Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 41—Ukiwa wa Dunia

    “Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake. Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu. Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe. Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu. Na hao wafalme wa nchi, waliozini naye na kufanya anasa pamoja naye, watalia na kumwombolezea; ...wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu, Babeli, mji ule ulio na nguvu! Kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja” (Ufunuo 18:5-10).PKSw 498.1

    “Na wafanya biashara ya vitu hivyo, waliopata mali kwake, watasimama mbali, kwa hofu ya maumivu yake; wakilia na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule mkuu! Uliovikwa kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na nguo nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu! kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa” (Ufunuo 18:11, 3, 15-17).PKSw 498.2

    Hizo ndizo hukumu ambazo zinaanguka juu ya Babeli katika siku ya ujio wa hasira ya Mungu. Babeli umejaza kipimo cha uovu wake; wakati wake umefika; umekomaa kwa ajili ya kuangamizwa.PKSw 498.3

    Wakati sauti ya Mungu inapogeuza kifungo cha watu Wake, kuna mwamko wa kutisha wa wale ambao wamepoteza vyote katika pambano kuu la maisha. Wakati pambano lilipokuwa likiendelea walipofushwa na madanganyifu ya Shetani, na walihalalisha njia yao ya dhambi. Matajiri walijivunia ukuu wao kwa kujilinganisha na wale waliokuwa na kipato cha chini kuliko wao; lakini walipata utajiri wao kwa kuvunja sheria ya Mungu. Walipuuza kuwalisha wenye njaa, kuwavika walio uchi, kutenda kwa haki, na kupenda rehema. Walitafuta kujiinua na kuabudiwa na viumbe wenzao. Sasa wamenyang'anywa vyote vilivyowafanya kujiona wakubwa na wameachwa bila kitu na bila ulinzi. Wanaangalia kwa hofu uangamizaji wa sanamu walizozipatia umuhimu zaidi kuliko Muumbaji wao. Waliuza roho zao kwa ajili ya utajiri na furaha za kidunia, na hawakutafuta kuwa matajiri mbele za Mungu. Matokeo yake, maisha yao yameishia kushindwa kabisa; raha zao zimegeuzwa kuwa uchungu, hazina zao zimegeuka kuwa uozo. Mapato ya maisha yao yote yanafutiliwa mbali kwa muda mfupi, kufumba na kufumbua. Matajiri wanaombolezea uharibiwaji wa majumba yao makubwa, kutawanywa kwa dhahabu na fedha zao. Lakini maombolezo yao yananyamazishwa na hofu kuwa wao wenyewe wanakwenda kuangamizwa pamoja na sanamu zao.PKSw 498.4

    Waovu wanajazwa na masikitiko, siyo kwa sababu ya dhambi yao kumpuuza Mungu na wanadamu wenzao, bali kwa sababu Mungu ameshinda. Wanaomboleza kwa sababu ya jinsi matokeo yalivyo; lakini hawatubii uovu wao. Wasingeweza kuacha kujaribu kutumia njia yo yote ili waweze kushinda ikiwezekana.PKSw 499.1

    Ulimwengu unawaona wale ambao waliwadhihaki na kuwakejeli, na kutamani kuwaangamiza, wakipita bila kudhurika katikati ya magonjwa, tufani, na tetemeko. Yeye ambaye kwa wavunjaji wa sheria Yake ni moto ulao, kwa watu Wake ni hema salama.PKSw 499.2

    Mchungaji ambaye alitoa kafara ya ukweli kupata ukubali wa watu sasa anagundua asili na mvuto wa mafundisho yake. Inaonekana wazi kuwa jicho linalojua mambo yote lilikuwa likimfuatilia aliposimama kibwetani, alipotembea mitaani, alipojichanganya na watu katika mazingira mbali mbali ya maisha. Kila mhemko wa roho, kila mstari ulioandikwa, kila neno lililotamkwa, kila tendo lililowafanya kutulia katika maficho ya uongo, alikuwa akitawanya mbegu; na sasa katika roho maskini, zilizopotea zinazomzunguka, anaona mavuno.PKSw 499.3

    Bwana anasema: “Kwa maana wameiponya jeraha ya binti ya watu wangu kwa juu-juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.” “Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika” (Yeremia 8:11; Ezekieli 13:22).PKSw 499.4

    “Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! ... Angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo.” “Pigeni yowe, enyi wachungaji, na kulia; na kugaagaa katika majivu, enyi mlio hodari katika kundi; maana siku za kuuawa kwenu zimetimia kabisa; ... Nao wachungaji watakuwa hawana njia ya kukimbia, wala walio hodari katika kundi hawataokoka” (Yeremia 23:1, 2; 25:34, 35).PKSw 499.5

    Wachungaji na watu wanaona kuwa hawakudumisha uhusiano mzuri na Mungu. Wanaona kuwa wamemwasi Mwasisi wa sheria yote ya haki na takatifu. Kuziacha kanuni takatifu za Mungu kulifungulia chemchemi maelfu za uovu, mashindano, chuki, ubaya, mpaka dunia ikawa uwanja mkubwa wa mapambano, eneo la ufisadi. Huu ndio uhalisia ambao sasa unaonekana kwa wale wanaokataa ukweli na kuchagua kukumbatia uongo. Hakuna lugha inaweza kuelezea shauku ambayo wasiokuwa watiifu na wasiokuwa wanyenyekevu wanayo kwa ajili ya kile ambacho wamekipoteza milele—uzima wa milele. Watu ambao ulimwengu uliwaabudu kwa sababu ya talanta zao na ufasaha wao sasa wanaona mambo haya katika nuru yake ya kweli. Wanagundua kile ambacho wamejinyima kwa uasi wao, na wanaanguka chini kwenye nyayo za wale ambao uaminifu wao waliudhihaki na kuukejeli, na wanakiri kuwa Mungu alikuwa anawapenda.PKSw 499.6

    Watu wanaona kuwa walidanganywa. Wanalaumiana kwa kupelekana katika maangamizi; lakini wote wanaungana pamoja katika kurundika lawama zao chungu juu ya wachungaji. Wachungaji wasiokuwa waaminifu waliwatabiria mambo laini; waliwaongoza wasikilizaji wao kuibatilisha sheria ya Mungu na kuwatesa walioitakasa. Sasa, katika kukata tamaa kwao, walimu hawa wanakiri mbele ya ulimwengu kuwa kazi yao ilikuwa ya uongo. Umati wa watu unajazwa hasira kali. “Tumepotea!” wanapiga kelele, “na ninyi ndio sababu ya kuangamia kwetu;” na wanawashambulia wachungaji wa uongo. Watu wale wale ambao huko nyuma waliwastahi sana watatamka maneno ya kutisha ya laana juu yao. Mikono ile ile ambayo huko nyuma iliwavalisha taji za heshima itainuliwa juu kwa ajili ya kuwaangamiza. Panga ambazo zilikuwa zimenolewa kuwaua watu wa Mungu sasa zinatumika kuwaua adui zao. Kila mahali kuna migogoro na umwagaji damu.PKSw 500.1

    “Mshindo utafika hata mwisho wa dunia; Maana Bwana ana mashindano na mataifa, Atateta na watu wote wenye mwili; Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga” (Yeremia 25:31). Kwa miaka elfu sita, pambano kuu limekuwa likiendelea; Mwana wa Mungu na wajumbe Wake wa mbinguni wamekuwa wakipambana na nguvu ya mwovu, kuonya, kuangazia, na kuwaokoa wanadamu. Sasa wote wamefanya maamuzi yao; waovu wameungana kikamilifu na Shetani katika vita yake dhidi ya Mungu. Wakati umefika wa Mungu kuthibitisha mamlaka ya sheria Yake iliyokanyagwa. Sasa pambano siyo la Shetani peke yake, bali ni la Shetani pamoja na watu. “Bwana ana mashindano na mataifa;” “Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga.”PKSw 500.2

    Alama ya ukombozi imewekwa kwa wale “wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake.” Sasa malaika wa kifo anatoka, akiwakilishwa katika njozi ya Ezekieli na watu walio na silaha za kuulia, ambao wanapewa amri: “Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu.” Nabii anasema: “Wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba” (Ezekieli 9:1-6). Kazi ya uangamizaji inaanzia kwa wale waliokuwa walinzi wa kiroho wa watu. Walinzi waongo wanakuwa wa kwanza kuanguka. Hakuna wa kuhurumiwa au kubakiza. Wanaume, wanawake, wasichana, na watoto wachanga wanaangamia pamoja.PKSw 500.3

    “Bwana anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa” (Isaya 26:21). “Na hii ndiyo tauni, ambayo Bwana atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa Bwana yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake” (Zekaria 14:12, 13). Katika migogoro yenye hasira ya mihemko yao mikali, na umwagaji mkubwa wa hasira ya Mungu isiyochanganywa na rehema, wanaanguka wakazi waovu wa dunia—makuhani, watawala, na watu wengine, matajiri na maskini, walio juu na walio chini. “Na waliouawa na Bwana siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.” (Yeremia 25:33).PKSw 500.4

    Wakati wa kuja kwa Kristo waovu wanafutiliwa mbali kutoka katika uso wa dunia nzima—wakiteketezwa kwa roho ya kinywa Chake na kuangamizwa kwa ukali wa nuru ya utukufu Wake. Kristo anawachukua watu Wake hadi katika Jiji la Mungu, na dunia inabaki tupu bila wakazi. “Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake.” “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana Bwana amenena neno hilo” “Kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea” (Isaya 24:1, 3, 5, 6).PKSw 501.1

    Dunia yote itaonekana kama jangwa tupu. Mabaki ya miji na vijiji vilivyoharibiwa na tetemeko, miti iliyong'olewa, mawe makubwa yanayokwaruza yaliyotupwa kutoka baharini au yaliyokatwa na kurushwa kutoka ardhini, vitakuwa vimesambaa juu ya uso wote wa dunia, wakati mashimo makubwa yatakuwa alama ya mahali ambapo milima iling'olewa kutoka katika misingi yake. Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayariPKSw 501.2

    Sasa tukio linatokea lililoashiriwa katika huduma nzito ya Siku ya Upatanisho. Wakati huduma katika patakatifu pa patakatifu ilipokuwa imekamilika, na dhambi za Israeli kuondolewa kutoka katika hema kwa njia ya damu ya sadaka ya dhambi, ndipo mbuzi wa Azazeli aliwasilishwa akiwa hai mbele za Bwana; na mbele ya mkutano kuhani mkuu aliungama “uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye akaziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi” (Walawi 16:21). Hali kadhalika, wakati kazi ya upatanisho itakapokamilika katika hekalu la mbinguni, ndipo mbele za Mungu na malaika wa mbinguni na majeshi ya waliokomboleewa dhambi za watu wa Mungu zitawekwa juu ya Shetani; atatangazwa kuwa na hatia ya uovu aliosababisha waufanye. Na kama mbuzi wa Azazeli alivyopelekwa katika nchi isiyokaliwa na watu, kadhalika Shetani atalazimishwa kukaa katika dunia iliyo tupu, jangwa lisilokaliwa na watu na linalochosha.PKSw 501.3

    Nabii wa Ufunuo anatabiri kifungo cha Shetani na hali ya machafuko na ukiwa utakaoipata dunia, na anaeleza hali hii itadumu kuwepo kwa miaka elfu moja. Baada ya kuwasilisha mandhari za ujio wa pili wa Bwana na uangamizwaji wa waovu, unabii unaendelea kueleza: “Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache” (Ufunuo 20:1-3).PKSw 502.1

    Kwamba neno “kuzimu” huwakilisha dunia katika hali ya vitu vyake vilivyosambaratika huko na huko na ikiwa imefunikwa na giza huthibitishwa na maandiko mengine. Kuhusiana na hali ya dunia “hapo mwanzo,” kumbukumbu za Biblia zinasema kuwa ilikuwa “ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji.” [Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa “vilindi” limetafsiriwa katika Biblia ya Kigiriki cha Septuaginta cha Agano la Kale kwa neno lile lile lililotafsiriwa “kuzimu” katika Ufunuo 20:13.] (Mwanzo 1:2). Unabii hufundisha kuwa dunia itarudishwa, angalau kwa sehemu, katika hali hii. Akiangalia mbele na kuiona siku kuu ya Mungu, nabii Yeremia alisema: “Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru. Naliiangalia milima, na tazama, ilitetemeka, na milima yote ilisogea huko na huko. Nikaangalia, na tazama, hapakuwa na mtu hata mmoja, na ndege wote wa angani wamekwenda zao. Nikaangalia, na tazama, shamba lililozaa sana limekuwa ukiwa, na miji yake yote ilikuwa imebomoka” (Yeremia 4:23-26).PKSw 502.2

    Hapa patakuwa nyumbani kwa Shetani na malaika zake waovu kwa miaka elfu moja. Akiwa kizuizini duniani, hatakuwa na uwezo wa kwenda katika sayari zingine kuwajaribu na kuwaudhi wale ambao hawajawahi kuanguka. Ni katika maana hii anakuwa kifungoni: hakuna mtu ye yote aliyebaki, ambaye Shetani anaweza kutumia uwezo wake juu yake. Ameachanishwa kabisa na kazi ya udanganyifu na uharibifu ambao kwa karne nyingi ilikuwa chanzo pekee cha furaha yake.PKSw 502.3

    Nabii Isaya, akitazama mbele hadi wakati wa kushindwa kwa Shetani, anasema: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! ... Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; ... Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo. Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme; Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” (Isaya 14:12-17).PKSw 503.1

    Kwa miaka elfu sita, kazi ya Shetani ya uasi imeitetemesha dunia. Ameufanya ulimwengu wote ukiwa, na ameipindua “miji yake yote.” Na “hakuwafungulia wafungwa wake waende kwao.” Kwa miaka elfu sita nyumba yake ya gereza imepokea watu wa Mungu, na angeendelea kuwaweka kifungoni milele; lakini Kristo alizikata kamba zake na kuwaweka huru.PKSw 503.2

    Hata waovu sasa wamewekwa nje ya uwezo wa Shetani, na yeye peke yake na malaika zake wanabaki wakiangalia madhara ya laana iliyoletwa na dhambi. “Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba [kaburi] yake mwenyewe. Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa.... Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako” (Isaya 14:18-20).PKSw 503.3

    Kwa miaka elfu moja, Shetani atakuwa akizunguka huku na huko katika dunia iliyo na ukiwa akiangalia matokeo ya uasi wake dhidi ya sheria ya Mungu. Katika kipindi hiki mateso yake ni makubwa mno. Tangu kuanguka kwake maisha yake ya shughuli zisizokoma yaliondoa muda wa kutafakari; lakini sasa amenyang'anywa uwezo na ameachwa kutafakari sehemu aliyoifanya tangu alipoasi kwa mara ya kwanza dhidi ya serikali ya mbinguni, na kutazama mbele kwa kutetemeka na hofu hadi wakati ujao unaotisha wakati ambao atalazimika kuteseka kwa ajili ya uovu alioutenda na adhabu atakayoipata kwa ajili ya dhambi alizosababisha watu wa Mungu kuzitenda.PKSw 503.4

    Kwa watu wa Mungu, kifungo cha Shetani kitaleta shangwe na furaha. Nabii alisema: “Itakuwa katika siku ile, ambayo Bwana atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa; utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli [hapa akimwakilisha Shetani], na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri! ... Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala. Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu” (Aya 3-6).PKSw 503.5

    Katika kipindi cha miaka elfu moja, katikati ya ufufuo wa kwanza na wa pili hukumu ya waovu itafanyika. Mtume Paulo anaongelea hukumu hii kama tukio litakalofuata baada ya ujio wa pili. “Msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo” (1 Wakorintho 4:5). Danieli anaeleza kuwa wakati Mzee wa Siku alipokuja, “watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu” (Danieli 7:22). Wakati huu wenye haki wanatawala kama wafalme na makuhani kwa Mungu. Yohana katika Ufunuo anasema: “Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu.” “Watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu” (Ufunuo 20:4, 6). Ni wakati huu ambapo, kama ilivyotabiriwa na Paulo, “watakatifu watauhukumu ulimwengu” (1 Warintho 6:2). Wakiungana na Kristo wanawahukumu waovu, wakilinganisha matendo yao na kitabu cha sheria, Biblia, na kuamua kila kesi kulingana na matendo yaliyotendwa katika mwili. Na kipimo cha adhabu watakayopata waovu kinapangwa, kulingana na matendo yao; na kinaandikwa dhidi ya majina yao katika kitabu cha mauti.PKSw 504.1

    Shetani na malaika waovu pia wanahukumiwa na Kristo na watu Wake. Paulo anasema: “Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika?” (Aya 3). Na Yuda anatangaza kuwa “malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu” (Yuda 6).PKSw 504.2

    Mwishoni mwa miaka elfu moja ufufuo wa pili utatokea. Ndipo waovu watafufuliwa kutoka katika wafu na kutokea mbele ya Mungu kwa jili ya utekelezaji wa “hukumu iliyoandikwa.” Nabii wa Ufunuo, baada ya kuelezea ufufuo wa wenye haki, anasema: “Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu” (Ufunuo 20:5). Na Isaya anatangaza, kuhusiana na waovu: “Nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa” (Isaya 24:22).PKSw 504.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents