Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 22—Unabii Watimia

    Muda ulipopita ambao ujio wa Bwana ulikuwa umetarajiwa kwanza,— majira ya kuchipua ya mwaka 1844,—wale waliokuwa wametazamia kwa imani ujio Wake kwa kipindi fulani walipatwa na mashaka na kutokuwa na hakika. Wakati ambapo ulimwengu uliwaona kama watu ambao wameshindwa vibaya na kuthibitika kuwa walikuwa wameamini uongo, chanzo cha faraja yao bado kilikuwa ni neno la Mungu. Wengi wao waliendelea kuchunguza Maandiko, wakipima upya ushahidi wa imani yao na kujifunza kwa makini unabii ili wapate nuru zaidi. Ushuhuda wa Biblia uliounga mkono msimamo wao ulioonekana kuwa wazi na hitimivu. Dalili ambazo zisingeweza kukosewa zilielekeza kwa ujio wa Kristo kama uliokuwa karibu. Mbaraka maalum wa Bwana, katika uongofu wa wenye dhambi na uamsho wa maisha ya kiroho miongoni mwa Wakristo, ulikuwa umethibitisha kuwa ujumbe ulikuwa wa Mbinguni. Na ingawa waaminio hawakuweza kueleza kukatishwa tamaa kwa matarajio yao, walihisi kuwa Mungu alikuwa amewaongoza katika uzoefu wao uliokuwa umepita.PKSw 299.1

    Katika aya zenye unabii ambao waliamini kuwa ulihusu wakati wa ujio wa pili, yalikuwemo mafundisho mahsusi yaliyoshughulikia hali yao ya kutokuwa na hakika na ya kujawa na mashaka, na mafundisho hayo yaliwapa shime na kuwafanya wawe na uvumilivu na imani kuwa kile ambacho kilikuwa giza kwa ufahamu wao kingeweza kwa wakati mwafaka kueleweka wazi kwao.PKSw 299.2

    Miongoni mwa aya hizo za unabii ni ile ya Habakuki 2:1-4: “Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake”PKSw 299.3

    Mapema kabisa mwaka 1842 agizo lililotolewa katika unabii huu la “Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji,“lilipendekeza kwa Charles Fitch kuandaa chati ya unabii kuonesha njozi za Danieli na Ufunuo. Uchapishaji wa chati hii ulichukuliwa kama utimizaji wa amri iliyotolewa na Habakuki. Hakuna hata mmoja, hata hivyo, aliyegundua wakati huo kuwa kuonekana kuchelewa kwa namna fulani katika utimizwaji wa njozi—muda wa kusubiri—kumewasilishwa katika unabii uo huo. Baada ya kukatishwa tamaa, andiko hili lilionekana kuwa na maana sana: “Njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.... Mwenye haki ataishi kwa imani yake.”PKSw 299.4

    Sehemu ya unabii wa Ezekieli pia ilikuwa chanzo cha nguvu na faraja kwa walioamini: “Neno la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi.... Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote.... Mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena.” “Hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa” (Ezekieli 12:21-25, 27, 28).PKSw 300.1

    Waliokuwa wakingoja walifurahia, wakiamini kuwa Yeye ajuaye mwisho tangu mwanzo aliangalia kupitia katika zama zote na, akiona zama nyingi kabla kukatishwa tamaa kwao, aliwapa maneno ya ujasiri na tumaini. Isingekuwa kwa njia ya sehemu hizo za Maandiko, zilizowahimiza kungoja kwa uvumilivu na kushikilia kwa uthabiti neno la Mungu, imani yao ingeshindwa katika saa ile ya kujaribiwa.PKSw 300.2

    Mfano wa wanawali kumi wa Mathayo 25 pia huonesha kielelezo cha uzoefu wa Waadventista. Katika Mathayo 24, katika kujibu swali la wanafunzi Wake kuhusiana na dalili ya ujio Wake na ya mwisho wa dunia, Kristo alionesha baadhi ya matukio muhimu sana katika historia ya ulimwengu na ya kanisa tangu ujio Wake wa kwanza hadi ujio Wake wa pili; ambayo ni, kuharibiwa kwa Yerusalemu, dhiki kuu ya kanisa chini ya mateso ya kipagani na ya kipapa, kutiwa giza jua na mwezi, na kuanguka kwa nyota. Baada ya hayo alisema juu ya ujio Wake katika ufame Wake, na alisimulia mfano unaoeleza makundi mawili ya watumishi wanaotazamia kuja Kwake. Sura ya 25 huanza kwa maneno: “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi.” Hapa linaoneshwa kanisa linaloishi katika siku za mwisho, lile lile ambalo limetajwa katika sehemu ya mwisho ya sura ya 24. Katika mfano huu uzoefu wao unaelezwa kwa njia ya kielelezo cha matukio ya ndoa ya Mashariki.PKSw 300.3

    “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.”PKSw 300.4

    Ujio wa Kristo, kama unavyotangazwa na malaika wa kwanza, ulieleweka kuwakilishwa na ujio wa bwana arusi. Matengenezo yaliyoenea mahali pengi kama matokeo ya utangazwaji wa ujio Wake wa haraka, yanalinganishwa na kutoka kwa wanawali kumi. Katika mfano huu, kama ilivyo katika mfano wa Mathayo 24, makundi mawili ya watu yamewakilishwa. Wote walichukua taa zao, Biblia, na kwa njia ya nuru yake waliondoka kwenda kumlaki Bwana arusi. Lakini wakati ambapo“wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao,” “wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.” Kundi la pili lilipokea neema ya Mungu, nguvu inayoumba upya, inayoleta ufahamu wa Roho Mtakatifu, ambaye hulifanya neno la Mungu kuwa taa ya miguu na mwanga wa njia. Katika kicho cha Mungu walijifunza Maandiko kuujua ukweli, na walitafuta kwa dhati usafi wa moyo na wa maisha. Hawa walikuwa na uzoefu binafsi, imani kwa Mungu na kwa neno Lake, ambayo isingeweza kushindwa kwa kukatishwa tamaa au kuchelewa. Wengine “walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao.” Hawa walikwenda kwa mhemko. Hofu zao zilichochewa na ujumbe wa kutisha, lakini walitegemea imani ya ndugu zao, waliridhishwa na nuru ya hisia nzuri, bila ufahamu wa kina wa ukweli au kazi halisi ya neema ndani ya moyo. Hawa walitoka kwenda kumlaki Bwana, wakiwa na tumaini la kupokea zawadi haraka; lakini hawakuwa wamejiandaa kwa ajili ya kuchelewa na kukatishwa tamaa. Majaribu yalipokuja, imani yao ilishindwa, na nuru yao ilififia.PKSw 301.1

    “Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.” Kuchelewa kwa bwana arusi kunawakilishwa na kupita kwa wakati ambao Bwana alikuwa ametarajiwa, kukatishwa tamaa, na kuchelewa kulikojitokeza. Katika wakati huu wa kutokuwa na hakika, shauku ya wale walio na imani ya juu juu na waliojitokeza kumlaki Bwana wakiwa mguu mmoja ndani na mguu mwingine nje walianza kubabaika, na juhudi zao zilipungua; lakini wale ambao imani yao ilikuwa imejengwa juu ya ujuzi binafsi wa Biblia walikuwa na mwamba chini ya nyayo zao, ambao mawimbi ya kukatishwa tamaa hayakuweza kuuondosha. “Wote wakasinzia wakalala usingizi;” kundi moja likiwa katika hali ya kutojali na kutupilia mbali imani yao, kundi jingine likingoja kwa uvumilivu mpaka nuru ya wazi zaidi iweze kutolewa. Hata hivyo katika usiku wa kujaribiwa kundi la pili lilionekana kupoteza, kwa kiasi fulani, juhudi na imani yao. Wale waliojitoa nusu na wenye imani ya juu juu hawakuweza tena kutegemea imani ya ndugu zao. Kila mmoja anapaswa kusimama au kuanguka mwenyewe.PKSw 301.2

    Karibu na muda huu, ushikiliaji sana wa mambo bila kutumia akili ulianza kujitokeza. Baadhi ya wale waliokuwa wamedai kuwa waumini wenye bidii wa ujumbe wa marejeo walitupilia mbali neno la Mungu kama mwongozo pekee usiokosea na, wakidai kuongozwa na Roho, walijiachia na kutawaliwa na mihemko, maono, na mawazo yao. Walikuwepo baadhi yao walioonesha juhudi zisizo na maana na kukosa uvumilivu kwa wengine, wakiwalaumu wale wote ambao hawakukubaliana na njia zao. Mawazo na matendo yao hayakupokelewa na kundi kubwa la Waadventista; hata hivyo walileta aibu kwa njia ya ukweli.PKSw 301.3

    Shetani alitaka kutumia njia hii kupinga na kuharibu kazi ya Mungu. Watu walikuwa wamepata uamsho mkubwa kutokana na vuguvugu la marejeo, maelfu ya wenye dhambi waliongoka, na watu waaminifu walijitolea kutangaza ukweli, hata wakati wa kujaribiwa. Mfalme wa uovu alikuwa anapoteza raia wake; na ili kuiaibisha kazi ya Mungu, alijaribu kuwadanganya baadhi ya watu walioikiri imani na kuwafanya wawe na misimamo mikali. Ndipo mawakala wake walijiandaa kutumia kila kosa, kila kushindwa, kila tendo la kipuuzi, na kuliweka mbele ya watu katika namna iliyokuzwa sana, kuwafanya Waadventista na imani yao wachukiwe. Hivyo kwa kadiri alivyopata idadi kubwa ya watu ambao angeweza kuwakusanya na kuwafanya wadai kuamini injili ya ujio wa pili wakati nguvu yake ikitawala mioyo yao, ndivyo angenufaika zaidi kwa kuwafanya watu wawaone kuwa wawakilishi wa jamii yote ya waaminio.PKSw 302.1

    Shetani ni “mshitaki wa ndugu” na ni roho yake ambayo huwachochea watu watafute makosa na mapungufu ya watu wa Bwana, na kuwafanya watu wengine wayaone, ilhali matendo yao mema yanapitwa bila kutajwa. Yeye yuko kazini daima wakati Mungu akiwa kazini kwa ajili ya wokovu wa roho. Wakati wana wa Mungu wanapokuja mbele za Bwana, Shetani anakuja pia miongoni mwao. Katika kila uamsho yuko tayari kuingiza wale ambao hawajatakaswa mioyoni mwao na ambao akili zao zina mashaka. Wakati hawa wanapopokea baadhi ya vipengele vya ukweli, na kupata nafasi miongoni mwa waaminio, anafanya kazi kupitia kwao kuingiza nadharia zinazowapotosha wasio na tahadhari. Hakuna mtu anayethibitika kuwa ni Mkristo wa kweli kwa sababu tu yumo miongoni mwa watu wa Mungu, hata katika nyumba ya ibada na kwenye meza ya Bwana. Shetani yupo daima katika matukio muhimu kwa njia ya wale ambao anaweza kuwatumia kama mawakala wake.PKSw 302.2

    Mfalme wa uovu anapinga kila hatua ambayo watu wa Mungu wanaipiga katika safari yao ya kuelekea katika mji wa mbinguni. Katika historia yote ya kanisa hakuna matengenezo ambayo yamewahi kufanywa bila kukutana na vikwazo vya kutisha. Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Paulo. Kila mahali ambapo mtume alianzisha kanisa, wapo baadhi waliodai kupokea imani, lakini ambao waliingiza mafundisho ya uongo, ambayo, ikiwa yangepokelewa, yangeweza hatimaye kufutilia mbali roho ya kuupenda ukweli. Luther pia alipata mashaka makubwa na udhia kutokana na kazi ya watu wanaoshikilia sana mambo bila kutumia akili waliodai kuwa Mungu aliongea moja kwa moja kupitia, na ambao hatimaye waliweka mawazo na maoni yao juu ya ushuhuda wa Maandiko. Wengi ambao hawakuwa na imani na uzoefu, lakini waliokuwa na kiasi fulani cha kujitumainia na kuridhika, na waliopenda kusikiliza na kusimulia mambo mapya, walidanganywa na maigizo ya walimu wapya, na walijiunga na mawakala wa Shetani katika kazi yao ya kubomoa kile ambacho Mungu alikuwa amemwongoza Luther kukijenga. Na akina Wesley, na wengine walioubariki ulimwengu kwa mvuto wao na imani yao, walikutana katika kila hatua na hila za Shetani akiwasukuma watu wenye bidii kupita kiasi, wenye mashaka, na wasiotakaswa na kuwafanya wawe washupavu wa kidini wa kila kiwango.PKSw 302.3

    William Miller alipinga sana mivuto iliyokuwa na mwelekeo wa kujenga ushupavu wa kidini. Alisema, kama alivyosema Luther, kuwa kila roho lazima ipimwe kwa neno la Mungu. “Shetani,” Miller alisema, “ana nguvu nyingi juu ya akili za baadhi ya watu waliopo hapa leo. Na tutajuaje ni roho gani waliyo nayo? Biblia inajibu: ‘Mtawatambua kwa matunda yao.'... Kuna roho nyingi zimeenea duniani; na tumeagizwa kuzijaribu roho. Roho ambayo haituongozi kuishi maisha ya kiasi, ya haki, na ya utauwa, katika ulimwengu huu, sio Roho ya Kristo. Nimeshawishika zaidi na zaidi kuwa Shetani anahusika na hizi vurugu.... Wengi miongoni mwetu wanaojifanya kuwa wametakaswa kikamilifu, wanafuata mapokeo ya wanadamu, na kwa kiasi kikubwa hawajui ukweli kama wengine ambao hawafanyi maigizo hayo.”—Bliss, ukurasa 236, 237. “Roho ya uongo itatusababisha kuuacha ukweli; na Roho wa Mungu atatuongoza katika ukweli. Lakini, mnasema, mtu anaweza kukosea, na akadhani yuko sahihi. Sasa inakuwaje? Tunajibu, Roho na neno vinakubaliana. Ikiwa mtu anaamua mwenyewe kwa njia ya neno la Mungu, na anapata mwafaka kamili katika Maandiko yote, ana haki ya kuamini kuwa ana ukweli; lakini ikiwa anakuta roho inayomwongoza haiafikiani na mwongozo wote wa sheria ya Mungu au Kitabu chote, hapo hebu aende pole, asije akanaswa katika mtego wa Shetani.”—The Advent Herald and Signs of the Times Reporter, January 15, 1845.PKSw 303.1

    Katika siku za Matengenezo, maadui wa matengenezo walidai maovu yanayotokana na ushikiliaji sana wa mambo bila kutumia akili yalitokana na kazi ya wanamatengenezo—ingawa wanamatengenezo ndio waliokuwa wakifanya kazi kubwa na ya dhati kuuupinga. Njia kama hiyo ilifuatwa na wapinzani wa vuguvugu la marejeo. Na kwa kutoridhika na uwakilishaji potovu na kukuza makosa yanayofanana na ukweli ya watu wenye misimamo mikali na washikiliaji sana wa mambo bila kutumia akili, walisambaza taarifa mbaya ambazo hazikuwa na ukweli hata kidogo. Watu hawa walisukumwa na ubaguzi na chuki. Amani yao ilibughudhiwa na mahubiri ya ujio wa haraka wa Kristo. Waliogopa kuwa inaweza kuwa kweli, lakini walitumaini haikuwa hivyo, na hii ilikuwa siri ya vita yao dhidi ya Waadventista na imani yao.PKSw 303.2

    Ukweli kuwa washupavu wa kidini wachache walikuwa miongoni mwa makundi ya Waadventista sio sababu ya kuamua kuwa vuguvugu hilo halikuwa la Mungu kuliko uwepo wa watu kama hao na wadanganyaji katika siku za Paulo au siku za Luther au kuwa kisingizio cha kuikataa kazi yao. Hebu watu wa Mungu waamke kutoka usingizini na waanze kazi ya toba na matengenezo; hebu wachunguze Maandiko ili wajifunze ukweli kama ulivyo ndani ya Yesu; hebu wajisalimishe kikamilifu kwa Mungu, na ushahidi hautakosekana kuwa Shetani bado anafanya kazi na yuko macho. Kwa njia zote zinazowezekana za uongo ataonesha nguvu yake, na kuwakusanya malaika wote walioanguka walioko chini ya himaya yake kumsaidia.PKSw 304.1

    Sio utangazaji wa ujio wa pili uliosababisha ushupavu wa kidini na migawanyiko. Mambo haya yalitokea katika msimu wa kiangazi mwaka 1844, wakati Waadventista walipokuwa katika hali ya mashaka na sintofahamu kuhusiana na msimamo wao hasa. Utangazaji wa ujumbe wa malaika wa kwanza na wa “kilio cha usiku wa manane” ulikuwa na mwelekeo wa kudhibiti ushikiliaji sana mambo bila kutumia akili na migawanyiko. Wale walioshiriki katika mahubiri haya makini walikuwa na upatanifu mkamilifu; mioyo yao ilijazwa na upendo wa kila mmoja kwa mwingine na wa kila mmoja kwa Yesu, ambaye walitarajia kumwona muda mfupi uliokuwa unakuja. Imani moja, tumaini moja lenye baraka, viliwainua juu ya utawala wa mvuto wowote wa kibinadamu, na vilikuwa ngao dhidi ya mashambulizi ya Shetani.PKSw 304.2

    “Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao” (Mathayo 25:5-7). Wakati wa kiangazi cha mwaka 1844, katikati ya wakati ambao ulikuwa umefikiriwa mwanzoni kuwa siku 2300 zingekomea, na wakati wa vuli ya mwaka huo huo, ambao ilionekana baadaye kuwa siku hizo zilifika, ujumbe ulitangazwa kwa kutumia maneno yale yale ya Maandiko: “Haya, Bwana arusi anakuja!” Kilichofanya vuguvugu hili litokee ilikuwa ugunduzi wa ile amri ya Artashasta ya kuujenga upya mji wa Yerusalemu, ambayo ilichukuliwa kama tarehe ya kuanza kwa kipindi cha siku 2300, ambayo ilianza kutekelezwa wakati wa vuli ya mwaka 457 K.K., na siyo mwanzoni mwa mwaka, kama ilivyokuwa imeaminiwa mwanzoni. Kwa kukokotoa kuanzia wakati wa vuli ya 457, miaka 2300 iliishia wakati wa vuli ya mwaka 1844. (Tazama Kiambatanisho kwa ajili ya ukurasa 329.)PKSw 304.3

    Hoja zilizochukuliwa kutoka katika mifano ya Agano la Kale zilielekeza pia kwa wakati wa vuli kama wakati ambao tukio lililowakilishwa na “kutakaswa kwa patakatifu” lingetokea. Hili lilielezwa vizuri pale mkazo ulipowekwa katika namna mifano iliyohusu ujio wa kwanza wa Kristo ilivyotimizwa.PKSw 305.1

    Kuchinjwa kwa mwanakondoo wa Pasaka kulikuwa kivuli cha kifo cha Kristo. Paulo anasema:“Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo” (1 Wakorintho 5:7). Mganda wa malimbuko, ambao wakati wa Pasaka ulitikiswa mbele ya Bwana, ulikuwa mfano wa ufufuko wa Kristo. Paulo anasema, akiongelea kuhusu ufufuo wa Bwana na wa watu Wake wote: “Limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja” (1 Wakorintho 15:23). Kama mganda wa kutikiswa, ambao ulikuwa nafaka za kwanza kukomaa kwanza zilizokusanywa kabla ya mavuno, Kristo ni limbuko la mavuno yale yasiyopatikana na mauti ya waliokombolewa ambao wakati wa ufufuo ujao watakusanywa katika ghala la Mungu. Atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, , kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yakePKSw 305.2

    Mifano hii ilitimizwa, sio tu kama tukio, bali pia kama wakati. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza wa Kiyahudi, siku ile ile na mwezi ule ule ambao kwa karne kumi na tano kondoo wa Pasaka alikuwa akichinjwa, Kristo, akiwa amekula Pasaka na wanafunzi Wake, alianzisha sherehe ambayo ilipaswa kuadhimisha kumbukumbu ya kifo Chake mwenyewe kama “Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Usiku ule ule alikamatwa na mikono miovu na kupelekwa kusulubiwa na kuuawa. Na kama Yule ambaye mfano wa mganda wa kutikiswa ulimlenga, Bwana wetu alifufuliwa kutoka katika wafu siku ya tatu, “limbuko lao waliolala,” mfano wa wenye haki wote watakaofufuliwa, ambapo, (mwili wetu wa unyonge” utabadilishwa, “upate kufanana na mwili wake wa utukufu” (Aya ya 20; Wafilipi 3:21).PKSw 305.3

    Kwa jinsi iyo hiyo mifano inayohusu ujio wa pili wa Kristo inapaswa kutimizwa kwa wakati uliotajwa katika huduma ya mifano. Katika mfumo wa Musa, utakaso wa patakatifu, au Siku kuu ya Upatanisho, ulitokea siku ya kumi ya mwezi wa saba wa Kiyahudi (Walawi 16:29-34), wakati kuhani mkuu, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa njia hiyo kuondoa dhambi zao zote kutoka katika patakatifu, alitoka nje na kuwabariki watu. Kwa hiyo iliaminika kuwa Kristo, Kuhani wetu Mkuu, angetokea kutakasa dunia kwa njia ya kuangamiza dhambi na wenye dhambi, na kuwabariki watu Wake wanaongojea kwa kuwapa hali ya kutokufa. Siku ya kumi ya mwezi wa saba, Siku kuu ya Upatanisho, wakati wa kutakasa patakatifu, ambayo mwaka 1844 ilikuwa siku ya ishirini na mbili ya mwezi Oktoba, ilichukuliwa kuwa wakati wa kuja kwa Bwana. Tarehe hii iliafikiana na uthibitisho uliokuwa umekwishatolewa kuwa siku 2300 inaishia wakati wa vuli, na hitimisho lililoonekana kutozuilika.PKSw 305.4

    Katika mfano wa Mathayo 25, kipindi cha kungojea na kusinzia hufuatwa na ujio wa bwana arusi. Hili lilikuwa sawasawa na hoja zilizokuwa zimewasilishwa, kutoka sehemu zote mbili—kutoka katika unabii na kutoka katika mifano. Walikuwa wameshawishika sana kuhusiana na ukweli waliohubiri; na “kilio cha usiku wa manane” kilihubiriwa na maelfu ya walioamini.PKSw 306.1

    Kama wimbi la maji kupwa na kujaa, vuguvugu la marejeo lilifagia katika nchi. Kutoka jiji hadi jiji, kutoka kijiji hadi kijiji, na sehemu za pembezoni mwa nchi vuguvugu lilifika, mpaka watu wa Mungu waliokuwa wakingoja walipoamshwa kikamilifu. Ushupavu wa kidini ulitoweka wakati wa vuguvugu hili kama umande wa asubuhi unavyoyeyuka wakati jua linapochomoza. Waaminio waliona mashaka na fadhaa zao zikitoweka, na tumaini na ujasiri vilichangamsha mioyo yao. Kazi haikuwa na misimamo mikali ambayo daima hujitokeza wakati kunapokuwepo msisimko wa kibinadamu pasipokuwepo nguvu inayodhibiti ya neno na Roho wa Mungu. Uzoefu ule ulifanana katika tabia na misimu ya unyenyekevu na kumrudia Mungu kulikotokea miongoni mwa Waisraeli wa zamani baada ya kupokea ujumbe wa onyo kutoka kwa watumishi Wake. Ulibeba tabia inayoonekana katika kazi ya Mungu katika kila zama. Furaha ilikuwepo, lakini kulikuwa na msisimko mdogo, badala yake kulikuwepo kujichunguza mioyo kwa kina, kuungama dhambi, na kuachana na ulimwengu. Kujiandaa kwa ajili ya kukutana na Bwana ulikuwa ndiyo mzigo wa roho zilizokuwa zikiumia. Kulikuwepo maombi ya dhati na kujiweka wakfu kwa Mungu kikamilifu.PKSw 306.2

    Miller alisema akielezea uzoefu ule: “Hakuna onesho kubwa la furaha: yaani, ni kana kwamba, furaha ilitunzwa kwa ajili ya wakati ujao, wakati mbingu na dunia yote itakapofurahi pamoja kwa furaha isiyoneneka na ikiwa imejaa utukufu. Hakuna kupiga kelele: yaani, pia, zilihifadhiwa kwa ajili ya kupiga kelele za mbinguni. Waimbaji wako kimya: wanasubiri kujiunga na majeshi ya mbinguni, kwaya ya mbinguni.... Hakuna mgongano wa hisia: wote wana moyo mmoja na akili moja.”—Bliss, ukurasa 270, 271.PKSw 306.3

    Mwingine aliyeshiriki katika vuguvugu lile alishuhudia: “Vuguvugu lilileta kila mahali kujichunguza moyo kwa kina sana na kujinyenyekesha kwa kila roho mbele za Mungu wa mbinguni juu. Lilihamisha shauku ya watu kutoka kwa vitu vya ulimwengu huu, lilileta uponyaji dhidi ya mashindano na uadui, liliwafanya watu kuungama makosa yao, na kupondeka mbele za Mungu, lilileta toba, lilihamasisha maombi ya kuvunjika moyo kwa Mungu kwa ajili ya msamaha na kukubaliwa. Lilisababishwa kujishusha na kupondeka kwa roho, kwa namna ambayo haijapata kushuhudiwa kabla. Kama Mungu kupitia kwa Yoeli alivyoamuru, wakati siku kuu ya Mungu ilipokaribia, ilileta uraruaji wa mioyo na wala si mavazi, na kumrudia Bwana kwa kufunga, na kulia, na kuomboleza. Kama Mungu alivyosema kwa njia ya Zakaria, roho ya neema na dua ilimwagwa juu ya watoto Wake; walimwangalia Yeye waliyemchoma kwa mikuki, kulikuwepo maombolezo katika nchi, ... na wale waliomtazamia Bwana waalijitesa roho zao mbele Yake.”—Bliss, in Advent Shield and Review, vol. I, uk. 271 (January, 1845).PKSw 306.4

    Katika harakati zote za kidini tangu siku za mitume, hakuna harakati hata moja ambayo ilikuwa na kiasi kidogo cha mapungufu ya kibinadamu na hila za Shetani chache zaidi ya ile ya msimu wa vuli ya mwaka 1844. Hata sasa, baada ya kupita miaka mingi, wote walioshiriki katika vuguvugu lile na wale waliosimama imara juu ya jukwaa la ukweli bado wanahisi mvuto mtakatifu wa kazi ile iliyobarikiwa na wanatoa ushuhuda kuwa lilikuwa vuguvugu la Mungu.PKSw 307.1

    Baada ya kusikia wito, “Haya, bwana arusi amekuja; tokeni mwende kumlaki,” waliokuwa wakingojea “wakaondoka, wakazitengeneza taa zao;” walijifunza neno la Mungu kwa shauku kubwa kabla hawajajulikana. Malaika walitumwa kutoka mbinguni kuwaamsha wale waliokuwa wamekatishwa tamaa na kuwaandaa waweze kupokea ujumbe. Kazi haikusimama katika hekima na elimu ya watu, bali katika nguvu ya Mungu. Hawakuwa watu wenye talanta kubwa zaidi kuliko watu wengine wote, bali walikuwa watu wanyenyekevu na waliojiweka wakfu sana, ambao walikuwa wa kwanza kusikia na kutii wito. Wakulima waliacha mazao yao yakiwa yamesimama katika mashamba yao, mafundi waliweka chini zana zao, na wakiwa na machozi na furaha walitoka kwenda kutoa onyo. Wale waliokuwa wa kwanza kuongoza kazi walikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kujiunga na vuguvugu hili. Makanisa, kwa jumla, walifunga milango yao dhidi ya ujumbe huu, na kundi kubwa la wale walioupokea waliojiondoa katika ushirika wa makanisa. Kwa uongozi wa Mungu, utangazaji huu uliungana na ujumbe wa malaika wa pili na kuleta nguvu kwa kazi ile.PKSw 307.2

    Ujumbe, “Haya, bwana arusi amekuja!” halikuwa suala hasa la kubishania, ingawa ushahidi wa Maandiko ulikuwa wazi na hitimishi. Ulikwenda ukiwa na nguvu shinikizi ambayo ilitikisa roho. Hakukuwa na mashaka, na hakukuwa na maswali. Wakati Kristo alipoingia Yerusalemu kwa shangwe watu walipokuwa wamekusanyika kutoka sehemu zote za nchi kuadhimisha sikukuu walikusanyika katika Mlima wa Mizeituni, na walipojiunga na umati uliokuwa ukimsindikiza Yesu walidaka hamasa ya saa ile na kusaidia kuongeza sauti ya kelele: “Ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana!” (Mathayo 21:9). Hali kadhalika, wasioamini walifurika katika mikutano ya Waadventista—baadhi kwa sababu ya udadisi, baadhi kwa kusudi la kudhihaki—kuhisi nguvu ya ushawishi iliyoandamana na ujumbe: “Haya, bwana arusi amekuja!”PKSw 307.3

    Wakati huo ilikuwepo imani iliyoleta majibu kwa maombi—imani iliyoheshimiwa kwa kupewa tunu. Kama manyunyu ya mvua kwenye ardhi yenye kiu, Roho wa neema alishuka juu ya watafutaji wa dhati. Wale waliotarajia kusimama haraka uso kwa uso na Mkombozi wao walihisi furaha kuu ambayo isingeweza kuelezeka. Nguvu ya Roho Mtakatifu inayolainisha na kutiisha iliyeyusha mioyo wakati mbaraka Wake uliposhushwa kwa wingi juu ya waaminifu, waaminio.PKSw 308.1

    Kwa uaminifu na uchaji wale waliokuwa wameupokea ujumbe walifikia wakati ambao walitumaini kukutana na Bwana wao. Kila asubuhi walihisi kuwa ilikuwa wajibu wao wa kwanza kupata ushahidi wa kukubaliwa kwao na Mungu. Mioyo yao iliunganishwa pamoja, na waliomba pamoja na waliombeana sana. Mara nyingi walikutana pamoja katika maeneo yaliyojitenga ili kuzungumza na Mungu, na sauti za kuombeana zilipaa kwenda mbinguni kutoka katika mashamba na vichaka. Uhakikisho wa kukubaliwa na Mwokozi ulikuwa muhimu kwao kuliko chakula chao cha kila siku; na ikiwa wingu lilitia giza akilini mwao, hawakupumzika mpaka lilipoondoka. Kwa kadiri walivyohisi ushuhuda wa neema inayosamehe, walitamani kumwona Yeye ambaye roho zao zilimpenda.PKSw 308.2

    Lakini pia walikuwa wakielekea kukatishwa tamaa. Wakati wa matarajio ulipita, na Mwokozi wao hakutokea. Kwa uhakika usioyumba walikuwa wametazamia ujio Wake, na sasa walihisi kama Mariamu wakati, alipokuja kwenye kaburi la Mwokozi na kulikuta likiwa tupu, alisema kwa mshangao na machozi machoni: “Wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka” (Yohana 20:13).PKSw 308.3

    Hisia ya kicho, hofu kuwa ujumbe unaweza kuwa wa kweli, kwa muda fulani uliudhibiti ulimwengu usioamini. Baada ya kupita wakati hofu hii haikuondoka mara moja; mwanzoni hawakuthubutu kushangilia ushindi wao dhidi ya wale waliokatishwa tamaa; lakini kwa kuwa hakuna dalili za ghadhabu ya Mungu zilizoonekana, walipona hofu zao na wakaendelea na kejeli na dhihaka zao. Kundi kubwa la wale waliokuwa wamedai kuamini ujio wa haraka wa Bwana, walikana imani yao. Baadhi waliokuwa na uhakika sana wa tukio la ujio wa pili kiburi chao kiliumizwa sana kiasi ambacho walitamani waondoke ulimwenguni. Kama Yona alivyofanya, walimlaumu Mungu, na walichagua kifo kuliko kuishi. Wale waliokuwa wamejenga imani yao juu ya maoni ya wengine, na siyo juu ya neno la Mungu, walikuwa sasa tayari kubadili maoni yao. Wenye dhihaka waliwaongoa walio dhaifu na waoga na kuwaingiza upande wao, na hawa wote waliungana pamoja katika kutangaza kuwa kulikuwa hakuna hofu wala matarajio sasa. Wakati ulikuwa umepita, Bwana hakuja, na ulimwengu ungebaki vilevile kwa maelfu ya miaka.PKSw 308.4

    Walioamini kwa dhati, kutoka moyoni, walikuwa wametoa vyote kwa ajili ya Kristo na walikuwa wameshiriki uwepo Wake kuliko wakati mwingine wote uliopita. Walikuwa, kama walivyoamini, wametoa onyo lao la mwisho kwa ulimwengu; na, wakisubiri kwa muda mfupi kupokelewa katika jamii ya Bwana wao wa Kimungu na malaika wa mbinguni, walikuwa, kwa kiwango kikubwa, wamejitenga na jamii ya wale ambao hawakupokea ujumbe. Kwa shauku kubwa walikuwa wakiomba: “Uje, Bwana Yesu, na uje upesi” Lakini hakuja. Na sasa kuchukua majukumu mazito ya mashaka na kadhia za maisha, na kustahimili kejeli na matusi ya ulimwengu wenye dhihaka, lilikuwa jaribu la kutisha la imani na uvumilivu.PKSw 309.1

    Hata hivyo, kukatishwa tamaa huku, hakukuwa kukubwa sana kama kukata tamaa kulikowapata wanafunzi wakati wa ujio wa kwanza wa Kristo. Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa juu ya mwanapunda, wafuasi Wake waliamini kuwa alikuwa karibu kukalia kiti cha enzi cha Daudi na kuwakomboa Israeli kutoka katika utawala uliowakandamiza. Kwa matumaini makubwa sana na matazamio ya furaha walipigana vikumbo wao kwa wao, kila mmoja akijaribu kuonesha heshima kwa mfalme wao. Wengi walitandaza nguo zao za nje kama zulia katika njia Yake, au walisambaza matawi yenye majani ya mitende. Katika bashasha zao waliungana pamoja na kuimba wimbo wa furaha:“Hosana Mwana wa Daudi!“Wakati Mafarisayo, kwa kuudhiwa na kukasirishwa na kelele hizi za shangwe, walipomwomba Yesu awakemee wanafunzi Wake, alijibu: “Wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele” (Luka 19:40). Unabii lazima utimizwe. Wanafunzi walikuwa wakitimiza kusudi la Mungu; hata hivyo, walikuwa wakielekea kukatishwa tamaa sana. Siku chache tu zilipopita walishuhudia kifo cha kutisha cha Mwokozi wao, na wakaona akilazwa kaburini. Matarajio yao hayakukidhiwa hata chembe, na matumaini yao yakafa pamoja na Yesu. Ni mpaka wakati Bwana wao alipofufuka kutoka kaburini kwa ushindi ndipo waliweza kuelewa kuwa yote yalikuwa yametabiriwa na unabii, na “kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu” (Matendo 17:3).PKSw 309.2

    Miaka mia tano kabla, Bwana alikuwa ametangaza kupitia kwa nabii Zekaria: “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda” (Zekaria 9:9). Ikiwa wanafunzi wangegundua kuwa Kristo alikuwa anaenda kuhukumiwa na kufa, wasingetimiza unabii huu.PKSw 309.3

    Hali kadhalika, Miller na wenzake walitimiza unabii na walitoa ujumbe ambao uvuvio ulitabiri kuwa ungetolewa kwa ulimwengu, lakini ambao wasingeutoa kama wangeelewa kikamilifu unabii ulioeleza kukatishwa tamaa kwao, na ukiwaambia ujumbe mwingine wa kuhubiri kwa mataifa yote kabla ya marejeo ya Bwana. Ujumbe wa kwanza na wa pili ulitolewa kwa wakati sahihi na ulitimiza kazi ambayo Mungu alikusudia itekelezwe nao.PKSw 310.1

    Ulimwengu ulikuwa ukifuatilia, ukitarajia kuwa ikiwa wakati ungepita na Kristo asitokee, mfumo mzima wa Uadventista ungekufa. Lakini wakati wengi, kwa kujaribiwa sana, wakiikana imani yao, walikuwepo baadhi waliosimama imara. Matunda ya vuguvugu la marejeo, roho ya unyenyekevu na kujichunguza moyo, ya kuuacha ulimwengu na kufanya matengenezo ya maisha, iliyoandamana na kazi ile, vilishuhudia kuwa vuguvugu lile lilikuwa la Mungu. Hawakuthubutu kukanusha kuwa nguvu ya Roho Mtakatifu ilishuhudia utangazaji wa ujio wa pili, na hawakuweza kugundua kosa la ukokotoaji wa vipindi vya kiunabii. Wapinzani wao wenye uwezo mkubwa kabisa hawakuweza kuukosoa mfumo wao wa tafsiri ya unabii. Hawakuweza kuafiki, bila ushahidi wa Biblia, kuachana na misimamo yao ambayo ilifikiwa kwa njia ya kujifunza Maandiko kwa bidii kubwa na maombi mengi, kwa akili zilizoangaziwa na Roho wa Mungu na mioyo iliyokuwa ikiwaka kwa nguvu iliyo hai; misimamo iliyostahimili kukosolewa sana na upinzani mkali wa walimu mashuhuri wa dini na watu wenye hekima ya kidunia, na ambayo ilistahimili kwa uimara mkubwa dhidi ya majeshi ya pamoja ya elimu na ufasaha, na shutuma na dharau za watu wenye heshima zao na watu wa kawaida wa mitaani.PKSw 310.2

    Ni kweli, kulikuwepo kukosea kuhusiana na tukio lililotarajiwa, lakini hata hivyo, hili halikuweza kuyumbisha imani yao katika neno la Mungu. Wakati Yona alipotangaza katika mitaa ya Ninawi kuwa ndani ya siku arobaini mji ungeangamizwa, Mungu alikubali unyenyekevu wa watu wa Ninawi na akawaongezea muda wao wa rehema; pamoja na hayo ujumbe wa Yona ulitoka kwa Mungu, na Ninawi ilijaribiwa kulingana na mapenzi ya Mungu. Waadventista waliamini kuwa kwa jinsi kama hiyo Mungu aliwaongoza kutoa onyo la hukumu. “Ujumbe,“walisema,“umeijaribu mioyo ya wote waliousikia, na umeamsha upendo kwa ajili ya ujio wa Bwana; au umechochea chuki, inayojulikana au isiyojulikana kwa wanadamu, lakini inayojulikana kwa Mungu, dhidi ya ujio Wake. Umechora mstari, ... ili kwamba wale watakaopima mioyo yao, waweze kujua ni upande gani wa mstari wangekutwa, ikiwa Bwana angekuwa amekuja wakati ule— iwapo wangesema kwa furaha, ‘Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie;’ au ikiwa wangeiita miamba na milima iwaangukie ili kuwaficha wasiuone uso Wake Yeye aketie juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwanakondoo. Mungu, hivyo basi, tunavyoamini, amewajaribu watu Wake, ameijaribu imani yao, amewathibitisha, na kuona ikiwa wataogopa, katika saa ya kujaribiwa, na kuicha nafasi ambayo angeona inafaa kuwaweka; na ikiwa wangeweza kuachia ulimwengu huu na kuliamini neno la Mungu kwa uthabiti usioyumba.”—The Advent Herald and Signs of the Times Reporter, vol. 8, No. 14 (Nov 13, 1844).PKSw 310.3

    Hisia za wale ambao bado waliamini kuwa Mungu aliwaongoza katika uzoefu wao uliopita zimeelezwa katika maneno ya William Miller:PKSw 311.1

    “Ikiwa ningekuwa na uwezo kuishi kwa mara nyingine tena, kwa ushahidi ule ule ambao nilikuwa nao wakati ule, niwe mwaminifu kwa Mungu na kwa mwanadamu, ningefanya kama nilivyofanya.” “Ni tumaini langu kuwa nimetakasa mavazi yangu kutoka kwa damu za watu. Ninahisi kuwa, kwa kadiri ya uwezo wangu, nimejinasua kutoka katika hatia zao zote na hukumu yao.” “Ingawa nimekatishwa tamaa mara mbili,” aliandika huyu mtu wa Mungu, “Sijahuzunika sana au kuvunjika moyo kabisa .... Tumaini langu katika ujio wa Kristo lina nguvu na litadumu kuwa na nguvu daima. Nimefanya tu kile ambacho, baada ya miaka ya tafakari ya kina, nilihisi ilikuwa wajibu wangu kulifanya. Ikiwa nimekosea, imekuwa hivyo kwa upande wa ukarimu, upendo kwa wanadamu wenzangu, na usadikisho wa wajibu wangu kwa Mungu.” “Jambo moja nalijua, sikuhubiri chochote kile isipokuwa kile tu ambacho nimekiamini; na Mungu amekuwa pamoja nami; nguvu Yake imedhihirika katika kazi, na mengi mazuri yametokea.” “Maelfu ya watu, kwa mtazamo wa kibinadamu, wamehamasishwa kujifunza Maandiko kwa kuhubiri juu ya wakati; na kwa njia hiyo, kwa njia ya imani na umwagikaji wa damu ya Kristo, wamepatanishwa na Mungu.”— Bliss, ukurasa 256, 255, 277, 280, 281. “Sikutafuta tabasamu kutoka kwa watu wenye kiburi, wala kutetemeka wakati ulimwengu ulipokunja uso. Siwezi kununua sasa upendeleo wao, wala siwezi kufanya zaidi ya wajibu wangu ili kuchokoza chuki zao. Sitafuti uhai wangu mikononi mwao, wala siogopi, natumaini, kuupoteza, ikiwa Mungu katika uongozi wake mwema ataamuru hivyo.”—J. White, Life of Wm. Miller, ukurasa 315.PKSw 311.2

    Mungu hakuwaacha watu Wake; Roho Wake aliendelea kuwa na wale ambao hawakuikataa mara moja nuru waliyoipokea, na kukana hadharani vuguvugu la marejeo. Katika Waraka kwa Waebrania kuna maneno ya kutia moyo na ya onyo kwa waliojaribiwa, waliongoja wakati wa janga hili: “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu” (Waebrania 10:35-39).PKSw 311.3

    Kwamba onyo hili limeelekezwa kwa kanisa la siku za mwisho huthibitishwa kwa maneno yanayoelekeza kwa ukaribu wa ujio wa Bwana: “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.” Na imedokezwa moja kwa moja kuwa kungekuwepo mwonenakano wa kuchelewa. Maelekezo yaliyotolewa hapa yanahusiana moja kwa moja na uzoefu wa Waadventista wakati huu. Watu wanaoonywa hapa walikuwa katika hatari ya kutokuwa na imani. Walikuwa wamefanya mapenzi ya Mungu kwa kufuata uongozi wa Roho Wake na neno Lake; lakini hata hivyo walishindwa kuelewa kusudi Lake katika uzoefu wao uliopita, wala hawakuweza kutambua njia mbele yao, na walijaribiwa kuwa na mashaka kama kweli Mungu alikuwa akiwaongoza. Wakati huu maneno haya yalikuwa na maana kwao: “Sasa mwenye haki ataishi kwa imani.” Wakati nuru kali ya “kilio cha usiku wa manane” ilipoangazia juu ya njia yao, na wakaona unabii ukifunuliwa na utimizwaji wa dalili zilizoashiria kuwa ujio wa Kristo ulikuwa karibu, walikwenda, kama hali yenyewe ilivyokuwa, kwa kuona kwa macho. Lakini sasa, wakiwa wameinamishwa chini kwa matumaini yaliyokatishwa tamaa, wangeweza kuinuka na kusimama tu kwa kumwamini Mungu na kuliamini neno Lake. Ulimwengu wa dhihaka ulisema: “Mmedanganywa. Acheni imani yenu, na semeni kuwa vuguvugu la marejeo lilikuwa la Shetani.” Lakini neno la Mungu lilitangaza: “Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.” Kuikana imani yao hadharani sasa, na kuikataa nguvu ya Roho Mtakatifu iliyoambatana na ujumbe, ingekuwa kurudi nyuma na kuelekea upotevuni. Walitiwa moyo na kupata ujasiri kutokana na maneno haya ya Paulo: “Basi msiutupe ujasiri wenu;” “mnahitaji saburi,” “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.” Usalama wao pekee ulikuwa kushikilia nuru ambayo tayari walikuwa wameipokea kutoka kwa Mungu, kushikilia sana ahadi Zake, na kuendelea kuchunguza Maandiko, na kwa uvumilivu mwingi kungoja ili kupokea nuru zaidi.PKSw 312.1

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents