Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 29—Chimbuko la Uovu

    Kwa akili za watu wengi, chimbuko la dhambi pamoja na sababu ya kuwepo kwake ni jambo linalotatanisha sana. Wanaona kazi ya uovu, na matokeo yake ya kutisha ya huzuni na taabu, na wanahoji ni kwa jinsi gani haya yote yanaweza kuwepo chini ya utawala wa Mungu ambaye hana kikomo katika hekima, nguvu, na upendo. Hapa kuna siri ambayo hawana maelezo yake. Na katika kutokuwa na hakika kwao na kwa sababu ya mashaka yao wanapofushwa wasione ukweli uliofunuliwa kwa uwazi katika neno la Mungu na ulio muhimu kwa ajili ya wokovu. Kuna wale ambao, katika maswali yao kuhusu uwepo wa dhambi, wanajaribu kutafuta mambo ambayo Mungu hakuyafunua; matokeo yake hawapati suluhisho la matatizo yao; na kwa kuwa wanasukumwa na mashaka wanachukulia kukosa suluhisho huko kama udhuru wa kutupilia mbali maneno ya Maandiko Matakatifu. Wengine, hata hivyo, hawana uelewa wa kutosha wa tatizo kubwa na uovu, kutokana na ukweli kuwa mapokeo na tafsiri potovu vimefunika fundisho la Biblia kuhusu tabia ya Mungu, msingi wa serikali Yake, na kanuni Zake za kushughulikia dhambi.PKSw 376.1

    Haiwezekani kueleza chimbuko la dhambi kwa namna ambayo inawezesha kutoa sababu za kuwepo kwake. Hata hivyo inawezekana kuelewa chimbuko na mwisho wa dhambi kwa namna ambayo inawezesha kudhihirisha kikamilifu haki na ukarimu wa Mungu katika kushughulikia uovu.PKSw 376.2

    Hakuna wazo ambalo limefundishwa kwa uwazi zaidi katika Maandiko kuliko wazo kuwa Mungu kwa namna yo yote ile hawajibiki kwa ajili ya uingiaji wa dhambi; kwamba hakukuwa na uondoaji wa kiimla wa neema ya Mungu, kwamba hakukuwa na dosari katika serikali ya Mungu, iliyosababisha kuinuka kwa uasi. Dhambi ni mvamizi, ambaye hakuna sababu inaweza kutolewa kwa ajili ya uwepo wake. Dhambi ni fumbo, haielezeki; kuitolea udhuru ni kuitetea. Ikiwa udhuru kwa ajili ya dhambi ungepatikana, au sababu ioneshwe kwa ajili ya uwepo wake, ingekoma kuwa dhambi. Fasili pekee ya dhambi ni ile iliyotolewa katika neno la Mungu; dhambi ni “uasi wa sheria;” ni matokeo ya utekelezaji wa kanuni inayopingana na sheria kuu ya upendo ambao ni msingi wa serikali ya Mungu.PKSw 376.3

    Kabla ya kuingia kwa uovu kulikuwa na amani na furaha katika Ulimwengu wote. Mambo yote yalikuwa katika mwafaka na mapenzi ya Mungu. Upendo kwa Mungu ulikuwa juu, upendo wa mtu mmoja kwa mwingine ulikuwa hauna upendeleo. Kristo aliye Neno, Mwana Pekee wa Mungu, alikuwa mmoja na Baba wa milele,—mmoja katika asili, katika tabia, na katika kusudi,—mwenye uhai pekee katika Ulimwengu wote aliyekuwa na fursa ya kushiriki mashauri na makusudi ya Mungu. Kwa njia ya Kristo Baba alitekeleza uumbaji wa wote wenye uhai walioko mbinguni. “Katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni...ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka” (Wakolosai 1:16); na kwa Kristo, sawasawa na Baba, mbingu yote ilitoa utii.PKSw 376.4

    Sheria ya upendo ikiwa ndiyo msingi wa serikali ya Mungu, furaha ya viumbe wote ilitegemea utii wao kamili kwa kanuni kuu zake za haki. Mungu hutamani kupata kwa viumbe Wake wote huduma ya upendo—heshima inayotokana na utambuzi wa kina wa tabia Yake. Hafurahishwi na utii wa shuruti, na kwa wote anatoa uhuru wa uchaguzi, kwamba wamtumikie kwa hiari.PKSw 377.1

    Lakini kuna kiumbe mmoja aliyechagua kutumia vibaya uhuru huu. Dhambi ilitokana na yeye ambaye, akiwa wa pili baada ya Kristo, aliheshimiwa sana na Mungu na alikuwa juu sana katika nguvu na utukufu miongoni mwa wakazi wa mbinguni. Kabla ya kuanguka kwake, Lusifa alikuwa wa kwanza miongoni mwa makerubi wafunikao, akiwa mtakatifu na safi. “Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri. Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako....Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (Ezekieli 28:12-15).PKSw 377.2

    Kulikuwa na uwezekano wa Lusifa kudumisha fadhila aliyopewa na Mungu, akipendwa na kuheshimiwa na jeshi la malaika, akitumia uwezo wake mkubwa kuwabariki wengine na kumtukuza Muumbaji wake. Lakini, nabii anasema,“Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako” (Aya ya 17). Kidogo kidogo, Lusifa aliendekeza shauku ya kujiinua. “Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.” “Nawe ulisema, ... Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano....Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu” (Aya ya 6; Isaya 14:13, 14). Badala ya kutafuta kumfanya Mungu awe juu katika kupendwa na kuheshimiwa na viumbe Wake, Lusifa alielekeza nguvu zake kuwashawishi viumbe wa Mungu wamtumikie na kumheshimu yeye binafsi. Na akitamani heshima ambayo Baba wa milele alimpa Mwana Wake, huyu mkuu wa malaika alipigania kuchukua mamlaka ambayo yalikuwa ya Kristo peke Yake.PKSw 377.3

    Mbingu yote ilifurahia kuakisi utukufu wa Muumbaji na kuimba sifa Zake. Na wakati Mungu alipoheshimiwa hivyo, hali ilikuwa ya amani na furaha. Lakini tabia hii ya kujiinua ya Lusifa iliharibu utangamano wa mbinguni. Huduma ya uinuaji wa nafsi, kinyume na mpango wa Mungu, iliamsha hisia za uovu katika akili za yule ambaye utukufu wa Mungu ulikuwa mwingi sana. Mabaraza ya mbinguni yalimbeleleza sana Lusifa. Mwana wa Mungu aliwasilisha mbele yake ukuu, wema, na haki ya Muumbaji, na asili takatifu, isiyobadilika ya sheria Yake. Mungu Mwenyewe aliweka utaratibu mbinguni; na kwa kuuvunja, Lusifa alimvunjia heshima Muumbaji wake, na alileta maangamizi juu yake mwenyewe. Lakini onyo, lililotolewa katika upendo na rehema zisizo na kikomo, liliamsha roho ya upinzani. Lusifa aliruhusu wivu wake dhidi ya Kristo ushinde, na alidhamiria kuendeleza mapambano.PKSw 378.1

    Kiburi kilichotokana na utukufu wake kilipalilia hamu yake ya ukubwa. Heshima kubwa aliyopewa hakuichukulia kama karama kutoka kwa Mungu na haikumpa shauku ya kumshukuru Muumbaji wake. Alijitukuza kwa sababu ya mwangaza wake na cheo chake cha juu, na alipigania kuwa sawa na Mungu. Alipendwa na aliheshimiwa na jeshi la mbinguni. Malaika walifurahia kutekeleza amri zake, na alivikwa hekima na utukufu mwingi zaidi kuliko wengine wote. Lakini Mwana wa Mungu alitambuliwa kuwa Mtawala wa mbingu, akiwa mmoja na Baba katika nguvu na mamlaka. Katika mabaraza yote ya Mungu, Kristo alikuwa mshiriki, lakini Lusifa hakuruhusiwa kushiriki katika makusudi ya Kimungu kama Kristo alivyoruhusiwa. “Kwa nini,” malaika huyu mwenye nguvu nyingi alihoji, “Kristo awe mkubwa kiasi hicho? Kwa nini apewe heshima kubwa zaidi kuliko Lusifa?”PKSw 378.2

    Akiondoka mahali pake ambapo palikuwa karibu sana na uwepo wa Mungu, Lusifa alikwenda kueneza roho ya kutoridhika miongoni mwa malaika. Akifanya kazi kwa siri iliyofichika sana, na kwa muda fulani akificha kusudi lake halisi chini ya mwonekano wa kicho kwa Mungu, alichochea roho ya kutoridhika kuhusiana na sheria zilizotawala wenye uhai wa mbinguni, akieleza kuwa ziliweka mipaka isiyokuwa ya lazima. Kwa kuwa asili zao zilikuwa takatifu, alidai kuwa malaika walipaswa kutii maagizo ya nia zao wenyewe. Alitafuta kujenga mazingira ya kuhurumiwa kwa kuwasilisha hoja kuwa Mungu hakumtendea haki kwa kumpa Kristo heshima kubwa kiasi kile. Alidai kuwa kwa kupigania madaraka makubwa zaidi hakuwa na kusudi la kujiinua, bali alitafuta uhuru kwa ajili ya wakazi wote wa mbinguni, na kwamba kwa njia hiyo wakazi wa mbinguni wangepata maisha yaliyo juu na bora zaidi.PKSw 378.3

    Mungu katika rehema yake kuu alimvumilia Lusifa kwa muda mrefu. Lusifa hakushushwa kutoka nafasi yake ya juu alipoonesha kwa mara ya kwanza roho ya kutoridhika, wala hata alipoanza kuwasilisha madai yake ya uongo mbele ya malaika watiifu. Kwa muda mrefu alibakizwa mbinguni. Tena na tena alipewa fursa ya msamaha kwa sharti la kutubu na kujisalimisha. Juhudi ambazo upendo usio na mwisho na hekima isiyo na kikomo pekee ndiyo ingeweza kubuni zilifanywa kumsaidia aone kosa lake. Roho ya kutoridhika ilikuwa haijawahi kujulikana mbinguni kabla ya hapo. Lusifa mwenyewe mwanzoni hakuelewa kule alikokuwa akielekea; hakuelewa asili hasa ya hisia zake. Lakini alipoona kuwa kutoridhika kwake hakuna msingi, Lusifa alishawishika kuwa alikuwa amekosea, kuwa madai ya Mungu yalikuwa ya haki, na kuwa ilimpasa ayakubali kama yalivyokubaliwa mbinguni kote. Ikiwa angefanya hivyo, angeweza kuokoa nafsi yake na kuwaokoa malaika wengi. Wakati huo alikuwa bado hajaondoa utii wake wote kwa Mungu. Ingawa alikuwa ameicha nafasi yake kama kerubi afunikaye, lakini ikiwa angekuwa tayari kurudi kwa Mungu, akiikubali hekima ya Mungu, na kuridhika kujaza nafasi aliyopangiwa katika mpango mkuu wa Mungu, angeweza kurudishwa katika ofisi yake. Lakini kiburi kilimzuia kujisalimisha. Alishikilia msimamo wake na kutetea njia yake, alisimama kidete kuwa hakuwa na haja ya kutubu, na alijisalimisha kwa nafsi yake mwenyewe kikamilifu, na kujipanga kuingia katika pambano kuu, dhidi ya Mwumbaji wake.PKSw 378.4

    Nguvu zote za akili yake yenye uwezo mkubwa zilielekezwa katika kazi ya udanganyifu, ili aungwe mkono na malaika waliokuwa chini ya usimamizi wake. Hata ukweli kuwa Kristo alimwonya na kumshauri ulipotoshwa ili kujenga hoja ya kuunga mkono mipango yake ya usaliti. Kwa wale ambao upendo wao wenye dhamana kwake ulishikamana naye kwa karibu, Shetani alieleza kuwa alihukumiwa kwa makosa, kuwa cheo chake hakikuheshimiwa, na kuwa uhuru wake uliminywa. Kutoka kuwakilisha vibaya maneno ya Kristo alianza kukwepa kusema ukweli na hatimaye alisema uongo moja kwa moja, akimtuhumu Mwana wa Mungu kuwa alikuwa na mpango wa kumdhalilisha mbele ya wakazi wa mbinguni. Alitafuta pia kuleta fitina kati yake na malaika watiifu. Wote wale ambao hakufaulu kuwapotosha na kuwavuta upande wake aliwatuhumu kuwa walikuwa hawajali maslahi ya wenye uhai wa mbinguni. Kazi ambayo alikuwa akiifanya mwenyewe ndiyo aliyowatuhumu kufanywa na wale waliobaki wakiwa waaminifu kwa Mungu. Na ili kuthibitisha mashitaka yake dhidi ya dhuluma za Mungu dhidi yake, aliwakilisha vibaya maneno na matendo ya Muumbaji. Ilikuwa sera yake kuwatatanisha malaika kwa hoja zake zenye hila kuhusu makusudi ya Mungu. Kila kitu ambacho kilikuwa rahisi alikivika joho la usiri, na upotoshaji uliorembwa vizuri alitia mashaka juu ya maneno ya wazi ya Yehova. Nafasi yake ya juu, akiwa karibu kabisa na utawala wa Kimungu, ilichangia nguvu nyingi zaidi katika upotoshaji wake, na wengi waliungana naye katika uasi dhidi ya mamlaka ya Mbinguni.PKSw 379.1

    Mungu katika hekima Yake alimruhusu Shetani aendelee na kazi yake, mpaka roho ya kutoridhika ilipokomaa na kuwa uasi kamili. Ilikuwa muhimu mipango yake iendelezwe hadi ikomae kikamilifu, ili asili yake na mwelekeo wake halisi vidhihirike mbele ya wote. Lusifa, kama kerubi aliyepakwa mafuta, alikuwa na hadhi ya juu sana; alipendwa sana na wenye uhai wa mbinguni, na mvuto wake kwao ulikuwa mkubwa. Serikali ya Mungu ilijumuisha siyo tu wakazi wa mbinguni, bali pia wakazi wa sayari zingine zilizoumbwa na Mungu; na Shetani alifikiri kuwa ikiwa angefanikiwa kuwabeba malaika wote wa mbinguni katika uasi wake, angefaulu kubeba hata sayari zingine. Alikuwa amewasilisha upande wake wa mgogoro kwa ujanja sana, akitumia hila na ulaghai kutimiza makusudi yake. Nguvu yake ya kudanganya ilikuwa kubwa, na kwa kujifunika katika koti la uongo alifanikiwa. Hata malaika watiifu hawakutambua tabia yake wala kuona kile ambacho kingekuwa matokeo ya kazi yake.PKSw 380.1

    Shetani alikuwa akiheshimiwa sana, na matendo yake yote yalifunikwa na usiri mkubwa, kiasi ambacho ilikuwa vigumu kuwafunulia malaika asili halisi ya kazi yake. Bila kukomaa kikamilifu, dhambi isingeonekana kuwa ni jambo baya. Mpaka wakati huo dhambi haikuwepo katika ulimwengu wa Mungu, na wenye uhai watakatifu hawakujua asili yake na ubaya wake. Hawakujua matokeo ya kutisha ambayo yangefuata baada ya kuiweka kando sheria ya Mungu. Shetani, kwa mara ya kwanza, aliificha kazi yake chini ya madai maalumu ya utii kwa Mungu. Alidai alikuwa akitafuta kuhamasisha heshima kwa Mungu, uimara wa serikali Yake, na ustawi wa wakazi wa mbinguni. Wakati akipenyeza kutoridhika katika mawazo ya malaika walioko chini yake, kwa hila alifanya ionekane kana kwamba alikuwa akitaka kuondoa kutoridhika. Wakati akidai kuwa mabadiliko yafanywe katika utaratibu na sheria za serikali ya Mungu, alidai kuwa mabadiliko haya yalikuwa muhimu ili kudumisha utangamano mbinguni.PKSw 380.2

    Katika kushughulika na dhambi, Mungu alitumia haki na kweli tu. Shetani alitumia kile ambacho Mungu hawezi kutumia—udanganyifu na uongo. Alitafuta kubadilisha ukweli wa neno la Mungu uonekane uongo na aliwasilisha vibaya mpango wa serikali Yake mbele ya malaika, akidai kuwa Mungu hakuwa na haki ya kuweka sheria na kanuni za kuwaongoza wakazi wa mbinguni; kwamba katika kuwataka viumbe Wake wajisalimishe Kwake na kumtii Yeye, Mungu alikuwa akitafuta kujiinua tu. Kwa hiyo ilipasa idhihirike mbele ya wakazi wote wa mbinguni, na mbele ya sayari zote, kuwa serikali ya Mungu ilikuwa ya haki, sheria Yake ilikuwa kamili. Shetani alitengeneza mazingira yaliyoonesha kana kwamba yeye mwenyewe alikuwa akipambania usitawi wa Ulimwengu wote. Tabia halisi ya Ibilisi, na lengo lake halisi, ilikuwa lazima vieleweke kwa wote. Ilipasa apewe muda ili ajifunue mwenyewe kwa kazi zake ovu.PKSw 380.3

    Uhasama uliokuwa umesababishwa na matendo yake mwenyewe huko mbinguni, Shetani alidai kuwa ulisababishwa na sheria na serikali ya Mungu. Alitangaza kuwa maovu yote yalikuwa matokeo ya utawala wa Mungu. Alidai kuwa ilikuwa kusudi lake kuboresha sheria za Yehova. Kwa hiyo ilikuwa muhimu apewe nafasi aoneshe asili ya madai yake, na aoneshe utendaji wa mabadiliko aliyoyapendekeza katika sheria takatifu. Ilipasa kazi yake yenyewe imhukumu. Shetani alidai tangu mwanzo kuwa hakuwa anafanya uasi. Ilipasa ulimwengu wote umwone mwongo akiwa amefunuliwa wazi.PKSw 381.1

    Hata baada ya kuamriwa kuwa asingeweza kuendelea kubaki mbinguni, Hekima Isiyo na Kikomo haikumwangamiza Shetani. Kwa kuwa huduma ya upendo ndiyo pekee inayokubalika kwa Mungu, utii wa viumbe Wake inapasa ujengwe juu ya kushawishika kwao kuwa Mungu ni mwenye haki na mwenye ukarimu. Wakazi wa mbinguni na wa sayari zingine, kwa kutokujiandaa kuelewa asili na athari za dhambi, wasingeona haki na rehema za Mungu katika kumwangamiza Shetani. Ikiwa angeangamizwa asiwepo kabisa mara moja, wangemtumikia Mungu kwa hofu kuliko kwa upendo. Mvuto wa mdanganyaji usingeangamizwa kabisa, wala roho ya uasi isingeondolewa kabisa. Ilipasa uovu uruhusiwe ukomae kabisa. Kwa manufaa ya ulimwengu wote katika vizazi vyote, Shetani alipaswa kuendeleza kanuni zake kikamilifu, ili shutuma zake dhidi ya serikali ya Mungu zionekane katika nuru yake halisi kwa wenye uhai wote walioumbwa, ili haki na rehema za Mungu na kutobadilika kwa sheria Yake visihojiwe milele zote.PKSw 381.2

    Uasi wa Shetani ulipaswa uwe fundisho kwa ulimwengu wote katika zama zote zijazo, ushuhuda wa kudumu wa asili na athari za kutisha za dhambi. Utendaji kazi wa utawala wa Shetani, madhara yake kwa wanadamu na malaika, vingeonesha kile ambacho lazima kiwe tunda la kukiuka mamlaka ya Mungu. Utendaji kazi wa Shetani ungeshuhudia kuwa uwepo wa serikali ya Mungu na sheria Yake umeambatana na ustawi wa viumbe wote aliowaumba. Kwa hiyo, historia ya jaribio hili la uasi, litakuwa ulinzi wa daima kwa wote wenye akili, kuwazuia wasidanganywe kuhusiana na asili ya uasi, na kuwaepusha na dhambi na mateso ya adhabu zake.PKSw 381.3

    Karibu kabisa na mwisho wa pambano mbinguni, mdanganyaji mkuu aliendelea kujihesabia haki. Ilipotangazwa kuwa yeye pamoja wafuasi wake ilipasa wafukuzwe na watoke katika makao ya mbinguni, ndipo kiongozi wa uasi aliapa kwa ujasiri kuidharau sheria ya Muumbaji. Alirudia dai lake kuwa malaika hawakuhitaji kutawaliwa, bali ilipasa waachiwe wafuate mapenzi yao wenyewe, ambayo yangeweza kuwaongoza kwa usahihi. Alizishutumu amri za Mungu kuwa ni kizuizi dhidi ya uhuru wao na alitangaza kuwa ilikuwa kusudi lake kuhakikisha kuwa anafutilia mbali sheria; kuwa, wakiondolewa kizuizi hiki, majeshi ya mbinguni yataweza kuingia katika hali ya juu, ya utukufu zaidi ya maisha.PKSw 381.4

    Kwa nia moja, Shetani na jeshi lake walirusha lawama za uasi wao wote kwa Kristo, wakidai kuwa ikiwa wasingekemewa, wasingeasi hata kidogo. Pamoja na ugumu wa mioyo na ujeuri katika uasi wao, wakitafuta bila mafanikio kupindua serikali ya Mungu, lakini wakidai kwa kufuru kuwa wao ni wahanga wasiokuwa na hatia wa mamlaka kandamizi, mwasi mkuu na wafuasi wake wote hatimaye walifukuzwa mbinguni.PKSw 382.1

    Roho ile ile iliyoanzisha uasi mbinguni bado inachochea uasi duniani. Shetani akiwa na wanadamu anaendeleza sera ileile aliyotumia akiwa na malaika. Roho yake sasa inatawala ndani ya watoto wa uasi. Kama yeye, wanatafuta kuvunja vizuizi vya sheria ya Mungu na wanawaahidi watu uhuru kwa njia ya kukiuka kanuni zake. Kukemea dhambi kunaamsha roho ya chuki na upinzani. Wakati ujumbe wa Mungu wa onyo unapoletwa nyumbani katika dhamiri, Shetani anawaongoza kujihesabia haki na kutafuta huruma za watu katika njia yao ya dhambi. Badala ya kusahihisha makosa yao, wanaamsha hasira dhidi ya yule anayewakemea, kana kwamba yeye pekee ndiye chanzo cha tatizo. Tangu siku za Habili mwenye haki hadi wakati wetu roho hiyo imeoneshwa kwa wale wanaothubutu kukemea dhambi.PKSw 382.2

    Kwa kuwakilisha vibaya kama huko kwa tabia ya Mungu kama alivyofanya mbinguni, akisababisha Mungu aonekane kuwa ni mkali na katili, Shetani alishawishi wanadamu kutenda dhambi. Na baada ya kufaulu katika hilo, alitangaza kuwa vizuizi vya Mungu visivyokuwa vya haki vimesababisha wanadamu kuanguka, kama vilivyosababisha uasi wake mwenyewe mbinguni.PKSw 382.3

    Lakini Yule Ambaye Anaishi Milele anatangaza tabia Yake: “Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe” (Kutoka 34:6, 7).PKSw 382.4

    Katika kufukuzwa kwa Shetani kutoka mbinguni, Mungu alitangaza haki Yake na alidumisha heshima ya kiti Chake cha enzi. Lakini wakati mwanadamu alipotenda dhambi kwa kusikiliza uongo wa hii roho iliyoasi, Mungu alitoa ushahidi wa upendo Wake kwa kumtoa Mwana Wake wa pekee afe kwa ajili ya wanadamu walioanguka dhambini. Katika upatanisho tabia ya Mungu ilifunuliwa. Hoja ya nguvu ya msalaba huonesha kwa sayari zote kuwa ile njia ya dhambi ambayo Lusifa aliichagua kwa namna yoyote ile haikutokana na serikali ya Mungu.PKSw 382.5

    Katika shindano kati ya Kristo na Shetani, wakati wa huduma ya Mwokozi duniani, tabia ya mdanganyaji mkuu iliwekwa wazi. Hakuna jambo lo lote lile lingeweza kumng'oa Shetani na kumtoa katika mioyo ya malaika wa mbinguni na ya wakazi watiifu wa sayari zote kwa ufanisi kama pambano lake la kikatili dhidi ya Mkombozi wa ulimwengu. Kufuru yake ya kijasiri ya kumtaka Kristo amsujudie, ujasiri wake wa kiburi wa kumchukua hadi juu ya kilele cha mlima na mnara wa hekalu, kusudi lake lenye nia mbaya lililonekana wakati akimwagiza ajitupe chini kutoka katika kilele chenye kutia kizunguzungu, ubaya usiosinzia uliomwinda Kristo kila mahali alipokwenda, ukivuvia mioyo ya makuhani na watu kuukataa upendo Wake, na hatimaye wakapiga kelele, “Asulubiwe! Asulubiwe!”—yote haya yaliamsha mshangao na hasira ya Kimungu ya sayari zote.PKSw 383.1

    Shetani ndiye aliyeuchochea ulimwengu umkatae Kristo. Mkuu wa uovu alitumia nguvu na hila zake zote kumwangamiza Yesu; kwani aliona kuwa rehema na upendo wa Mwokozi, huruma Yake na uvumilivu Wake usiochoka, viliwakilisha kwa ulimwengu tabia ya Mungu. Shetani alipinga kila dai lililotolewa na Mwana wa Mungu na alitumia watu kama mawakala wake kujaza maisha ya Mwokozi kwa mateso na huzuni. Ulaghai na uongo aliotumia kuzuia kazi ya Yesu, chuki aliyoionesha kwa njia ya wana wa uasi, ukatili wake dhidi Yake Yeye ambaye maisha Yake yalijaa wema usiokuwa na mfano, yote yalitokana na ulipizaji kisasi wenye mizizi mirefu. Mioyo iliyominywa ya kijicho na ubaya, chuki na kulipiza kisasi, vilipasukia Kalwari dhidi ya Mwana wa Mungu, wakati mbingu yote ikitazama kwa ukimya wenye hofu kuu na mshangao.PKSw 383.2

    Wakati kafara kuu ilipokamilishwa, Kristo alipaa juu, akikataa kutukuzwa na malaika mpaka awasilishe ombi hili: “Hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo” (Yohana 17:24). Ndipo kwa upendo na nguvu zisizoelezeka jibu lilitoka katika kiti cha enzi cha Baba: “Na wamsujudu malaika wote wa Mungu” (Waebrania 1:6). Hakuna doa lililokuwa juu ya Yesu. Kudhalilishwa kuliisha, kafara Yake ilikamilika, na alipewa jina lipitalo majina yote.PKSw 383.3

    Sasa hatia ya Shetani ilionekana wazi bila udhuru. Alidhihirisha tabia yake ya kweli kuwa yeye ni mwongo na muuaji. Ilionekana kuwa roho ile ile ambayo kwayo aliwatawala wanadamu, ambao walikuwa chini ya mamlaka yake, ndiyo ambayo angeitumia ikiwa angeruhusiwa kuwatawala wakazi wa mbinguni. Alidai kuwa kukiuka sheria ya Mungu kungeleta uhuru na kuinuliwa juu; lakini ilionekana kuwa kulileta utumwa na kushushwa chini.PKSw 383.4

    Mashitaka ya uongo ya Shetani dhidi ya tabia na serikali ya Mungu yalionekana katika nuru yake ya kweli. Alikuwa amemshitaki Mungu kuwa alikuwa akitafuta kujiinua Mwenyewe tu kwa kuwataka viumbe Wake wajisalimishe Kwake na kumtii Yeye, na alikuwa ametangaza kuwa, wakati Muumbaji alidai wengine wote wajikane nafsi, Yeye Mwenyewe hakujikana nafsi na hakutoa kafara yoyote. Sasa ilikuwa imedhihirika kuwa kwa ajili ya wokovu wa jamii iliyoanguka na kutenda dhambi, Mtawala wa sayari zote alitoa kafara kubwa kuliko zote ambazo upendo ungeweza kutoa; kwa kuwa “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi Yake” (2 Wakorintho 5:19). Ilionekana, pia, kuwa wakati Lusifa alifungua mlango na dhambi kwa sababu ya tamaa yake ya heshima na ukuu, Kristo, ili kuangamiza dhambi, alijinyenyekesha na akawa mtii hadi mauti.PKSw 383.5

    Mungu alionesha chuki Yake dhidi ya kanuni za uasi. Mbingu yote iliona haki Yake ikiwa imefunuliwa, katika hukumu ya Shetani na katika ukombozi wa mwanadamu. Lusifa alikuwa ametangaza kuwa ikiwa sheria ya Mungu haibadiliki, na adhabu yake isingeondolewa, na mkosaji lazima asingekubaliwa na Mwumbaji tena. Alikuwa amedai kuwa jamii ya wanadamu waliotenda dhambi walikuwa nje ya wigo wa ukombozi na hivyo basi walikuwa mawindo yake halali. Lakini kifo cha Kristo kilikuwa hoja kwa ajili ya mwanadamu ambayo isingeshindwa. Adhabu ya sheria ilianguka juu Yake Yeye aliyekuwa sawa na Mungu, na mwanadamu walipewa uhuru wa kupokea haki ya Kristo na kwa maisha ya toba na unyenyekevu aweze kushinda, kama Mwana wa Mungu alivyoshinda, juu ya nguvu ya Shetani. Hivyo Mungu ni Mwenye haki na Mhesabiaji wa haki wa wale wote wanaomwamini.PKSw 384.1

    Lakini haikuwa kwa ajili ya utekelezaji wa ukombozi wa mwanadamu tu Kristo alikuja duniani kuteseka na kufa. Alikuja “kuitukuza sheria” na “kuiadhimisha” (Isaya 42:21). Siyo wakazi wa sayari hii pekee ambao walipaswa kuichukulia sheria kama ilivyopaswa kuchukuliwa; bali ilikuwa kwa ajili ya kuonesha kwa wakazi wa sayari zote kuwa sheria ya Mungu haibadiliki. Ikiwa madai yake yangeweza kuwekwa pembeni, basi Mwana wa Mungu asingelazimika kupoteza uhai Wake kwa ajili ya upatanisho wa dhambi. Kifo cha Kristo huthibitisha kuwa haibadiliki. Na kafara ambayo upendo usio na kikomo ulilazimisha Baba na Mwana kuitoa, ili wenye dhambi waweze kukombolewa, huonesha kwa sayari zote—hakuna kitu chochote chini ya mpango huu wa upatanisho kingeweza kukidhi upatanisho—kwamba haki na rehema ni msingi wa sheria ya serikali ya Mungu.PKSw 384.2

    Katika utekelezaji wa mwisho wa hukumu itakuja kuonekana kuwa hakuna sababu yo yote ya kuwepo kwa dhambi. Wakati Jaji Mkuu wa dunia yote atakapomwuliza Shetani, “Kwa nini uliniasi, na kuninyang'anya raia wa ufalme Wangu?” Mwasisi wa uovu hawezi kutoa udhuru wo wote. Kila mdomo utafumbwa, na majeshi yote walioasi watakaa kimya.PKSw 384.3

    Msalaba wa Kalvari, wakati ukitangaza kuwa sheria haibadiliki, unahubiri ulimwenguni kuwa mshahara wa dhambi ni mauti. Katika kilio cha kukata roho cha Mwokozi, “Imekwisha,” kengele ya kifo cha Shetani ilipigwa. Pambano kuu ambalo limedumu kuwepo kwa muda mrefu liliamriwa hapo, na uondoshwaji wa mwisho wa dhambi ulithibitishwa. Mwana wa Mungu alipita katika milango ya kaburi, ili “kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi” (Waebrania 2:14). Shauku ya Lusifa ya kujiinua ilimfikisha mahali ambapo aliweza kusema: “Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; ... Nitafanana na yeye Aliye juu.” Mungu anatangaza: “Nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, ... wala hutakuwapo tena” (Isaya 14:13, 14; Ezekieli 28:18, 19). Wakati siku ile itapofika, ikiwaka kama tanuru, “wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi” (Malaki 4:1).PKSw 385.1

    Ulimwengu wote utakuwa mashahidi wa asili na athari za dhambi. Na uondoshwaji wake kamili, ambao mwanzoni ungeleta hofu na dharau kwa Mungu, sasa utathibitisha upendo Wake na utaimarisha heshima Yake mbele ya ulimwengu wa wenye uhai wanaofurahia kutenda mapenzi Yake, na ambao mioyoni mwao wanayo sheria Yake. Kamwe uovu hautaonekana tena. Neno la Mungu linasema: “Mateso hayatainuka mara ya pili” (Nahumu 1:9). Sheria ya Mungu, ambayo Shetani aliikashifu kama kongwa la utumwa, itaheshimiwa kama sheria ya uhuru. Uumbaji uliojaribiwa na kuthibitishwa hautayumbishwa tena katika utii wake Kwake Yeye ambaye tabia Yake imedhihirishwa kwa uwazi mbele yao kama upendo usio kifani na hekima isiyo na kikomo. PKSw 385.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents