yaliyoingizwa na Urumi kwa karne nne za ukandamizaji wake.PKSw 188.3

    Halafu damu ya wafia dini ilileta msukumo mpya kwa vuguvugu. Viongozi wa upapa, wakiamka kwa ghafla kuhusiana na hatari iliyotishia kazi yao, waliwaleta pamoja watu mashuhuri wazaliwa wa Scotland ili kuwachoma moto. Walijenga jukwaa kubwa kwa ajili ya kuwachomea moto, ambapo maneno ya mashahidi waliokuwa wakifa yalisikika katika nchi nzima, yakisisimua roho za watu kwa kusudi la kutokukata tamaa na yakawapa hamasa ya kujivua minyororo ya Roma.PKSw 188.4

    Hamilton na Wishart, watu wema katika tabia na katika kuzaliwa, wakiacha nyuma yao msururu mrefu wa wanafunzi, walitoa maisha yao wachomwe moto jukwaani. Kutoka miongoni mwa wanafunzi wa Wishart alitokea mmoja ambaye ndimi za moto hazikuwa tishio kwake, ambaye chini ya uongozi wa Mungu alipiga pigo la mauti kwa upapa katika nchi ya Scotland.PKSw 189.1

    John Knox alikuwa ameachana na mapokeo na imani za kishirikina za kanisa, ili kujilisha kweli za neno la Mungu; na fundisho la Wishart lilikuwa limethibitisha azimio lake la kuacha ushirika wa Rumi na kujiunga na Wanamatengenezo walioteswa.PKSw 189.2

    Aliposhauriwa na marafiki zake afanye kazi ya kuhubiri, alikataa akitetemeka kwa uzito wa jukumu hilo, na ilikuwa baada ya siku nyingi za kujitenga na mgogoro wenye maumivu makali ndani ya nafsi yake mwenyewe aliweza kukubali. Lakini, mara tu alipokubali kazi hiyo, alisonga mbele akiwa na nia isiyoyumba na ujasiri usioshindwa kwa kadri alivyodumu kuwa hai. Mwanamatengenezo huyu mwenye moyo wa dhati hakuogopa uso wa mtu. Mioto ya kuunguza wafia dini, ikirusha ndimi zake kila upande wake, ilimchochea kuwa na bidii zaidi. Wakati alipotishiwa kuwa shoka la mtesaji katili litainuliwa juu ya kichwa chake, alisimama imara, akapiga mapigo mazito upande wa kulia na upande wa kushoto na kuvunja -vunja ibada ya sanamu.PKSw 189.3

    Alipoletwa mbele ya malkia wa Scotland, ambaye mbele yake juhudi za Waprotestanti wengi zilipungua, John Knox alitoa ushuhuda usioyumba kwa ajili ya ukweli. Hakushindwa kwa kubembelezwa; hakurudi nyuma kwa sababu ya vitisho. Malkia alimshitaki kwa kosa la uzushi. Alikuwa akiwafundisha watu wapokee dini iliyopigwa marufuku na serikali, malkia alisema, na kwa sababu hiyo John Knox alikuwa amevunja amri ya Mungu inayowataka raia kuwatii viongozi wa serikali. Knox alijibu kwa ujasiri:PKSw 189.4

    “Kwa kuwa dini ya kweli haipokei nguvu yake ya asili wala mamlaka kutoka kwa wakuu wa dunia, bali kutoka kwa Mungu wa milele pekee, kadhalika raia hawalazimiki kujenga dini yao kulingana na matakwa ya wakuu wao. Kwa kuwa mara nyingi, wakuu wa kidunia huwa hawana ujuzi wa dini ya kweli ya Mungu kuliko watu wengine wote.... Ikiwa wazao wote wa Ibrahimu wangekuwa wa dini ya Farao, ambao walikuwa raia wake kwa muda mrefu, ninakuomba, mama, kungekuwa na dini gani ulimwenguni? Au ikiwa watu wote katika siku za mitume wangekuwa wa dini ya wafalme wa Rumi, ni dini gani ingekuwepo kwenye uso wa dunia? ... Na kwa hiyo, mama, unaweza kuelewa kuwa raia hawalazimiki kutii dini ya wakuu wao, japokuwa wameamrishwa kuwatii.”PKSw 189.5

    Alisema Mary: “Mnatafsiri Maandiko kwa namna moja, na wao [walimu wa Wakatoliki wa Rumi] wanatafsiri kivyao; mimi nimwamini nani, na nani awe mwamuzi?”PKSw 190.1

    “Mwaminini Mungu, neno Lake linasema wazi,” alijibu Mwanamatengenezo; “na zaidi ya kile neno linachowafundisha, msimwamini huyu wala yule. Neno la Mungu liko wazi lenyewe; na kunapotokea kutoeleweka katika sehemu moja, Roho Mtakatifu, ambaye hawezi kujipinga Mwenyewe, hufafanua sehemu hiyo katika sehemu zingine, kwa hiyo hakuna mashaka yanayoweza kubaki isipokuwa kwa mtu ambaye anaamua kubaki mjinga kwa ugumu wa moyo wake.”—David Laing, The Collected Works of John Knox, vol. 2, pp. 281, 284.PKSw 190.2

    Hizo ndizo kweli ambazo Mwanamatengenezo asiyeogopa, kwa kuhatarisha maisha yake, alimwambia malkia. Kwa ujasiri huo huo usiotetereka, alishikilia kusudi lake, akiomba na kupigana vita vya Bwana, mpaka Scotland ilipoachana kabisa na upapa.PKSw 190.3

    Katika nchi ya Uingereza, ustawishaji wa Uprotestanti kama dini ya kitaifa ulipunguza, lakini haukukomesha kabisa, mateso. Wakati mengi ya mafundisho ya Kirumi yaliachwa, siyo machache yaliyobakizwa. Ukuu wa papa ulitupiliwa mbali, lakini mahali pake mfalme alitawazwa kama kiongozi mkuu wa kanisa. Huduma za kanisa bado zilitofautiana sana na usafi na usahili wa injili. Kanuni kuu ya uhuru wa dini ilikuwa bado haijaelekeweka. Ingawa mambo ya kutisha ya kikatili ambayo Rumi iliyatumia dhidi ya wazushi yalitumiwa mara chache na watawala wa Kiprotestanti, bado haki ya kila mtu kumwabudu Mungu kulingana na uchaguzi wa dhamiri yake mwenyewe haikutambuliwa. Wote walitakiwa kukubali na kufuata mifumo ya ibada iliyoelekezwa na kanisa linalotambuliwa na serikali. Walioenda kinyume waliteswa, sana au kidogo, kwa mamia ya miaka.PKSw 190.4

    Katika karne ya kumi na saba maelfu ya wachugaji walifukuzwa kazi. Watu walikatazwa, kwa tishio la faini kubwa, kifungo, na kufukuzwa nchini, kuhudhuria mikutano yoyote ya kidini isipokuwa ile tu iliyoidhinishwa na kanisa. Wale waaminifu ambao wasingeweza kuacha kukutana kumwabudu Mungu walilazimika kukutana katika vichochoro vyenye giza, katika upenu uliojificha, na nyakati zingine katika msitu wakati wa usiku wa manane. Katikati ya msitu mkubwa, hekalu lililojengwa na Mungu Mwenyewe, watoto wa Bwana waliokuwa wametawanywa na kuteswa walikusanyika kumimina roho zao kwa njia ya sala na sifa. Lakini licha ya tahadhari zao zote, wengi wao waliteswa kwa ajili ya imani yao. Magereza yalijaa watu. Familia zilivunjika. Wengi wao walifukuzwa nchini kwao wakakimbilia nchi za kigeni. Hata hivyo Mungu alikuwa pamoja na watu wake, na mateso hayakuweza kunyamazisha ushuhuda wao. Wengi walilazimika kuvuka bahari hadi Amerika na hapa wakaweka misingi ya uhuru wa kiraia na wa kidini ambao umekuwa nguzo na utukufu wa nchi ya Marekani.PKSw 190.5

    Kwa mara nyingine, kama ilivyokuwa katika siku za mitume, badala ya mateso kukomesha kazi ya injili, yalikuwa yakichochea zaidi kusambaa kwake. Katika gereza chafu lililojaa mafisadi na wauaji, John Bunyan alivuta hewa ya mbinguni; na akiwa humo aliandika sitiari yake ya ajabu ya Maendeleo ya Msafiri kutoka nchi ya uharibifu hadi mji mtakatifu. Kwa zaidi ya miaka mia mbili sauti ile kutoka gereza la Bedford imezungumza kwa nguvu inayosisimua na mioyo ya watu. Vitabu vya Bunyan, Pilgrim’s Progress (Maendeleo ya Msafiri) na Grace Abounding to the Chief of Sinners (Neema Tele kwa Mkuu wa Wenye Dhambi) vimeongoza miguu ya wengi katika njia ya uzima.PKSw 191.1

    Baxter, Flavel, Alleine, na watu wengine wenye talanta, elimu, na uzoefu wa kina wa Ukristo walisimama kwa ujasiri kutetea imani ambayo ilitolewa kwa watakatifu tangu zamani. Kazi iliyofanywa na watu hawa, iliyokuwa imepigwa marufuku na kuharamishwa na watawala wa dunia hii, haiwezi kamwe kufa. Vitabu vya Flavel, Fountain of Life (Chemchemi ya Uzima) na Method of Grace (Mbinu ya Neema) vimewafundisha maelfu ya watu jinsi ya kusalimisha roho zao kwa Kristo. Kitabu cha Baxter, Reformed Pastor (Mchungaji Mwanamatengenezo) kimekuwa mbaraka kwa wengi wanaotamani kuamsha kazi ya Mungu, na kitabu chake Saints’ Everlasting Rest (Pumziko la Milele la Watakatifu) limefanya kazi yake ya kuwaongoza watu kwa “pumziko) ambalo limesalia kwa watu wa Mungu.PKSw 191.2

    Miaka mia moja baadaye, wakati wa giza nene la kiroho, Whitefield na wafuasi wa Wesley walionekana kama wabeba nuru kwa ajili ya Mungu. Chini ya utawala wa kanisa la kitaifa watu wa Uingereza walikuwa wamerudi nyuma katika masuala ya kidini kiasi kwamba hawakutofautiana na wapagani. Dini ya asili ilikuwa ndiyo somo lao kuu lililopendwa na wachungaji, na lilihusu pia teolojia yao karibu yote. Matabaka ya juu ya watu yalidhihaki utakatifu wao, na walijidai kwa kuwa juu ya kile walichokiita ushikiliaji sana wao wa mambo bila akili. Matabaka ya chini walikuwa wajinga kupita kiasi na walijiingiza katika maovu bila mipaka, wakati kanisa lilikuwa halina ujasiri wala imani ya kuinua kazi ya injili iliyokuwa imeanguka chini.PKSw 191.3

    Fundisho kuu la kuhesabiwa haki kwa imani, lililofundishwa kikamilifu na Luther, lilikuwa limesahauliwa kwa kiasi kikubwa; na kanuni ya Kirumi ya kutegemea matendo mema kwa ajili ya wokovu, ilikuwa imechukua nafasi yake. Whitefield na Wesley, ambao walikuwa washiriki wa kanisa la kitaifa, walikuwa watafutaji wa dhati wa mapenzi ya Mungu, na walikuwa wamefundishwa kuwa mapenzi ya Mungu yalikuwa kuishi maisha maadilifu na kushika sheria za dini.PKSw 191.4

    Wakati Charles Wesley wakati mmoja alipoumwa, na kuamini kuwa kifo kilikuwa karibu, aliulizwa swali kuwa tumaini lake la uzima wa milele lilikuwa limejengwa juu ya nini. Jibu lake lilikuwa: “Nimetumia juhudi zangu zote kumtumikia Mungu.” Wakati rafiki aliyekuwa amemwuliza swali alipoonekana kutoridhika na jibu lake, Wesley alifikiri: “Nini! Je, juhudi zangu siyo msingi toshelevu wa tumaini? Je, anaweza kuniibia juhudi zangu? Sina kitu kingine zaidi cha kutumainia.”—John Whitehead, Life of the Rev. Charles Wesley, uk. 102. Hilo ndilo giza nene lililokuwa katika kanisa, lililoficha upatanisho, likamwibia utukufu Wake, na kugeuza akili za watu kutoka kwa tumaini lao pekee la wokovu—damu ya Mkombozi aliyesulubiwa.PKSw 192.1

    Wesley na marafiki zake waliongozwa kuona kuwa dini ya kweli inakaa moyoni, na kuwa sheria ya Mungu inapanuka na kuhusisha mawazo, maneno, na matendo. Akiwa ameshawishika juu ya umuhimu wa utakatifu wa moyo, na usahihi wa mwonekano wa nje, walijielekeza kwa moyo wa dhati kutafuta maisha mapya. Kwa maombi na juhudi kubwa walijaribu kudhibiti maovu ya moyo wa asili. Waliishi maisha ya kujinyima, ukarimu, na unyenyekevu, wakitekeleza kwa uaminifu na usahihi mkubwa kila hitaji walilofikiri lingewasaidia kupata kile walichokitamani zaidi—utakatifu ule ambao ungewawezesha kukubaliwa na Mungu. Lakini hakupata kile walichokitafuta. Zilikuwa juhudi za bure kujiokoa wenyewe kutoka katika hukumu ya dhambi au kuvunja nguvu yake. Ni pambano lilelile ambalo Luther alikuwanalo akiwa katika chumba chake kule Erfurt. Ni swali lilelile lililotesa roho yake—“Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?” (Ayubu 9:2).PKSw 192.2

    Mioto ya ukweli wa Kiungu, iliyokuwa karibu kuzimika juu ya madhabahu ya Uprotestanti, ilipaswa kuwashwa upya kwa kutumia mwenge wa zamani uliorithishwa katika zama zote miongoni mwa Wakristo Wabohemia. Baada ya Matengenezo, Uprotestanti katika nchi ya Bohemia ulifutiliwa mbali na waumini wa Urumi. Wote waliokataa kukana ukweli walilazimishwa kukimbia. Baadhi ya hawa, walipopata hifadhi katika huko Saxony, walidumisha imani ya zamani. Ilikuwa kutoka kwa wajukuu wa Wakristo hawa ambapo nuru ilikuja kwa Wesley na marafiki zake.PKSw 192.3

    John Wesley na Charles Wesley, baada ya kuwekewa mikono ya uchungaji, walitumwa kama wamishenari huko Amerika. Katika kundi hilo walikuwemo pia Wamoravian. Wakiwa njiani walikutana na dhoruba kali, na John Wesley, alipokutana uso kwa uso na kifo, alihisi kuwa hakuwa na uhakika wa amani na Mungu. Wajerumani, kinyume chake, walionesha utulivu na tumaini ambalo alikuwa hana uzoefu nao.PKSw 192.4

    “Kwa muda mrefu huko nyuma,” alisema, “alichunguza umakini mkubwa wa tabia yao. Waliendelea kuonesha unyenyekevu wao kikamilifu, kwa kufanya kazi za kiutumishi kwa ajili ya wasafiri wengine ambazo hakuna Mwingereza hata mmoja angeweza kuzifanya; ambazo kwazo walistahili lakini hawakuhitaji malipo, wakisema kufanya hivyo ilikuwa furaha kwao, kwa maana Mwokozi wao alikuwa amewafanyia makubwa zaidi. Na kila siku iliwapa fursa ya kuonesha unyenyekevu ambao haukubadilishwa na maumivu ya aina yo yote. Ikiwa walisukumwa, walipigwa, au kuangushwa chini, waliinuka tena na kwenda zao; lakini hawakuwa na manung'unuko yo yote katika midomo yao. Kulikuwa na fursa sasa ya kuwapima ikiwa walikuwa wamekombolewa kutoka katika roho ya hofu, na ya kiburi, hasira, na kulipiza kisasi. Katikati ya zaburi iliyokuwa inaanzishia ibada, bahari ilichafuka kwa ghafla, dhoruba kali ikavunja sehemu ya mbele ya meli, maji yakafunika meli, na kumwagikia katikati ya sitaha za meli kana kwamba kina kikuu cha bahari kimeshatumeza. Makelele ya kutisha yalianza miongoni mwa Waingereza. Wajerumani waliendelea kuimba kwa utulivu Zaburi. Nilimwuliza mmojawapo baadaye, ‘Hukuogopa?’ Alijibu, ‘Namshukuru Mungu, hapana.’ Niliuliza, ‘Lakini wake zenu na watoto wenu hawakuogopa?’ Alijibu kwa upole, ‘Hapana; wake zetu na watoto wetu hawaogopi kufa.'”—Whitehead, Life of the Rev. John Wesley, uk. 10.PKSw 193.1

    Baada ya kufika Savannah, Wesley alikaa na Wamoraviani kwa muda mfupi, na aliguswa sana na haiba yao ya Kikristo. Kuhusu moja ya ibada zao, kwa kutofautiana sana na ibada za kimfumo zisizo na uhai za Kanisa la Uingereza, aliandika: “Usahili mkubwa na utukufu wa ibada nzima karibu vinisahaulishe miaka elfu moja mia saba iliyokuwa imepita, nikahisi nilikuwa nashiriki katika mikutano ile ambayo mfumo na serikali ya kanisa havikuwepo; bali Paulo, mtengenezaji wa mahema, au Petro, mvuvi wa samaki, waliendesha huduma; ukiwepo udhihirisho wa Roho na nguvu.”— Ibid., pages 11, 12.PKSw 193.2

    Aliporudi Uingereza, Wesley, kutokana na mafundisho ya mhubiri wa Kimoraviani, alifanikiwa kuelewa vizuri zaidi imani ya Biblia. Alifikia hatua ya kushawishika kuwa ilimpasa aachane kabisa na kutegemea matendo yake mema kwa ajili ya wokovu na kwamba ilimpasa kumtumaini kabisa “Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Wakati wa mkutano wa Chama cha Moraviani katika jiji la London kauli ilisomwa kutoka kwa Luther, ikielezea badiliko ambalo Roho wa Mungu hulileta katika moyo wa mtu anayeamini. Wakati Wesley akisikiliza, imani iliwashwa moyoni mwake. “Nilihisi moyo wangu ukitiwa joto la ajabu,” alisema. “Nilihisi ninamtumaini Kristo, Kristo pekee, kwa ajili ya wokovu: na nilipata uhakikisho, kuwa alikuwa amezichukua dhambi zangu, zangu kabisa, na kuniokoa kutoka katika sheria ya dhambi na mauti.”—Ibid., uk. 52.PKSw 193.3

    Kwa miaka mingi ya kujitahidi kwingi kunakochosha na kukosesha raha—miaka ya kujinyima sana, ya kujidhili na kujinyenyekesha—Wesley alijitahidi daima kutekeleza kusudi moja tu la kumtafuta Mungu. Sasa alimpata; na aligundua kuwa neema ambayo alitesekeka kuipata kwa njia ya maombi na kufunga, kwa matendo ya ukarimu na kujikana nafsi, ilikuwa zawadi, “bila fedha na bila bei”PKSw 194.1

    Mara tu baada ya kuimarika katika imani ya Kristo, nafsi yake yote iliwaka moto wa shauku ya kutangaza kila mahali maarifa ya injili yenye utukufu ya neema ya bure ya Mungu. “Ninautazama ulimwengu wote kama parokia yangu,” alisema; “katika sehemu yo yote ile nilipo, panastahili, tena, ni wajibu wangu kamili, kutangaza kwa wote walio tayari kusikia, habari njema za wokovu.”—Ibid., uk. 74.PKSw 194.2

    Aliendeleza maisha yake yenye nidhamu na kujikana nafsi, siyo sasa kama msingi, bali matokeo ya imani; siyo mzizi, bali tunda la utakatifu. Neema ya Mungu katika Kristo ni msingi wa tumaini la Mkristo, na kwamba neema inadhihirika katika utii. Maisha ya Wesley yaliwekwa wakfu kuhubiri kweli kuu alizozipokea—kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika damu ya upatanisho ya Kristo, na nguvu ya Roho Mtakatifu inayoumba upya moyo, kuzaa tunda katika maisha linalopatana na mfano wa Kristo.PKSw 194.3

    Whitefield na Wesley walikuwa wameandaliwa kwa ajili ya kazi yao kwa kushawishika binafsi kuhusiana na hali yao ya kupotea; na kwamba wangeweza kuvumilia mazingira magumu kama askari wa Kristo, walikuwa wamekabiliana na moto wa mateso ya kudhalilishwa, kubezwa, na kuteswa, katika chuo kikuu na wakati wa kuingia kwao katika uchungaji. Wao na wenzao wachache waliowaunga mkono waliita kwa dhihaka Wamethodisti na wanafunzi wenzao wasiomcha Mungu—jina ambalo kwa sasa linaheshimiwa na moja ya madhehebu kubwa katika nchi ya Uingereza na Bara la Amerika.PKSw 194.4

    Kama washiriki wa Kanisa la Uingereza walikuwa wameshikamana na mifumo yake ya ibada, lakini Bwana alikuwa ameweka mbele yao katika neno la Mungu kiwango cha juu zaidi. Roho Mtakatifu aliwaagiza kumhubiri Kristo na Yeye aliyesulibiwa. Nguvu Zake Aliye Juu sana ziliandamana na kazi zao. Maelfu waliamini na kuongolewa kikamilifu. Ilikuwa lazima kondoo hawa walindwe dhidi ya mbwa mwitu wakali. Wesley hakuwa na wazo la kuanzisha madhehebu mapya, lakini aliwaunga pamoja chini ya kilichoitwa Mshikamano wa Kimethodisti.PKSw 194.5

    Wahubiri hawa walipata upinzani mkubwa wa kisirisiri toka kwa kanisa la kitaifa; lakini Mungu, katika hekima Yake, aliingilia kati kupitia matengenezo yaliyotokea ndani ya kanisa lenyewe. Ikiwa matengenezo yangetokea nje peke yake, yasingeweza kupenya na kuingia kule yalikotakiwa sana. Lakini kama wahubiri wana uamsho walikuwa watu wa kanisa, na walifanya kazi miongoni mwa washiriki wa kanisa kila mahali walipopata fursa, na ukweli uliingia mahali ambapo milango ingeweza kufungwa. Baadhi ya wachungaji waliamka kutoka katika usingizi wao na wakawa wahubiri wenye bidii katika parishi zao. Makaisa yaliyokuwa yamelala kwa sababu mifumo ya ibada ya kurudia-rudia na kukariri yaliamka na kuwa hai.PKSw 195.1

    Katika wakati wa Wesley, kama ilivyo katika zama zote za historia ya kanisa, watu wa talanta mbalimbali walitenda kazi walizopangiwa kuzifanya. Hawakuafikiana katika kila kipengele cha fundisho, lakini walisukumwa na Roho wa Mungu, na waliungana katika kusudi kuu la kuleta roho kwa Kristo. Tofauti kati ya Whitefield na Wesley ilitishia wakati fulani kujenga ufa kati yao; lakini kwa kadiri walivyojifunza unyenyekevu katika shule ya Kristo, uvumilivu na ukarimu viliwasaidia kupatana.PKSw 195.2

    Hawakuwa na muda wa kuzozana, wakati makosa na uovu vilikuwa vimeshamiri kila mahali, na wenye dhambi walikuwa wakiteremka kuelekea katika shimo la uharibifu.PKSw 195.3

    Watumishi wa Mungu walipitia katika barabara yenye mikwaruzo. Watu wenye mvuto na elimu kubwa walitumia uwezo wao dhidi yao. Baada ya muda wachungaji wengi walionesha uhasama wa wazi, na milango ya makanisa ilifungwa dhidi ya imani safi na wale walioitangaza. Hatua ya wachungaji kuwapiga marufuku kuhubiri mimbarani ilihamasisha vimelea vya giza, ujinga, na uovu. Tena na tena John Wesley alipona kifo kwa muujiza wa neema ya Mungu. Wakati hari ya watu ilipoamshwa dhidi yake, na ikaonekana hakuna njia ya kuokoka, malaika katika umbo la mwanadamu alikuja kando yake, kundi la watu lilirudi nyuma, na mtumishi wa Kristo alipita salama na kuondoka mahali palipo na hatari.PKSw 195.4

    Kuhusiana na kuokolewa kwake dhidi ya kundi la watu katika moja ya matukio hayo, Wesley alisema: “Wengi walijaribu kuniangusha chini wakati tukitembea kwenye mteremko, kwenye njia inayoteleza, iliyoelekea mjini; wakifikiri ikiwa ningeanguka chini, nisingeweza kuamka tena kirahisi. Lakini sikujikwaa hata kidogo, wala sikuteleza kabisa, mpaka nikawa huru mbali kabisa na mikono yao.... Ingawa wengi walijaribu kunishika kwenye ukosi wa shati langu au mavazi yangu mengine, ili waniangushe chini, hawakuweza kunishika kabisa: mmoja tu ndiye aliyefanikiwa kushika pindo la kizibao changu, ambacho muda si mrefu kipande cha kizibao kilibaki mkononi mwake; kipande kingine, ambacho ndani ya mfuko wake ilikuwemo noti kilibaki.... Mtu mmoja mwenye nguvu nyuma yangu, alinipiga mara kadhaa, kwa fimbo kubwa ya mwaloni; ambayo kama angenipiga mara moja kwenye kisogo, angeniua mara moja. Lakini kila wakati, pigo lilipelekwa pembeni, sijui ni kwa jinsi gani; kwa kuwa nisingeweza kukwepa kwenda kulia au kwenda kushoto.... Mwingine alikuja akikimbia katikati ya msongamano wa watu, na akainua mkono wake ili anipige, alichia mkono ukadondoka, na akanishika shika tu kichwani, akisema, ‘Una nywele laini sana!’ ... Watu wa kwanza kabisa ambao mioyo yao iligeuzwa walikuwa mashujaa wa mji, viongozi wa vikundi vya wapiganaji wa mjini nyakati zote, mmoja wao akiwa alishawahi kupata tuzo ya kupambana katika bustani za duma....PKSw 195.5

    “Kwa hatua za upole lakini za hakika Mungu hutuandaa kwa ajili ya mapenzi Yake! Miaka miwili iliyopita, kipande cha tofali la kuchoma kilikwangua mabega yangu. Ilikuwa mwaka mmoja baada ya hapo ambapo jiwe lilipiga katika macho yangu. Mwezi uliopita nilipokea pigo moja, na jioni ya leo mawili, moja kabla hatujafika mjini, na moja baada ya kutoka mjini; lakini yote mawili yalikuwa kana kwamba hakuna kitu kilichotokea: kwa kuwa ingawa mtu wa kwanza alinipiga kwenye kifua kwa nguvu zake zote, na mwingine alinipiga kwenye mdomo kwa nguvu nyingi kiasi kwamba damu ilitoka mara moja, sikuhisi maumivu yo yote makali zaidi kuliko yale ambayo ningeyapata kama wangenigusa kwa unyasi.”—John Wesley, Works, vol. 3, pp. 297, 298.PKSw 196.1

    Wamethodisti wa siku zile za awali—watu na wahubiri—walivumilia dharau na mateso, kutoka kwa washiriki wa kanisa na wasio na dini waliokasirishwa na mabaya ambayo Wamethodisti walipakaziwa. Walishtakiwa katika mahakama za haki—kwa jina, kwa kuwa haki haikuwepo, isipokuwa mara chache sana, katika mahakama za wakati huo. Mara nyingi walifanyiwa ukatili na watesaji wao. Makundi ya watu yalitembea kutoka nyumba moja hadi nyingine, wakiharibu samani na mali zingine, wakiiba chochote walichokichagua, na wakiwanajisi wanaume, wanawake, na watoto. Katika nyakati zingine, matangazo ya hadhara yalibandikwa, yakiwaita watu waliopenda kusaidia katika kuvunja madirisha na kuiba katika nyumba za Wamethodisti, wakusanyike mahali fulani na wakati fulani. Ukiukwaji huu wa wazi wa sheria ya binadamu na ya Mungu uliruhusiwa kutendeka bila kukemewa. Utesaji uliopangiliwa ulitekelezwa dhidi ya watu ambao kosa lao lilikuwa tu kutafuta kubadilisha miguu ya wenye dhambi kutoka katika njia ya uharibifu na kuielekeza katika njia ya utakatifu.PKSw 196.2

    Alisema John Wesley, akizungumzia mashitaka dhidi yake na dhidi ya wenzake: “Wengi wanadai kuwa mafundisho ya watu hawa ni ya uongo, yana makosa, na ni wenye shauku; kwamba ni mafundisho mapya na hayajawahi kusikiwa mpaka siku za hivi karibuni; kwamba ni jamii ya Wakristo wasiopenda mikutano rasmi, watu wanaoshikilia sana mambo bila akili, watetezi wa upapa. Maigizo yote haya yameshakatwa katika mizizi yake, hususani baada ya kuonesha kuwa kila kipengele cha fundisho hili ni fundisho la wazi la Maandiko lililotafsiriwa na kanisa. Hivyo basi haliwezi kuwa la uongo au lenye makosa, ili mradi tu Maandiko yawe ya kweli.” “Wengine wanadai, ‘Fundisho lao ni kali mno; wanaifanya njia ya kwenda mbinguni kuwa finyu mno.’ Na kwa kweli hiki ndicho kipingamizi halisi, (kwa kuwa ndicho kilikuwa kipingamizi pekee kwa wakati fulani,) na kwa siri ndio msingi wa vipingamizi elfu na zaidi, ambavyo huonekana katika miundo mbalimbali. Lakini vinaifanya njia ya kwenda mbinguni kuwa nyembamba zaidi kuliko Bwana wetu na mitume Wake walivyoifanya? Kuna fundisho kali zaidi kuliko lile la Biblia? Fikiria aya chache tu za wazi: ‘Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ ‘Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.’ ‘Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.’PKSw 196.3

    “Ikiwa fundisho lao ni kali zaidi kuliko hili, wanapaswa kulaumiwa; lakini unajua katika dhamiri yako kuwa sio kweli. Na ni nani anaweza kuwa mkali kidogo chini ya hapo bila kuharibu neno la Mungu? Inawezekanaje wakili wa siri za Mungu aonekane kuwa mwaminifu ikiwa anabadilisha sehemu yo yote ya hazina takatifu? Hapana. Hawezi kupunguza cho chote, hawezi kulainisha cho chote; analazimika kutangaza kwa watu wote, ‘Siwezi kushusha chini Maandiko kukidhi matakwa yako. Inakupasa kuja Biblia ilipo, au uangamie milele.’ Huu ndio msingi halisi wa kile kilio kingine maarufu kuhusu ‘kukosa ukarimu kwa watu hawa.’ Kukosa ukarimu, ni kweli kuwa hawana ukarimu? Katika mambo gani? Hawawapi chakula wenye njaa na kuwavika walio uchi? ‘Hapana; hili siyo kweli: hawana upungufu katika hili: lakini siyo wakarimu katika kuhukumu! Wanafikiri kuwa hakuna mtu anayeweza kuokolewa isipokuwa wale tu wanaofuata njia yao.'”—Ibid., vol. 3, uk. 152, 153.PKSw 197.1

    Kurudi nyuma kiroho kulikokuwepo katika nchi ya Uingereza mara kabla ya wakati wa Wesley kwa sehemu kubwa kulitokana na mafundisho kuwa neema ya Mungu inawaondolea Wakristo wajibu wa kutii sheria ya maadili. Wengi walidai kuwa Kristo alifuta sheria ya maadili na kwamba Wakristo, hivyo basi, hawalaziki kuifuata; kwamba Mkristo amewekwa huru kutoka katika “utumwa wa matendo.” Wengi, japokuwa walikiri uendelevu wa sheria, walifundisha kuwa ilikuwa lazima kwa wachungaji kuwahimiza watu kutii kanuni zake, kwa kuwa wale ambao Mungu aliwachagua waokolewe wangeweza, “kwa msukumo usiozuilika wa neema ya Mungu, kusukumwa kuishi maisha matakatifu na kutenda matendo mema,” wakati wale waliopangiwa kupotea milele “hawakuwa na uwezo wa kutii sheria ya Mungu.”PKSw 197.2

    Wengine, wakishikilia pia kuwa “waliochaguliwa hawawezi kuanguka kutoka kwenye neema na wala hawawezi kunyimwa fadhila ya Mungu,” walifikia majumuisho mabaya zaidi “matendo maovu wanayoyafanya kwa kweli siyo dhambi, wala hayapaswi kuchukuliwa kuwa uvunjaji wa sheria ya Mungu, na kwamba, matokeo yake, hawana haja ya kuungama dhambi au kuachana nazo kwa njia ya toba.”—McClintock and Strong, Cyclopedia, art. “Antinomians.” Kwa hiyo, walifundisha kuwa hata dhambi iliyo mbaya kabisa, “inayochukuliwa na watu wote kuwa uvunjanji mkubwa wa sheria ya Mungu, siyo dhambi mbele za Mungu,” ikiwa imetendwa na mmoja wa wateule, “kwa sababu ni moja ya tabia muhimu na bainishi za wateule, kwamba hawawezi kufanya jambo lo lote lisilompendeza Mungu au jambo ambalo limekatazwa na sheria.”PKSw 198.1

    Mafundisho haya potovu kimsingi yanafanana na fundisho la baadaye la walimu na wanateolojia mashuhuri—kuwa hakuna sheria isiyobadilika kama kiwango cha haki, bali kwamba kiwango cha uadilifu kinaoneshwa na jamii yenyewe, na imekuwa na uwezekano wa kubadilika daima. Mawazo haya yote yanavuviwa na roho ile ile kuu—na yeye ambaye, hata miongoni mwa wakazi wa mbinguni wasio na hatia, alianza kazi yake ya kutafuta kuharibu viwango vya haki vya sheria ya Mungu.PKSw 198.2

    Fundisho la maagizo ya Kiungu, yanayowapa wanadamu tabia isiyobadilika, limewafanya wengi, hatimaye, kutupilia mbali sheria ya Mungu. Kwa juhudi kubwa, Wesley aliyapinga makosa hayo ya walimu waliofundisha kuwa neema inawafanya wafuasi wa Kristo wasiwe na hitaji la sheria ya Mungu na alionesha kuwa fundisho hili lililowafanya watu waiache sheria ya Mungu lilikuwa kinyume na Maandiko. “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa.” “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake” (Tito 2:11; 1 Timotheo 2:3-6). Roho wa Mungu anatolewa bure kumwezesha kila mwanadamu kushikilia njia ya wokovu. Hivyo Kristo, “Nuru ya kweli,” “amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu” (Yohana 1:9). Wanadamu wanakosa wokovu kwa sababu ya uchaguzi wao wa hiari wa kuikataa zawadi ya uzima.PKSw 198.3

    Katika kujibu dai kuwa wakati wa kufa kwa Kristo kanuni za Amri Kumi zilifutwa pamoja na sheria ya sherehe, Wesley alisema: “Sheria ya Uadilifu, iliyomo katika Amri Kumi na ambayo manabii walisimamia utekelezaji wake, Kristo hakuiondoa. Ujio Wake hakuwa na lengo la kutangua hata sehemu yake yo yote ile. Hii ni sheria ambayo kamwe haiwezi kuvunjwa, yenyewe ‘husimama imara kama shahidi mwaminifu mbinguni.’ ... hii ilikuwa hivyo tangu mwanzo wa ulimwengu, ikiwa ‘bado haijaandikwa kwenye mbao za mawe,’ lakini ikiwa imendikwa juu ya mioyo ya wanadamu, walipotoka katika mikono ya Muumbaji. Na ingawa herufi zilizoandikwa na kidole cha Mungu kwa sasa zimefutwa na dhambi kwa kiwango kikubwa, lakini bado hazijafutika kabisa, kwa kuwa bado tuna ufahamu wa mema na mabaya. Kila kipengele cha sheria ya Mungu lazima kiwe na nguvu juu ya wanadamu wote, katika zama zote; kwa kuwa sheria ya Mungu haitegemei wakati au mahali, au hali yo yote ile nyingine inayoweza kubadilika, kwani sheria ya Mungu hueleza tabia ya Mungu asiyebadilika.PKSw 198.4

    “'Sikuja kutangua, bali kutimiliza.’ ... Bila swali, maana Yake katika sehemu hii ni (Bila kubadilika kwa yote yaliyotangulia kabla na yanayofuata baada),—nimekuja kustawisha katika ukamilifu wake, licha ya tafsiri zote za wanadamu: nimekuja kuweka mwonekano kamili na wa wazi kila kitu kilichokuwa giza au kilichokuwa hakionekani ndani yake kionekane: nimekuja kutangaza umuhimu wa kweli na kamili wa kila sehemu; kuonesha urefu na upana, na ukamilifu wake wote, wa kila amri iliyomo, na kimo na kina, kiini chake kiroho na usafi wake usiofikiriwa katika vipengele vyake vyote.”—Wesley, sermon 25.PKSw 199.1

    Wesley alifundisha upatanifu mkamilifu wa sheria na injili. “Kwa hiyo, kuna uhusiano wa karibu unaoweza kueleweka, kati ya sheria na injili. Kwa upande mmoja, sheria daima hutengeneza njia kwa ajili ya, na hutuelekeza kwa, injili; Kwa upande mwingine, injili daima hutuongoza katika utekelezaji mkamilifu zaidi wa sheria. Sheria, kwa mfano, hututaka tumpende Mungu, tumpende jirani yetu, tuwe wanyenyekevu, na tuwe watakatifu. Tunahisi kuwa tumepungua katika mambo haya; ndiyo, kwamba ‘kwa mwanadamu hii haiwezekani;’ lakini tunaona ahadi ya Mungu na kutupatia upendo huo, kutufanya tuwe wanyenyekevu, wapole, na watakatifu: tunashikilia hii injili, tunashikilia habari njema hizi; tunapewa kulingana na imani yetu; na ‘haki ya sheria inatimizwa ndani yetu,’ kwa njia ya imani iliyo katika Kristo Yesu....PKSw 199.2

    “Miongoni mwa maadui wakubwa wa injili ya Kristo,” alisema Wesley, “ni wale ‘wanaoihukumu sheria’ yenyewe, waziwazi na moja kwa moja, na ‘wanaoisema vibaya;'wanaowafundisha watu kuvunja (kuyeyusha, kulegeza, kuondoa ulazima wa) siyo tu moja peke yake, iwe ile ndogo kabisa au ile kubwa kabisa, bali amri zote kwa mpigo.... Kinachoshangaza kuliko yote yanayohusiana na udanganyifu huu mkubwa, ni kuwa wale wanotawaliwa na udanganyifu huu, huamini kwa dhati kuwa wanamheshimu Kristo kwa kuangusha sheria Yake, na kwamba wanaitukuza ofisi Yake wakati wanapoharibu fundisho Lake! Ndiyo, wanamheshimu kama vile Yuda Iskariote alivyomheshimu kwa kusema, ‘Salamu, Rabi, akambusu.’ Na anaweza kumwambia kwa haki kabisa kila mmoja wao, ‘Wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?’ Siyo jambo jingine zaidi ya kumsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu, kuzungumzia damu Yake, na kumwondolea taji Yake; kupuuza sehemu yo yote ya sheria Yake, kwa kujifanya unaeneza injili Yake. Kadhalika mtu ye yote hawezi kuepuka shitaka hili, ikiwa anahubiri imani kwa jinsi hiyo kama ama ana mwelekeo wa moja kwa moja au usiokuwa wa moja kwa moja wa kuweka pembeni kipengele cho chote cha utii: anayemhubiri Kristo huku anafuta, au anadhoofisha kwa namna yo yote ile, amri za Mungu zilizo ndogo kabisa.”—Ibid.PKSw 199.3

    Kwa wale waliohimiza kuwa “kuhubiri injili hujibu miisho yote ya sheria,” Wesley alijibu: “Hili tunalikataa kabisa. Hakujibu hata mwisho wa kwanza wa sheria, maana yake, haiwezi kumfanya mtu ahisi hatia ya dhambi, kuwaamsha wale ambao wamelala usingizi kwenye ukingo wa kuzimu.” Mtume Paulo anasema kuwa“kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria;““na ni mpaka pale tu mwanadamu anaposhawishika kuwa ni mwenye dhambi, ndipo atakapohisi hitaji lake la damu ya Kristo inayopatanisha.... ‘Walio wazima,’ kama Bwana wetu Mwenyewe alivyosema, ‘hawahitaji daktari, bali walio hawawezi.’ Ni jambo lisilokuwa na maana, hivyo basi, kuwapelekea daktari walio wazima, au angalau watu wanaojidhania kuwa ni wazima. Ni lazima kwanza kuwashiwishi wakubali kuwa ni wagonjwa; vinginevyo hawatakushukuru kwa kazi yako. Kadhalika ni jambo lisilo kuwa na maana kumtoa Kristo kwa watu ambao mioyo yao ni mizima, watu ambao bado hawajavunjika-vunjika.”—Ibid., sermon 35.PKSw 200.1

    Hivyo basi, alipokuwa akihubiri injili ya neema ya Mungu, Wesley, kama Bwana wake, alitafuta “kuikuza sheria, na kuifanya iheshimiwe.” Kwa uaminifu alitekeleza kazi aliyopewa na Mungu, na, aliruhusiwa kuyaona matokeo yenye utukufu ya kazi yake. Mwishoni mwa maisha yake marefu yaliyopata miaka themanini—zaidi ya nusu karne iliyotumiwa katika safari za kichungaji—wafuasi wake waaminifu walikuwa zaidi ya laki tano. Lakini watu maelfu ambao kwa njia ya kazi zake waliinuliwa kutoka katika uharibifu na kudharauliwa kunakosababishwa na dhambi hadi maisha ya juu na masafi zaidi, na idadi ya watu ambao kwa njia ya mafundisho yake walipata uzoefu wa kina na mkubwa zaidi wa kiroho, hawatajulikana kamwe mpaka familia nzima itakapokusanywa katika ufalme wa Mungu. Maisha yake yanawasilisha somo la thamani isiyopimika kwa kila Mkristo. Hebu imani ile na unyenyekevu ule, juhudi zisizochoka, kujitoa mhanga, na ujisalimishaji mkamilifu wa mtumishi huyu wa Kristo uakisiwe katika makanisa ya leo!PKSw 200.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents