Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 9—Mwanamatengenezo wa Kiswisi

    Katika uchaguzi wa watu kwa ajili ya kutengeneza kanisa, mpango ule ule wa Mungu unaonekana kama ule unaoonekana katika kupanda kanisa. Mwalimu wa mbinguni aliwapita watu wakuu wa dunia, wenye vyeo, na wenye mali, waliokuwa wamezoea kupokea sifa na heshima kama viongozi wa watu. Walikuwa na kiburi na kujitumainia kwa sababu ya ukuu wao waliojivunia kiasi kwamba wasingeweza kuumbwa upya ili wawahurumie wanadamu wenzao na waweze kuwa watendakazi pamoja na Mtu mnyenyekevu wa Nazareti. Kwa wavuvi wa samaki, wasio na elimu, wanaohangaika wa Galilaya wito ulitolewa: “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu” (Mathayo 4:19). Wanafunzi hawa walikuwa wanyenyekevu na wanaofundishika. Kwa kadiri walivyokuwa wameathiriwa kidogo na mafundisho ya uongo ya wakati ule, ndivyo ilivyokuwa rahisi zaidi kwa Kristo kufanikiwa kuwafundisha na kuwaandaa kwa ajili ya huduma Yake. Kadhalika ndivyo ilivyokuwa katika siku za Matengenezo Makuu. Wanamatengenezo wakuu walikuwa watu waliotoka katika maisha ya chini—watu ambao hawakuwa wameathiriwa kwa wakati wowote na kiburi cha madaraka na mvuto wa itikadi kali na ujanja wa makasisi. Ni mpango wa Mungu kutumia vyombo dhaifu kufanikisha matokeo makubwa. Ndipo utukufu hautatolewa kwa wanadamu, bali kwake Yeye atendaye kupitia kwao kutaka na kutenda mapenzi Yake mema.PKSw 127.1

    Majuma machache baada ya kuzaliwa kwa Luther katika kibanda cha mfanyakazi katika mgodi mjini Saxony, Ulric Zwingli alizaliwa katika nyumba ndogo ya mfugaji katika milima ya Alps. Mazingira ya Zwingli wakati wa utoto wake, na katika mafunzo yake ya awali, yalifaa kwa ajili ya maandalizi ya utume wake wa baadaye. Akiwa amelelewa katikati ya mandhari yenye kuvutia sana, uzuri, na fahari ya ajabu ya uoto wa asili, akili yake tangu awali iliguswa na hisia ya adhama, nguvu, na utukufu wa Mungu. Historia ya matendo ya kishujaa yaliyofanyika juu ya milima alipozaliwa iliwasha moto wa matarajio ya ujana wake. Na kando ya bibi yake mcha Mungu alisikiliza visa vichache vya thamani vya Biblia ambavyo Bibi yake aliviokoteza kutoka miongoni mwa hadithi za wahenga na mapokeo ya kanisa. Kwa shauku kubwa alisikia matendo makuu ya wazee na manabii, ya wachungaji waliochunga kwa zamu mifugo yao kwenye vilima vya Palestina ambapo malaika waliongea nao, kuhusu mtoto mchanga wa Bethlehemu na juu ya Mtu wa Kalwari.PKSw 127.2

    Kama John Luther, baba yake Zwingli alikuwa na shauku ya elimu kwa ajili ya mwanae, na kijana alipelekwa shule mapema kutoka katika bonde lake alikozaliwa. Akili yake ilikua haraka, na haukupita muda mrefu swali likawa ni wapi pa kupata walimu wenye uwezo wa kumfundisha. Akiwa na umri wa miaka kumi na tatu alikwenda Bern, mji ambao wakati huo ulikuwa na shule bora katika nchi ya Switzerland. Hapa, hata hivyo, hatari iliibuka ambayo ilitishia kutia doa ahadi yake ya maisha. Juhudi za makusudi zilifanywa na watawa kumshawishi aingie katika nyumba ya watawa. Watawa wa Kidominika na wale wa Kifransiskani walishindana katika kutafuta kukubalika na kupendwa. Kufikia azma hii walijitahidi kwa kuweka mapambo yanayovutia katika makanisa yao, madoido katika sherehe zao, na vivutio vya mifupa ya watu maarufu na sanamu zilizodaiwa kutenda miujiza.PKSw 127.3

    Wadominika wa Bern waliona kuwa ikiwa wangeweza kumpata kijana huyu mwenye karama nyingi na msomi, wangepata mapato na heshima. Ujana wake, uwezo wake wa asili kama msemaji na mwandishi, na uwezo mkubwa katika muziki na ushairi, vingeweza kuleta mafanikio makubwa zaidi kuliko madoido na maonesho yao, katika kuwavuta watu na kuwaingiza katika huduma zao na kuongeza mapato ya shirika lao. Kwa njia ya udanganyifu na sifa za uongo walijaribu kumshawishi Zwingli aingie jumuia yao ya utawa. Luther, akiwa mwanafunzi shuleni, alijifungia katika chumba cha nyumba ya watawa, na ilikuwa apotee na asionekane ulimwenguni kama isingekuwa kwa uongozi wa Mungu kuingilia kati na kumtoa nje. Zwingli hakuruhusiwa kukutana na hatari hiyo. Kwa uongozi wa Mungu baba yake alipata habari ya mipango ya watawa. Hakuwa na nia ya kumruhusu mwanae afuate maisha ya kivivu na yasiyo na thamani ya watawa. Aliona kuwa utumishi wake wa thamani wa baadaye ulikuwa hatarini, na aliagiza arudi nyumbani haraka.PKSw 128.1

    Agizo ilitiiwa; lakini kijana hakuweza kuridhika kukaa muda mrefu katika makazi yao ya bondeni, na haukupita muda mrefu alirudi masomoni kwake, akihamia, baada ya muda mfupi, katika mji wa Basel. Ni hapa ambapo kwa mara ya kwanza Zwingli alisikia injili ya neema ya Mungu ya bure. Wittembach, mwalimu wa lugha za kale, wakati akijifunza Kigiriki na Kiebrania aliongozwa kujifunza Maandiko Matakatifu, na hivyo miale ya nuru itokayo kwa Mungu iliangazia akili za wanafunzi aliokuwa akiwafundisha. Alisema kuwa kulikuwa na ukweli wa zamani zaidi, na wenye thamani kubwa zaidi, kuliko nadharia zilizofundishwa na walimu na wanafalsafa. Ukweli huu wa zamani ulikuwa kwamba kifo cha Kristo ni fidia pekee ya mwenye dhambi. Kwa Zwingli maneno haya yalikuwa ni mwale wa kwanza wa nuru inayotangulia mapambazuko.PKSw 128.2

    Zwingli aliitwa baada ya muda mfupi kutoka Basel kwenda kuanza kazi yake ya maisha. Eneo lake la kwanza la kazi lilikuwa parishi ya Alpine, ambapo siyo mbali sana na bondeni alikozaliwa. Baada ya kuwekewa mikono ya wakfu wa ukasisi, “alijiweka wakfu kwa moyo wake wote kuchunguza ukweli wa Kimungu; kwani alijua kikamilifu,” alisema Mwanamatengenezo mwenzake, “ni kiasi gani ilimpasa kujua yule ambaye kwake kondoo wa Kristo walikuwa wameaminiwa.”—Wylie, b. 8, ch. 5. Kwa kadiri alivyochunguza Maandiko, alizidi kuona kwa uwazi zaidi tofauti kati ya ukweli wa Maandiko na uongo wa Roma. Alijisalimisha kwa Biblia kama neno la Mungu, kanuni pekee inayojitosheleza, isiyokosea. Aligundua kuwa ilipaswa kujitafsiri yenyewe. Hakuthubutu kueleza Maandiko kutetea nadharia au fundisho lililojulikana, bali alichukulia kuwa wajibu wake kujifunza kilicho cha wazi na kila fundisho lililo dhahiri. Alijitahidi kupata kila msaada alioweza kuupata wa kumwezesha kupata uelewa sahihi wa maana yake, na aliomba msaada wa Roho Mtakatifu, ambao ungeweza, alisema, kulifunua kwa wale wote waliotafuta kwa moyo wa dhati na maombi mengi.PKSw 128.3

    “Maandiko,” alisema Zwingli, “yalitoka kwa Mungu, siyo kwa mtu, na hata hivyo Mungu anayeangazia atawapa ufahamu kuwa maneno hayo hutoka kwa Mungu. Neno la Mungu... haliwezi kushindwa; ni angavu, linajifundisha lenyewe, linajifunua lenyewe, linaangazia moyo juu ya wokovu wote na neema yote, linafariji moyo kwa msaada wa Mungu, linanyenyekesha moyo, kiasi kwamba moyo unajiachia na hata unajinyima wenyewe, na unamkumbatia Mungu.” Ukweli wa maneno haya Zwingli mwenyewe alikuwa ameuthibitisha. Akizungumzia uzoefu wake wakati huu, aliandika baadaye: “Wakati ... nilipoanza kujitolea mwenyewe kujifunza Maandiko Matakatifu, falsafa na teolojia (kielimu) daima vilipendekeza migogoro kwangu. Hatimaye nilifikia hili, kuwa nilifikiri, ‘Unapaswa kuachana na uwongo, na ujifunze maana ya Mungu kutokana na neno Lake sahili peke yake.’ Ndipo nilianza kumwomba Mungu anipe nuru Yake, na Maandiko yalianza kuwa mepesi zaidi kwangu.”—Ibid., b. 8, ch. 6.PKSw 129.1

    Fundisho alilolihubiri Zwingli halikutoka kwa Luther. Lilikuwa fundisho la Kristo. “Ikiwa Luther anamhubiri Kristo,” alisema Mwanamatengenezo wa Kiswisi, “anafanya kile ninachokifanya. Wale ambao amewaleta kwa Kristo ni wengi zaidi kuliko wale ambao mimi nimewaongoza. Lakini hili siyo muhimu. Sitashuhudia jina jingine zaidi ya lile la Kristo, ambaye mimi ni askari Wake, na ambaye Yeye ni Mkuu wangu. Sijawahi kuandika hata neno moja kwa Luther, wala Luther hajawahi kuniandikia. Na kwa nini? ... Ili ionekane jinsi ambavyo Roho wa Mungu ni Yule Yule, kwa kuwa sisi sote wawili, bila kufanya kazi pamoja, tunafundisha fundisho la Kristo linalofanana.”—D'Aubigne, b. 8, ch. 9.PKSw 129.2

    Mnamo mwaka 1516 Zwingli alialikwa kuwa mhubiri katika nyumba ya watawa jijini Einsiedeln. Hapa ndipo ambapo angeona kwa karibu ufisadi wa Kanisa la Roma na ndipo alikuwa anakwenda kuweka mvuto kama Mwanamatengenezo ambao ungeenda ng'ambo ya mipaka ya eneo lake la Alps. Miongoni mwa vivutio vya jiji la Einsiedeln ilikuwa sanamu ya Bikira ambayo ilisemekana kuwa ilikuwa na nguvu ya kutenda miujiza. Juu ya lango la nyumba ya watawa kulikuwa na maandishi, “Hapa ondoleo kamili la dhambi linaweza kupatikana.”— Ibid., b. 8, ch. 5. Mahujaji nyakati zote walifika katika jengo la kumbukumbu la Bikira; lakini wakati wa sherehe ya kila mwaka ya kuwekwa wakfu kwake maelfu ya watu walifurika kutoka kona zote za Switzerland, na hata kutoka Ufaransa na Ujerumani. Zwingli, akiwa ameumizwa sana na kile alichokiona, alichukua fursa hiyo kutangaza uhuru upatikanao katika injili kwa hawa watumwa wa ushirikina.PKSw 129.3

    “Msidhani,” alisema, “kuwa Mungu yupo katika hekalu hili zaidi kuliko alivyo katika sehemu nyingine ya uumbaji. Haijalishi kuwa unaishi katika nchi gani, Mungu yuko pamoja nawe, na anakusikia.... Je, inawezekana kazi zisizokuwa na manufaa, safari ndefu, sadaka, sanamu, kumwomba Bikira au kuwaomba watakatifu, kukupatia neema ya Mungu? ... Kuna faida gani kuwa na maneno mengi katika maombi yetu? Kuna faida gani kuvaa kofia inayong'aa, kuwa na kichwa kilichonyolewa, kuvaa joho refu linalozagaa, au kuvaa kandambili zilizopakwa rangi ya dhahabu? ... Mungu anaangalia moyo, na mioyo yetu iko mbali Naye.” “Kristo,” alisema, “ambaye alitolewa mara moja juu ya msalaba, ni kafara na kondoo wa kafara, ambayo imetosheleza kwa ajili ya dhambi za waaminio wote milele zote.”—Ibid., b. 8, ch. 5.PKSw 130.1

    Kwa wasikilizaji walio wengi mafundisho haya hayakuwa ya kufurahisha. Lilikuwa jambo la kukatisha tamaa kwao kuambiwa kuwa safari yao ya kuchosha ilikuwa imefanyika bure. Msamaha uliotolewa bure kwao kwa njia ya Kristo hawakuweza kuuelewa. Walikuwa wameridhishwa na njia ya zamani ya kwenda mbinguni ambayo Roma ilikuwa imewaelekeza. Walisita kujiingiza katika mashaka ya kutafuta kitu kingine bora zaidi. Ilikuwa rahisi kwao kupata wokovu wao kupitia kwa makasisi na papa kuliko kutafuta usafi wa moyo.PKSw 130.2

    Lakini tabaka lingine lilipokea kwa furaha habari za wokovu kwa njia ya Kristo. Maadhimisho yaliyofundishwa na Roma yalikuwa yameshindwa kuleta amani ya rohoni, na kwa imani waliipokea damu ya Mwokozi kama upatanisho wao. Hawa walirudi nyumbani kwao kuwafunulia wengine nuru ya thamani waliyokuwa wameipokea. Kwa njia hiyo ukweli ulipelekwa kutoka mtaa mmoja hadi mwingine, kutoka mji mmoja hadi mwingine, na idadi ya mahujaji wa hekalu la kumbukumbu ya Bikira ilipungua sana. Kulikuwepo kushuka kiasi kibaya kwa makusanyo ya sadaka, na matokeo yaliyoonekana hata kwenye mshahara wa Zwingli, ambao ulitokana na sadaka hiyo. Lakini jambo hili lilisababisha furaha tu kwake kwa kuona kuwa nguvu ya unafiki na ushirikina ilikuwa ikivunjwa.PKSw 130.3

    Sio kwamba mamlaka za kanisa zilikuwa hazioni kazi ambayo Zwingli alikuwa anaifanya; lakini kwa muda huu waliacha kuingilia. Wakitumaini kuwa watamvuta mpaka awe upande wao, walijaribu kumshawishi kwa kutumia sifa za uongo; na wakati huo huo ukweli ulikuwa ukipata nguvu katika mioyo ya watu.PKSw 130.4

    Kazi za Zwingli mjini Einsiedeln zilimuandaa kwa ajili ya eneo kubwa la kazi, kama alikuwa karibu kuanza kazi hiyo muda mfupi uliofuata. Baada ya miaka mitatu hapa aliitwa kufanya kazi ya mhubiri katika kanisa kuu la Zurich. Wakati ule huu ulikuwa mji muhimu kuliko miji yote katika shirikisho la Uswisi, na mvuto uliotolewa hapa uligusa kona nyingi za shirikisho. Viongozi wa dini waliokuwa wamemwita kuja Zurich walikuwa, hata hivyo, wakitamani kuzuia ubunifu wowote, na kweli walichukua hatua ya kumuelekeza majukumu yake.PKSw 131.1

    “Utatumia kila juhudi,” walisema, “kukusanya mapato kutoka kila chanzo, bila kupuuza hata chanzo kidogo sana. Utawahimiza waaminifu, kutoka katika kibweta na katika kizimba cha maungamo, kulipa zaka na kodi zote, na waoneshe sadaka zao na upendo wao kwa kanisa. Utakuwa na bidii katika kuongeza mapato yanayotokana na huduma kwa wagonjwa, yanayotokana na misa, na kwa jumla yanayotokana na kila huduma ya kanisa.” Waelekezaji wake walisema, “Kuhusiana na utoaji wa sakramenti, mahubiri, na utunzaji wa kundi, haya pia ni majukumu ya mlezi wa kiroho. Lakini kwa ajili ya haya unaweza kutumia mtu mbadala, na hususani katika kuhubiri. Inakupasa kugawa sakramenti kwa watu wanaoeleweka tu, na pale tu unapoalikwa; unakatazwa kufanya hivyo bila kutofautisha watu.”—Ibid., b. 8, ch. 6.PKSw 131.2

    Zwingli alisikiliza maelekezo haya akiwa kimya, na katika kujibu, baada ya kutoa shukurani zake kwa heshima ya kuitwa kuhudumu katika kituo hiki muhimu, aliendelea kueleza mwelekeo aliokuwa anakusudia kuuchukua. “Maisha ya Kristo,” alisema, “kwa muda mrefu yamefichwa mbali na watu. Nitahubiri juu ya kitabu chote cha Injili ya Mathayo Mtakatifu, ... nikichota kutoka katika Maandiko pekee, nikizama katika vina vyake, nikilinganisha aya moja na nyingine, na nikitafuta ufahamu kwa maombi ya kudumu na ya dhati. Ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, kwa ajili ya sifa ya Mwana Wake pekee, kwa ajili ya wokovu halisi wa roho, na kwa ajili ya kuwajenga katika imani ya kweli, kwamba nitaiweka wakfu huduma yangu.”— Ibid., b. 8, ch. 6. Pamoja na kuwa baadhi ya viongozi wa kanisa hawakukubaliana na mpango wake, na walijaribu kumshawishi aachane nao, Zwingli alisimama imara. Alisema kuwa hakukusudia kuanzisha mbinu mpya, bali mbinu ya zamani iliyotumiwa na kanisa la awali na nyakati safi.PKSw 131.3

    Tayari shauku ilikuwa imeamshwa kwa ajili ya ukweli alioufundisha; na watu walifurika katika idadi kubwa kusikiliza mahubiri yake. Wengi wa wale waliokuwa wameacha kuhudhuria ibada walikuwa miongoni mwa wasikilizaji wake. Alianza huduma yake kwa kufungua Injili na kusoma na kueleza kwa wasikilizaji wake visa vilivyovuviwa vya maisha, mafundisho, na mauti ya Kristo. Hapa, kama ilivyokuwa kule Einsiedeln, aliwasilisha neno la Mungu kama mamlaka pekee isiyokosea na mauti ya Kristo kama kafara pekee kamilifu. “Ni kwa Kristo,” alisema, “ambapo ninatamani kuwaongoza—kwa Kristo, chanzo cha kweli cha wokovu.”—Ibid., b. 8, ch. 6. Watu wa matabaka mbalimbali walimzunguka mhubiri, tangu viongozi wakuu wa nchi na wasomi hadi mafundi na wakulima wadogo. Kwa shauku kubwa walisikiliza maneno yake. Siyo kuwa alitangaza toleo la wokovu wa bure, lakini pia bila hofu alikemea maovu na ufisadi wa nyakati zile. Wengi walitoka kanisani wakimtukuza Mungu. “Mtu huyu,” walisema, “ni mhubiri wa ukweli. Atakuwa Musa wetu, atuongoze kutoka katika Misri hii ya giza.”—Ibid., b. 8, ch. 6.PKSw 131.4

    Lakini ingawa mwanzoni kazi zake zilipokelewa kwa furaha, baada ya muda upinzani uliibuka. Watawa walijipanga kuzuia kazi yake na kukosoa mafundisho yake. Wengi walimshambulia kwa kebehi na dhihaka; wengine walimshambulia kwa dharau na vitisho. Lakini Zwingli aliyabeba yote hayo kwa uvumilivu, akisema: “Ikiwa shauku yetu ni kuwashinda waovu kwa ajili ya Yesu Kristo, ni lazima tufumbe macho yetu dhidi ya mambo mengi.”—Ibid., b. 8, ch. 6.PKSw 132.1

    Mnamo wakati huu, mtendakazi mpya alikuja kuendeleza kazi ya matengenezo. Mtu mmoja aitwaye Lucian alitumwa kutoka Zurich na rafiki wa mwana matengenezo aliyeishi Basel, akiwa na machapisho ya Luther, ambaye alipendekeza kuwa uuzaji wa vitabu hivi ungekuwa njia kubwa ya kutawanya nuru. “Hakikisha,” aliandika Zwingli, “kuwa mtu huyu na busara na ujuzi wa kutosha; ikiwa yuko hivyo, mruhusu avichukue kutoka jiji hadi jiji, kutoka mji hadi mji, kutoka kijiji hadi kijiji, hata kutoka nyumba hadi nyumba miongoni mwa Waswisi, kazi za Luther, na hasahasa ufafanuzi wake wa Sala ya Bwana ulioandikwa kwa ajili ya walei. Kwa kadiri kazi hizi zitakavyojulikana, ndivyo watakavyopata wanunuzi wengi zaidi.”—Ibid., b. 8, ch. 6. Kwa njia hiyo nuru iliweza kuingia.PKSw 132.2

    Wakati Mungu anapoandaa kuvunja vifungo vya ujinga na ushirikina, ndipo Shetani hufanya kazi kwa nguvu nyingi zaidi kuwafunika watu kwa giza na kuwafunga minyororo kwa nguvu zaidi. Watu walipokuwa wakiinuka katika nchi mbalimbali kuwaletea watu ujumbe wa msamaha na kuhesabiwa haki kwa njia ya damu ya Kristo, Roma aliendelea kwa nguvu mpya kufungua masoko yake katika nchi zote za Kikristo, kuuza msamaha kwa pesa.PKSw 132.3

    Kila dhambi ilikuwa na bei yake, na watu walipewa leseni ya bure kwa ajili ya uhalifu ikiwa hazina ya kanisa ilijazwa vizuri kwa pesa. Kwa hiyo, harakati mbili ziliendelea,—moja ikitoa msamaha wa dhambi kwa pesa, na nyingine msamaha kwa njia ya Kristo,—Roma ikitoa leseni ya dhambi na kufanya jambo hilo kuwa chanzo cha mapato; Wana matengenezo wakishutumu dhambi na kuwaelekeza watu kwa Kristo kama mpatanishi na mkombozi.PKSw 132.4

    Katika nchi ya Ujerumani kazi ya uuzaji wa vyeti vya msamaha walikabidhiwa watawa wa Kidominika na waliongozwa na Tetzel mkorofi. Katika nchi ya Switzerland biashara hiyo iliwekwa katika mikono ya Wafransiskani, chini ya uongozi wa Samson, mtawa Muitaliano. Samson alikuwa tayari amefanya kazi kubwa kwa kanisa, akiwa amepata fedha nyingi kutoka Ujerumani na Switzerland kujaza hazina ya papa. Sasa alitembelea nchi nzima ya Uswisi, akivutia makundi makubwa ya watu, akiwanyang'anya wakulima maskini mapato yao madogo, na akidai zawadi kubwa kutoka kwa matabaka ya kitajiri. Lakini mvuto wa matengenezo tayari ulikuwa umegusa watu wengi na ulipunguza, japokuwa haukukomesha kabisa, biashara hiyo. Zwingli alikuwa bado yuko Einsiedeln wakati Samson, mara tu baada ya kuingia Switzerland, alifika na vyombo vyake katika mji jirani. Baada ya kuambiwa kusudio la ujio wa Samson, Mwana matengenezo alianza mara moja kumpinga. Hao watu wawili hawakukutana, lakini Zwingli alifanikiwa kuanika uongo wa Samson kiasi kwamba Samson alilazimika kuondoka na kwenda maeneo mengine.PKSw 133.1

    Akiwa Zurich, Zwingli alihubiri kwa bidii dhidi ya wafanya biashara wa misamaha; na wakati Samson alipokaribia mji ule, alikutana na mjumbe kutoka katika baraza akiwa na ujumbe wa Samson kuwa Samson alitarajiwa kupita na kuendelea na safari yake. Hata hivyo Samson alifanikiwa kuingia mjini kwa ujanja, lakini alifukuzwa kutoka katika mji bila kuuza hata msamaha mmoja, na mara baada ya hapo aliondoka katika nchi ya Uswisi.PKSw 133.2

    Matengenezo yaliongezwa nguvu zaidi na ujio wa tauni, au Mauti Kuu, ambayo ilienea katika nchi nzima ya Uswisi katika mwaka 1519. Watu walipokutana uso kwa uso na mwuaji, wengi waliongozwa kujisikia jinsi misamaha waliyokuwa wameinunua hivi karibuni ilivyokuwa haina thamani na ilivyokosa maana; na walitamani kupata msingi wa uhakika zaidi kwa imani zao. Zwingli akiwa Zurich alipigwa na tauni kali sana; alizidiwa sana kiasi kwamba matumaini yote ya kupona kwake yaliisha kabisa, na taarifa ilienea kuwa alikuwa amekufa. Katika saa ile ya kujaribiwa, tumaini lake na ujasiri wake havikutetereka. Aliutazama msalaba wa Kalwari kwa imani, akitumainia upatanisho kamili kwa ajili ya dhambi. Aliporudi kutoka karibu na malango ya mauti, alikuwa na kazi moja tu ya kuihubiri injili kwa nguvu zaidi kuliko wakati wote uliopita; na maneno yake yalikuwa na nguvu isiyokuwa ya kawaida. Watu walimkaribisha kwa furaha mchungaji wao mpendwa, aliyerudishwa kwao kutoka ukingoni mwa kaburi. Wao wenyewe walikuwa wametoka kuhudumia wagonjwa na waliokuwa wanakufa, na walihisi, zaidi kuliko wakati mwingine wowote uliopita, thamani ya injili.PKSw 133.3

    Zwingli alikuwa amefikia uelewa mkamilifu zaidi wa ukweli wa injili, na alikuwa amepata uzoefu mkamilifu zaidi ndani yake wa nguvu ya injili inayobadilisha. Kuanguka kwa mwanadamu na mpango wa wokovu yalikuwa masomo aliyochukua muda mwingi kujifunza. “Ndani ya Adamu,” alisema, “sisi sote tumekufa, tumezama katika ufisadi na tumehukumiwa.”— Wylie, b. 8, ch. 9. “Kristo ... alinunua kwa ajili yetu ukombozi usioisha.... shauku Yake ni ... kafara ya milele, na uwezo usiokoma wa kuponya; inakidhi haki ya Kimungu ya milele kwa niaba ya wote wanaoitegemea kwa imani thabiti na isiyoyumba.” Hata hivyo alifundisha kwa uwazi kuwa siyo, kwa sababu ya neema ya Kristo, hawako huru kuendelea katika dhambi. “Mahali palipo na imani kwa Mungu, hapo yupo Mungu; na popote Mungu alipo, hapo kuna juhudi inayosihi na inayoshurutisha watu kutenda matendo mema.”— D'Aubigne, b. 8, ch. 9.PKSw 134.1

    Shauku kwa ajili ya mahubiri ya Zwingli ilikuwa kubwa kiasi kwamba kanisa lilijaa hadi kufurika watu waliokuja kumsikiliza. Kidogo kidogo, kwa kadiri walivyoweza kuelewa, alifunua ukweli kwa wasikilizaji. Alikuwa mwangalifu kuanza kufundisha vipengele ambavyo vingewashtua na kuzalisha upinzani. Kazi yake ilikuwa kuongoa mioyo yao ipokee mafundisho ya Kristo, kuwalainisha kwa upendo Wake, na kuweka mbele yao mfano Wake; na baada ya kupokea kanuni za injili, imani na matendo ya ushirikina vingeshindwa hatimaye.PKSw 134.2

    Hatua kwa hatua Matengenezo yalipanuka katika jiji la Zurich. Katika hali ya tahadhari maadui zake waliamka na kuanzisha upinzani. Mwaka mmoja kabla, mtawa wa Wittenberg alikuwa amesema “Hapana” kwa papa na mfalme pale Worms, na sasa kila kitu kilionekana kuonesha kuhimili madai ya upapa pale Zurich. Mashambulizi mengi yalifanywa dhidi ya Zwingli. Katika maeneo ya upapa, mara kwa mara, wanafunzi wa injili waliuawa juu ya mti wenye ncha kali, lakini hii ilikuwa haitoshi; mwalimu wa uzushi lazima anyamazishwe. Hali kadhalika askofu wa Constance alituma wajumbe watatu wa Baraza la Zurich, akimshtaki Zwingli kwa kufundisha watu kuvunja sheria za kanisa, na hivyo kuhatarisha amani na utengemano katika jamii. Ikiwa mamlaka ya kanisa itapuuzwa, alisisitiza, uasi utatokea duniani kote. Zwingli alijibu kuwa amekuwa kwa miaka minne akifundisha injili katika jiji la Zurich, “ambayo imekuwa na ukimya na amani zaidi kuliko mji mwingine wowote katika shirikisho.” “Siyo, kwamba,” alisema, “Ukristo ni uhakikisho bora zaidi wa usalama kwa jumla?”—Wylie, b. 8, ch. 11.PKSw 134.3

    Manaibu walikuwa wamewashauri wanabaraza waendelee kuwemo kanisani, ambamo, walisema, kulikuwa hakuna wokovu. Zwingli alijibu: “Hebu mashtaka haya yasiwatetemeshe. Msingi wa kanisa ni Mwamba ule ule, Kristo yule yule, ambao ulimpa Petro jina lake kwa sababu alimkiri kwa uaminifu. Katika kila taifa kila amwaminiye kwa moyo wake wote katika Bwana Yesu anakubaliwa na Mungu. Hapa, kwa kweli, ni kanisa, ambamo hakuna hata mmoja anayeweza kuokolewa.”—D'Aubigne, London ed., b. 8, ch. 11. Kama matokeo ya mkutano huo, mmoja wa manaibu wa askofu aliipokea imani ya matengenezo.PKSw 134.4

    Baraza lilikataa kuchukua hatua dhidi ya Zwingli, na Roma ilijiandaa kwa ajili ya mashambulizi mapya. Mwanamatengenezo alipojulishwa kuhusu mipango ya adui zake, alisema: “Acha waje; ninawaogopa kama vile mwamba uliotokeza juu ya bahari unavyoogopa mawimbi yanayounguruma kwenye nyayo zake.”—Wylie, b. 8, ch. 11. Juhudi za viongozi wa kanisa zilisukuma mbele zaidi kazi ambayo walikuwa wakitafuta kuiangusha. Ukweli uliendelea kusambaa. Katika nchi ya Ujerumani, wafuasi wake, wakiwa wamenyong'onyea kwa sababu ya kutoweka kwa Luther, walipata ujasiri tena, walipoona maendeleo ya injili katika nchi ya Uswisi. Matengenezo yalipoimarika katika jiji la Zurich, matunda yake yalionekana kikamilifu katika kupungua kwa uhalifu na ongezeko la utulivu na utengamano.” Amani imejaa tele katika mji wetu,” aliandika Zwingli; “hakuna ugomvi, hakuna unafiki, hakuna wivu, hakuna migogoro. Wapi umoja kama huo unaweza kupatikana kama siyo kwa Bwana, na mafundisho yetu, yanayotujaza kwa matunda ya amani na upendo?” (Ibid., b. 8, ch. 15).PKSw 135.1

    Ushindi ambao Matengenezo yaliupata uliwatetemesha viongozi wa Roma na kuwafanya waongeze juhudi za kuyashinda. Wakiona jinsi ambavyo mateso yalifaulu kidogo sana kudhibiti kazi ya Luther katika nchi ya Ujerumani, waliamua kupambana na matengenezo kwa kutumia salaha za wana matengenezo wenyewe. Walipanga kuwa na mdahalo na Zwingli, na kwa kuwa wao ndio waliosimamia mdahalo huo, wangejihakikishia ushindi kwa kuchagua, wao wenyewe, siyo tu mahali pa kufanyia mdahalo, bali pia waamuzi ambao wangeamua kati ya wao na Zwingli. Na ikiwa wangemnasa Zwingli na kumweka chini ya mamlaka yao, wangehakikisha kuwa haponyoki. Ikiwa kiongozi angenyamazishwa, harakati ingevunjika mara moja kirahisi. Kusudi hili, hata hivyo, lilifichwa kwa uangalifu.PKSw 135.2

    Mdahalo ulipangwa kufanyika katika mji wa Baden; lakini Zwingli hakuwepo. Baraza la Zurich, kwa kuhisi njama za wafuasi wa upapa, na kuonywa na marundo ya kuni ambazo zilikuwa zimekwisha washwa moto katika majimbo ya upapa kwa ajili ya wafuasi wa injili, walimkataza mchungaji wao asijipeleke katika hatari hii. Mjini Zurich alikuwa tayari kukutana na wafuasi ambao Roma ingepeleka; lakini kwenda Baden, mahali ambapo damu ya wafia dini kwa ajili ya ukweli ilikuwa imemwagwa siku za karibuni, ilikuwa kwenda katika kifo cha hakika. Okolampadio na Halla walichaguliwa kuwakilisha Wanamatengenezo, wakati Dkt. Eck, mtu mashuhuri, akisaidiwa na jopo la wasomi madaktari na maaskofu, ndiye alikuwa mwakilishi wa Roma.PKSw 135.3

    Ingawa Zwingli hakuwepo katika mdahalo, nguvu yake ilihisiwa. Makatibu mhutasi wote walichaguliwa na wafuasi wa papa, na wengine walikatazwa wasiandike cho chote, kwa tishio la kifo. Pamoja na hayo, Zwingli alipokea kila siku maelezo kamili ya kile kilichosemwa kule Baden. Mwanafunzi aliyehudhuria kwenye mdahalo aliandika kila siku juu ya hoja zote zilizowasilishwa siku hiyo. Karatasi hizi zilipelekwa na wanafunzi wengine wawili, pamoja na barua za kila siku za Okolampadio, kwa Zwingli jijini Zurich. Mwanamatengenezo alijibu, akitoa ushauri na mapendekezo. Barua zake ziliandikwa usiku, na wanafunzi walirudi nazo Badeni asubuhi. Kukwepa kukamatwa na walinzi waliowekwa kulinda katika malango ya jiji, wajumbe hawa walileta makapu ya kuku vichwani mwao, na waliruhusiwa kupita bila kikwazo.PKSw 136.1

    Kwa njia hiyo Zwingli aliendeleza vita na wapinzani wake. Zwingli “amefanya kazi zaidi,” alisema Mikonio, “kwa kutafakari kwake, kukesha usiku, na ushauri alioupeleka Baden, kuliko ambavyo angefanya kwa kujadiliana uso kwa uso katikati ya maadui zake.”—D'Aubigne, b. 11, ch. 13.PKSw 136.2

    Wafuasi wa Roma, wakiwa na matumaini makubwa ya kushinda, walikuja Baden wakiwa wamevaa majoho ya kifahari na wakimeremeta kwa vito vya thamani. Walikula kianasa, meza zao zilifurika vyakula vinono vya gharama kubwa na pombe kali na za bei kubwa. Mzigo wa majukumu yao ya kikanisa ulipunguzwa kwa burudani na sherehe. Mwonekano wa Wanamatengenezo ulikuwa kinyume kabisa, walionekana mbele ya watu kama kundi la omba omba, ambao chakula chao kidogo na cha kimaskini kiliwafanya wakae mezani kwa muda mfupi. Baba mwenye nyumba wa Okolampado, alipokwenda kumwangalia katika chumba chake, alimkuta mara nyingi akisoma au akiomba, na kwa mshangao mkubwa, alisema kuwa mzushi alikuwa angalau “mcha Mungu sana.”PKSw 136.3

    Kwenye mdahalo, “Kwa kiburi Eck alipanda kwenye mimbari iliyopambwa kifahari, wakati maskini Okolampadio, akiwa amevaa nguo za kimaskini, alilazimishwa kukaa mbele ya mpinzani wake kwenye kigoda kilichochongwa vibaya-vibaya.”—Ibid., b. 11, ch. 13. Sauti kubwa ya Eck na kujiamini kusikokuwa na mipaka havijawahi. Juhudi zake zilichochewa na tumaini la utajiri na umaarufu; kwa kuwa mtetezi wa imani alipewa malipo makubwa. Wakati hoja nzuri zaidi ziliposhindwa, alipaswa kutumia matusi, na hata laana.PKSw 136.4

    Okolampadio, mtu mnyenyekevu na asiyejitumainia, alikuwa ameogopa mdahalo, na aliuingia akiwa na kiapo cha nguvu kuwa: “Sikubali kiwango kingine cha uamuzi zaidi ya neno la Mungu.”—Ibid., b. 11, ch. 13. Ingawa alikuwa mpole na muungwana katika tabia, alithibitika kuwa na uwezo na asiyetetereka. Wakati wafuasi wa Uroma, kwa mujibu wa mazoea yao, walijielekeza kwenye mamlaka ya desturi za kanisa, Mwanamatengenezo alishikilia kikamilifu Maandiko matakatifu. “Desturi,” alisema, “hazina nguvu katika nchi yetu ya Switzerland, labda tu kama zitaendana na katiba; sasa, katika masuala ya imani, Biblia ndiyo katiba yetu.”— Ibid., b. 11, ch. 13.PKSw 136.5

    Tofauti iliyojitokeza kati ya hawa washindani wawili wa mdahalo haikukosa kuwa na matokeo. Hoja ya Mwanamatengenezo iliyotolewa kwa utulivu, uwazi, upole na uungwana, ilikuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa akili zilizokuwa zimechukizwa na maneno ya majigambo na kujikweza ya Eck.PKSw 137.1

    Mdahalo uliendelea kwa siku kumi na nane. Ulipofungwa wafuasi wa upapa kwa kujiamini walidai kuwa wameshinda. Wengi wa manaibu waliungana na Roma, na Baraza Kuu lilitangaza kuwa Wanamatengenezo wamekwisha na walitangaza kuwa wao, pamoja na Zwingli, kiongozi wao, walikuwa wametengwa na kanisa. Lakini matunda ya mdahalo yalidhihirisha ni nani hasa walionufaika kutokana na mdahalo huo. Shindano lile lilizalisha ari kubwa katika kazi ya Uprotestanti, na haukupita muda mrefu baadaye majiji muhimu ya Bern na Basel yalitangaza kuunga mkono Matengenezo. PKSw 137.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents