Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 34—Je, Wafu Wetu Wanaweza Kuongea Nasi?

    Huduma ya malaika watakatifu, kama ilivyoelezwa katika Maandiko, ni ukweli unaofariji na wa thamani sana kwa kila mfuasi wa Kristo. Lakini fundisho la Biblia juu ya mada hii limefunikwa na kupotoshwa na makosa ya theolojia inayokubaliwa na watu wengi. Fundisho la hali ya asili ya kutokufa, lililoazimwa kwanza kutoka katika falsafa ya kipagani, na katika giza nene la uasi likaingizwa katika imani ya Kikristo, limechukua nafasi ya ukweli, ambao umefundishwa wazi katika Maandiko, kuwa “wafu hawajui neno lo lote.” Watu wengi wamefikia kuamini kuwa ni roho za watu waliokufa ambazo ni “roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu.” Imefikia kueleweka hivyo licha ya ushuhuda wa Maandiko kuhusiana na uwepo wa malaika wa mbinguni, na mshikamano wao na historia ya mwanadamu, kabla ya kifo cha mwanadamu.PKSw 421.1

    Fundisho la ufahamu wa mwanadamu katika hali ya kifo, hususani imani kuwa roho za watu waliokufa hurudi kuwatumikia watu walio hai, limeandaa njia kwa ajili ya imani ya kisasa ya kuwasiliana na mizimu. Ikiwa watu waliokufa wamekwenda kwa Mungu na kwa malaika watakatifu, na wakiwa na fursa ya maarifa makubwa zaidi waliyokuwa nayo kabla, kwa nini wasirudi duniani kuwaangazia na kuwafundisha walio hai? Ikiwa, kama inavyofundishwa na wanatheolojia walio wengi, roho za waliokufa zinaruka ruka juu ya rafiki zao walio duniani, kwa nini wasiruhusiwe kuwasiliana nao, kuwaonya dhidi ya uovu, au kuwafariji wakati wa huzuni? Inawezekanaje watu wanaoamini katika ufahamu wa mwanadamu aliyekufa wakatae kile kinachowajia kama nuru ya Kiungu iliyowasilishwa na roho zenye utukufu? Hapa kuna mfereji unaochukuliwa kama mfereji mtakatifu, ambao Shetani anautumia kutimiza makusudi yake. Malaika walioanguka wanaotekeleza maagizo yake hutokea kama wajumbe kutoka ulimwengu wa roho. Wakati wakidai kuleta walio hai katika mawasiliano na waliokufa, mfalme wa uovu anatumia nguvu zake za kichawi kuteka akili zao.PKSw 421.2

    Ana uwezo wa kuleta mbele ya watu mfano wa marafiki zao waliokufa. Igizo linakuwa kamili; mwonekano uliozoeleka, maeneo, sauti, vinatokea kwa usahihi wa kushangaza. Wengi wanafarijika kuwa wapendwa wao wanafurahia uzuri wa mbinguni, na bila tahadhari ya hatari, wanasikiliza “roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.”PKSw 421.3

    Wanapoongozwa kuamini kuwa waliokufa wanarudi kweli kuongea nao, Shetani anawezesha kutokea kwa wale waliozikwa makaburini bila kujiandaa kiroho. Wakitokea, wanadai kuwa wana furaha mbinguni na hata wanashika nyadhifa za juu huko, na kwa njia hiyo uongo unazidi kuenezwa ukifundishwa kuwa hakuna tofauti iliyopo kati ya wenye haki na waovu. Wageni hao wa kuigiza kutoka ulimwengu wa pepo, wakati mwingine hutoa tahadhari na maonyo ambayo huweza kuwa sahihi kabisa. Ndipo, wakati kuaminiwa kunapojengeka, wageni hao huwasilisha mafundisho huwafanya watu wapoteze imani katika Maandiko. Kwa mwonekano wa kuwa na nia ya kuwaletea mambo mema marafiki zao wa duniani, wanawafanya wauamini uongo wa hali ya juu sana. Ukweli kuwa wanasema baadhi ya mambo yaliyo ya kweli, wakati mwingine wanaweza kutabiri matukio ya wakati ujao, hufanya kauli zao ziwe na mwonekano wa kuaminiwa; na mafundisho yao ya uongo yanakubaliwa na watu wengi kwa urahisi, na huaminiwa bila maswali, kana kwamba ni ukweli mtakatifu sana wa Biblia. Sheria ya Mungu inawekwa pembeni, Roho wa neema anadhihakiwa, damu ya agano huhesabiwa kuwa kitu kisicho kitakatifu. Pepo wanakataa uungu wa Kristo na wanamweka Muumbaji katika daraja lao. Hivyo, katika joho jipya mwasi mkuu anaendesha vita yake dhidi ya Mungu, iliyoanzia mbinguni na kwa miaka elfu sita ameendelea kuifanya duniani.PKSw 421.4

    Wengi hujaribu hueleza kuwa vitendo hivi vya maonesho ya pepo ni maigizo na viini macho tu vinavyofanywa na wahusika. Lakini, ingawa ni kweli kuwa viini macho vinaweza kuwazuga watu wakafikiri ni matukio ya kweli, huwa kunakuwepo, pia, matukio halisi yanayotokana na nguvu kubwa zaidi kuliko za mwanadamu wa kawaida. Milio ya kugonga-gonga inayosikika bila kujua inatokea wapi ambayo imani ya kuwasiliana na mizimu ilianza nayo haikuwa matokeo ya ujanja au viini macho, bali ilikuwa kazi ya moja kwa moja ya malaika waovu, ambao walianzisha moja ya mambo ya uongo unaoharibu roho kwa ufanisi mkubwa sana. Wengi watanaswa kwa kuamini kuwa imani ya kuongea na mizimu ni udanganyifu wa kibinadamu pekee; wanapokutana uso kwa uso na matukio ambayo hawawezi kuyachukulia vinginevyo zaidi ya kuamini kuwa ni zaidi ya nguvu za kibinadamu, watadanganywa, na watajikuta wakiongozwa kuyapokea kama nguvu kuu ya Mungu.PKSw 422.1

    Watu hawa wanapuuza ushahidi wa Maandiko kuhusu maajabu yanayofanywa na Shetani na mawakala wake. Ilikuwa kwa msaada wa kishetani ambapo wachawi wa Farao waliwezeshwa kuigiza kazi ya Mungu. Paulo anathibitisha kuwa kabla ya kuja kwa Kristo mara ya pili, kutakuwepo matukio ya nguvu za kishetani zinazofanana na hizo. Kuja kwa Kristo mara ya pili kutatanguliwa na “kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu” (2 Wathesalonike 2:9, 10). Na mtume Yohana, akieleza utendaji kazi wa miujiza katika siku za mwisho, anasema: “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya ” (Ufunuo 13:13, 14). Hapa siyo wadanganyaji wanaotabiriwa kuwa watafanya ishara. Watu watadanganywa kwa miujiza itakayofanywa na mawakala wa Shetani wenye nguvu ya kuifanya, siyo wanaoigiza kuifanya.PKSw 422.2

    Mfalme wa giza, ambaye kwa muda mrefu anaelekeza nguvu za akili yake kufanya mambo ya uongo, kwa ufundi mkubwa akipanga majaribu yake kulingana na tabaka na hali mbali mbali za watu. Kwa wasomi na watu wenye uelewa mpana anawasilisha imani ya kuongea na mizimu katika namna ambayo imeboreshwa na kuwa ya kisasa, na hivyo anafanikiwa sana kuwavuta watu katika mtego wake. Hekima ambayo hutolewa na imani ya kuongea na mizimu ni ile ambayo imeelezwa na Yakobo, ambayo “siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani” (Yakobo 3:15). Hii, hata hivyo, mdanganyaji mkuu anaficha pale ufichaji unapomsaidia kufanikisha malengo yake. Yeye aliyeweza kutokea akiwa na nuru ya maserafi wa mbinguni mbele ya Kristo katika jangwa la majaribu, anakuja kwa watu katika namna inayovutia sana kama malaika wa nuru. Anashawishi akili kwa kuwasilisha mwonekano mzuri; anapenda ubunifu wa mandhari zinazosisimua; na anavutia watu wampende kwa njia ya maonesho fasaha ya upendo na ukarimu. Anaamsha fikra juu ya mambo ya makubwa, akiwaongoza kuwa na kiburi katika hekima yao ambapo katika mioyo yao wanamdhihaki Yeye aliye wa Milele. Yule kiumbe mwenye nguvu ambaye aliweza kumchukua Mwokozi wa ulimwengu hadi katika kilele cha mlima mrefu sana na kuleta mbele Yake falme zote za dunia na utukufu wa falme hizo, ataleta majaribu yake kwa watu katika namna ambayo ataharibu hisia za wote ambao hawana ulinzi wa nguvu ya Mungu.PKSw 423.1

    Shetani anawadanganya watu kama alivyomdanganya Hawa kwa ghiliba, kwa kuamsha shauku ya kupata ujuzi uliokatazwa, kwa kuamsha tamaa ya kujiinua. Ilikuwa kupalilia maovu haya kulikosababisha anguko lake, na kwa njia ya maovu hayo analenga kuangamiza watu. “Nanyi mtakuwa kama Mungu,” alisema, “mkijua mema na mabaya” (Mwanzo 3:5). Imani ya kuongea na mizimu inafundisha “kuwa mwanadamu ni kiumbe wa maendeleo; kwamba ni lengo lake tangu anapozaliwa kuendelea, hata hatimaye afikie, hadi umilele, hadi Uungu.” Na tena: “Kila mtu ataamua mwenyewe na siyo mwingine.” “Hukumu itakuwa sahihi, kwa sababu ni hukumu ya nafsi yake mwenyewe.... Kiti cha enzi kimo ndani yako mwenyewe.” Mwalimu wa imani ya kuongea na mizimu alisema, “ufahamu wa kiroho” ulipoamka ndani yake: “Ndugu zangu, wote walikuwa nusu miungu ambayo haijaanguka.” Mwalimu mwingine anatangaza kuwa: “Kila kiumbe mwenye haki na aliye mkamilifu ni Kristo.”PKSw 423.2

    Hivyo, badala ya haki na ukamilifu wa Mungu asiyekuwa na kikomo, ambaye ndiye anapaswa kutukuzwa; badala ya haki kamilifu ya sheria Yake, kiwango cha kweli cha upeo wa kibidamu, Shetani ameweka asili ya mwanadamu mwenyewe mwenye dhambi na anayekosea kuwa kitu pekee cha kutukuzwa, kanuni pekee ya hukumu, au kiwango cha tabia. Haya ni maendeleo, lakini siyo ya kwenda juu, bali ya kwenda chini.PKSw 424.1

    Ni sheria ya kiakili na ya asili ya kiroho kuwa kwa kutazama tunabadilika. Akili, pole pole inabadilika na kupatana na mambo ambayo imeruhusiwa kuyatafakari. Inajiunga na kile ambacho imezoea kukipenda na kukiheshimu. Mwanadamu hawezi kuinuka juu kuliko kiwango cha usafi au wema au ukweli. Ikiwa nafsi ndiyo kitu cha juu sana kwake, hatainuka juu zaidi ya kitu ambacho kiko juu ya nafsi yake. Badala yake, atakuwa kila wakati akifikiria kuzama chini na chini zaidi. Ni neema ya Mungu pekee iliyo na nguvu ya kumwinua mwanadamu. Mwanadamu akiachwa peke yake, njia yake lazima ielekee chini tu.PKSw 424.2

    Kwa mtu mwenye kujipenda, mpenda anasa, mwenye tamaa za mwili, imani ya kuongea na mizimu hujitokeza kwa uwazi zaidi kuliko kwa mtu mstaarabu na msomi zaidi; katika muundo usio wa kistaarabu zaidi wanapata mambo ambayo wana mwelekeo wa kuwa na mwafaka nayo zaidi. Shetani anasoma kila kiashiria cha udhaifu katika asili ya mwanadamu, anaona viashiria vya dhambi ambazo kila mtu ana mwelekeo wa kuzitenda, na ndipo huhakikisha kuwa fursa zinakuwepo za kutosha kukidhi huo mwelekeo wa uovu. Anawajaribu watu kuzidisha kile ambacho chenyewe ni halali, na kuwafanya, kwa kutokuwa na kiasi, kudhoofisha nguvu yao wa kimwili, kiakili, na kimaadili. Ameharibu na anaharibu maelfu ya watu kwa njia ya uchu na tamaa za mwili, na kwa njia hiyo kuharibu utu wa mtu. Na kuhitimisha kazi yake, anasema, kupitia pepo kuwa “ujuzi wa kweli humweka mwanadamu juu ya sheria zote;” kuwa “chochote kile, ni sahihi;” kuwa “Mungu hakikatazi;” na kuwa “dhambi zote zilizotendwa hazina hatia.”PKSw 424.3

    Watu wanapoongozwa kwa njia hiyo kuamini kuwa hamu ndiyo sheria ya juu kabisa, kuwa uhuru ni kuipuuza sheria, na kuwa mwanadamu anawajibika kwa nafsi yake mwenyewe, ni nani anayeweza kushangaa kuwa ufisadi na uhalifu vimeenea kila mahali? Watu wengi hupokea mafundisho yanayowaacha huru kutii misukumo ya myoyo isiyozaliwa upya. Uwezo wa kujitawala unaachwa kupelekeshwa na tamaa za mwili, nguvu za akili na roho zinawekwa chini ya mamlaka ya mielekeo ya kinyama, na Shetani kwa furaha anafagilia katika wavu wake maelfu ya wale wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo.PKSw 424.4

    Lakini hakuna mtu anayelazimika kudanganywa na madai ya uongo ya imani ya kuongea na wafu. Mungu ameupatia ulimwengu nuru ya kutosha kuwawezesha kugundua mtego. Kama ilivyokwisha kuoneshwa, nadharia ambayo ni msingi hasa wa imani ya kuongea na wafu inashindana na kauli za wazi za Maandiko. Biblia inatangaza kuwa wafu hawajui neno lo lote, kuwa mawazo yao yamepotea; hawana sehemu yo yote katika mambo yanayotokea chini ya jua; hawajui lo lote la furaha au huzuni la wale waliokuwa wapendwa sana duniani.PKSw 425.1

    Zaidi ya hapo, Mungu amekataza moja kwa moja mawasiliano bandia na watu waliokufa. Katika siku za Waebrania kulikuwepo na tabaka la watu waliodai, kama wanavyodai leo kuamini katika mawasiliano na wafu, kuwa huwa wanaongea na wafu. Lakini “roho za utambuzi,” kama wageni hawa kutoka ulimwengu mwingine walivyoitwa, zinaelezwa na Biblia kuwa ni “roho za mashetani.” (Linganisha na Hesabu 25:1-3; Zaburi 106:28; 1 Wakorintho 10:20; Ufunuo 16:14.) Kazi ya kushughulika na roho za utambuzi ilitangazwa kuwa chukizo kwa Bwana, na ilipigwa marufuku kabisa na adhabu ya mkosaji katika suala hili ilikuwa kifo. Walawi 19:31; 20:27. Jina la uchawi kwa sasa linadharauliwa. Dai kuwa watu wanaweza kuongea na roho wachafu huchukuliwa kama hekaya za Zama za Giza. Lakini imani katika kuongea na wafu, ambayo wafuasi wake wanafikia mamia ya maelfu, ndiyo, hata mamilioni, ambayo imeshaingia katika ulimwengu wa sayansi, ambayo imevamia makanisa, na imekubaliwa na vyombo vya kutunga sheria, na hata katika ikulu za wafalme—uongo huu mkubwa ni uamsho wa uchawi, katika joho jipya uliokatazwa na kupigwa marufuku wakati ule wa zamani.PKSw 425.2

    Ikiwa kusingekuwa na ushahidi mwingine wowote wa tabia halisi ya imani ya kuwasiliana na wafu, ingetosha kwa Mkristo kuwa roho za mashetani hazitofautishi kati ya haki na dhambi, kati ya mitume waungwana na safi wa Kristo na watumishi wa Shetani walio waovu sana. Kwa kusema kuwa watu waovu kabisa wako mbinguni, na wameinuliwa pale, Shetani anauambia ulimwengu: “Haidhuru jinsi mtu alivyo mwovu; haidhuru ikiwa unamwamini Mungu na unaiamini Biblia. Ishi upendavyo; mbinguni ni nyumbani mwako.” Walimu wa imani ya kuongea na mizimu wanatangaza moja kwa moja: “Kila atendaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, naye huwafurahia watu hao, au, Mungu mwenye kuhukumu yuko wapi?” (Malaki 2:17). Neno la Mungu linasema: “Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza” (Isaya 5:20).PKSw 425.3

    Mitume, wanapoigizwa na roho hizi zidanganyazo, wanaongozwa kupinga kile walichokiandika kwa uongozi wa Roho Mtakatifu walipokuwa duniani. Wanakanusha chimbuko la Kiungu la Biblia, na kwa njia hiyo wanavunja vunja msingi wa tumaini la Mkristo na kuzima nuru inayofunua njia ya kwenda mbinguni. Shetani anaufanya ulimwengu uamini kuwa Biblia ni riwaya tu, au angalau ni kitabu kilichofaa jamii changa, lakini sasa kitiliwe maanani kidogo tu, au kiwekwe pembeni kama kitabu kilichopitwa na wakati. Na kuchukua nafasi ya neno la Mungu huonesha utendaji wa imani ya kuongea na wafu. Hapa pana njia mawasiliano yaliyoko chini ya utawala wake kamili; kwa njia hii anaweza kuufanya ulimwengu uamini cho chote anachokitaka. Kitabu ambacho kitamhukumu na wafuasi wake anakiweka kivulini, mahali anapotaka kiwe; Mwokozi wa ulimwengu anamfanya aonekana kuwa kama mwanadamu wa kawaida. Na kama vile mlinzi wa Kirumi aliyelilinda kaburi la Yesu alivyosambaza taarifa za uongo ambazo makuhani na wazee waliwawekea midomoni ili kuthibitisha kutokufufuka Kwake, ndivyo waumini wa imani ya kuongea na wafu wanavyojaribu kufanya ionekane kuwa hakuna cho chote cha kimuujiza katika asili ya maisha ya Mwokozi. Baada ya kutafuta kumweka Yesu nyuma ya pazia, wanawaonesha miujiza yao, wakitangaza kuwa miujiza yao ni mikubwa zaidi kuliko kazi za Kristo.PKSw 425.4

    Ni kweli kuwa imani ya kuongea na mizimu sasa inabadilisha muundo wake na, huku ikificha baadhi ya mambo yake mabaya, inajivika joho la Ukristo. Lakini matamko yake kutoka mimbarani na kupitia vyombo vya habari yamekuwa mbele ya umma kwa miaka mingi, na katika mambo haya tabia yake halisi inadhihirika. Mafundisho haya hayawezi kupingwa au kufichwa.PKSw 426.1

    Hata katika muundo wake wa sasa, mbali na kustahili kuvumilika zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma, wakati huu imani ya kuongea na wafu ni ya hatari zaidi, kwa sababu ni uongo ambapo umepangwa kijanja zaidi. Wakati pale mwanzoni imani hii ilimkataa Kristo na Biblia, kwa sasa inadai kumkiri Kristo na Biblia. Lakini Biblia inatafsiriwa katika namna ambayo inaufurahisha moyo usiozaliwa mara ya pili, wakati ukweli wake muhimu ukivurugwa ili usiwe na mguso. Upendo unachukuliwa kuwa sifa kuu ya Mungu, lakini unadhoofishwa hadi kuwa hisia dhaifu, na kuweka tofauti ndogo kati ya wema na uovu. Haki ya Mungu, makemeo Yake dhidi ya dhambi, matakwa ya sheria Yake takatifu, vinafichwa visionekane machoni pa watu. Watu wanafundishwa Amri Kumi kama kanuni zilizopitwa na wakati. Hadithi zinazopendeza, zinazochangamsha zinatia ganzi fahamu na kuwaongoza watu kuikataa Biblia kama msingi wa imani yao. Kristo anakataliwa kweli kweli kama alivyokataliwa kabla; lakini Shetani amepofusha macho ya watu kiasi kwamba uongo haugunduliwi.PKSw 426.2

    Kuna watu wachache walio na utambuzi kamili wa nguvu ya imani ya kuongea na wafu na hatari ya kuwa chini ya mvuto wake. Wengi wanaichezea kukidhi udadisi wao. Hawaiamini na wangejazwa hofu dhidi ya kujazwa na wazo la kujiweka chini ya utawala wa roho za mashetani. Lakini wanathubutu kwenda uwanja uliokatazwa, na mharibifu mkuu anatumia nguvu yake juu yao dhidi ya nia yao. Wakijaribiwa tu kusalimisha akili zao chini ya uongozi wake, mara moja atawafanya kuwa mateka wake. Haiwezekani, kwa nguvu zao wenyewe, kupona kunaswa na mtego wake unaoteka, unaovutia. Ni nguvu ya Mungu pekee, inayotolewa kama jibu kwa ombi la imani, inayoweza kuziokoa roho hizi zilizonaswa.PKSw 426.3

    Wote wanaojenga tabia ya dhambi, au wanaopalilia kwa makusudi dhambi inayojulikana, wanaalika majaribu ya Shetani. Wanajitenga na Mungu na ulinzi wa malaika Wake; wakati Shetani anapoleta uongo wake, hawana ulinzi na wanakuwa mawindo rahisi. Wale wanaojiweka hivyo katika nguvu yake wanatambua kidogo mahali ambapo njia yao itaishia. Baada ya kufanikisha anguko lao, mjaribu atawatumia kama mawakala wake kuwajaribu wengine na kuwaharibu.PKSw 427.1

    Nabii Isaya anasema: “Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi” (Isaya 8:19, 20). Ikiwa watu wangekuwa tayari kupokea ukweli ambao umeelezwa wazi wazi katika Maandiko kuhusu asili ya mwanadamu na hali ya wafu, wangeweza kuona katika madai na vituko vya imani ya kuongea na wafu utendaji kazi wa Shetani kwa nguvu na ishara na miujiza ya uongo. Lakini badala ya kusalimisha uhuru unaopatana na moyo usioongoka, na kuachana na dhambi wanazozipenda, watu wengi hufumba macho yao wasiione nuru na kutembea katika hiyo nuru na wanasonga mbele, licha ya maonyo, wakati Shetani akisuka mitego yake kuwazunga pande zote, na wanakuwa mawindo yake. “Kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa,” kwa hiyo “Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo” (2 Wathesalonike 2:10, 11).PKSw 427.2

    Watu wanaopinga mafundisho ya imani za kuongea na wafu wanashambulia, siyo wanadamu peke yao, bali Shetani na malaika zake. Wameingia katika pambano dhidi ya mamlaka na nguvu na roho wachafu katika anga za juu. Shetani hatarudi nyuma hata inchi moja katika pambano isipokuwa tu asukumwe nyuma kwa nguvu ya wajumbe wa mbinguni. Watu wa Mungu wanapaswa kukabiliana naye, kama Mwokozi alivyokabiliana Naye, kwa maneno: “Imeandikwa.” Shetani anaweza kunukuu Maandiko sasa kama alivyofanya katika siku za Kristo, na anapotosha mafundisho yake ili kuunga mkono uongo wake. Watu wanaoweza kusimama katika wakati huu wa hatari lazima waelewe wao wenyewe ushuhuda wa Maandiko.PKSw 427.3

    Wengi watakutana na roho za mashetani wakiwa wamejigeuza na kujifanya ndugu au rafiki zao wapendwa waliokufa na wakifundisha mafundisho ya uongo wa hatari sana. Wageni hawa watagusa hisia zetu upendo na huruma na watatenda miujiza kuunga mkono maigizo yao. Inatupasa kujiandaa kusimama imara dhidi yao kwa ukweli wa Biblia kuwa wafu hawajui neno lo lote na kuwa hao wanaotokea ni roho za mashetani.PKSw 428.1

    Karibuni mbele yetu kuna “saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi” (Ufunuo 3:10). Wote wale ambao imani yao haina mizizi katika neno la Mungu watadanganywa na watashindwa na adui. Shetani “hufanya kazi kwa madanganyo yote ya udhalimu” kuwatawala wanadamu, na madanganyo yake daima yataongezeka. Lakini anaweza kufikia lengo lake pale tu wanadamu wanapojisalimisha wenyewe chini ya majaribu yake. Wale ambao wanatafuta kwa dhati ujuzi wa ukweli na wajitahidi kutakasa roho zao kwa njia ya uvumilivu, huku wakifanya kila wanachoweza kukifanya kujiandaa kwa ajili ya shindano, watagundua, kwa Mungu wa ukweli, ulinzi wa hakika. “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda” (aya ya 10), ni ahadi ya Mwokozi. Angeweza kumtuma kila malaika kutoka mbinguni kuwalinda watu Wake kuliko kuacha roho moja inayomtumaini Mungu ishindwe na Shetani.PKSw 428.2

    Nabii Isaya anafunua uongo wa kutisha utakaokuja juu ya waovu, utakaowafanya wajihesabu kuwa salama dhidi ya hukumu za Mungu: “Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli” (Isaya 28:15). Katika tabaka lililoelezewa hapa wamejumuishwa wale ambao katika ugumu wao wa kutokutubu wanajifariji kwa imani kuwa hakutakuwa na adhabu kwa mwenye dhambi; kwamba wanadamu wote, haidhuru jinsi walivyo mafisadi, wanatarajia kuinuliwa mbinguni, kuwa kama malaika wa Mungu.PKSw 428.3

    Lakini bado, kwa mkazo zaidi, kuna wale ambao wanafanya agano na kifo na makubaliano na kuzimu, wanaokataa ukweli ambao Mbingu imeutoa kama ulinzi kwa ajili wenye haki katika siku ya taabu, na wanakubali hifadhi ya uongo inayotolewa na Shetani mahali pake—maigizo ya uongo wa imani ya kuongea na wafu.PKSw 428.4

    Jambo la kushangaza kuliko maelezo ni upofu wa watu wa kizazi hiki. Maelfu ya watu hulikataa neno la Mungu kama lisilofaa kuaminiwa na kwa imani na shauku kubwa hupokea madanganyo ya Shetani. Wenye mashaka na wenye dhihaka hukemea ubaguzi wenye chuki wa wale wanaotetea imani ya manabii na mitume, na wanapotoka kwa kudharau matamshi makuu ya Maandiko kuhusu Kristo na mpango wa wokovu, na adhabu inavyokaribia kuja juu ya wale wanaoukataa ukweli. Yana athari kubwa sana kwa akili ambazo ni finyu, dhaifu, na zinazoamini ushirikina kiasi kwamba wahusika hawawezi kutambua madai ya Mungu na kutii maagizo ya sheria Yake. Wanakuwa na uhakika mkubwa, kwa kweli, kana kwamba wamefanya agano na kifo na wamekubaliana na kuzimu—kana kwamba wamejenga ukuta usiopenywa kati yao na adhabu ya Mungu. Hakuna jambo lo lote linaloweza kuamsha hofu zao. Wamejisalimisha kikamilifu katika mikono ya mjaribu, wameshikamana naye kwa karibu sana, na kujazwa na roho wake kikamilifu, kiasi kwamba hawana nguvu wala wazo la kutoka katika mtego wake.PKSw 428.5

    Shetani kwa muda mrefu amekuwa akijiandaa kwa ajili ya juhudi yake ya mwisho ya kuudanganya ulimwengu. Msingi wa kazi yake ulijengwa kwa uhakikisho aliompa Hawa katika Bustani ya Edeni kuwa: “Hakika hamtakufa.” “Siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwanzo 3:4, 5). Kidogo kidogo amekuwa akiandaa kwa ajili ya udanganyifu mkubwa kwa kuanzisha imani ya kuongea na wafu. Hajafikia kilele cha mafanikio yake katika mipango yake; lakini itafikiwa katika sehemu ya mwisho ya wakati. Nabii anasema: “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” (Ufunuo 16:13, 14). Isipokuwa wale tu ambao wanatunzwa na nguvu za Mungu, kwa njia ya imani katika neno Lake, ulimwengu wote utatekwa na kuwa wahanga wa uongo wake. Watu wanabembelezwa ili wasinzie huku wakihatarisha usalama wao, ili hatimaye waamshwe tu na mvua ya hasira ya Mungu.PKSw 429.1

    Bwana Mungu anasema: “Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri. Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo” (Isaya 28:17, 18).PKSw 429.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents