Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 39—Wakati wa Taabu

    “Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile” (Danieli 12:1).PKSw 467.1

    Ujumbe wa malaika wa tatu utakapofungwa, rehema haitasihi tena kwa ajili ya wakazi wa dunia wenye hatia. Watu wa Mungu watakuwa wamekamilisha kazi yao. Tayari watakuwa wamekwishapokea “mvua ya masika,” “kuburudishwa kwa kuwepo kwa Bwana,” na watakuwa wamekwishajiandaa kwa ajili ya saa ya kujaribiwa iliyoko mbele yao. Malaika wanaharakisha kutoka na kuingia mbinguni. Malaika anayerudi kutoka duniani atatangaza kuwa kazi yake imekamilika; jaribio la mwisho limefanyika duniani, na wote ambao wamethibitika kuwa watiifu kwa amri za Mungu wamepokea “muhuri wa Mungu.” Ndipo Yesu anasitisha maombezi Yake katika patakatifu pa mbinguni. Ananyanyua juu mikono Yake na kwa sauti kubwa anasema, “Imekwisha;” na jeshi lote la malaika wanavua taji zao anapotoa tangazo hili zito: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa” (Ufunuo 22:11). Kila kesi itakuwa imeamriwa kwa ajili ya uzima au mauti. Kristo atakuwa ameshafanya upatanisho kwa ajili ya watu Wake na atakuwa ameshafuta dhambi zao. Idadi ya raia Wake itakuwa imeshajulikana; “ufalme na mamlaka, na ukuu wa ufalme chini ya mbingu yote,” karibu utatolewa kwa warithi wa wokovu, na Yesu karibu atatawazwa kama Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.PKSw 467.2

    Anapotoka katika patakatifu, giza linawafunika wakazi wa dunia. Katika wakati ule wa kutisha wenye haki watapaswa kuishi mbele za Mungu mtakatifu bila mwombezi. Kizuizi kilichokuwa kimewekwa kuwadhibiti waovu kinaondolewa, na Shetani anapata utawala kamili juu ya watu wasiotubu. Uvumilivu wa Mungu umefikia kikomo chake. Ulimwengu umekataa rehema Yake na umedhihaki upendo Wake, na umeikanyaga sheria Yake. Waovu wamevuka mpaka wa rehema yao; Roho wa Mungu, amepingwa kabisa kwa muda mrefu, hatimaye ameondolewa. Bila wigo wa neema ya Mungu, hawana ulinzi dhidi ya yule mwovu. Shetani atawaingiza wakazi wa dunia katika taabu moja, kubwa. Malaika wa Mungu wanapoacha kuzuia pepo kali za tamaa za kibinadamu, nguvu zote za asili za mapambano zitaachiliwa. Ulimwengu mzima utatumbukizwa katika maangamizi ya kutisha zaidi ya yale yaliyoupata mji wa Yerusalemu ya zamani.PKSw 467.3

    Malaika mmoja aliwaangamiza wazaliwa wote wa kwanza wa Wamisri na kuijaza nchi yote kwa kilio. Wakati Daudi alipomkosea Mungu kwa kuhesabu watu, malaika mmoja alisababisha maangamizi ambayo kwa njia ya hayo dhambi ya Daudi iliadhibiwa. Nguvu hiyo ya maangamizi inayotumiwa na malaika watakatifu Mungu anapowaamrisha kufanya hivyo, inatumiwa na malaika waovu Mungu anaporuhusu. Kuna majeshi sasa kila mahali yaliyo tayari, na ambayo yanasubiri tu ruhusa ya Mungu, kusambaza ukiwa kila mahali.PKSw 468.1

    Wale wanaoheshimu sheria ya Mungu wamekuwa wakishitakiwa kwa kuleta hukumu juu ya ulimwengu, na watachukuliwa kuwa chanzo cha matetemeko ya nguvu za asili na migogoro na umwagaji damu miongoni mwa watu vitu ambavyo vinajaza misiba duniani kote. Nguvu iliyomo katika onyo la mwisho itaamsha ghadhabu ya waovu; hasira inawashwa dhidi ya wote waliopokea ujumbe, na Shetani atachochea tena kwa nguvu zaidi roho ya chuki na mateso.PKSw 468.2

    Wakati uwepo wa Mungu ulipoondolewa hatimaye kutoka kwa taifa la Kiyahudi, makuhani na watu wa kawaida hawakujua. Ingawa walikuwa chini ya utawala wa Shetani, na wakiendeshwa na tamaa za kutisha sana na mbaya kuliko kawaida, bado walijihesabu kuwa wao ni wateule wa Mungu. Huduma katika hekalu ziliendelea; kafara ziliendelea kutolewa juu ya madhahabu zake zilizonajisiwa, na kila siku mbaraka wa Mungu ulikuwa ukiombwa kwa ajili ya watu ambao walikuwa na hatia ya kumwaga damu ya Mwana mpendwa wa Mungu na waliokuwa wakitafuta kuwaua waumishi na mitume Wake. Kadhalika wakati uamuzi usioweza kubadilishwa wa patakatifu utakapotangazwa na hatima ya ulimwengu kuamriwa milele, wakazi wa dunia hawatajua kinachoendelea. Ibada za aina mbalimbali za dini zitakuwa zikiendelezwa na watu ambao Roho wa Mungu atakuwa ameondolewa kwao hatimaye; na bidii ya kishetani ambayo mwovu ataivuvia ndani yao ili watekeleze mipango yake mibaya, itafanana na bidii kwa ajili ya Mungu.PKSw 468.3

    Kwa kuwa Sabato itakuwa imekuwa suala maalumu linalobishaniwa katika ulimwengu wote wa Ukristo, na mamlaka za kidini na kiserikali zitakuwa zimeungana pamoja kulazimisha uadhimishaji wa Jumapili, kukataa bila kubadilika kwa kundi la watu wachache kujisalimisha kwa matakwa ya watu wengi kutawafanya kuwa walengwa wa laana ya ulimwengu wote. Itadaiwa kuwa watu wachache wanaopingana na taasisi ya kanisa na sheria ya nchi hawapaswi kuvumiliwa; kuwa ni bora kwao wateswe kuliko mataifa yote kuingizwa katika machafuko na uasi. Hoja hiyo hiyo karne nyingi zilizopita ilitolewa dhidi ya Kristo na “wakubwa wa watu.” “Wala hamfikiri ya kwamba,” alisema Kayafa mwerevu, “yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima” (Yohana 11:50). Hoja hii itaonekana kuwa hitimisho; na amri itatolewa hatimaye dhidi ya wale wote wanaotukuza Sabato ya amri ya nne, ikiwahukumu kuwa wanaostahili adhabu kali sana na ikiwapa watu uhuru, baada ya muda fulani, kuwaua. Urumi katika Ulimwengu wa Kale na Uprotestanti ulioasi katika Ulimwengu Mpya watapitia njia hiyo hiyo dhidi ya wale wanaoheshimu amri zote za Mungu.PKSw 468.4

    Watu wa Mungu watatumbukizwa katika zile mandhari za mateso na maudhi yaliyoelezwa na nabii kama wakati wa taabu ya Yakobo. “Maana Bwana asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani. ... nyuso zote zimegeuka rangi. Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo” (Yeremia 30:5-7).PKSw 469.1

    Usiku wa maumivu ya moyoni ya Yakobo, alipopambana katika maombi kwa ajili ya ukombozi kutoka katika mkono wa Esau (Mwanzo 32:24-30), huwakilisha uzoefu wa watu wa Mungu katika wakati wa taabu. Kwa sababu ya udanganyifu uliotumiwa na Yakobo kupata mbaraka wa baba yake, mbaraka uliokuwa umekusudiwa kwa ajili ya Esau kaka yake, Yakobo alikimbia kuokoa maisha yake, akijihami dhidi ya vitisho vya kifo vya kaka yake. Baada ya kukaa kwa miaka mingi uhamishoni, aliamua kurudi nyumbani, kwa amri ya Mungu, kurudi pamoja na wake zake na watoto wake, kondoo na ng'ombe, katika nchi alikozaliwa. Alipokaribia katika mpaka wa nchi, alijazwa na hofu alipopata habari kuwa Esau alikuwa anakaribia akiongoza kundi la watu wa vita, bila shaka akiwa amejielekeza kulipiza kisasi. Kundi la Yakobo, likiwa halina silaha na bila ulinzi, lilionekana kukaribia kuwa wahanga wa ukatili na kifo bila msaada wowote. Na juu ya mzigo wa wasiwasi na hofu uliongezeka uzito uliomwumiza zaidi wa aibu binafsi, kwa sababu ilikuwa dhambi yake iliyoleta hatari hii. Tumaini lake pekee lilikuwa katika rehema ya Mungu; ulinzi wake pekee lazima uwe maombi. Lakini haachi kufanya kila jambo lililo katika uwezo wake kufanya upatanisho kwa kosa alilomfanyia kaka yake ili kuepusha hatari iliyotishia kutokea. Kadhalika inawapasa wafuasi wa Kristo, wanapokaribia wakati wa taabu, wafanye kila linalowezakana kujiweka katika nuru sahihi mbele ya watu, kupunguza chuki isiyokuwa na sababu, na kuepusha hatari inayotishia uhuru wa dhamiri.PKSw 469.2

    Baada ya kuondoa familia, ili wasione taabu yake, Yakobo anabaki peke yake kumwomba Mungu. Anaungama dhambi yake na anakiri, kwa shukurani kubwa, rehema ya Mungu kwake wakati huo huo, kwa unyenyekevu mkubwa, anajenga hoja ya maombi yake kwa kurejea agano ambalo Mungu alifanya na baba zake na ahadi ambazo Mungu alizitoa kwake yeye mwenyewe katika njozi ya usiku kule Betheli na wakati akiwa katika nchi ya uhamishoni. Kilele cha taabu katika maisha yake kilikuwa kimefika; kila kitu kipo hatarini. Akiwa gizani na akiwa mpweke anaendelea kuomba na kujinyenyekesha mbele ya Mungu. Kwa ghafla mkono unalazwa juu ya bega lake. Anafikiri kuwa adui anatafuta uhai wake, na kwa nguvu zake zote za kukata tamaa anashikana mweleka na mpinzani wake. Kunapoanza kupambazuka, mgeni anaongeza nguvu zake zisizo za kibinadamu; kwa mguso wa huyo mgeni Yakobo aliyekuwa na nguvu nyingi anaonekana kama aliyepigwa na kiharusi, na Yakobo, mwombaji asiye na msaada, anayelia, anaangukia kwenye shingo ya mpinzani wake wa maajabu. Yakobo anagundua sasa kuwa ni Malaika wa agano ambaye alikuwa akipigana naye mieleka. Japokuwa alipata ulemavu na kubaki na maumivu makali, hakuacha kusudi lake. Kwa muda mrefu amehimili mashaka, huzuni, na taabu kwa ajili ya dhambi yake; sasa ni lazima apate uhakika kuwa dhambi yake imesamehewa. Mgeni wa Kimungu anaonekana kama anataka kuondoka; lakini Yakobo anamng'ang'ania, akimwomba ambariki. Malaika anasisitiza, “Niache, niende, maana kunapambazuka;” lakini mzee akapiga kelele, “Sikuachi, usiponibariki” Ni ujasiri, uimara, na uthabiti mkubwa kiasi gani unaooneshwa hapa! Kama lingekuwa dai la kujivuna, lenye kiburi, Yakobo angeuawa mara moja; lakini dai lake lilikuwa la uhakikisho wa mtu anayeungama udhaifu wake na kutokufaa kwake, lakini linalotumaini rehema ya Mungu atunzaye agano.PKSw 469.3

    “Alikuwa na uwezo juu ya malaika akashinda” (Hosea 12:4). Kwa njia ya kujishusha, toba, na kujisalimisha, mtu huyu mwenye dhambi, mkosaji, na anayekufa, alishinda pamoja na Mungu Mkuu wa mbinguni. Ingawa alikuwa akitetemeka alidumu kushikilia ahadi za Mungu, na moyo wenye Upendo usio na Kikomo haukuweza kutupilia mbali ombi la mwenye dhambi. Kama ushahidi wa ushindi wake na neno la kuwatia moyo wengine wajifunze mfano wake, jina lake lilibadilishwa kutoka lile lililokumbushia dhambi yake, hadi lile lililosherehekea ushindi wake. Na ukweli kuwa Yakobo alishinda pamoja na Mungu ulikuwa uhakikisho kuwa angeweza kushinda pamoja na wanadamu. Hakuwa na hofu tena ya kukutana na hasira ya kaka yake, kwa kuwa Bwana alikuwa ulinzi wake.PKSw 470.1

    Shetani alikuwa amemshitaki Yakobo mbele ya malaika wa Mungu, akidai haki ya kumwua kwa sababu ya dhambi yake; alikuwa amemsukuma Esau dhidi yake; na katika usiku mrefu wa mzee kupigana mieleka na Malaika, Shetani alijaribu kumshinikiza Yakobo ajisikie kuwa mwenye hatia ili amkatishe tamaa hatimaye ajiondoe kwa Mungu. Karibu Yakobo afikie hatua ya kukata tamaa; lakini alijua kuwa bila msaada wa Mungu alikuwa amekwisha kabisa. Alikuwa ametubu kwa dhati dhambi yake kubwa, na alimwomba Mungu amrehemu. Asingeweza kugeuzwa aliache kusudi lake, badala yake alimshikilia Malaika na akasisitiza ombi lake kwa kilio cha dhati na uchungu mwingi hadi akapata ushindi.PKSw 470.2

    Kama Shetani alivyomshawishi Esau aende dhidi ya Yakobo, kadhalika Shetani atawachochea waovu wawaangamize watu wa Mungu katika wakati wa taabu. Na kama alivyomshitaki Yakobo, atashinikiza mashitaka yake dhidi ya watu wa Mungu. Anahesabu watu wote ulimwenguni kama raia wake; lakini kundi dogo la watu wanaotunza amri za Mungu wanapinga utawala wake. Ikiwa angeweza kuwafutilia mbali wote watoke duniani, ushindi wake ungekuwa kamili. Anaona kuwa malaika wanawalinda, na anagundua kuwa dhambi zao zimesamehewa; lakini hajui kuwa kesi zao zimekwisha kuamriwa katika patakatifu mbinguni. Anayo taarifa kamili ya dhambi ambazo aliwajaribu wakazitenda, na anaziwasilisha mbele ya Mungu katika mwonekano ulioongezwa chumvi, akiwakilisha watu hawa kuwa wanaostahili kama yeye kuwekwa nje ya ukubali wa Mungu. Anatangaza kuwa Bwana hawezi kwa haki kusamehe dhambi zao na bado amwangamize yeye na malaika zake. Anadai kuwa wao ni mawindo yake na anasisitiza kuwa wawekwe mikononi mwake awaangamize.PKSw 471.1

    Shetani anapowashitaki watu wa Mungu kuhusiana na dhambi zao, Bwana anamruhusu awajaribu kwa nguvu zake zote. Matumaini yao kwa Mungu, imani yao na uimara wao, vitajaribiwa sana. Wanapotafakari maisha yao ya nyuma, matumaini yao yanazama; kwa kuwa katika maisha yao hawaoni jambo lo lote jema walilolitenda. Wanatambua zaidi udhaifu wao na kutokufaa kwao. Shetani anajitahidi kuwatishia akiwa na wazo kuwa kesi zao hazina matumaini, kuwa doa la uchafu wao halitasafishika kamwe. Anatumaini kuwaharibu imani yao kiasi cha kufanya wajisalimishe kwa majaribu yake na waache kumtii Mungu.PKSw 471.2

    Ingawa watu wa Mungu watazungukwa na adui wanaojielekeza kuwaangamiza, taabu waliyonayo siyo hofu ya mateso kwa ajili ya ukweli; wanaogopa kuwa kila dhambi haijatubiwa, na kwamba kwa njia ya kosa lao wao wenyewe watashindwa kutimiziwa ahadi ya Mwokozi: “mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kujaribiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi” Ufunuo 3:10). Ikiwa wangekuwa na hakika ya msamaha wasingekuwa na hofu ya mateso au kifo; lakini ikiwa wataonekana hawastahili, na watapoteza maisha yao kwa sababu ya dosari zao za tabia, maana yake jina takatifu la Mungu lingedharauliwa.PKSw 471.3

    Kila upande wanasikia mipango ikifanywa ya uhaini na wanaona utendaji wa harakati za uasi; na shauku kubwa inaamka ndani yao, tamanio la dhati la moyoni, kwamba uasi huu mkubwa ukomeshwe na uovu wa waovu ufike mwisho. Lakini wakati wakimlilia Mungu asitishe kazi ya uasi, ni katika hali ya utambuzi makini wa kujidhili kuwa wao wenyewe hawana nguvu zaidi ya kupinga na kurudisha nyuma mkondo wenye unguvu wa uovu. Wanahisi kuwa ikiwa wangetumia siku zote uwezo wao wote katika huduma ya Kristo, wakienda mbele kutoka nguvu hadi nguvu, majeshi ya Shetani yangekuwa na nguvu ndogo ya kushindana nao.PKSw 471.4

    Wanatesa roho zao mbele ya Mungu, wakielekeza akili zao kwa toba za zamani za dhambi zao nyingi, na kudai ahadi ya Mwokozi:“Au azishike nguvu zangu, Afanye amani nami; Naam, afanye amani nami” (Isaya 27:5). Imani yao haitindiki kwa sababu maombi yao hayajibiwi upesi. Ingawa wanapata wasiwasi, hofu, na udhia, hawaachi kufanya maombi. Wanang'ang'ania nguvu ya Mungu kama Yakobo alivyomng'ang'ania Malaika; na lugha ya roho zao ni: “Sikuachi, usiponibariki.”PKSw 472.1

    Kama Yakobo angekuwa hajatubu dhambi yake ya kupata haki ya uzaliwa wa kwanza kwa udanganyifu, Mungu asingesikia ombi lake na asingehifadhi maisha yake. Kadhalika, wakati wa taabu, ikiwa watu wa Mungu wangekuwa na dhambi zisizoungamwa zikatokea mbele yao wakati wakiteswa kwa hofu na maumivu, wangezidiwa; kukata tamaa kungekata imani yao, na wasingekuwa na ujasiri wa kuendelea kumwomba Mungu awaokoe. Lakini wakati wakiwa na ufahamu wa kina wa kutokustahili kwao, hawana makosa yaliyofichwa ya kufunua. Dhambi zao zimetangulia hukumuni na zimekwisha kufuta, na hawawezi kuzikumbuka.PKSw 472.2

    Shetani huwaongoza wengi kuamini kuwa Mungu hajali ukosefu wa uaminifu katika mambo madogo ya maisha; lakini Bwana anaonesha katika jinsi alivyoshughulika na Yakobo kuwa kwa vyo vyote vile hawezi kuidhinisha au kuvumilia uovu. Wote wanaojaribu kutolea udhuru au kuficha dhambi zao, na wanaruhusu zibaki katika vitabu vya mbinguni, bila kuungamwa na kusamehewa, watashindwa na Shetani. Kwa kadiri kazi zao zinavyokuwa za juu na vyeo vyao vinavyokuwa vya heshima zaidi, ndivyo mwonekano wao mbele za Mungu unavyokuwa mbaya zaidi na ndivyo ushindi wa adui mkuu unavyokuwa wa hakika zaidi. Wale wanaochelewa kufanya matayarisho kwa ajili ya siku ya Mungu hawatakuwa tayari wakati wa taabu au wakati mwingine wo wote utakaofuata. Kesi za wote kama hao hazina matumaini.PKSw 472.3

    Wakristo wanaokuja katika pambano la mwisho la kutisha bila kujiandaa, katika hali ya kukata tamaa, wataungama dhambi zao kwa maneno yenye maumivu makubwa, wakati waovu wakifurahia dhiki zao. Maungamo haya yana sifa zinazofanana na zile za maovu ya Esau na Yuda. Wanaofanya maungamo ya jinsi hiyo, huhuzunikia matokeo ya makosa yao, siyo hatia yao. Hawahisi toba ya kweli, hakuna chuki dhidi ya dhambi. Wanakiri dhambi yao, kwa sababu ya kuogopa adhabu; lakini, kama alivyokuwa Farao wa zamani, wanarudia kumkufuru Mungu baada ya hukumu kuondolewa.PKSw 472.4

    Historia ya Yakobo pia ni uhakikisho kuwa Mungu hawatupi watu wanaodanganywa na kujaribiwa kutenda dhambi, lakini ambao wanamrudia kwa toba ya kweli. Wakati ambapo Shetani hutafuta kuliangamiza tabaka hili la watu, Mungu hutuma malaika kuwafariji na kuwalinda wakati wa hatari. Mashambulizi ya Shetani ni makali na ya kudhamiria, madanganyifu yake ni ya kutisha; lakini jicho la Bwana liko juu ya watu Wake, na jina Lake husikia vilio vyao. Mateso yao ni makali, ndimi za mioto za tanuru zinaonekana kuwaangamiza; lakini Mtakasaji atawatoa wakiwa safi kama dhahabu iliyojaribiwa katika moto. Upendo wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake wakati wa kipindi cha majaribu yao makali una nguvu na huruma kama ulivyo nyakati za mafanikio makubwa; lakini ni muhimu kwao kuwekwa katika tanuru la moto; kutofaa kwao lazima kuunguzwe, ili sura ya Kristo iakisiwe kikamilifu.PKSw 473.1

    Kipindi cha taabu na maumivu kilichopo mbele yetu kitahitaji imani inayoweza kustahimili uchovu, kuchelewa, na njaa—imani ambayo haitazimia hata kama ikijaribiwa vikali. Wakati wa rehema umetolewa kwa wote kujiandaa kwa ajili ya wakati huo. Yakobo alishinda kwa sababu alivumilia bila kukata tamaa na alidhamiria. Ushindi wake ni ushahidi wa nguvu ya maombi ya kutokukata tamaa. Wote wanaoshikilia ahadi za Mungu, kama alivyofanya, na wakawa wenye moyo wa dhati na wasiokata tamaa kama alivyokuwa, watafanikiwa kama alivyofanikiwa. Wale ambao hawako tayari kujikana nafsi, kuomboleza mbele za Mungu, kuomba kwa muda mrefu na kwa dhati kwa ajili ya mbaraka Wake hawataupata. Kupigana mieleka na Mungu—ni wachache kiasi gani! Ni wachache kiasi gani wameruhusu roho zao zivutwe kumtafuta Mungu kwa shauku kubwa mpaka kila msuli wa nguvu zao umefika kikomo chake. Mawimbi ya kukata tamaa ambayo hakuna lugha inayoweza kueleza juu ya mwombaji, ni wachache kiasi gani hung'ang'ania kwa imani isiyokata tamaa ahadi za Mungu.PKSw 473.2

    Wale ambao wana imani kidogo sasa, wapo katika hatari ya kuangukia chini ya nguvu ya udanganyifu wa kishetani na amri ya kulazimisha dhamiri. Na hata kama wakistahimili jaribu watatumbukizwa katika udhia na huzuni zaidi wakati wa taabu, kwa sababu hawana mazoea ya kumtumaini Mungu. Masomo ya imani ambayo watalazimishwa kujifunza chini ya shinikizo kubwa la kukata tamaa.PKSw 473.3

    Inatupasa kujielimisha wenyewe kuhusu Mungu kwa kuthibitisha ahadi zake. Malaika wanaandika kumbukumbu ya kila ombi la dhati na kung'ang'ania. Inatupasa zaidi kuachana na tamaa za kujipendeza nafsi kuliko kuacha mawasiliano na Mungu. Umaskini wa kutupwa, kujikana nafsi sana, kwa idhini Yake, ni muhimu zaidi kuliko utajiri, heshima, urahisi, na urafiki bila idhini yake. Ikiwa tutaruhusu akili zetu zitawaliwe na mambo ya kidunia, Bwana anaweza kutupatia muda kwa kutunyang'anya miungu yetu ya dhahabu, ya nyuma, au ya ardhi yenye rutuba.PKSw 473.4

    Vijana wasingedanganywa kutenda dhambi ikiwa wangekataa kuingia katika njia yo yote ile isipokuwa ile ambayo wakiipita wangeweza kuomba mbaraka wa Mungu. Ikiwa wajumbe wanaochukua onyo kuu la mwisho ulimwenguni wangeomba kwa ajili ya mbaraka wa Mungu, siyo kwa ubaridi, ulegevu, na uvivu, bali kwa hamasa na imani, kama Yakobo alivyofanya, wangepata mahali pengi ambapo wangeweza kusema: “Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka” (Mwanzo 32:30). Wangehesabiwa na mbingu kuwa wakuu, wakiwa na nguvu ya kushinda pamoja na Mungu na wanadamu.PKSw 474.1

    “Wakati wa taabu, ambao mfano wake haujawahi kuwapo,” umekaribia; na tutahitaji uzoefu ambao hatuna kwa sasa na ambao tunaweza kuwa wavivu kuupata. Mara nyingi taabu ni kubwa katika kuitarajia kuliko uhalisia; lakini haiko hivyo katika uzoefu wa zahama iliyoko mbele yetu. Wasilisho la wazi zaidi kuliko yote haliwezi kuelezea vizuri kiwango cha mateso hayo. Katika wakati huo wa majaribu, kila roho itapaswa kusimama yenyewe peke yake mbele za Mungu. “Wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao” (Ezekieli 14:20).PKSw 474.2

    Sasa, wakati Kuhani wetu Mkuu anafanya upatanisho kwa ajili yetu, inatupasa kutafuta kuwa wakamilifu katika Kristo. Siyo hata kwa wazo angeweza Mwokozi wetu kushindwa na jaribu. Shetani hupata katika mioyo ya wanadamu jambo analoweza kushikilia; shauku ya dhambi inayolelewa, ambayo kwa njia yake majaribu yake huelekeza nguvu zake. Lakini Kristo Mwenyewe alisema: “Yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu” (Yohana 14:30). Shetani hakuweza kupata chochote ndani ya Mwana wa Mungu ambacho kingemwezesha kupata ushindi. Alitunza amri za Baba Yake, na hakukuwa na dhambi ndani Yake ambayo Shetani angeweza kuitumia kwa maslahi yake. Hii ndiyo hali ambayo wanapaswa kuwa nayo wale watakaosimama wakati wa taabu.PKSw 474.3

    Ni katika maisha haya ambapo inatupasa kujitenga na dhambi, kwa njia ya imani katika damu ya upatanisho ya Kristo. Mwokozi wetu wa thamani anatualika tushikamane Naye, tuunganishe udhaifu wetu na nguvu Yake, ujinga wetu na hekima Yake, kutostahili na kustahili Kwake. Uongozi wa Mungu ni shule ambayo inatuwezesha kujifunza unyenyekevu na upole wa Yesu. Bwana anaweka daima mbele yetu, siyo kama tunavyochagua, kinachoonekana kuwa rahisi kwetu na kinachotupendeza zaidi, lakini kilicho na makusudi ya kweli katika maisha. Inabaki wajibu wetu kushirikiana na mawakala ambao Mbingu huwatumia katika kazi ya kujenga tabia zetu kulingana na mfano wa Mungu. Hakuna anayeweza kupuuzia au kuahirisha kazi hii bila kuhatarisha roho yake.PKSw 474.4

    Mtume Yohana katika njozi alisikia sauti kuu mbinguni ikitangaza: “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (Ufunuo 12:12). Mandhari zinazosababisha kutolewa kwa sauti hii ya mbinguni ni za kutisha. Hasira ya Shetani inaongezeka kwa kadiri wakati wake unavyozidi kuwa mfupi, na kazi ya uongo na uuaji itafikia kilele chake wakati wa taabu.PKSw 475.1

    Matukio yanayopita akili za kibinadamu siyo muda mrefu yataanza kuonekana mbinguni, kama ishara ya nguvu ya utendaji kazi wa kimiujiza wa mashetani. Roho za mashetani zitawaendea wafalme wa dunia na ulimwengu wote, kuwafungia katika uongo, na kuwasihi wajiunge na Shetani katika pambano lake la mwisho dhidi ya serikali ya mbinguni. Kwa njia ya mawakala hawa, watawala na watawaliwa kwa pamoja watadanganywa. Watu watainuka wakijifanya kuwa Kristo Mwenyewe, na wakidai kuwa na cheo na hadhi ya kuabudiwa ambavyo vinamstahili Mkombozi wa ulimwengu. Watatenda miujiza ya ajabu ya uponyaji na watadai kuwa na mafunuo kutoka mbinguni yanayopingana na ushuhuda wa Maandiko.PKSw 475.2

    Kama tendo la juu kabisa katika sakata kuu la uongo, Shetani mwenyewe atajifanya kuwa Kristo. Kwa muda mrefu kanisa limetangaza kuwa ujio wa pili wa Kristo ndiyo kilele cha matumaini yake. Sasa mdanganyaji mkuu atafanya ionekane kana kwamba Kristo amekuja. Katika sehemu mbalimbali za dunia, Shetani atajidhihirisha miongoni mwa wanadamu kama mfalme mkuu mwenye nuru kuu, akifanana na mwonekano wa Mwana wa Mungu aliyeelezewa na Yohana katika kitabu cha Ufunuo (Ufunuo 1:13-15). Utukufu unaomzunguka haupitwi na kitu chochote ambacho macho ya mwanadamu anayekufa yamewahi kukiona. Kelele za ushindi zinasikika hewani: “Kristo amekuja! Kristo amekuja!” Watu wanaanguka kifudifudi chini kwa heshima mbele yake, wakati ameinua mikono yake juu na anatamka baraka juu yao, kama vile Kristo alivyowabariki wanafunzi Wake alipokuwa duniani. Sauti yake ni laini na tulivu, lakini ikiwa tamu. Kwa sauti ya upole na huruma anasema baadhi ya mambo ya neema ile ile, kweli za mbinguni ambazo Kristo alizisema; anaponya magonjwa ya watu, na ndipo, katika kujifanya kwake Kristo, anadai aliibadili Sabato na kuifanya Jumapili, na anawaamrisha watu wote kuiadhimisha siku ambayo ameibariki. Anatangaza kuwa wale watakaoendelea kutunza siku ya saba wanakufuru jina lake kwa kukataa kuwasikiliza malaika zake aliowatuma kwao wakiwa na nuru na ukweli. Huu ni uongo wenye nguvu, unaowanasa karibu watu wote. Kama vile Wasamaria walivyodanganywa na Simoni Magusi, umati wa watu, kutoka mdogo hadi mkubwa kabisa, wanasikiliza uchawi huu, wakisema: Huu ni “uweza wa Mungu, ule Mkuu” (Matendo 8:10).PKSw 475.3

    Lakini watu wa Mungu hawatapotoshwa. Mafundisho ya Kristo bandia yanapingana na Maandiko. Mbaraka unatamkwa juu ya watu wanaomwabudu mnyama na sanamu yake, tabaka lile lile ambalo Biblia inasema kuwa ghadhabu ya Mungu isiyochanganywa itamwagwa juu yao.PKSw 476.1

    Na, zaidi ya hapo, Shetani hapewi ruhusa ya kuigiza jinsi Kristo atakavyokuja mara ya pili. Mwokozi aliwaonya watu Wake dhidi ya uongo kuhusiana na kipengele hiki, na alieleza kwa uwazi jinsi ujio Wake wa pili utakavyokuwa. “Watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.... Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:24-27, 31; 25:31; Ufunuo 1:7; 1 Wathesalonike 4:16, 17). Ujio huu hakuna uwezekano wa kuuigiza. Utajulikana mahali pote—utashuhudiwa na ulimwengu wote.PKSw 476.2

    Ni wale tu ambao watakuwa wanafunzi wa Maandiko wenye bidii na ambao wanaupenda ukweli watakingwa dhidi ya madanganyifu yenye nguvu ambayo yatauteka ulimwengu. Kwa njia ya ushuhuda wa Biblia hawa watamgundua mdanganyaji katika joho lake bandia. Wakati wa kujaribiwa utakuja kwa watu wote. Kwa njia ya chekeche la jaribu Mkristo wa kweli atafunuliwa. Je, watu wa Mungu sasa wameimarishwa juu ya neno Lake kiasi kwamba hawataangushwa na ushahidi wa hisia zao? Je, katika zahama hiyo, wataweza kung'ang'ania Biblia na Biblia pekee? Shetani, ikiwezekana, atawazuia wasifanye maandalizi ya kuwawezesha kusimama katika siku ile. Anapanga mambo kwa namna ambayo anazuia njia yao, anawanasa kwa hazina za dunia, kuwafanya wabebe mzigo mzito, unaochosha, kwamba kazi yao iweze kuzidiwa na shughuli za maisha haya na siku ya kujaribiwa iwajie kama mwizi.PKSw 476.3

    Wakati amri itakayotolewa na watawala mbalimbali wa ulimwengu wa Kikristo dhidi ya watunzao amri kumi watakapoondoa ulinzi wa serikali na kuwaachia mikononi mwa wale wanaotamani kuwaua, watu wa Mungu watakimbia kutoka mijini na vijijini na watajiunga pamoja katika vikundi, wakiishi katika maeneo ya mbali na yaliyojificha. Wengi watajificha katika miamba na milima. Kama Wakristo wa mabonde ya Piedmonti, watatumia vilele vya milima kuwa maficho na watamshukuru Mungu kwa ajili ya“ngome ya majabali” (Isaya 33:16). Lakini mengi ya mataifa yote na ya matabaka ya wote, ya juu na ya chini, tajiri na maskini, weusi na weupe, watatupwa katika utumwa wa kidhalimu na katili kuliko utumwa wa mwingine wo wote ule. Wapendwa wa Mungu wanapitia katika siku za uchovu, wakiwa wamefungwa kwa minyororo, wakiwa wamefungwa magerezani, baadhi wakiwa wameachwa wafe kwa njaa gizani na magereza machafu.PKSw 476.4

    Hakuna sikio la kibinadamu liko wazi kusikia vilio vyao; hakuna mkono wa kibinadamu ulioko tayari kutoa msaada.PKSw 477.1

    Je, Bwana atawasahau watu wake katika saa hii ya majaribu? Je, Mungu alimsahau Nuhu mwaminifu wakati hukumu zilipomwagwa juu ya ulimwengu wakati wa Gharika? Je, Mungu alimsahau Lutu wakati moto uliposhuka kutoka mbinguni kuiteketeza miji ya uwandani? Je, Mungu alimsahau Yusufu alipokuwa amezungukwa na waabudu sanamu wa Misri? Je, Mungu alimsahau Eliya wakati kiapo cha Yezebeli kilipomtisha baada ya kuwaua manabii wa Baali? Je, alimsahau Yeremia katika shimo lenye giza na kina kirefu la nyumba ya gereza lake? Je, Mungu aliwasahau vijana watatu wa Kiebrania katika tanuru liwakalo moto? Je, Mungu alimsahau Danieli katika tundu la sima?PKSw 477.2

    “Sayuni alisema,YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu” (Isaya 49:14-16). Bwana wa majeshi anasema: “Yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake” (Zekaria 2:8).PKSw 477.3

    Ingawa adui waweza kuwatupa gerezani, bado kuta za gereza haziwezi kukata mawasiliano kati ya roho zao na Kristo. Yeye aonaye kila udhaifu wao, Yeye ajuaye kila jaribu lao, yuko juu ya mamlaka zote za kidunia; na malaika watawatembelea katika vyumba vyao vya upweke, kuwaletea nuru na amani kutoka mbinguni. Gereza litakuwa kama ikulu; kwa kuwa wenye imani kubwa wanaishi pale, na kuta zenye huzuni zitaangaziwa kwa nuru ya mbinguni kama wakati ule Paulo na Sila walipoimba nyimbo za sifa katika usiku wa manane katika gereza la Filipi.PKSw 477.4

    Hukumu za Mungu zitamwagwa juu ya watu wanaotafuta kuwatesa na kuwaua watu wa Mungu. Huruma Yake kwa waovu inawapa watu ujasiri katika uovu, lakini adhabu yao, ni ya hakika na ya kutisha kwa sababu imecheleweshwa kwa muda mrefu. “Bwana ataondoka kama vile katika mlima Perasimu, ataghadhibika kama vile katika bonde la Gibeoni; apate kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu; na kulitimiza tendo lake, tendo lake la ajabu” (Isaya 28:21). Kwa Mungu wetu mwenye rehema tendo la kuadhibu ni tendo la ajabu. “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu” (Ezekieli 33:11). Bwana ni “mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli,... mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi.” Hata hivyo siyo “mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe.” “Bwana si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe” (Kutoka 34:6, 7; Nahumu 1:3). Kwa njia ya mambo ya kutisha ya haki atathibitisha mamlaka ya sheria Yake iliyokanyagwa. Ukali wa adhabu inayomsubiri mkosaji inaweza kupimwa kwa subira ya Mungu katika kutekeleza hukumu. Taifa ambalo Mungu analivumilia sana, taifa ambalo hatalipiga mpaka lijaze kipimo cha uovu wake katika akaunti ya Mungu, hatimaye litakunywa kutoka katika kikombe cha hasira isiyochanganywa na rehema.PKSw 477.5

    Wakati Kristo anapomaliza maombezi Yake katika patakatifu, hasira isiyochanganywa na kitu inayotishia wale wanaomwabudu mnyama na sanamu yake na kuipokea chapa yake (Ufunuo 14:9, 10), itamwagwa. Mapigo juu ya Misri wakati Mungu alipokuwa karibu kuwaokoa Waisraeli yalifanana katika sifa na zile hukumu za kutisha na kubwa zaidi zitakazoanguka juu ya ulimwengu mara tu kabla ya ukombozi wa mwisho wa watu wa Mungu. Anasema nabii wa Ufunuo, akielezea mapigo yale ya kutisha: “Pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.” Bahari “ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.” Na “mito na chemchemi za maji ... zikawa damu.” Mapigo haya, ya kutisha kama yalivyo, yanathibitisha haki ya Mungu kikamilifu. Malaika wa Mungu anatangaza: “Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili” (Ufunuo 16:2-6). Kwa kuwahukumu watu wa Mungu wafe, wamejipatia hatia ya damu kana kwamba ilimwagwa na mikono yao. Kwa jinsi iyo hiyo Kristo aliwatangaza Wayahudi wa wakati Wake kuwa wenye hatia ya damu ya watakatifu iliyomwagwa tangu siku za Habili; kwani walikuwa na roho ile ile na walikuwa wakitafuta kufanya kazi ile ile ya wauaji wa manabii.PKSw 478.1

    Katika pigo linalofuata, nguvu inatolewa kwa jua “kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa” (Aya ya 8, 9). Manabii wanaeleza hali ya dunia wakati huu wa kutisha kama ifuatavyo: “Nchi inaomboleza; ... Maana mavuno ya mashamba yamepotea.... Miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu.” “Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa.... Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng'ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho.... Vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.” “Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya” (Yoeli 1:10-12, 17-20; Amosi 8:3).PKSw 478.2

    Mapigo haya hayatokei duniani kote, vinginevyo wakazi wote wa dunia wangefyekwa. Hata hivyo, yatakuwa mapigo ya kutisha zaidi kuliko mapigo yo yote yanayojulikana kwa wanadamu. Hukumu zote juu ya wanadamu, kabla ya kufungwa kwa mlango wa rehema, yamekuwa yakichanganywa na rehema. Damu ya Kristo inayosihi imekuwa ikimkinga mwenye dhambi asipokee kipimo kamili cha hatia yake; lakini katika hukumu ya mwisho, hasira inamwagwa pasipo kuchanganywa na rehema.PKSw 479.1

    Katika siku hiyo, watu watatamani hifadhi ya rehema ya Mungu ambayo wamekuwa wakiidhihaki kwa muda mrefu. “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana. Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione” (Amosi 8:11, 12).PKSw 479.2

    Watu wa Mungu hawataepuka kabisa mateso; lakini hata katika mateso na fadhaa, pamoja na umaskini na ukosefu wa chakula, hawataachwa waangamie. Kwamba Mungu aliyemtunza Eliya hatamwacha hata mmojawapo wa watoto Wake waliojitoa kafara kwa ajili Yake. Yeye ajuaye idadi ya nywele za vichwa vyao atawatunza, na wakati wa njaa watashibishwa. Wakati waovu wakifa kwa njaa na magonjwa, malaika watawalinda wenye haki na kuwapa mahitaji yao. Kwake “yeye aendaye kwa haki” kuna ahadi: “Atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.” “Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha” (Isaya 33:15, 16; 41:17).PKSw 479.3

    “Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;” lakini wanaomcha Bwana “watamfurahia Bwana” na kumshangilia Mungu wa wokovu wao (Habakuki 3:17, 18).PKSw 479.4

    “Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.” “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako” (Zaburi 121:5-7; 91:3-10).PKSw 479.5

    Walakini kwa macho ya kibinadamu itaonekana kana kwamba watu wa Mungu muda si mrefu watalazimika kuweka muhuri ushuhuda wao kwa damu yao kama walivyofanya wafia dini kabla yao. Wao wenyewe wanaanza kuogopa kuwa Bwana amewaacha wafie katika mikono ya maadui zao. Ni kipindi cha uchungu wa kutisha. Mchana na usiku wanamlilia Mungu awakomboe. Waovu wanafurahia, na vicheko vyao vya kejeli vinasikika: “Imani yenu sasa iko wapi? Kwa nini Mungu asiwaokoe kutoka katika mikono yetu ikiwa kweli ninyi ni watu Wake?” Lakini wenye subira wanamkumbuka Yesu akifa juu ya msalaba wa Kalwari na makuhani wakuu na watawala wakipiga kelele kwa dhihaka: “Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini” (Mathayo 27:41, 42). Kama Yakobo, wote wanapigana mieleka na Mungu. Nyuso zao zinaeleza pambano lililoko ndani yao. Kusinyaa kunaonekana katika kila uso. Lakini hawaachi maombi yao.PKSw 480.1

    Ikiwa watu wangeona kwa macho ya kimbingu, wangeona makundi ya malaika wenye nguvu nyingi na za ajabu wakiwa wamewazunguka wale ambao wamelitunza neno la subira ya Kristo. Kwa huruma na upole, malaika wameshuhudia fadhaa zao na wamesikia maombi yao. Wanasubiri neno la Kamanda wao wawachomoe na kuwatoa katika hatari inayowakabili. Lakini inawapasa wasubiri kidogo zaidi. Inawapasa watu wa Mungu kukinywea kikombe na kubatizwa kwa ubatizo. Kuchelewa, pamoja na maumivu yake, ndiyo jibu zuri zaidi kuliko yote kwa maombi yao. Wanapojitahidi kusubiri, huku wakimtumainia Bwana atende kazi wanajikuta wakitumia imani, tumaini, na uvumilivu, ambao ulitumiwa kidogo sana wakati wa uzoefu wao wa kidini. Lakini kwa ajili ya wateule muda wa taabu utafupishwa. “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? .... Nawaambia, atawapatia haki upesi” (Luka 18:7, 8). Mwisho utafika kwa haraka zaidi kuliko watu wanavyotegemea. Ngano itakusanywa na kufungwa matita matita kwa ajili ya kuwekwa katika ghala la Mungu; magugu yatafungwa pamoja kama miganda kwa ajili ya kuteketezwa.PKSw 480.2

    Walinzi wa mbinguni, wakiwa waaminifu kwa dhamana yao, wanaendelea na ulinzi wao. Japokuwa amri ya jumla imeweka tarehe maalumu ya kuwaua watunza amri za Mungu, maadui zao katika baadhi ya mazingira watatarajia amri hiyo, na kabla ya wakati ulioamriwa, watajaribu kuwaua watunza amri za Mungu. Lakini hakuna hata mmoja atakayeweza kupenya jeshi la malaika wenye nguvu kubwa waliomzunguka kila mtu wa Mungu mwaminifu. Baadhi wanashambuliwa katika kukimbia kwao wakitoka katika miji na vijiji; lakini panga zilizoinuliwa dhidi yao zinavunjika na zinakosa nguvu na kuwa kama mabua. Wengine wanalindwa na malaika katika mfano wa watu wa vita.PKSw 480.3

    Katika zama zote, Mungu ametenda kazi kwa njia ya malaika kuwasaidia na kuwaokoa watu Wake. Wenye uhai wa mbinguni wameshiriki katika masuala ya wanadamu. Wametokea katika mavazi yao yanayong'aa kama umeme wa radi; wamekuja kama watu waliovaa mavazi ya watu maskini. Malaika wametokea katika umbo la watu wa Mungu. Wamepumzika, kama watu waliochoka, mwaloni. Wamepokea ukarimu wa nyumba za wanadamu. Wamefanya kazi ya waongozaji kwa wasafiri waliochelewa kufika nyumbani. Kwa mikono yao, wamewasha mioto kwenye madhabahu. Wamefungua milango ya magereza na kuwaachilia watumishi wa Bwana. Wakiwa wamevikwa mavazi ya mbinguni, walikuja kuliondoa jiwe kwenye mlango wa kaburi la Yesu.PKSw 481.1

    Katika umbo la wanadamu, malaika daima wako katika mikutano ya wenye haki; na wanatembelea mikutano ya waovu, kama walivyokwenda Sodoma, kuandika kumbukumbu za matendo yao, kuamua ikiwa wamevuka mpaka wa uvumilivu wa Mungu. Bwana hupenda rehema; na kwa sababu ya watu wachache wanaomtumikia kwa moyo wa dhati, anazuia majanga na anaendeleza utangamano miongoni mwa makundi ya watu. Kidogo sana wenye dhambi dhidi ya Mungu hutambua kuwa wanawiwa kwa ajili ya maisha yao na waaminifu wachache ambao wanapenda kuwadhihaki na kuwatesa.PKSw 481.2

    Ingawa watawala wa ulimwengu huu hawalitambui hili, lakini katika mabaraza yao malaika wamekuwa wasemaji. Macho ya wanadamu yamewaangalia; masikio ya wanadamu yamesikiliza hoja zao; midomo ya wanadamu imepinga mapendekezo yao na kudhihaki mashauri yao; mikono ya wanadamu imekutana nao kwa matusi na dharau. Katika ukumbi wa baraza na mahakama hawa wajumbe wa mbinguni wameonesha uelewa wa kina wa historia ya wanadamu; wamekuwa watetezi wazuri wa watu wanaokandimizwa kuliko watetezi wao wenye uwezo mkubwa na wenye ufasaha mkubwa. Wameshinda makusudi na kusitisha uovu ambao ungerudisha sana nyuma kazi ya Mungu na kusababisha mateso ya watu wa Mungu. Katika saa ya hatari na udhia “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa” (Zaburi 34:7).PKSw 481.3

    Kwa shauku ya dhati, watu wa Mungu wanasubiri kuona ishara za Mfalme wao ajaye. Kama walinzi walivyolikabili, “Habari gani za usiku?” jibu linatolewa bila kusita sita, “‘Mchana unakuja na usiku pia’ (Isaya 21:11, 12). Nuru inaangaza juu ya mawingu yaliyoko juu ya vilele vya milima. Siyo muda mrefu kutakuwepo na udhihirishaji wa utukufu Wake. Jua la haki litaangaza. Asubuhi na usiku vimekaribia—kufunguliwa kwa siku isiyo na mwisho kwa wenye haki, kuingia kwa usiku wa milele kwa waovu.”PKSw 481.4

    Wakati wapiga mieleka wanapeleka maombi yao ya dhati kwa Mungu, pazia linalowatenga na wenye uhai wasioonekana linaondolewa kwa sehemu kubwa. Mbingu zinang'aa kwa pambazuko la siku ya umilele, na kama sauti nzuri ya nyimbo za malaika maneno yanasikika: “Simama imara katika utii wako. Msaada unakuja.” Kristo, Mshindi Mwenyezi, anawavalisha askari Wake waliochoka taji ya utukufu usioharibika; na sauti inatoka nje ya malango yaliyofunguliwa wazi: “Tazama, niko pamoja nawe. Usiogope. Ninazijua huzuni zako; nimeyachukua masikitiko yako. Vita yako siyo dhidi ya maadui ambao hawajajaribiwa. Nimepigana vita kwa ajili yenu, na katika jina Langu ninyi ni zaidi ya washindi.”PKSw 482.1

    Mwokozi wa thamani atatuma msaada wakati tunaouhitaji. Njia ya kwenda mbinguni imewekwa wakfu kwa njia ya alama ya nyayo. Kila mwiba unaoumiza nyayo zetu ulijeruhi nyayo Zake. Kila msalaba ambao tunaitwa kuubeba ameubeba kabla yetu. Bwana huruhusu mashindano, kuindaa roho kwa ajili ya amani. Wakati wa taabu ni wa mateso makubwa kwa watu wa Mungu; lakini ni wakati wa kila muumini wa kweli kutazama juu, na kwa imani waweze kuuona upinde wa ahadi ukiwazunguka pande zote.PKSw 482.2

    “Nao waliokombolewa na Bwana watarejea, Watafika Sayuni, wakiimba; Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; Watapata shangwe na furaha; Huzuni na kuugua zitakimbia. Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani? Ukamsahau Bwana, Muumba wako, ... nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye? Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka. Maana mimi ni Bwana, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma. Bwana wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu” (Isaya 51:11-16).PKSw 482.3

    “Basi, kwa sababu ya hayo, ulisikilize neno hili, ewe uliyeteswa, na kulewa, lakini si kwa mvinyo; Bwana, Bwana wako na Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi, Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe cha kulevya-levya, hilo bakuli la kikombe cha hasira yangu; hutakinywea tena; nami nitakitia mikononi mwao wakutesao; waliokuambia nafsi yako, Inama, tupate kupita; nawe uliufanya mgongo wako kuwa kama nchi, na kama njia, kwa hao wapitao juu yake” (Aya 21-23).PKSw 482.4

    Jicho la Mungu, likitazama katika zama zote, liliona zahama ambayo itawakabili watu Wake, wakati mamlaka za kidunia zitakapojipanga dhidi yao. Kama mateka wanavyokuwa uhamishoni, wataogopa kifo kwa kukosa chakula au kwa kufanyiwa ukatili. Lakini Yule Aliye Mtakatifu aliyegawanya Bahari ya Shamu, ataonesha nguvu Yake na kubadili umateka wao. “Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye” (Malaki 3:17). Ikiwa damu ya mashahidi waaminifu ingemwagwa wakati huu, isingekuwa, kama ilivyokuwa damu ya wafia dini, kama mbegu iliyopandwa kutoa mavuno kwa ajili ya Mungu. Uaminifu wao usingekuwa ushuhuda wa kuwashawishi wengine waukubali ukweli; kwa kuwa moyo mgumu umerudisha nyuma mawimbi ya rehema mpaka hayawezi kuja tena. Ikiwa wenye haki wangeachwa wawe mawindo ya maadui zao, ingekuwa ushindi kwa upande wa mfalme wa giza. Mwandishi wa zaburi anasema: “Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba” (Zaburi 27:5). Kristo alisema: “Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita. Kwa maana, tazama, Bwana anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao” (Isaya 26:20, 21). Ukombozi wa wale ambao wamesubiri kwa uvumilivu kwa ajili ya ujio Wake na wale ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima utakuwa wa utukufu. PKSw 483.1

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents