Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 6—Huss na Jerome

    Injili ilipandwa katika nchi ya Bohemia mapema katika karne ya tisa. Biblia ilitafsiriwa, na ibada ya wazi iliendeshwa, katika lugha ya watu. Lakini kadiri nguvu ya papa ilivyoongezeka, ndivyo neno la Mungu lilivyofichika. Gregori VII, aliyekuwa amedhamiria kuwanyenyekesha wafalme wenye kiburi, alikusudia pia kuwafanya watu kuwa watumwa wake, na wakati huo huo amri ilitolewa kupiga marufuku ibada ya hadhara kuendeshwa katika lugha ya Kibohemia. Papa alitangaza kuwa “inampendeza Mungu Mwenyezi kuwa ibada Yake iendeshwe katika lugha isiyoeleweka, na kwamba uovu na uzushi mwingi umeibuka kwa kutokuzingatia kanuni hii.”— Wylie, b. 3, ch. 1. Hivyo Rumi iliagiza kuwa nuru ya neno la Mungu ilipaswa izimwe na watu iliwapasa wafungiwe gizani. Lakini Mbingu ilikuwa imeweka mawakala wengine kwa ajili ya kuhifadhi kanisa. Wengi wa Wawaldensia na Waalbigensia, waliofukuzwa na mateso kutoka katika nyumba zao katika nchi ya Ufaransa na Italia, walikuja Bohemia. Japokuwa hawakuthubutu kufundisha kwa uwazi, walifanya kazi kwa siri. Kwa njia hiyo imani ya kweli ilihifadhiwa kutoka karne moja hadi moja.PKSw 70.1

    Kabla ya siku za Huss kulikuwepo watu katika nchi ya Bohemia walioinuka na kukemea wazi ufisadi katika kanisa na ubadhirifu wa watu. Kazi zao ziliamsha shauku katika maeneo mengi. Hofu za Kanisa la Roma ziliamshwa, na mateso yalianzishwa dhidi ya wanafunzi wa injili. Wakiwa wamelazimishwa kuabudu katika misitu na milima, waliwindwa na maaskari, na wengi waliuawa. Baada ya muda iliamriwa kuwa wote walioacha ibada ya Kiroma inapasa wachomwe moto. Lakini wakati Wakristo walisalimisha maisha yao, walitazamia ushindi wa msimamo wao. Mmoja wa wale “waliofundisha kwamba wokovu ulipatikana kwa imani tu kwa Mwokozi aliyesulubiwa,” alitamka wakati wa kufa: “Hasira ya maadui wa ukweli sasa inawaka dhidi yetu, lakini haitakuwa ya milele; atainuka mmoja miongoni mwa watu wa kawaida, bila upanga au mamlaka, na watapigana dhidi yake lakini hawatamshinda.”—Ibid., b. 3, ch. 1. Wakati wa Luther ulikuwa bado uko mbali; lakini tayari mmoja alikuwa akiinuka, ambaye ushuhuda wake dhidi ya Roma ungetikisa mataifa.PKSw 70.2

    John Huss alizaliwa katika familia maskini, na katika miaka ya awali aliachwa yatima kwa kifo cha baba yake. Mama yake mcha Mungu, kwa kuthamini elimu na kicho cha Mungu kama raslimali za thamani sana, alitafuta kumpa mwanawe urithi huu. Huss alisoma katika shule ya jimbo, na ndipo akajiunga na chuo kikuu cha Prague, ambapo alidahiliwa kwa ufadhili. Alisindikizwa kwenda Prague na mama yake; ambaye alikuwa mjane na maskini, hakuwa na zawadi za utajiri wa kidunia za kumpa mwanawe, lakini walipokaribia jiji kubwa, alipiga magoti kando ya kijana asiyekuwa na baba yake na kumwombea baraka kutoka kwa Baba yao wa mbinguni. Mama alijua kidogo sana jinsi ambavyo ombi lake lingekuja kujibiwa.PKSw 70.3

    Akiwa chuoni, mara moja Huss alijitambulisha kwa juhudi zisizochoshwa na maendeleo ya kasi, wakati maisha yake yasiyolaumika na ya uungwana, na haiba inayogusa watu vilimpa heshima kwa watu wote. Alikuwa muumini mwaminifu wa Kanisa la Roma na mtafutaji wa dhati wa baraka za kiroho ambazo Kanisa linaahidi kuzitoa. Katika tukio la jubilee Huss alikwenda kuungama, alilipa sarafu za mwisho kutoka katika hazina yake ndogo, na alijiunga katika misafara, ili aweze kushiriki katika msamaha ulioahidiwa. Baada ya kumaliza kozi yake ya chuo kikuu, aliingia upadre, na akipata umaarufu upesi, mara moja alishikamanishwa na nyumba ya mfalme. Alifanywa pia kuwa profesa na baadaye paroko wa chuo kikuu alipopatia elimu yake. Katika miaka michache mwanafunzi maskini mfadhiliwa alikuwa mtu wa kujivunia katika nchi yake, na jina lake lilijulikana katika Ulaya yote.PKSw 71.1

    Lakini Huss alianzia kazi ya matengenezo katika uwanja mwingine. Miaka kadhaa baada ya upadirisho alichaguliwa kuwa mhubiri wa kanisa la Bethlehemu. Jambo la muhimu kuzingatia hapa, mwasisi wa kanisa hili aligeuka kuwa mtetezi wa mahubiri ya Maandiko katika lugha ya watu. Licha ya upinzani dhidi ya mtindo huu wa mahubiri yanayotokana na Biblia, haukuwa umesimamishwa kabisa katika nchi ya Bohemia. Lakini watu hawakuwa na elimu ya Biblia, na maovu makubwa yalishamiri miongoni mwa watu wa matabaka yote. Huss alikemea bila hofu maovu hayo, akitumia neno la Mungu kuimarisha kanuni za ukweli na usafi aliouhimiza.PKSw 71.2

    Mkazi wa Prague, Jerome, ambaye baadaye alikuja kuwa karibu sana na Huss, aliporudi kutoka Uingereza, alileta maandishi ya Wycliffe. Malkia wa Uingereza, ambaye alikuwa mwongofu wa mafundisho ya Wycliffe, alikuwa binti wa mfalme wa Bohemia, na kwa mvuto wake pia kazi za Mwanamatengenezo zilisambazwa katika maeneo mengi ya nchi yake alikozaliwa. Huss alisoma maandishi haya kwa shauku kubwa; aliamini mwandishi wa maandishi yale alikuwa Mkristo wa kweli na Huss alichukua mwelekeo wa kuyakubali mafundisho ya Wycliffe. Tayari, japokuwa alijua hivyo, Huss alikuwa ameshika njia ambayo ingempeleka mbali sana na Roma.PKSw 71.3

    Karibu na wakati huu watu wawili walifika Prague kutoka Uingereza, wasomi, waliokuwa wamepokea nuru na walikuwa wamekuja kueneza nuru hiyo katika nchi hii ya mbali. Wakianza na shambulizi la wazi dhidi ya ukuu wa papa, mamlaka ziliwanyamazisha mara moja; lakini kwa kutokuwa tayari kukubali kuacha lengo lao, walitafuta njia zingine. Kwa kuwa walikuwa wanasanaa na wahubiri, waliendelea kwa kutumia sanaa yao. Katika eneo la wazi walichora picha mbili. Moja ilimwakilisha Kristo akiingia Yerusalemu, “mnyenyekevu, na akiwa ameketi juu ya mwanapunda” (Mathayo 21:5), na akifuatwa na wanafunzi Wake wakiwa wamevaa nguo zilizochakaa kwa sababu ya safari na wakiwa na miguu isiyokuwa na viatu. Picha nyingine ilionesha msafara wa papa—papa akiwa amevalia majoho ya kitajiri na taji tatu, akiwa amekaa juu ya farasi aliyepambwa kwa mapambo ya gharama kubwa, akiwa ametanguliwa na wapiga tarumbeta na akiwa amefuatwa na makadinali na maaskofu waliovalia mavazi yanayomeremeta.PKSw 71.4

    Hapa kulikuwa na hubiri lililovuta hisia za watu wa matabaka yote. Makundi makundi makubwa ya watu yalikuja kuangalia michoro hii. Hakuna hata mtu mmoja aliyeshindwa kuelewa fundisho la michoro hiyo, na wengi waliguswa sana na tofauti kati ya upole na unyenyekevu wa Kristo Bwana na kiburi na majivuno ya papa, aliyedai kuwa mtumishi wa Kristo. Kulikuwa na taharuki kubwa mjini Prague, na wageni baada ya muda mfupi waliona umuhimu, kwa ajili ya usalama wao, wa kuondoka pale. Zile picha ziligusa sana akili za Huss na zilimsukuma kujifunza kwa makini zaidi Biblia na maandishi ya Wycliffe. Japokuwa hakuwa taari, mpaka wakati huo, kupokea matengenezo yote yaliyofundishwa na Wycliffe, aliona kwa uwazi zaidi tabia halisi ya upapa, na kwa juhudi kubwa alikemea kiburi, tamaa, na ufisadi wa mfumo wa upapa.PKSw 72.1

    Kutoka katika nchi ya Bohemia nuru ilisambaa katika nchi ya Ujerumani, kwani machafuko katika Chuo Kikuu cha Prague yalisababisha mamia ya wanafunzi kutoka Ujerumani kuondoka. Wengi wao walikuwa wameshapokea mafundisho ya awali ya Biblia, na waliporudi nyumbani walieneza injili katika nchi yao.PKSw 72.2

    Habari za kazi iliyofanyika kule Prague ilipelekwa Roma, na Huss aliitwa kujibu mashtaka mbele ya papa. Kutii wito huo kulimaanisha kifo moja kwa moja. Mfalme na malkia wa Bohemia, chuo kikuu, waheshimiwa wasaidizi wakuu wa mfalme, na maofisa wa serikali wote waliungana pamoja kutoa wito kwa papa kuwa Huss aruhusiwe kubaki Prague na ajibu mashtaka yake kupitia kwa mwakilishi wa Roma. Badala ya kukubali ombi hili, papa aliendelea na kusikiliza shtaka na kutoa hukumu ya Huss, na ndipo alitangaza kuwa jiji la Prague lilikuwa limefungiwa.PKSw 72.3

    Katika zama zile hukumu kama hii, ilipotolewa, ilileta hofu kubwa kwa watu wengi. Hatua zilizoambatana na hukumu hii zilibuniwa kuzalisha hofu kubwa mioyoni mwa watu waliomwamini papa kuwa ni mwakilishi wa Mungu Mwenyewe, aliyeshikilia funguo za mbingu na kuzimu, na aliyekuwa na mamlaka ya kutamka hukumu za hapa duniani na za kiroho. Iliaminika kuwa milango ya mbinguni ilifungwa dhidi ya eneo lililohukumiwa kufungiwa; kuwa mpaka pale ambapo papa angependezwa kuondoa kufungiwa huko, waliokufa walikuwa wakifungiwa nje ya makao ya amani. Kama ishara ya janga hili la kutisha, huduma zote za dini zilisitishwa. Makanisa yalifungiwa. Ndoa zilifungiwa katika viwanja vya makanisa. Wafu, kwa kunyimwa mazishi katika maeneo yaliyowekwa wakfu, walizikwa, bila kaida za mazishi, katika mitaro au mashamba. Hivyo basi, kwa hatua hizi zilizogusa fikra za watu, Roma ilifanikiwa kutawala dhamiri za watu.PKSw 72.4

    Jiji la Prague liliingia katika machafuko makubwa. Kundi kubwa la watu walimlaumu Huss kama chanzo cha majanga yao yote na walidai kuwa akabidhiwe kwa mamlaka za Roma ili kisasi cha kanisa kichukue mkondo wake. Kutuliza dhoruba, Mwanamatengenezo aliondoka kwa muda kwenda kukaa kijijini kwake alikozaliwa. Akiwaandikia marafiki zake aliowaacha pale Prague, alisema: “Ikiwa nimetoweka kutoka katikati yenu, ni ili nifuate kanuni na mfano wa Yesu Kristo, nisitoe nafasi kwa watu wenye nia mbaya kujiletea hukumu ya milele juu yao, na ili nisiwe chanzo cha usumbufu na mateso kwa watakatifu. Nimepumzika pia kwa sababu ya hofu kuwa mapadre waovu wasiendelee kuzuia kazi ya kuhubiri neno la Mungu miongoni mwenu; lakini sikuondoka ili ninyi muukane ukweli wa neno la Mungu, ambao kwa ajili yake, kwa msaada wa Mungu, niko tayari kufa.”—Bonnechose, The Reformers Before the Reformation, vol. 1, uk. 87. Huss hakuacha kufanya kazi zake, lakini alisafiri katika maeneo yote ya nchi jirani, akihubiri injili kwa watu waliokuwa na shauku. Hivyo hatua ambazo papa alijielekeza kuzitumia kukandamiza injili zilikuwa zikiiwezesha kusambaa zaidi. “Maana hatuwezi kutenda neno lo lote kinyume cha kweli, bali kwa ajili ya kweli” (2 Wakorintho 13:8).PKSw 73.1

    “Akili ya Huss, katika hatua hii ya kazi yake, ingeonekana kuwa mandhari ya mgogoro wenye maumivu. Ingawa kanisa lilikuwa likitafuta kumshinda kwa kutumia vitisho, Huss hakuwa ameacha kutambua mamlaka yake. Kanisa la Roma lilikuwa bado mke wa Kristo, na papa alikuwa mwakilishi na msadizi wa karibu wa Mungu. Huss alikuwa akipiga vita dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka, na siyo kanuni yenyewe. Jambo hili lilileta mgogoro wa kutisha kati ya imani ya uelewa wake na madai ya dhamiri yake. Ikiwa mamlaka ya kanisa ilikuwa ya haki na isiyokosea, kama alivyoamini kuwa hivyo, ilikuwaje tena ajisikie kulazimika kutoitii mamlaka yenyewe? Aliona kuitii ni kutenda dhambi; lakini kwa nini utii kwa kanisa lisilokosea limfanye kujisikia kutenda dhambi? Hili lilikuwa tatizo lililomshinda kutanzua; haya yalikuwa mashaka yaliyomtesa saa hadi saa. Suluhisho lililoelekea kumsaidia lilikuwa kwamba jambo lile lilikuwa limejirudia tena, kama ilivyowahi kutokea zamani katika siku za Mwokozi, kuwa viongozi wa kanisa walikuwa wameharibika na kuwa waovu na walikuwa wakitumia mamlaka halali kukidhi malengo yasiyokuwa halali. Wazo hili alilifanya kuwa mwongozo wake, na aliwahubiria wengine wazo hilo liwe mwongozo wao, msemo kuwa kanuni za Maandiko, zilizopatikana kwa njia ya uelewa, zinapaswa kutawala dhamiri; kwa maneno mengine, kwamba Mungu akizungumza katika Biblia, na siyo kanisa likisema kupitia upapa, ndiyo mwongozo pekee usiokosea.”—Wylie, b. 3, ch. 2.PKSw 73.2

    Baada ya vurugu katika jiji la Prague kutulia, Huss alirudi katika kanisa lake la Bethlehemu, kuendelea kwa juhudi na ujasiri mkubwa kuhubiri neno la Mungu. Maadui zake walikuwa kazini na walikuwa na nguvu, lakini malkia na wengi wa waheshimiwa wasaidizi wa karibu wa mfalme walikuwa marafiki zake, na watu wengi walisimama upande wake. Wakilinganisha mafundisho safi na yanayoinua na maisha matakatifu dhidi ya mafundisho yanayodhalilisha yasiyokosolewa yaliyohubiriwa na viongozi wa Roma, na tamaa ya mali na uovu walioufanya, wengi waliona kuwa heshima kuwa upande wa Huss.PKSw 74.1

    Hadi wakati huo, Huss alikuwa amesimama peke yake katika kazi zake; lakini sasa Jerome, ambaye wakati akiwa Uingereza aliyakubali mafundisho ya Wycliffe, alijiunga na kazi ya matengenezo. Tangu wakati huo na siku zilizofuata watu hawa wawili waliunganisha maisha yao, na katika kifo hawakupaswa kutengana. Uwezo wa kiakili, ufasaha na elimu—karama zinazowezesha mtu kukubaliwa na wengi—zilimilikiwana kwa kiwango kikubwa na Jerome; lakini katika zile sifa zinazounda nguvu ya tabia, Huss alikuwa juu zaidi. Maamuzi yake yaliyotulia yalisaidia kudhibiti roho yenye harara ya Jerome, ambaye, kwa unyenyekevu wake wa kweli, alielewa mantiki yake, na alijisalimisha kwa ushauri wake. Kwa kazi zao zilizounganishwa pamoja, matengenezo yalienea kwa haraka.PKSw 74.2

    Mungu aliruhusu nuru kubwa iangazie akili za watu hawa waliochaguliwa, ikiwafunulia makosa mengi ya Roma; lakini hawakupokea nuru yote iliyopaswa kutolewa kwa ulimwengu. Kwa njia ya hawa, watumishi Wake, Mungu alikuwa akiwaongoza watu kutoka katika giza la Uroma; lakini vilikuwepo vikwazo vingi na vikubwa ambavyo viliwakabili, na aliwaongoza kusonga mbele, hatua kwa hatua, kwa kadiri walivyoweza kubeba. Hawakuwa tayari kupokea nuru yote kwa mara moja. Kama mwanga mkali wa jua la mchana kwa watu ambao wamekaa kwa muda mrefu gizani, ingeweza, kama ingeruhusiwa kuwaangazia, ingeweza kuwafanya wageukie upande mwingine. Kwa hiyo aliifunua nuru kwa viongozi kidogo kidogo, kwa kadiri watu walivyoweza kuipokea. Kutoka karne moja hadi karne nyingine, watendakazi wengine waaminifu walipaswa kufuata, kuwaongoza watu kusonga mbele zaidi katika njia ya matengenezo.PKSw 74.3

    Mpasuko katika kanisa uliendelea. Mapapa watatu walikuwa wakigombania madaraka, na mgogoro wao ulijaza uhalifu na vurugu katika ulimwengu wote wa Kikristo. Kwa kutoridhishwa na kurushiana maneno ya laana, waligeukia matumizi ya silaha za kidunia. Kila mmoja wao alijielekeza kununua silaha na kupata askari. Ili kufanikisha suala hilo ilikuwa lazima pesa ipatikane; na ili kupata pesa, zawadi, vyeo, na baraka za kanisa vilikuzwa. (Tazama Kiambatisho.) Mapadre pia, wakiwaiga wakubwa wao, waligeukia matumizi ya nguvu na vita kuwanyenyekesha wapinzani wao na kuimarisha nguvu yao. Kwa ujasiri uliokuwa ukiongezeka kila siku Huss aliunguruma dhidi ya machukizo yaliyolelewa katika jina la dini; na watu waliwalaumu viongozi wa Uroma kama chanzo cha mateso yaliyogubika Ukristo.PKSw 74.4

    Kwa mara nyingine jiji la Prague lilionekana kuwa kwenye ukingo wa mgogoro na umwagaji damu. Kama ilivyokuwa katika vizazi vya zamani, mtumishi wa Mungu alishitakiwa kama “mtaabishaji wa Israeli” (1 Wafalme 18:17). Jiji lilifungiwa tena, na Huss alikwenda kujificha kijijini kwake alikozaliwa. Ushuhuda uliotolewa kwa uaminifu kutokea kanisa lake pendwa la Bethlehemu ulikomeshwa. Alikuwa anakwenda kuzungumza kutokea jukwaa pana zaidi, kwa ulimwengu wa Ukristo wote, kabla ya kusalimisha maisha yake kwa ajili ya kweli.PKSw 75.1

    Kutibu maovu yaliyokuwa yameshika usikivu wa watu wa Ulaya, baraza kuu liliitwa kukutana katika jiji la Constance. Baraza liliitwa kwa utashi wa mfalme Sigismund, kupitia kwa mmoja wa mapapa watatu waliokuwa wakisigana, ambaye alikuwa Yohana XXIII. Hitaji la kuwepo kwa baraza lilikuwa mbali kabisa na utashi wa Papa Yohana, ambaye tabia na sera yake isingefaa kutathminiwa, hata na maaskofu waliokuwa dhaifu kama walivyokuwa waumini wa kanisa wa nyakati zile. Hakuthubutu, hata hivyo, kupinga matakwa ya Sigismund (Tazama Kiambatisho).PKSw 75.2

    Malengo makuu yaliyokusudiwa kutimizwa na baraza yalikuwa kuponya utengano katika kanisa na kung'oa mizizi ya uzushi. Hivyo watu wawili waliokuwa wapinzani wa mapapa waliitwa kuja kujibu mashtaka mbele ya baraza hilo, akiwemo msambazaji mkuu wa hayo maoni mapya, John Huss. Mfalme Sigismund, kwa kuhofia usalama wake, hakuhudhuria yeye mwenyewe binafsi, lakini aliwakilishwa na wajumbe. Papa Yohana, wakati akionekana kuwa mwalikaji wa baraza, alikuja barazani akiwa na mashaka mengi, akishuku lengo la siri la mfalme la kumwondoa madarakani, na akihofia kuwajibishwa kwa maovu yaliyochafua cheo cha upapa, na uhalifu uliotumika kukipata. Hata hivyo aliingia katika jiji la Constance kwa mbwembwe sana, akisindikizwa na viongozi wa kanisa wa ngazi ya juu sana na msafara wa watendaji katika ofisi yake. Viongozi wote wa dini na jiji, pamoja na kundi kubwa la wakazi wa jiji, walikwenda kumlaki. Juu ya kichwa chake kulikuwepo mwavuli wa dhahabu, uliobebwa na majaji wakuu wanne. Mwenyeji alikuwa amebebwa mbele yake, na mavazi ya gharama ya makadinali na waheshimiwa vilitengeneza mandhari ya kuvutia sana.PKSw 75.3

    Wakati huo huo msafiri mwingine alikuwa akikaribia jiji la Constance. Huss alijua hatari zilizotishia maisha yake. Aliachana na marafiki zake kana kwamba hataweza kukutana nao tena, na alisonga mbele akihisi safari yake ilikuwa ikimpeleka kwenye ncha kali ya mti. Pamoja na hayo alikuwa amepata hakikisho la usalama kutoka kwa mfalme wa Bohemia, na alipata tena hakikisho la usalama kutoka kwa mfalme wa Sigismund akiwa katika safari yake, alifanya mipango yake yote akitazamia uwezekano wa kifo chake.PKSw 76.1

    Katika barua yake kwa marafiki zake wa Prague alisema: “Ndugu zangu, ... ninaondoka nikiwa na hakikisho la usalama kutoka kwa mfalme kwenda kukutana na maadui wengi na wanaokufa.... ninaweka tumaini langu lote kwa Mungu mweza wa yote, Mwokozi wangu; ninaamini atayasikia maombi yenu ya dhati, ili aweke maono na hekima katika mdomo wangu, ili kwamba niweze kuwapinga; na kwamba aniwezeshe kwa njia ya Roho Wake Mtakatifu kusimama imara katika ukweli, ili nikabiliane, kwa ujasiri, na majaribu, gereza, na, ikiwa lazima, na kifo cha kikatili.PKSw 76.2

    Yesu Kristo aliteseka kwa ajili ya wapendwa Wake aliowapenda sana; na hivyo, tushangae kuwa alituachia mfano Wake, ili na sisi tukabiliane kwa uvumilivu na mambo yote kwa ajili ya wokovu wetu? Yeye ni Mungu, na sisi ni viumbe Wake; Yeye ni Bwana, na sisi ni watumishi Wake; Yeye ni Bwana wa ulimwengu, na sisi ni wanadamu wenye hali ya kufa katika hali dhalili—na bado aliteseka! Kwa nini, hivyo basi, sisi tusiteseke pia, hususani kwa kuwa mateso kwetu ni utakaso? Kwa hiyo, wapendwa, ikiwa kifo changu kinaweza kuchangia kuleta utukufa Wake, ombeni ili kije haraka, na kwamba aniwezeshe kukabiliana na mikasa yangu yote bila kuyumba. Lakini ikiwa itakuwa bora nirudi kwenu, tuombe kwa Mungu kuwa nirudi bila doa—yaani, kwamba nisije nikaminya hata nukta moja ya ukweli wa injili, ili niwaachie ndugu zangu mfano mzuri wa kufuata. Pengine, hivyo basi, hamtauona uso wakngu tena hapa Prague; lakini ikiwa mapenzi ya Mungu yataruhusu kunirudisha, inatupasa kusonga mbele kwa moyo imara zaidi katika ujuzi na upendo wa sheria Yake.”—Bonnechose, vol. 1, uk. 147, 148.PKSw 76.3

    Katika barua nyingine, kwa kasisi aliyekuwa ameongoka na kuwa mfuasi wa injili, Huss alizungumzia kwa unyenyekevu mkubwa juu ya makosa yake, akijishitaki mwenyewe“kuhusiana na kuhisi raha ya kuvaa mavazi ya gharama kubwa na kuwapoteza muda katika kazi zisizokuwa na maana.” Ndipo aliongeza maonyo haya yanayogusa: “Hebu utukufu wa Mungu na wokovu wa roho ujaze akili yako, na siyo mali na mashamba. Jihadhari kuipamba nyumba yako kuliko roho yako; na, juu ya yote, jali jengo lako la kiroho. Uwe mtakatifu na mnyenyekevu na watu maskini, na usile chakula kwa ulafi. Ikiwa hutatengeneza maisha yako na kuachana na mambo ya juu juu, ninaogopa utapigwa sana kama mimi.... Wewe unayajua sana mafundisho yangu, kwa kuwa wewe umeyapokea maelekezo yangu tangu utoto wako; kwa hiyo sina haja ya kukuandikia tena. Lakini ninakusihi, kwa rehema ya Bwana wetu, usiniige kwa cho chote miongoni mwa mambo yasiyofaa ambamo umeona kuwa nimetumbukia.” Juu ya bahasha ilimokuwa barua hiyo aliongeza maneno haya: “Ninakusihi, rafiki yangu, usiichane bahasha hii mpaka umepata cheti cha uthibitisho kuwa nimekufa.”—Ibid., vol. 1, uk. 148, 149.PKSw 76.4

    Katika safari yake, Huss aliona kila mahali alama za kusambaa kwa mafundisho yake na jinsi kazi yake ilivyoungwa mkono. Watu walijikusanya kumlaki, na katika baadhi ya miji, mahakimu walijitokeza kuwa naye kwenye mitaa yao.PKSw 77.1

    Alipowasili katika jiji la Constance, Huss alipewa uhuru kamili. Pamoja na hakikisho la usalama kutoka kwa mfalme, kuliongezeka hakikisho la ulinzi binafsi wa papa. Lakini, kinyume na ahadi hizi za usalama zilizotolewa kwa matamko ya dhati na kwa kurudia rudia, Mwanamatengenezo alikamatwa baada ya muda mfupi, kwa amri ya papa na makadinali, na alitupwa katika gereza la kuchukiza. Baadaye alihamishiwa katika jumba moja ng'ambo ya mto Rhine na huko alishikiliwa kama mfungwa. Papa, akifaidi kidogo sana kutokana na hila yake, naye baada ya muda mfupi alitupwa katika gereza lile lile. Ibid., vol. 1, uk. 247. Alithibitika mbele ya baraza kuwa na hatia ya uhalifu wa kutisha, mbali na mauaji, utoaji wa hongo ili kupata cheo kanisani, na uzinzi, “dhambi zisizostahili kutajwa.” Hivyo ndivyo baraza lenyewe lilivyotangaza, na hatimaye alivuliwa kofia ya upapa na alitupwa gerezani. Na wapinzani wa upapa pia waliondolewa madarakani, na papa mpya alichaguliwa.PKSw 77.2

    Ingawa papa mwenyewe alikuwa na hatia ya kutenda uhalifu mkubwa zaidi kuliko hata Huss alivyokuwa amewatuhumu makasisi, na ambao Huss alikuwa akidai ufanyiwe matengenezo, hata hivyo baraza lile lile lililomdhalilisha papa liliendelea kumkandamiza Mwanamatengenezo. Kufungwa kwa Huss kuliamsha hasira kali katika nchi ya Bohemia. Watu waungwana wenye nguvu walipeleka malalamiko kwenye baraza dhidi ya ukatili huu mkubwa. Mfalme, ambaye alichukia kwa kuruhusu ukiukwaji wa hakikisho la usalama, alipinga hatua hiyo ya mashitaki dhidi yake. Lakini maadui wa Mwanamatengenezo walikuwa waovu na walikuwa wamedhamiria. Walijitahidi kumshawishi mfalme awaunge mkono wakijaribu kupata fadhila yake, na kumtia hofu, wakimhamasisha kuwa upande wa kanisa. Walitoa hoja nyingi kuthibitisha kuwa“imani haipaswi kuchanganywa na wazushi, wala watu wanaotuhumiwa kuwa wazushi, hata kama wamepewa hati za hakikisho la usalama kutoka kwa mkuu wa dola au wafalme wa kawaida.”—Jacques Lenfant, History of the Council of Constance, vol. 1, p. 516. Hatimaye walishinda.PKSw 77.3

    Akiwa amedhoofika kwa sababu ya ugonjwa na kifungo,—kwa sababu ya hewa nzito na unyevunyevu wa gereza alipata homa ambayo karibu ikatishe uhai wake,— Huss hatimaye alifikishwa mbele ya baraza. Akiwa na mzigo mzito wa minyororo alisimama mbele ya mfalme, ambaye heshima na nia yake nzuri ilikuwa imeahidi kumlinda. Wakati wa majaribu yake alisimamia daima ukweli, na mbele ya viongozi wakuu wa kanisa na serikali waliokusanyika pamoja alitamka maneno adhimu na uaminifu ya kupinga ufisadi wa kanisa. Alipotakiwa kuchagua kati ya kukana mafundisho yake au kuuawa, alikubali kifo cha mfia dini.PKSw 77.4

    Neema ya Mungu ilimshikilia. Katika majuma ya mateso yaliyopita kabla ya hukumu yake ya mwisho, amani ya mbinguni ilijaza moyo wake. “Ninaandika barua hii,” alimwambia rafiki yake, “katika gereza langu, na mkono wangu wenye pingu, nikitarajia hukumu yangu ya kifo kesho.... Wakati, kwa msaada wa Yesu Kristo, tutakapoonana tena katika amani tamu ya maisha yajayo, utaelewa jinsi Mungu alivyojionesha kuwa mwenye rehema kwangu, jinsi alivyonisaidia kati kati ya majaribu na mitihani.”—Bonnechose, vol. 2, uk. 67.PKSw 78.1

    Katika giza la gereza lake aliona kabla ushindi wa imani ya kweli. Akirejea katika ndoto zake katika kanisa lake la Prague ambapo alikuwa amehubiri injili, aliona papa na maaskofu wake wakiziharibu picha za Kristo alizokuwa amezichora kwenye kuta zake. “Njozi hii ilimsumbua: lakini siku iliyofuata aliona wachoraji wengi wakiwa katika kazi ya kuzirudisha picha zile kwa wingi zaidi na kwa rangi zinazong'aa zaidi. Mara tu kazi yao ilipokwisha, wachoraji waliokuwa wamezungukwa na kundi kubwa la watu, walisema kwa sauti kubwa, ‘Sasa acha mapapa na maaskofu waje; hawataweza kuzifuta tena!’” Alisema Mwanamatengenezo, aliposimulia ndoto yake: “Nina imani thabiti kuwa, sura ya Kristo haitafutika kamwe. Wametamani kuiharibu, lakini itachorwa upya katika mioyo yote kwa wahubiri bora zaidi kuliko mimi.”— D'Aubigne, b. 1, ch. 6.PKSw 78.2

    Kwa mara ya mwisho, Huss aliletwa mbele ya baraza. Ulikuwa mkutano mkubwa sana—mfalme, wakuu wengine wa ngazi za juu za ufalme, manaibu wakuu katika ufalme, makadinali, maaskofu, na makasisi, na kundi kubwa la watu waliokuja kama watazamaji wa matukio wa siku ile. Kutoka sehemu zote za Ukristo walikuwa wamekusanyika kushuhudia kafara kuu hii ya kwanza katika pambano refu ambalo kwalo uhuru wa dhamiri ungeweza kupatikana.PKSw 78.3

    Akiwa ameitwa kwa ajili ya uamuzi wake wa mwisho, Huss alitamka kukataa kwake kukana, na, akikaza macho yake yanayopenya huku akimwangalia mfalme ambaye alikuwa amekiuka ahadi yake bila aibu, alisema: “Nilidhamiria, kwa uhuru na utashi wangu mwenyewe, kuja mbele ya baraza, chini ya ulinzi na imani ya mfalme aliyeko hapa.”— Bonnechose, vol. 2, uk. 84. Wekundu uliokolea sana ulipamba uso wa Sigismund huku macho ya wote waliokusanyika hapo yakigeuka kumwangalia.PKSw 78.4

    Baada ya hukumu kutamkwa, sherehe ya dhihaka ilianza. Maaskofu walimvika mfungwa wao vazi la kipadre, na alipokuwa akivalishwa vazi hilo, alisema: “Bwana wetu Yesu Kristo alivikwa joho jeupe, ili kumdhihaki, wakati Herode alipompeleka mbele ya Pilato.”—Ibid., vol. 2, p. 86. Alipotakiwa tena kukana, alijibu, akiwageukia watu: “Ni kwa uso gani, tena, ningeweza kutazama mbinguni? Ni kwa jinsi gani niwaangalie umati wa watu ambao nimewahubiria injili? Hapana; ninachukulia wokovu wao kuwa wa muhimu zaidi kuliko mwili huu maskini, ambao sasa umepangiwa kuuawa.” Nguo ziliondolewa moja baada ya nyingine, na kila askofu alitamka laana alipokuwa akifanya sehemu yake ya sherehe. Hatimaye “waliweka kichwani mwake kofia ya karatasi yenye muundo wa piramidi, ambayo juu yake ilichorwa picha za kutisha za mashetani, pamoja na maneno ‘Mzushi Mkuu’ yakionekana mbele. ‘Kwa furaha kuu,’ Huss alisema, ‘nitavaa taji hii ya aibu kwa ajili Yako, Ee Yesu, uliyevaa taji ya miiba kwa ajili yangu.’”PKSw 79.1

    Baada ya kuvalishwa hivyo, “maaskofu walisema, ‘Sasa tunaiweka roho yako wakfu kwa yule mwovu.’ ‘Na mimi,’ John Huss alisema, huku akiinua macho yake juu mbinguni, ‘ninaisalimisha roho yangu mikononi Mwako, Ee Bwana Yesu, kwa kuwa Wewe ulinikomboa.'”—Wylie, b. 3, ch. 7.PKSw 79.2

    Sasa alikabidhiwa katika mamlaka za kidunia na kupelekwa mahali pa kuuawa. Msafara mkubwa ulifuata, mamia ya watu wakiwa na silaha, mapadre na maaskofu wakiwa katika mavazi yao ya gharama, na wakazi wa Constance. Alipokuwa amefungiwa kwenye mti wa kuulia, na kila kitu kikiwa tayari ili moto uwashwe, mfia dini aliulizwa mara nyingine tena kujiokoa kwa kukana makosa. “Makosa gani,” alisema Huss, “napaswa kuyakana? Najua kuwa sina hatia yo yote. Ninamwita Mungu ashuhudie kuwa yote niliyoandika na niliyoyahubiri yalikusudiwa kuokoa roho kutoka dhambini na kuwaepusha na adhabu; na, kwa hiyo, kwa furaha kabisa nitathibitisha kwa damu yangu ukweli niliouandika na niliouhubiri.”—Ibid., b. 3, ch. 7. Wakati moto ulipowashwa na kumzunguka pande zote, alianza kuimba, “Yesu, Wewe Mwana wa Daudi, unihurumie,” na aliendelea kuimba mpaka sauti yake iliponyamazishwa kabisa.PKSw 79.3

    Hata maadui zake waliguswa na ushujaa wake wa kipekee. Mfuasi mkereketwa wa upapa, akielezea kifo cha Huss, na cha Jerome, ambaye alikufa muda mfupi baadaye, alisema: “Wote wawili walidumisha msimamo wao wa kiakili wakati saa yao ya mwisho ilipokaribia. Walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya moto kana kwamba walikuwa wakienda kwenye sherehe ya harusi. Hawakutoa sauti ya kilio cha maumivu. Wakati moto ulipoinuka, walianza kuimba; na ukali wa moto haukuweza kuzuia uimbaji wao.”—Ibid., b. 3, ch. 7.PKSw 79.4

    Wakati mwili wa Huss ulipoteketezwa kabisa, majivu yake, pamoja na udongo uliokuwa umekaliwa na majivu, vilikusanywa na kutupwa katika mto wa Rhine, na hivyo kuchukuliwa hadi baharini. Watesi wake walijidanganya kuwa wameng'oa mizizi yote ya ukweli aliouhubiri. Hawakuwa na ndoto yo yote kuwa majivu yaliyochukuliwa siku ile yalikuwa kama mbegu iliyosambazwa katika nchi zote duniani; kwamba katika nchi ambazo walikuwa hawazijui wakati ule ingezaa matunda kuwa ushuhuda kwa ajili ya ukweli. Sauti iliyokuwa imesema katika ukumbi wa baraza la Constance ilikuwa imeamsha miangwi ambayo ingesikika katika zama zote zilizofuata. Huss hakuwepo tena, lakini ukweli alioufia usingeangamia kamwe. Mfano wake wa imani na msimamo usioyumba vingewatia moyo watu wengi kusimama imara kwa ajili ya ukweli, wakikabiliwa na mateso na kifo. Kuuawa kwake kuliudhihirishia ulimwengu wote ukatili wa kutisha wa Roma. Maadui wa ukweli, ingawa hawakujua, walikuwa wakihamasisha kazi ambayo walikuwa wakijaribu kuiharibu bila mafanikio.PKSw 79.5

    Hata hivyo bado mti mwingine wa kuunguzia mtu ulikuwa unaandaliwa jijini Constance. Damu ya shahidi mwingine ilipaswa kutoa ushuhuda kwa ajili ya ukweli. Jerome, baada ya kumuaga Huss alipokuwa akienda kwenye baraza, alimtia moyo awe jasiri na imara, akitangaza kuwa ikiwa angekutana na hatari yo yote, yeye mwenyewe angeruka mara moja kwenda kumsaidia. Alipopata taarifa za kufungwa kwake gerezani, mwanafunzi mwaminifu alijiandaa haraka kutimiza ahadi yake. Bila hati ya uhakikisho wa usalama aliondoka kwenda Constance akiwa na msaidizi mmoja. Alipofika pale alitambua kuwa alikuwa amejipeleka mwenyewe katika hatari, pasipokuwa na uwezekano wo wote wa kumwokoa Huss. Alikimbia kutoka katika jiji, lakini alikamatwa akiwa njiani kuelekea nyumbani na kurudishwa akiwa amefungwa minyororo na akiwa chini ya ulinzi wa kikosi cha maaskari. Alipotokea mbele ya baraza kwa mara ya kwanza jitihada zake za kujibu mashtaka yaliyoletwa dhidi yake zilikutana na makelele, “Motoni pamoja naye! Motoni pamoja naye!”—Bonnechose, vol. 1, p. 234. Alitupwa gerezani, akiwa amefungwa minyororo na kukalishwa katika mkao uliomletea mateso makali sana, na aliishi kwa kula mkate na kunywa maji tu. Baada ya miezi kadhaa ya ukatili wa kifungo chake ulimletea Jerome ugonjwa ambao ulitishia maisha yake, na maadui zake, wakihofia kuwa anaweza kuwatoka, walimtendea kwa ukatili nafuu kidogo, ingawa alibaki gerezani kwa mwaka mmoja.PKSw 80.1

    Kifo cha Huss hakikuleta matokeo ambayo wafuasi wa papa waliyatarajia. Ukiukwaji wa hati ya usalama iliamsha dhoruba ya hasira, na kama njia iliyo salama zaidi, baraza liliazimia, badala ya kumchoma moto Jerome, limlazimishe, ikiwezekana, akanushe. Aliletwa mbele ya mkutano wa baraza, na likampa njia mbadala ya kukanusha, au kufa kwenye mti. Kifo mwanzoni mwa kifungo chake kingekuwa jambo jema zaidi kuliko mateso makali ambayo aliyapitia; lakini sasa, akiwa amedhoofishwa na ugonjwa, kwa ukali wa gereza, na mateso ya wasiwasi na hofu ya mambo yajayo, akiwa ametengwa na marafiki, na akiwa amekatishwa tamaa kwa kifo cha Huss, ujasiri wa Jerome ulizidiwa, na alikubali kujisalimisha kwa baraza. Aliahidi kufuata imani ya kikatoliki, na alikubaliana na uamuzi wa baraza la kuhukumu mafundisho ya Wycliffe na Huss, akikubaliana, hata hivyo, na “ukweli mtakatifu” ambao waliufundisha.—Ibid, vol. 2, uk. 141.PKSw 80.2

    Kwa kitendo hiki cha makusudi Jerome alijaribu kunyamazisha sauti ya dhamiri na kuepuka hukumu yake ya mwisho. Lakini katika upweke wa gereza lake alielewa vizuri kile alichokuwa amekifanya. Alifikiria juu ya ujasiri na uaminifu wa Huss, na kinyume alitafakari juu ya kuukana kwake ukweli. Alimtafakari Bwana mwenye Uungu aliyekuwa ameahidi kumtumikia, na ambaye kwa ajili yake alivumilia kifo cha msalaba. Kabla hajakana alipata faraja, katikati ya mateso yake, katika uhakikisho wa upendeleo wa Mungu; lakini sasa huzuni na mashaka vilitesa roho yake. Alijua kuwa bado atatakiwa kukana mambo mengine zaidi ili awe na imani na Roma. Njia aliyokuwa anaichukua ingeishia katika uasi kamili. Alifanya uamuzi: Kuepuka kipindi kifupi cha mateso hakupaswa kumkana Bwana wake.PKSw 81.1

    Kwa mara nyingine tena alirudishwa mbele ya baraza. Kujisalimisha kwake hakukuwaridhisha mahakimu wake. Kiu yao ya damu, iliyokuwa imechochewa na kifo cha Huss, ilidai wahanga wapya. Ili kuokoa maisha yake Jerome alipaswa kuukana ukweli kabisa. Lakini aliazimia kushikilia imani yake na kumfuata ndugu yake mfia dini katika ndimi za moto.PKSw 81.2

    Alibadilisha msimamo wake wa awali wa kuikana imani yake na, kama mtu anayekufa, alitamani sana apewe fursa ya kujitetea. Kwa kuogopa mvuto wa maneno yake, maaskofu walisisitiza kuwa yeye alitakiwa kukubali au kukanusha ukweli wa mashitaka yaliyoletwa dhidi yake. Jerome aliupinga ukatili na udhalimu mkubwa kama ule. “Mmenishikilia kifungoni kwa siku mia tatu na arobaini katika gereza linalotisha,” alisema, “katikati ya uchafu, kelele, harufu mbaya, bila mahitaji yo yote muhimu; halafu mnanileta mbele yenu, na mnawasikiliza maadui wangu wa kimaadili, mnakataa kunisikiliza.... Ikiwa kweli ninyi ni watu wenye busara, na nuru ya ulimwengu, muwe waangalifu basi msitende dhambi dhidi ya haki. Mimi kama mimi, ni mtu dhaifu na mwenye hali ya kufa; maisha yangu yana umuhimu mdogo sana; ninapowasihi kuwa msitoe hukumu isiyo ya haki, ninazungumza kidogo sana kwa ajili yangu bali zaidi kwa ajili yenu.”—Ibid., vol. 2, uk. 146, 147.PKSw 81.3

    Hatimaye ombi lake lilikubaliwa. Akiwa mbele ya majaji wake, Jerome alipiga magoti na kuomba kuwa Roho wa Mungu atawale mawazo na maneno yake, na kwamba asiseme jambo lolote linalopingana na ukweli au lolote lisilofaa kwa Bwana wake. Kwake siku ile ilitimizwa ahadi ya Mungu kwa wanafuzi wa kwanza: “Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu.... Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu” (Mathayo 10:18-20).PKSw 81.4

    Maneno ya Jerome yaliamsha mshangao na mvuto, hata kwa maadui zake. Kwa mwaka mzima alikuwa kifungoni, akiwa hawezi kusoma au kuona, katika maumivu makali ya kimwili na mashaka ya akili. Pamoja na hayo hoja zake ziliwasilishwa kwa uwazi na nguvu kana kwamba alikuwa na wakati usiobughudhiwa wa kujisomea. Aliwaelekeza wasikilizaji wake kwenye mlolongo wa watu watakatifu waliohukumiwa na majaji dhalimu. Karibu katika kila kizazi kulikuwepo na watu ambao, wakati walikuwa wakitafuta kuwainua watu wa wakati wao, walidhihakiwa na kutupwa nje, lakini ambao katika nyakati zilizofuata walikuja kuonekana kuwa walistahili heshima. Kristo mwenyewe alihukumiwa kama mkosaji katika mahakama dhalimu.PKSw 82.1

    Wakati wa kukana, Jerome alikuwa amekubaliana na uhalali wa hukumu iliyomwadhibu Huss; sasa alitangaza toba yake na kushuhudia kutokuwa na hatia na utakatifu wa mfia dini yule. “Nilimjua toka utoto wake,” alisema. “Alikuwa mtu mwema sana, mwenye haki na mtakatifu; alihukumiwa, licha ya kutokuwa na hatia yo yote.... Na mimi pia—niko tayari kufa: sitarudi nyuma kwa sababu ya mateso yaliyoandaliwa na maadui zangu na mashahidi wa uongo, ambao siku moja itawapasa kutoa hesabu ya uovu wao kwa Mungu mkuu, ambaye hawezi kudanganywa na cho chote.”—Bonnechose, vol. 2, p. 151.PKSw 82.2

    Kwa kujidhalilisha mwenyewe kwa kuukana kwake ukweli, Jerome aliendelea: “Miongoni mwa dhambi zote nilizowahi kuzitenda toka ujana wangu, hakuna hata moja iliyo na uzito mkubwa akilini mwangu, na kunifanya niumie sana, kama ile niliyoitenda mahali hapa pa mauaji, wakati nilipoidhinisha hukumu dhalimu iliyotoloewa dhidi ya Wycliffe, na dhidi ya mfia dini mtakatifu, John Huss, kiongozi na rafiki yangu. Ndiyo! Naiungama kwa dhati kutoka moyoni mwangu, na natangaza nikiwa na hofu na aibu kuwa nilitetereka wakati, kwa sababu tishio la kifo, niliyakana mafundisho yao. Kwa hiyo ninaomba... Mwenyezi Mungu anihurumie na kunisamehe dhambi zangu, na hususani dhambi hii, iliyo mbaya zaidi kuliko zote.” Akiwaelekea majaji wake, alisema kwa mkazo: “Mliwahukumu Wycliffe na John Huss, siyo kwa kutikisa mafundisho ya kanisa, bali kwa kukemea kashifa za viongozi wa kanisa—majivuno yao, kiburi chao, na maovu yote ya maaskofu na mapadre. Mambo ambayo waliyasema, na ambayo hawezi kukanushika, mimi pia ninafikiri na kusema, kama wao.”PKSw 82.3

    Maneno yake yalikatishwa. Maaskofu, wakitetemeka kwa ghadhabu walipiga kelele:“Tunahitaji ushahidi mwingine wa nini? Tumeona kwa macho yetu sisi wenyewe wazushi wakorofi!”PKSw 83.1

    Bila kuyumbishwa na dhoruba, Jerome alisema: “Nini! Mnadhani mimi naogopa kufa? Mmeniweka rumande kwa mwaka mzima katika gereza linalotisha, ambalo ni baya kuliko kifo chenyewe. Mmenishughulikia kwa ukatili zaidi kuliko Mturuki, Myahudi au mpagani, na nyama ya mwili wangu imeoza na kutaka kutoka kwenye mifupa nikiwa hai; na bado sijalalamika, kwa kuwa maombolezo ni jambo baya kwa mtu mwenye moyo na roho; lakini siwezi kujizuia kueleza mshangao wangu kwa unyama mkubwa mnaomtendea Mkristo.”—Ibid., vol. 2, uk. 151-153.PKSw 83.2

    Dhoruba ya hasira ililipuka tena, na Jerome alipelekwa haraka gerezani. Lakini walikuwepo baadhi ya watu ambao waliguswa sana na maneno yake na ambao walitamani kuokoa maisha yake. Alitembelewa na viongozi wa kanisa na walimsihi ajisalimishe kwa baraza. Marupu-rupu makubwa yaliahidiwa kwa ajili yake kama zawadi za kuachana na upinzani wake dhidi ya Roma. Lakini kama Bwana wake alipoahidiwa utukufu wa ulimwengu, Jerome alidumisha msimamo wake.PKSw 83.3

    “Nithibitishieni makosa yangu katika Maandiko Matakatifu,” alisema, “nami nitayakana.”PKSw 83.4

    “Maandiko Matakatifu!“alifoka mmoja wa wajaribu wake,“ndiyo yatumike kuhukumu kila kitu? Ni nani atayaelewa kanisa lisipoyatafsiri?”PKSw 83.5

    “Je, mapokeo ya wanadamu ndiyo yastahili kuaminiwa zaidi kuliko injili ya Mwokozi wetu?” Jerome alijibu. “Paulo hakuwaagiza aliowaandikia kusikiliza mapokeo ya wanadamu, bali alisema, ‘Chunguzeni Maandiko.’”PKSw 83.6

    “Mzushi!” ndiyo lilikuwa jibu, “Ninajuta kwa kuwabembeleza kwa muda mrefu. Ninaona kuwa mnasukumwa na Shetani.”—Wylie, b. 3, ch. 10.PKSw 83.7

    Kabla hukumu ya adhabu haijapitishwa dhidi yake. Alipelekwa mahali pale pale ambapo Huss alifia. Alienda akiimba njiani, uso wake ukiwa umeng'aa kwa furaha na amani. Macho yake yalikuwa yameelekezwa kwa Kristo, na kwake kifo kilikuwa siyo tishio tena. Wakati mwuaji alipokuwa karibu kuwasha kuni moto, alisimama nyuma yake, mfia dini alisema: “Njoo kwa ujasiri; washa moto mbele ya uso wangu. Kama ningekuwa mwoga, nisingekuwa hapa.”PKSw 83.8

    Maneno yake ya mwisho, yaliyosemwa wakati moto ulipomzunguka, yalikuwa ya sala. “Bwana, Baba Mwenyezi,” alilia, “nihurumie, na unisamehe dhambi zangu; kwa kuwa unajua kuwa daima ninaupenda ukweli Wako.”— Bonnechose, vol. 2, p. 168. Sauti yake ilikoma, lakini midomo yake iliendelea kucheza akiwa anaomba. Wakati moto ulipomaliza kazi yake, majivu ya mfia dini, pamoja na udongo uliokuwa umekaliwa na majivu, vilikusanywa, na kama ya Huss, yalitupwa katika mto wa Rhine.PKSw 83.9

    Hivyo ndivyo wabeba nuru waaminifu wa Mungu walivyouawa. Lakini nuru ya ukweli walioutangaza—nuru ya mfano wao wa kishujaa— haikuzimwa. Kama vile ambavyo watu wasingeweza kugeuza mwelekeo wa jua sawa na jinsi wasingeweza kuzuia mapambazuko ya siku ile ambayo yalikuwa yakitokea ulimwenguni.PKSw 84.1

    Kifo cha Huss kiliwasha moto wa hasira katika nchi ya Bohemia. Ilihisiwa na taifa lote kuwa alikufa kama mawindo ya chuki ya mapadre na hila za mfalme. Alitangazwa kuwa mwalimu mwaminifu wa ukweli, na baraza lililoamrisha kifo chake lilishitakiwa kwa kuhusika na mauaji. Mafundisho yake sasa yalikuwa na mvuto mkubwa zaidi kuliko wakati uliopita. Kwa njia ya maagizo ya papa maandishi ya Wycliffe yalitakiwa kuchomwa moto. Lakini yale yaliyokuwa yamepona kuangamizwa sasa yaliletwa kutoka mafichoni na kusomwa huku yakilinganishwa na Biblia, au sehemu zake kwa kadiri watu walivyoweza kuzipata, na wengi waliweza kuongozwa kuikubali imani iliyofanyiwa matengenezo.PKSw 84.2

    Wauaji wa Huss hawakuweza kuendelea kuwa kimya na kushuhudia ushindi wa kazi yake. Papa na mfalme waliungana kuzima vuguvugu, na majeshi ya Sigismund yalitumwa Bohemia.PKSw 84.3

    Lakini mkombozi aliinuliwa. Ziska, ambaye baada ya kuanza vita alipofuka kabisa, lakini ambaye alikuwa jenerali mwenye nguvu nyingi kuliko majenerali wote katika zama zake, alikuwa kiongozi wa Wabohemia. Akitumainia msaada wa Mungu na ukweli waliousimamia, watu wale waliweza kukabiliana na majeshi yenye nguvu kubwa kabisa ambayo yangeletwa dhidi yao. Tena na tena mfalme, akiandaa majeshi mapya, aliivamia Bohemia, lakini mara zote walirudishwa nyuma kwa aibu kubwa. Wafuasi wa Huss walikuwa wameinuliwa juu ya hofu ya kifo, na hakuna cho chote kingeweza kusimama dhidi yao. Miaka michache baada ya vita kuanza, Ziska jasiri alikufa; lakini nafasi yake ilijazwa na Procopius, ambaye naye alikuwa jenerali mwenye stadi nyingi za kivita, na katika mambo mengine alikuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa zaidi kuliko hata Ziska.PKSw 84.4

    Maadui wa Wabohemia, wakijua kuwa mpiganaji kipofu alikuwa amekufa, waliona na fursa muafaka kwao kurudisha vyote walivyokuwa wamepoteza. Sasa papa alitangaza vita ya msalaba dhidi ya wafuasi wa Huss, na tena jeshi kubwa liliandaliwa dhidi ya Bohemia, lakini walishindwa vibaya sana. Vita nyingine ya msalaba ilitangazwa. Katika nchi zote zilizokuwa chini ya utawala wa papa huko Ulaya, watu, pesa, na silaha vilikusanywa. Makundi kwa makundi ya watu walifurika upande wa bendera ya papa, wakiwa na hakika kuwa hatimaye mwisho wa waumini wa uzushi wa Huss ulikuwa umefika. Wakiwa na hakika ya ushindi, jeshi kubwa liliingia Bohemia. Watu wa Bohemia walijipanga kuwafukuza. Majeshi haya mawili yalikabiliana na mto uliokuwa katikati yao ndio uliowatenganisha. “Maaskari wa msalaba walikuwa jeshi kubwa mno, lakini badala ya kuvuka mto mara moja, na kuwavamia wafuasi wa Huss ambao ndio walikuwa wamekuja kuwakabili, walisimama kimya wakiwaangalia tu wale wapiganaji.”—Wylie, b. 3, ch. 17. Ndipo kwa ghafla tishio lisilojulikana kuwa lilitoka wapi liliwaangukia wanajeshi wa msalaba. Bila kufanya shambulio lolote, jeshi lile kubwa lilisambaratika na maaskari walitawanyika kana kwamba walifukuzwa na nguvu isiyoonekana. Idadi kubwa miongoni mwao waliuawa na jeshi la wafuasi wa Huss, lililowafuatilia wanajeshi wa msalaba waliokuwa wakijaribu kukimbia, na nyara nyingi ziliangukia katika mikono ya washindi, matokeo yake, vita, badala ya kuwaacha maskini, iliwatajirisha Wabohemia.PKSw 84.5

    Miaka michache iliyofuata, chini ya papa mpya, tena vita nyingine ya msalaba ilitangazwa. Kama ilivyokuwa siku zilizotangulia, watu na mali vilikusanywa kutoka nchi zote za Ulaya zilizokuwa chini ya upapa. Vishawishi vilivyotolewa kwa watu ambao wangeweza kuingia katika shughuli hii ya hatari vilikuwa vikubwa sana. Msamaha kamili wa uhalifu mkubwa kabisa uliahidiwa kwa kila askari wa msalaba. Wote waliofia vitani waliahidiwa zawadi nono mbinguni, na waliotoka salama vitani waliahidiwa kuvuna heshima na utajiri katika uwanja wa vita. Jeshi kubwa lilikusanywa tena, na, wakifaulu kuvuka mpaka waliingia Bohemia. Majeshi ya wafausi wa Huss walirudi nyuma mbele yao, na kwa njia hiyo waliwavuta wavamizi ndani ya nchi zaidi, na kuwafanya waone kuwa tayari wameshapata ushindi. Mwishoni jeshi la Procopius lilisimama, na likimgeukia adui, lilisonga mbele kupambana nao. Maaskari wa msalaba, sasa wakigundua kosa lao, walilala katika makambi yao wakisubiri mashambulizi yaanze. Wakati sauti ya majeshi yaliyokuwa yakisogea iliposikika, hata kabla wafuasi wa Huss hawajaonekana machoni pao, hofu iliwashika tena maaskari wa msalaba. Wakuu, majenerali, na maaskari wa kawaida, wakitupilia mbali silaha zao, walikimbia kuelekea pande zote. Bila mafanikio, mwakilishi wa papa, ambaye alikuwa kiongozi wa uvamizi, alijaribu kuyahamasisha majeshi yaliyokuwa yametishika na kusambaratika. Licha ya jitihada zake nyingi, yeye mwenyewe alijikuta amechukuliwa na mkondo wa maaskari waliokuwa wakikimbia kwa hofu. Walishindwa kabisa, na kwa mara nyingine tena nyara nyingi ziliangukia katika mikono ya washindi.PKSw 85.1

    Hivyo kwa mara ya pili jeshi kubwa, lililotumwa na mataifa yenye nguvu kubwa kuliko yote huko Ulaya, jeshi la watu jasiri, wazoefu wa vita, waliofundishwa na wenye silaha zote za kivita, walikimbia bila kutumia silaha yote mbele ya walinzi wa nchi ambayo wakati huo ilikuwa dhaifu. Hapa kulikuweko udhihirisho wa nguvu ya Mungu. Wavamizi walipigwa kwa hofu inayopita nguvu za kibinadamu. Yeye aliyeyashinda majeshi ya Farao katika bahari ya Shamu, aliyeyakimbiza majeshi ya Midiani mbele ya Gideoni na watu wake mia tatu, ambaye katika usiku moja aliwanyenyekesha majeshi ya Ashuru yenye kiburi, alikuwa amenyosha tena mkono Wake kukausha nguvu za mkandamizaji. “Hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hofu, Maana Mungu ameitawanya mifupa yake aliyekuhusuru. Umewatia aibu, Kwa sababu MUNGU amewadharau” (Zaburi 53:5).PKSw 85.2

    Viongozi wa upapa, baada ya kukata tamaa ya kushinda kwa kutumia nguvu, hatimaye walijielekeza katika kujenga mahusiano mema. Maafikiano yalifanywa, kuwa wakati wakidai kuwapa watu wa Bohemia uhuru wa dhamiri, kiuhalisia waliwasaliti na kuwaweka chini ya mamlaka ya Roma. Wabohemia walikuwa wameweka masharti manne ya amani na Roma: uhuru wa kuhubiri Biblia; haki ya kanisa lote kushiriki mkate na divai wakati wa ushirika mtakatifu, na matumizi ya lugha ya nyumbani katika ibada; kuwaondoa kabisa viongozi wa kanisa katika majukumu na mamlaka zisizo za kidini; na, kukitokea uhalifu, mahakama za kiraia ziwe na mamlaka juu ya viongozi wa kidini na waumini wa kawaida. Mamlaka za kipapa hatimaye “ziliafiki kuwa vipengele vinne vya wafuasi wa Huss vikubaliwe, lakini waliweka sharti kuwa haki ya kuvifafanua vipengele hivyo, yaani, haki ya kuamua maana yake hasa, ibakie kuwa ya baraza—kwa maneno mengine, ibakie kwa papa na mfalme.”—Wylie, b. 3, ch. 18. Kwa msingi huu mkataba uliandikwa, na Roma ilipata kwa ujanja na hila kile ambacho ilishindwa kupata kwa kutumia mapambano; kwa kuwa, kuweka tafsiri yake ya masharti ya wafuasi wa Huss, kama ilivyokuwa kwa Biblia, Roma ingeweza kupotosha maana yake ili kutekeleza makusudi yake.PKSw 86.1

    Kundi kubwa katika Bohemia, baada ya kuona kuwa walisaliti uhuru wao, hawakuweza kukubaliana na mkataba. Mipasuko na migawanyiko iliibuka, ikasababisha migogoro na umwagaji damu miongoni mwao. Katika migogoro hii Procopio alianguka, na uhuru wa Wabohemia uliondoka.PKSw 86.2

    Sigismund, msaliti wa Huss na Jerome, sasa akawa mfalme wa Bohemia, na bila kujali kiapo chake cha kuunga mkono haki za Wabohemia, alisonga mbele kuimarisha upapa. Lakini alinufaika kidogo sana kwa kujiweka kwake chini ya mamlaka ya Roma. Kwa miaka ishirini ya maisha yake ilikuwa imejaa shughuli na hatari nyingi. Majeshi yake yalidhoofika na hazina zake zilikaushwa kwa mapambano yasiyokuwa na faida na ya muda mrefu; na sasa, baada ya kutawala kwa mwaka mmoja, alikufa, akiuacha ufalme wake kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na akirithisha kwa vizazi vilivyofuata jina linaloaibisha.PKSw 86.3

    Mizozo, migogoro, na umwagaji damu viliendelea. Kwa mara nyingine tena majeshi ya kigeni yaliivamia Bohemia, na migawanyiko ya ndani iliendelea kulitafuna taifa. Wale waliobaki wakiwa waaminifu kwa injili walijikuta wakiteswa na kuuawa.PKSw 86.4

    Kama ndugu zao wa awali, kuingia mkataba na Roma, walikumbatia makosa yake, wale walioshikilia imani ya zamani walijiunga pamoja na kuwa kanisa kamili linalojitegemea, wakijiita “Umoja wa Ndugu.” Tendo hili lilivuta laana kutoka kwa makundi yote ya watu. Lakini uimara wao haukuyumbishwa. Walipolazimishwa kujificha katika misitu na mapango, bado waliendelea kukusanyika kusoma neno la Mungu na kumwabudu Mungu.PKSw 87.1

    Kwa njia ya wajumbe waliotumwa kwa siri katika nchi mbalimbali, waligundua kuwa hapa na pale kulikuwa na “wafuasi wa ukweli waliotawanyika huko huko, wachache katika mji huu na wengine katika mji ule, walengwa, kama wao, wa mateso; na kwamba katikati ya milima ya Alps lilikuwepo kanisa la zamani, likiwa limejengwa juu ya misingi ya Maandiko, na wakipinga ufisadi wa ibada ya sanamu za Roma.”—Wylie, b. 3, ch. 19. Kundi hili lilipokelewa kwa furaha kubwa, na mawasiliano yalianzishwa na Wakristo wa Kiwaldensia.PKSw 87.2

    Wakiwa waaminifu kwa injili, Wabohemia walikesha kucha katika usiku wa mateso, katika saa ya giza wakiwa bado wanatazama hadi upeo wa macho yao kama vile watu wanavyoisubiri asubuhi. “Sehemu yao iliamriwa siku za uovu, lakini ... waliyakumbuka maneno yaliyosemwa kwanza na Huss, na kurudiwa na Jerome, kuwa karne ingepita kabla mapambazuko. Haya maneno yalikuwa kwa Watabori [wafuasi wa Huss] kama maneno ya Yusufu yalivyokuwa kwa makabila katika nyumba ya utumwa: ‘Mimi ninakufa, na Mungu hakika atawajia, na kuwatoa.'”—Ibid., b. 3, ch. 19. “Kipindi cha mwisho wa karne ya kumi na tano kilishuhudia ongezeko la pole pole lakini la hakika la makanisa ya Umoja wa Ndugu. Japokuwa siyo kweli kuwa halikushambuliwa, lakini kwa sehemu kubwa walikuwa na utulivu. Mwanzoni mwa karne ya kumi na sita makanisa yao yalikuwa mia mbili katika nchi ya Bohemia na Moravia.”—Ezra Hall Gillett, Life and Times of John Huss, vol. 2, uk. 570. “Hivyo ndivyo walivyokuwa watu wema waliosalia ambao, kwa kuepuka maangamizi ya ukali wa moto na upanga, waliruhusiwa kuona mapambazuko ya siku iliyotabiriwa na Huss.”—Wylie, b. 3, ch. 19.PKSw 87.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents