Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 12—Matengenezo Ufaransa

    Upinzani wa Spires na Ungamo la pale Augsburg—matukio ambayo yaliweka alama ya ushindi wa Matengenezo katika nchi ya Ujerumani, yalifuatiwa na miaka ya migogoro na giza. Baada ya kudhoofishwa na migawanyiko miongoni mwa wafuasi wake, na baada ya kushambuliwa na maadui zake wenye nguvu, Uprotestanti ulionekana kama unaelekea kuangamizwa. Maelfu walitia muhuri ushuhuda wao kwa damu zao. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ililipuka; mmoja wa wafuasi wake wakuu aliisaliti kazi ya Uprotestanti; watu wema sana miongoni mwa wakuu waliokubali matengenezo waliangukia katika mikono ya mfalme mkuu na waliburuzwa kama mateka kutoka mji mmoja hadi mwingine. Lakini katika wakati ambao mfalme mkuu alionekana kuwa anaelekea kupata ushindi, alipoteza ushindi. Alishuhudia mawindo yake yakinyakuliwa kutoka katika mikono yake, na alilazimishwa hatimaye kuvumilia mafundisho ambayo lengo kuu la maisha yake lilikuwa kuyaangamiza. Alikuwa amechezea kamari ufalme wake, hazina zake na maisha yake yote ili kuangamiza uzushi. Sasa alishuhudia majeshi yake yakipukutika katika vita, hazina zake zikikauka, falme zake nyingi zikitishiwa na uasi, wakati kila mahali imani ambayo alijaribu kuidhibiti, ilikuwa ikisambaa. Charles V alikuwa akipambana na nguvu kubwa kuliko zote. Mungu alisema, “Na iwe nuru,” lakini mfalme mkuu alikuwa akipambana giza lisiondoke. Kusudi lake lilishindwa; na akiwa bado ana umri mdogo, kwa kuchoshwa sana na migogoro ya muda mrefu, alikimbia kiti cha enzi na kwenda kujificha katika nyumba ya watawa.PKSw 158.1

    Katika nchi za Uswisi na Ujerumani, kulikuja siku za giza dhidi ya Matengenezo. Wakati maeneo mengi yalipokea imani ya matengenezo, mengine yalishikilia kwa nguvu ya upofu kanuni za kiimani zisizobadilika za Roma. Mateso yao dhidi ya wale waliokuwa na shauku ya kupokea ukweli hatimaye yalisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Zwingli na wengi waliokuwa wameungana naye katika matengenezo walifia katika uwanja wa damu wa Cappel. Okolampadio, kwa kuzidiwa na hofu ya majanga haya ya kutisha alikufa muda mfupi baadaye. Roma ilishinda, na katika maeneo mengi ilionekana kana kwamba Roma ilirudisha mambo yote iliyokuwa imepoteza. Lakini Yeye ambaye mashauri Yake ni ya milele hakuwa ameiacha kazi Yake wala watu Wake. Mkono Wake ulileta ukombozi kwa ajili yao. Katika nchi zingine aliinua watenda kazi wengine waendeleze kazi ya matengenezo.PKSw 158.2

    Katika nchi ya Ufaransa, kabla jina la Luther halijasikika kama Mwanamatengenezo, kulishaanza kupambazuka. Mmoja wa watu wa awali kupokea nuru alikuwa mzee Lefevre, mtu mwenye elimu kubwa, profesa katika Chuo Kikuu cha Paris, na mfuasi wa papa wa dhati na mwenye juhudi kubwa. Katika utafiti wake katika maandishi ya kale macho yake yalielekezwa kwenye Biblia, na alianzisha mafundisho ya Biblia kwa wanafunzi wake.PKSw 158.3

    Lefevre alikuwa mtu aliyewaheshimu sana watakatifu, na alijielekeza kuandika historia ya watakatifu na wafia dini kama walivyosimuliwa katika mapokeo ya kanisa. Hii ilikuwa kazi iliyohitaji nguvu nyingi; lakini alikuwa amekwisha endelea sana katika hili, wakati, akidhania kuwa angepata msaada mkubwa kutoka katika Biblia, alianza kuisoma kwa lengo hilo. Katika Biblia, kwa hakika, aliwapata watakatifu, lakini wakiwa tofauti na jinsi walivyoelezwa katika kalenda ya Kiroma. Mafuriko ya nuru ya Mungu yalimwagika katika akili yake. Kwa mshangao na karaha aliacha kazi aliyokuwa amejipangia na kuanza kujifunza neno la Mungu kwa makini. Kweli za thamani alizozipata humo muda sio mrefu alianza kuzifundisha.PKSw 159.1

    Mwaka 1512, kabla Luther na Zwingli hawajaanza kazi ya matengenezo, Levre aliandika: “Ni Mungu anayetupatia, kwa imani, uadilifu ambao kwa huo peke yake tunahesabiwa haki kwa ajili ya umilele.”—Wylie, b. 13, ch. 1. Alipotafakari sana juu ya siri za ukombozi, alisema kwa mshangao: “Ee, ukuu usioelezeka wa kubadilishana,—Yeye asiyekuwa na dhambi anahukumiwa, na yeye aliye na hatia anaachwa huru; Mbaraka unabeba laana, na aliyelaaniwa anapata mbaraka; Mzima anakufa, na mfu anaishi; Utukufu unafichwa katika giza, na yule aliyekuwa hajui cho chote isipokuwa aibu anavikwa utukufu.”— D'Aubigne, London ed., b. 12, ch. 2.PKSw 159.2

    Na wakati akifundisha kuwa utukufu wa wokovu ni wa Mungu pekee, alisema pia kuwa wajibu wa utii ulikuwa wa mwanadamu. “Ikiwa wewe ni mshiriki wa kanisa la Kristo,” alisema, “wewe ni kiungo cha mwili wa Kristo; ikiwa wewe ni wa mwili Wake, basi wewe ni wa tabia ya Mungu.... Laiti, watu wangeweza kupata ufahamu wa fursa hii, kwa kiasi gani wangeishi maisha safi, ya haki, na matakatifu, na ni kwa kiasi gani wangepatana, wakilinganishwa na utukufu uliomo ndani yao,—utukufu ule ambao jicho la kimwili haliwezi kuuona,—ikiwa wangefikiria utukufu wote wa ulimwengu huu.”—Ibid., b. 12, ch. 2.PKSw 159.3

    Walikuwemo miongoni mwa wanafunzi wa Lefevre waliosikiliza kwa makini maneno yake, na ambao, muda mrefu baada ya sauti ya mwalimu wao kunyamazishwa, wangeendelea kutangaza ukweli. Mtu kama huyo alikuwa William Farel. Alikuwa mtoto wa wazazi wacha Mungu, na aliyeelimishwa kupokea kwa imani isiyo na maswali mafundisho ya kanisa, ambaye angeweza kusema, kama mtume Paulo, aliyesema juu yake mwenyewe: “Nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa” (Matendo 26:5). Mfuasi wa Kiroma madhubuti, aliwachoma moto kwa bidii na kuwaangamiza watu wote waliothubutu kulipinga kanisa. “Nilisaga meno yangu kama mbwa mwitu mwenye hasira,“alisema baadaye, akielezea kipindi hiki cha maisha yake, “niliposikia mtu ye yote akisema neno lolote dhidi ya papa.”—Wylie, b. 13, ch. 2. Alikuwa hachoki kuwaabudu watakatifu, akiwa na Lefevre wakizungukia makanisa ya Paris, wakiabudu kwenye madhabahu, na kuyapamba maeneo matatifu kwa zawadi. Lakini matendo haya ibada hayakuleta amani katika mioyo yao. Hatia ya dhambi ilibaki moyoni, ambayo matendo yote ya toba aliyoyafanya hayakuweza kuiondoa. Kama sauti iliyotoka mbinguni alisikia maneno ya Mwanamatengenezo: “Wokovu ni kwa neema.” “Asiye na hatia amehukumiwa, na mhalifu ameachiliwa.” “Ni msalaba wa Kristo pekee unaofunua malango ya mbinguni, na unaofunga malango ya kuzimu.”— Ibid., b. 13, ch. 2.PKSw 159.4

    Farel kwa furaha aliupokea ukweli. Kwa maongezi kama yale ya Paulo aliachana na utumwa wa mapokeo na badala yake alipokea uhuru wa wana wa Mungu. “Badala ya moyo wa mwuaji wa mbwa mwitu mkali,” aligeuka, alisema, “akawa mkimya kama mwanakondoo mpole, asiye na madhara, moyo wake ukiwa umehamishwa kabisa kutoka kwa papa na kuwekwa kwa Yesu Kristo.”—D'Aubigne, b. 12, ch. 3.PKSw 160.1

    Wakati Lefevre akiendelea kueneza nuru miongoni mwa wanafunzi wake, Farel, akiwa na juhudi upande wa Kristo kama aliyokuwa nayo upande wa papa, alitoka na kutangaza ukweli hadharani. Kiongozi mkubwa wa kanisa, askofu wa Meaux, muda mfupi baadaye, aliungana nao. Walimu wengine waliokuwa mashuhuri kwa sababu ya uwezo wao na elimu yao kubwa waliungana nao katika kutangaza injili, na injili ilipata wafuasi miongoni mwa matabaka yote ya watu, kutoka katika nyumba za mafundi na wakulima hadi katika ikulu ya mfalme. Dada wa Fransis I, mfalme aliyetawala wakati huo, aliipokea imani ya matengenezo. Mfalme mwenyewe, na mama malkia, walionekana kwa muda fulani kuunga mkono kazi ya injili, na kwa matumaini makubwa Wanamatengenezo walitarajia kufika wakati ambao nchi yote ya Ufaransa ingeongolewa na kuiamini injili.PKSw 160.2

    Lakini matumaini yao hayakutimia. Majaribu na mateso yaliwasubiri wanafunzi wa Kristo. Jambo hili, hata hivyo, lilifichwa lisionekana machoni pao. Wakati wa amani ulitangulia kwanza, ili wajenge uimara wa kukutana na dhoruba; na Matengenezo yalipiga hatua kubwa ya maendeleo. Askofu wa Meaux alifanya kazi kwa juhudi kubwa katika daiyosisi yake kuwafundisha mapadri na watu wa kawaida. Mapadri wasio na elimu na wasio na maadili waliondolewa kazini, na, kwa kadiri ilivyowezekana, waliwekwa watu wenye elimu na wacha Mungu. Askofu alikuwa na shauku kuwa watu wake wapate neno la Mungu wao wenyewe, na jambo hili kwa muda mfupi lilifanikiwa. Lefevre alifanya kazi ya kutafsiri Agano Jipya; na wakati uleule ambao Biblia ya Kijerumani ya Luther ilikuwa ikitoka katika mitambo ya uchapishaji ya jiji la Wittenberg, Agano Jipya la Kifaransa lilichapishwa katika jiji la Meaux. Askofu alitumia nguvu zake zote na mali zake zote kuhakikisha kuwa Agano Jipya hilo linasambazwa katika parishi zake zote, na si muda mrefu wakulima wa Meaux walimiliki Maandiko Matakatifu.PKSw 160.3

    Kama wasafiri wanaoangamia kwa sababu ya kiu wanavyoshangilia kukutana na chemchemi ya maji, ndivyo roho hizi zilivyopokea ujumbe kutoka mbinguni. Wafanya kazi katika mashamba, mafundi katika karakana, walifurahia kazi zao za suluba kwa kujadili kweli za thamani za Biblia. Nyakati za jioni, badala ya kwenda kuburudika katika vilabu vya pombe, walijifunza katika nyumba zao ili wajisomee neno la Mungu na kuungana katika maombi na kusifu. Badiliko kubwa lilionekana kwa muda mfupi katika jumuia hizi. Ingawa walikuwa watu wa tabaka la chini, wakulima wasio na elimu wachapa kazi, nguvu inayobadilisha, inayoinua ya neema ya Mungu ilionekana katika maisha yao. Wakiwa wanyenyekevu, wenye upendo, na watakatifu, walisimama kama mashahidi wa kile ambacho injili inaweza kufanya kwa wale wanaoipokea kwa moyo wa dhati.PKSw 161.1

    Nuru iliyowashwa pale Meaux ilitupa miale yake mbali. Kila siku idadi ya waongofu ilikuwa ikiongezeka. Hasira ya viongozi wa kanisa ilidhibitiwa kwa muda na mfalme ambaye alidharau ufinyu wa mawazo na ubinafsi wa watawa; lakini viongozi wa upapa walishinda hatimaye. Sasa mateso yalianza. Askofu wa Meaux, alilazimishwa kuchagua kati ya moto na kukana, akachagua kukana; lakini pamoja na anguko la kiongozi, kondoo wake walibaki wakiwa na msimamo imara. Wengi walitoa ushuhuda wa ile kweli katikati ya ndimi za moto. Kwa ujasiri wao na uaminifu wao wakiwa motoni, Wakristo hawa wanyenyekevu walihubiri maelfu ya watu ambao katika siku za amani hawakuwahi kusikia ushuhuda wao.PKSw 161.2

    Siyo watu wa chini na walio maskini peke yao ambao katikati ya mateso na dharau walidiriki kushuhudia kwa ajili ya Kristo. Katika vyumba vya kifahari vya majumba makubwa na ikulu walikuwepo watu wa tabaka la juu ambao kwao ukweli ulikuwa wa thamani zaidi kuliko mali au cheo au hata uhai wenyewe. Ngao ya kifalme ilificha roho ya juu na imara zaidi kuliko ya joho na kofia ya kiaskofu. Louis de Berquin alikuwa mzaliwa wa ukoo wa kifalme. Mshauri wa ikulu aliye jasiri, alikuwa msomi makini, muungwana, na mwadilifu. Mwandishi anasema, “Alikuwa mfuasi mkubwa wa taasisi za kipapa, na msikilizaji mkubwa wa misa na mahubiri; ... na alifunika sifa zake zote zingine kwa chuki maalumu dhidi ya Ulutheri.” Lakini, kama watu wengi wengine, aliongozwa na Mungu kuipata na kuisoma Biblia, alishangazwa kukuta humo, “hakuna mafundisho ya Roma, badala yake aliyakuta mafundisho ya Luther.”—Wylie, b. 13, ch. 9. Tangu hapo alijiweka wakfu kikamilifu kujifunza injili.PKSw 161.3

    “Msomi wa juu kabisa miongoni mwa waungwana wa daraja la juu wa Ufaransa,” akili zake nyingi na uwezo wake wa kuongea kwa ufasaha, ujasiri wake usiokubali kushindwa na juhudi zake za kishujaa, na mvuto wake katika nyumba ya mfalme,—kwani alikuwa na upendeleo maalumu wa mfalme,— vilimfanya achukuliwe na wengi kuwa mtu ambaye alikuwa amechaguliwa na Mungu awe Mwanamatengenezo wa nchi yake. Alisema Beza: “Berquin angeweza kuwa Luther wa pili, ikiwa Fransis I angekuwa elekta wa pili.” “Yeye ni mbaya zaidi kuliko Luther,” walisema watetezi wa upapa.—Ibid., b. 13, ch. 9. Wafuasi wa Uroma wa Ufaransa walimwogopa sana. Walimtupa gerezani kama mzushi, lakini aliachiwa huru na mfalme. Kwa miaka mgogoro uliendelea. Fransis, akiyumba kati ya Uroma na Matengenezo, kwa mpokezano alistahimili na alizuia juhudi za kikatili za watawa. Berquin alifungwa gerezani mara tatu na mamlaka za kipapa, lakini aliachiliwa na mfalme, ambaye, kwa kuvutiwa na uwezo wake wa akili na tabia yake ya kiungwana, alikataa kumtoa kafara katika uovu ule wa ukasisi.PKSw 162.1

    Berquin alionywa mara kwa mara juu ya hatari iliyomkabili nchini Ufaransa, na alisihiwa afuate nyayo za wale waliopata usalama kwa kukimbilia uhamishoni kwa hiari. Erasmus, mtu mwoga na mtu aliyejali maslahi ya muda mfupi, ambaye pamoja na upana wa elimu yake alishindwa katika ukuu wa kimaadili ambao unasalimisha maisha na heshima chini ya ile kweli; alimwandikia Berquin: “Omba upelekwe kama balozi katika nchi ya kigeni; nenda na ukasafari katika nchi ya Ujerumani. Unamjua Beda na jinsi alivyo—yeye ni jitu la kutisha lenye vichwa elfu moja, linalorusha sumu kali kila upande. Maadui zako wanaitwa jeshi. Hata kama kazi yako ingekuwa bora zaidi kuliko ya Yesu Kristo, hawangekuacha uondoke bali wangekuua kikatili. Usiamini sana ulinzi wa mfalme. Kwa hali yo yote ile, usinihusishe na kitivo cha teolojia.”—Ibid., b. 13, ch. 9.PKSw 162.2

    Lakini hatari zilivyoongezeka, juhudi za Berquin zilizidi kuimarika zaidi. Licha ya kuukataa ushauri wa kisiasa na kinafsi wa Erasmus, aliazimia kuchukua hatua za kijasiri zaidi. Siyo tu kuwa alisimama kuutetea ukweli, bali alishambulia makosa pia. Shitaka la uzushi ambalo viongozi wa Roma walilielekeza kwake, alilielekeza kwao. Wapinzani wake wakuu na wenye uchungu na juhudi kubwa walikuwa madaktari na watawa wasomi wa idara ya teolojia katika chuo kikuu mashuhuri cha Paris, moja ya mamlaka kuu ya kidini katika jiji na taifa. Kutokana na maandishi ya hawa madaktari wasomi, Berquin alipata hoja kumi na mbili ambazo alitangaza hadharani kuwa “pinzani dhidi ya Biblia, na uzushi;” na alimwomba mfalme awe mwamuzi katika pambano hilo.PKSw 162.3

    Mfalme, kwa kutokuona tatizo lolote la kukutanisha pande hizi mbili zinazosigana za wasomi wazamivu na wabobezi, na kwa kufurahia kupata fursa ya kunyenyekeza kiburi cha hawa watawa wenye majivuno, aliwaagiza viongozi wa kipapa kutetea hoja zao kwa kutumia Biblia. Silaha hii, walijua kabisa, isingewafaa sana; kifungo, mateso, na mti wenye ncha kali ndizo silaha walizojua jinsi ya kuzitumia kwa mafanikio makubwa zaidi. Sasa meza zilikuwa zimepinduliwa, na walijiona wakiwa karibu kutumbukia katika shimo walilokuwa wametumaini kumtumbukiza Berquin. Kwa mshangao walitafuta karibu yao njia ya kutorokea.PKSw 163.1

    “Karibu na wakati huo sanamu ya Bikra kwenye kona ya moja ya mitaa, iliharibiwa.” Kulikuwa na taharuki katika jiji. Makundi ya watu walifurika mahali pale, wakiwa na mwonekano wa maombolezo na hasira. Mfalme pia alishitushwa sana. Hapa kulikuwa na fursa ambayo watawa waliweza kuigeukia ili kujenga hoja, na walidaka na kuiwekea maelezo haraka haraka. “Haya ni matunda ya mafundisho ya,” walipiga kelele. “Kila kitu kinakwenda kupinduliwa—dini, sheria, kiti cha enzi chenyewe—na hila za KiLutherrani.”— Ibid., b. 13, ch. 9.PKSw 163.2

    Berquin alikamatwa tena. Mfalme aliondoka katika jiji la Paris, na kwa njia hiyo watawa waliachwa wafanye walivyopenda wenyewe. Mwanamatengenezo alishitakiwa na alihukumiwa kifo, na ili Fransis asije akaingilia kati kumwokoa, hukumu ilitekelezwa siku hiyo hiyo iliposomwa. Wakati wa mchana Berquin alipelekwa mahali pa kifo. Umati wa watu ulikusanyika kushuhudia tukio lile, na kulikuwa na watu wengi waliotazama kwa mshangao na mashaka kuwa mhanga alikuwa amechaguliwa kutoka miongoni mwa watu wema na wajasiri katika familia za kiungwana za Kifaransa. Mshangao, hasira, dharau, na chuki kali vilitia giza katika nyuso za kundi la watu lililokuwa likiongezeka; lakini katika uso mmoja hakukuwa na kivuli cho chote. Mawazo ya mfia dini yalikuwa mbali na mandhari ile ya makelele; alihisi tu uwepo wa Bwana wake.PKSw 163.3

    Mkokoteni mbovu alioupanda, nyuso zilizokunjamana za watesaji wake, kifo cha kutisha alichokuwa akikiendea, haya hakuyajali; Yeye aliye hai aliyewahi kufa, na yu hai milele na milele, na anazo funguo za mauti na kuzimu, alikuwa kando yake. Uso wa Berquin uling'aa kwa nuru na amani ya mbinguni. Alikuwa amevaa nguo nzuri, alikuwa amevaa “joho la mahameli, jaketi la kubana la mchanganyiko wa hariri na pamba, na soksi za rangi ya dhahabu.”—D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 2, ch. 16. Alikuwa anakwenda kushuhudia kwa ajili ya imani yake mbele ya Mfalme wa wafalme na ulimwengu uliokuwa ukishuhudia, na hakuna kilio ambacho kificha furaha yake.PKSw 163.4

    Wakati msafara ukitembea pole pole, ukipita katika mitaa iliyofurika watu, watu waligundua kwa mshangao amani isiyokuwa na mawingu, ushindi wenye furaha wa mwonekano na mwenendo wake. Walisema, “Yeye ni, kama mtu anayekaa katika hekalu, na anatafakari juu ya mambo matakatifu.”— Wylie, b. 13, ch. 9.PKSw 163.5

    Akiwa amefungwa kwenye mti kwa ajili ya kuchomwa moto, Berquin alijaribu kusema maneno machache kwa watu; lakini watawa, wakihofia matokeo, walianza kupiga kelele, na maaskari waligonganisha silaha zao, na kelele zao zilizima sauti ya mfia dini. Kwa njia hiyo mwaka 1529 mamlaka ya juu kabisa ya uandishi na ya kikanisa ya Paris iliyoendelea “iliuwekea umma wa 1793 mfano mbaya wa kuzima maneno matakatifu ya watu wanaokufa juu ya jukwaa la kunyongea wahalifu.”—Ibid., b. 13, ch. 9.PKSw 164.1

    Berquin alinyongwa, na mwili wake ulichomwa kwa ndimi za moto. Habari za kifo chake zilileta huzuni kwa marafiki wa Matengenezo katika nchi yote ya Ufaransa. Lakini mfano wake haukupotea. “Sisi, pia, tuko tayari,” walisema mashahidi wa ukweli, “kukabiliana na kifo kwa furaha, tukielekeza macho yetu kwa maisha yajayo.”—D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 2, ch. 16.PKSw 164.2

    Wakati wa mateso ya Meaux, walimu wa imani ya matengenezo walinyang'anywa leseni za kuhubiri, na walijiunga na shughuli zingine. Baada ya muda mfupi, Lefevre aliondoka na kwenda zake nchini Ujerumani. Farel alirudi katika mji alikozaliwa upande wa mashariki ya Ufaransa, kueneza nuru katika mji wa nyumbani alikolelewa. Tayari habari zilikuwa zimepokelewa za kile kilichokuwa kikiendelea mjini Meaux, na ukweli, ambao aliufundisha bila woga na kwa juhudi kubwa, ulipata wasikilizaji. Muda si mrefu mamlaka zilishituka na kuanza kutafuta jinsi ya kumnyamazisha, na alifukuzwa mjini. Ingawa alikuwa hawezi tena kuhubiri hadharani, alisafiri huko na huko katika nyika na vijiji, akifundisha katika nyumba za watu binafsi na maeneo yenye nyasi yaliyo pweke, na kutafuta maficho katika misitu na mapango yaliyokuwa katikati ya miamba, maeneo ambayo aliyatembelea wakati wa ujana wake. Mungu alikuwa akiwaandaa kwa ajili ya majaribu makubwa zaidi. “Misalaba, mateso, na vitendea kazi vya Shetani, ambavyo nilionywa juu yake hapo awali, havijaondoka,” alisema; “vimekuwa vikali zaidi kuliko ninavyoweza kuhimili mwenyewe; lakini Mungu ni Baba yangu; Yeye amenipa na daima atanipa nguvu ninayoihitaji.”—D'Aubigne, History of the Reformation of the Sixteenth Century, b. 12, ch. 9.PKSw 164.3

    Kama ilivyokuwa katika siku za mitume, mateso yalikuwa “yametokea zaidi kwa kuieneza Injili” (Wafilipi 1:12). Wakiwa wamefukuzwa Paris na Meaux, “wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno” (Matendo 8:4). Na kwa njia hiyo nuru iliweza kuenea katika maeneo ya mbali ya nchi ya Ufaransa.PKSw 164.4

    Mungu alikuwa bado akiandaa watenda kazi wa kueneza injili Yake. Katika moja ya shule za Paris kulikuwepo na kijana mwenye tafakari ya kina, mkimya, tayari akionesha ushahidi wa kuwa na akili yenye nguvu na inayopenya, na alijukana kwa maisha safi yasiyokuwa na lawama kama alivyojulikana kwa uwezo wa akili na bidii katika masuala ya dini. Uwezo wake wa kiakili na uchapakazi wake kwa muda mfupi vilimfanya awe mtu wa kujivunia hapo chuoni, na ilitarajiwa kuwa John Calvin angekuwa mmoja wa watetezi wa kanisa mwenye uwezo mkubwa na heshima nyingi. Lakini nuru ya Mungu ilipenya hata katika kuta za falsafa za uanazuoni na ushirikina ambamo Calvin alikuwa amefungwa ndani yake. Alisikia mafundisho mapya kwa mshtuko, na hakuwa na shaka kuwa wazushi walistahili moto ambao walichomwa nao. Lakini bila kukusudia alikutana uso kwa uso na uzushi na alilazimishwa kupima uwezo wa teolojia ya Kiroma kukabiliana na mafundisho ya Kiprotestanti.PKSw 165.1

    Binamu wa Calvin, aliyekuwa amejiunga na Wanamatengenezo, alikuwa jijini Paris. Ndugu hawa wawili walikutana mara kwa mara kujadili masuala yaliyokuwa yakisumbua ulimwengu wa Kikristo. “Kuna dini mbili katika ulimwengu,“alisema Olivetan, Mprotestanti.” Dini ya kwanza ni ile iliyobuniwa na wanadamu, ambayo ndani yake mwanadamu anajiokoa mwenyewe kwa njia ya sherehe na matendo mema; nyingine ni ile ambayo imefunuliwa katika Biblia, na ambayo humfundisha mwanadamu kutafuta wokovu kutoka kwa neema ya Mungu pekee.” “Sipokei hata moja ya mafundisho yenu mapya,” Calvin alisema kwa mkazo; “mnadhani mimi nimeishi katika makosa siku zangu zote?”—Wylie, b. 13, ch. 7.PKSw 165.2

    Lakini fikra zilikuwa zimeamshwa katika akili yake ambazo asingeweza kuziondoa kwa utashi wake mwenyewe. Akiwa peke yake chumbani aliyatakafari maneno ya binamu yake. Hatia ya dhambi ilimshika; alijiona mwenyewe, bila mwombezi, mbele ya Jaji mtakatifu na mwenye haki. Maombi ya watakatifu, matendo mema, sherehe za kanisa, vyote havikuwa na nguvu ya kuondoa hatia ya dhambi. Hakuweza kuona kitu cho chote zaidi ya giza la kukata tamaa milele. Madaktari wasomi wa kanisa walijaribu kupoza maumivu yake ya rohoni bila mafanikio. Ungamo na kitubio vilijaribishwa bila mafanikio; visingeweza kupatanisha roho na Mungu.PKSw 165.3

    Akiwa bado katika mapambano haya yasiyokuwa na matunda, Calvin, bila kupanga, alitembelea moja ya viwanja vya umma vilivyotumika kutesea watu, akashuhudia kuchomwa moto kwa mzushi. Alishangazwa na amani iliyokuwa katika uso wa mfia dini. Katikati ya maumivu ya kifo kile cha kutisha, na chini ya hukumu ya kutisha zaidi ya kanisa, alionesha imani na ujasiri ambao kijana huyu mwanafunzi, Calvin, aliutofautisha kwa maumivu makali na kukata tamaa kwake mwenyewe na giza la moyoni mwake, wakati akilitii kanisa kikamilifu. Alijua kuwa wazushi walikita imani yao katika Biblia. Aliazimia kuisoma, ili agundue, ikiwezekana, siri ya furaha yao.PKSw 165.4

    Katika Biblia alimpata Kristo. “Ee Baba,” alilia, “Kafara Yake imepoza hasira Yako; Damu Yake imeosha uchafu wangu; Msalaba Wake umebeba laana yangu; Kifo chake kimenipatanisha na Mungu. Tumebuni kwa ajili yetu wenyewe mambo mengi ya kipumbavu ambayo hayana faida, lakini umeweka mbele yangu neno Lako kama mwenge, nawe umegusa moyo wangu, ili nichukie mambo yote mengine isipokuwa yale tu ya Yesu.”— Martyn, vol. 3, ch. 13.PKSw 166.1

    Calvin alisomea upadri. Wakati akiwa na umri wa miaka kumi na mbili alichaguliwa kuwa mlezi wa kanisa dogo, na kichwa chake kilinyolewa na askofu kulingana na sheria za kanisa. Hakufanyiwa huduma ya upadrisho, wala hakufanya majukumu ya upadri, lakini alihesabiwa kuwa miongoni mwa mapadri, akishikilia cheo chake, na akipokea posho kwa kazi hiyo.PKSw 166.2

    Sasa, akihisi kwamba kamwe asingekuwa padri, aliamua kujifunza sheria kwa muda fulani, lakini hatimaye aliachana na lengo hilo na aliazimia kutoa maisha yake kwa kazi ya injili. Lakini alisita kuwa mwalimu wa hadhara. Kwa asili alikuwa mtu mwoga, na alikuwa na mzigo kwa ajili ya wajibu mzito wa cheo chake, na alitamani kuwekeza maisha yake katika kujifunza. Mashauri ya dhati ya marafiki, hatimaye, yalipata ukubali. “Ni jambo la kushangaza sana,” alisema,“kwamba mtu mwenye asili hali ya chini hivyo anaweza kuinuliwa na kupewa heshima kubwa kiasi hicho.”—Wylie, b. 13, ch. 9.PKSw 166.3

    Calvin alianza kazi yake kimya kimya, na maneno yake yalikuwa kama matone ya umande yanayoburudisha ardhi. Alikuwa ameondoka Paris, na sasa alikuwa katika mji wa jimbo chini ya ulinzi wa binti wa mfalme aliyeitwa Margaret ambaye, kwa kuipenda injili, alipanua ulinzi wake kwa wanafunzi wengine wa injili. Calvin alikuwa bado kijana, mwenye haiba ya uungwana, isiyojikuza. Kazi yake ilianza na watu katika nyumba zao. Akiwa amezungukwa na watu wa nyumbani, alisoma Biblia na alifungua ukweli wa wokovu. Waliosikia ujumbe walichukua habari njema kwa wengine, na muda si mrefu mwalimu alivuka mipaka ya jiji hadi katika miji na mitaa ya nje ya jiji. Aliingia katika majumba na vijumba, na alisonga mbele, akiweka msingi wa makanisa ambayo yangeweza kutoa ushuhuda kwa ajili ya ukweli bila hofu.PKSw 166.4

    Baada ya miezi mitatu alirudi Paris. Kulikuwepo na misukosuko isiyokuwa ya kawaida miongoni mwa watu wenye elimu na wasomi. Masomo ya lugha za kale yaliwaongoza watu kuisoma Biblia, na wengi ambao mioyo yao haikuguswa na ukweli wake walijadili kwa ukweli huo kwa shauku kubwa na hata kupambana na mashujaa wa Uroma. Calvin, japokuwa alikuwa mpambanaji katika tasnia ya malumbano ya hoja za kiteolojia, alikuwa na utume wa juu zaidi wa kutekeleza kuliko ule wa kelele za wasomi. Akili za watu zilitikiswa, na sasa ulikuwa wakati wa kuwafungulia ukweli. Wakati kumbi za vyuo vikuu zilijazwa kwa makelele ya malumbano ya kiteolojia, Calvin alikuwa akitembea kutoka nyumba kwa nyumba, akiwafungulia watu Biblia, na akiwaelezea habari za Kristo na Yeye aliyesulubiwa.PKSw 166.5

    Kwa uongozi wa Mungu, Paris ilipewa wito mwingine wa kuipokea injili. Wito wa Lefevre na wa Farel ilikuwa imekataliwa, lakini tena ujumbe ilipaswa usikiwe na watu wa matabaka yote katika jiji lile kubwa. Kwa sababu za kisiasa, mfalme alikuwa hajaamua kuwa upande wa Roma kikamilifu dhidi ya Matengenezo. Margaret bado aling'ang'ania tumaini kuwa Uprotestanti ulikuwa unakwenda kushinda. Margaret aliazimia kuwa imani ya matengenezo ilipaswa kuhubiriwa katika jiji la Paris. Wakati wa kutokuwepo kwa mfalme, aliamuru mchungaji wa Kiprotestanti ahubiri katika makanisa ya jiji. Baada ya jambo hili kukataliwa na viongozi wakuu wa upapa, binti wa mfalme alifungua milango ya ikulu. Chumba kiliandaliwa kitumike kama kanisa, na ilitangazwa kuwa kila siku, katika saa fulani maalumu iliyopangwa, hubiri lingehubiriwa, na watu wa kila tabaka na hadhi walialikwa kuhudhuria. Makundi ya watu walifurika kusikiliza mahubiri. Siyo tu kwenye kanisa dogo, lakini pia vyumba vya kungojea na kumbi zilijaa. Maelfu ya watu kila siku walikusanyika—wana wa mfalme, wanasiasa, wanasheria, wafanya biashara, na mafundi. Mfalme, badala ya kupiga marufuku mikusanyiko, aliamrisha kuwa makanisa mawili ya jiji la Paris yafunguliwe. Ilikuwa haijawahi kutokea kwa jiji kutikiswa na neno la Mungu kama wakati huo. Roho ya uzima kutoka mbinguni ilionekana kama vile imepuliziwa kwa watu. Kiasi, usafi, utaratibu, na bidii vilikuwa vikichukua nafasi ya ulevi, ubadhirifu, migogoro, na uvivu.PKSw 167.1

    Lakini mamlaka za kanisa hazikujikalia kivivu. Mfalme bado alikataa kuingilia na kusimamisha mahubiri, na mamlaka za Kiroma ziliwageukia wananchi. Hakuna njia ambayo haikutumika kuamsha hofu, chuki, na itikadi kali kwa umati uliokuwa katika ujinga na ushirikina. Kwa kujisalimisha bila kuelewa mambo vizuri kwa walimu wao wa uongo, Paris, kama mji wa Yerusalemu wa zamani, hakujua wakati wa kujiliwa kwake wala hakujua mambo yaliyopasa kujua ili kudumisha amani yake. Kwa miaka miwili neno la Mungu lilihubiriwa katika mji mkuu; lakini, wakati wakiwepo wengi walioikubali injili, watu walio wengi zaidi waliikataa. Fransis alijifanya kuwa na uvumilivu wa kidini kwa muda, lakini ilikuwa kwa kusudi la kulinda maslahi yake binafsi, na watetezi wa upapa walifaulu kurudi Fansikatika umaarufu na utawala. Kwa mara nyingine makanisa yalifungwa, na mateso yakaanza.PKSw 167.2

    Calvin alikuwa bado Paris, akijiandaa kwa kujifunza, kutafakari, na kuomba kwa ajili ya kazi yake ya baadaye, na aliendelea kueneza nuru. Hatimaye, hata hivyo, mashaka yalijengeka juu yake. Mamlaka za kanisa ziliazimia kumleta katika ndimi za moto. Akijidhania kuwa salama katika chumba cha peke yake, hakuwa na wazo lo lote la hatari, wakati marafiki walipofika chumbani mwake wakiwa na haraka wakiwa na habari kuwa maofisa walikuwa njiani kuja kumkamata. Wakati huo huo walisikia watu wakigonga kwa nguvu kwenye lango la nje. Hakukuwa na muda wa kupoteza. Baadhi ya marafiki zake walifanya kazi ya kuwachelewesha maofisa mlangoni, wakati marafiki zake wengine wakimsaidia kutoroka kupitia dirishani, baada ya kutoka aliondoka haraka kuelekea katika maeneo ya nje ya jiji. Baada ya kupata hifadhi katika kibanda cha kibarua aliyekuwa muumini wa matengenezo, alijigeuza kwa kuvaa nguo za mwenyeji wake, na, akiwa amebeba jembe begani, alianza safari yake. Akisafiri kuelekea upande wa kusini, alipata tena kimbilio katika utawala wa Margaret. (Tazama D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 2, ch. 30.)PKSw 167.3

    Alibaki hapa kwa miezi michache, akiwa salama chini ya ulinzi wa marafiki wenye nguvu, na akiendelea kujifunza kama hapo awali. Lakini moyo wake ulikuwa umejielekeza kuihubiri Ufaransa, na hakuweza kutulia kwa muda mrefu. Muda mfupi baada ya dhoruba kutulia kwa kiasi fulani, alitafuta eneo la kufanyia kazi kule Pointiers, palipokuwa na chuo kikuu, na mahali ambapo mawazo mapya yalikuwa yamekubalika. Watu wa tabaka zote walisikiliza injili kwa furaha. Hakukuwa na mahubiri ya hadhara, bali katika nyumba ya hakimu mkuu, katika nyumba yake ya kulala, na nyakati zingine katika bustani ya umma, Calvin alifungua maneno ya uzima kwa wale waliopenda kusikiliza. Baada ya muda mfupi, idadi ya wasikilizaji ilipoongezeka, ilifikiriwa kuwa salama zaidi kukutania nje ya jiji. Pango lililokuwa ubavuni mwa bonde lenye kina kirefu na jembamba, mahali ambapo miti na miamba iliinamia liliweka mazingira yaliyojificha kikamilifu zaidi, lilichaguliwa kuwa mahali pa kukutania. Makundi madogo madogo, yakiondoka jijini kwa njia tofauti, yalielekea kule. Katika kituo hiki kitulivu Biblia ilisomwa kwa sauti na kufafanuliwa. Hapa Meza ya Bwana ilisherehekewa kwa mara ya kwanza na Waprotestanti wa Ufaransa. Kutokana na kanisa hili wainjilisti waaminifu walitumwa kwenda maeneo mengine.PKSw 168.1

    Kwa mara nyingine tena Calvin alirudi Paris. Hata wakati huo bado alikuwa na tumaini kuwa Ufaransa kama taifa itapokea Matengenezo. Lakini aligundua kuwa karibu kila mlango wa kazi ulikuwa umefungwa. Kufundisha injili ilikuwa kuingia katika barabara iliyoelekea moja kwa moja kwenye nguzo ya kuchomea watu moto, na hatimaye aliazimia kuondoka na kwenda Ujerumani. Muda mfupi tu baada ya kuondoka Ufaransa dhoruba ya mateso iliwapasukia Waprotestanti, kiasi kwamba, ikiwa angeendelea kukaa hapo, lazima angeingizwa katika maangamizi ya jumla.PKSw 168.2

    Wanamatengenezo Wafaransa, wakiwa na shauku ya kuiona nchi yao ikiwa na kasi sawa na Ujerumani na Uswisi, waliazimia kupiga bomu kwa ujasiri dhidi ya ushirikina wa Roma—bomu ambalo lingeamsha taifa lote. Katika kutekeleza jambo hilo mabango yaliyoshambulia misa katika usiku mmoja yalibandikwa katika nchi yote ya Ufaransa. Badala ya kuendeleza matengenezo, hatua hii ya kijasiri lakini isiyokuwa na busara ilileta madhara, siyo tu kwa walioitekeleza, bali pia kwa marafiki wa imani ya matengenezo katika nchi yote ya Ufaransa. Iliwapa viongozi wa Roma kile walichokuwa wakikitafuta kwa muda mrefu—kisingizio cha kudai kuwaua wazushi kama watu wenye fujo walio hatari kwa uimara wa kiti cha enzi na amani ya taifa.PKSw 168.3

    Kwa njia ya mkono wa siri—iwe wa rafiki asiye na tahadhari au wa adui mwenye hila haikuweza kujulikana—moja ya mabango lilibandikwa kwenye mlango wa chumba cha kulala cha mfalme. Mfalme alipata hofu sana. Kwenye bango hilo, mambo ya kishirikina yaliyoheshimiwa kwa zama nyingi yalikuwa yameshambuliwa kwa mkono usio na hofu. Na huu ujasiri usio na mfano wa kuandika maneno haya ya wazi na kushtusha mbele ya mfalme uliamsha ghadhabu ya mfalme. Kwa mshangao alisimama kwa muda mfupi akitetemeka huku akiwa kimya. Hatimaye ghadhabu yake ilianza kuongea maneno ya kutisha: “Wakamatwe wote bila kumwacha mtu ye yote anayeshukiwa kuwa mfuasi wa uzushi wa Luther. Nitawanyonga wote.— Ibid., b. 4, ch. 10. Uamuzi ukafanyika. Mfalme aliazimia kujitupa kikamilifu upande wa Roma.PKSw 169.1

    Hatua zilichukuliwa mara moja kumkamata kila mfuasi wa Luther katika jiji la Paris. Fundi mmoja maskini, mfuasi wa imani ya matengenezo, aliyekuwa na mazoea ya kuwaita waumini waende katika mikutano yao ya siri, alikamatwa na, kwa tishio la kuuawa mara moja kwenye nguzo ya kuchomea watu, aliamuriwa kuongoza wajumbe wa papa kwenda kwa nyumba ya kila Mprotestanti katika jiji. Alisita kwa hofu kubwa kukubaliana na pendekezo hilo, lakini hatimaye hofu ya ndimi za moto ilishinda, na alikubali kuwa msaliti wa ndugu zake. Akiwa ametanguliwa na mwenyeji wake, na akiwa amezungukwa na kundi la mapadri, wabeba vyetezo, watawa, na maaskari, Morin, mpelelezi wa mfalme, akiwa na msaliti, polepole na kimyakimya walipita katika mitaa ya jiji. Gwaride lilionekana kama la kuheshimu “sakramenti takatifu,” tendo la kulipa fidia kwa ajili ya tusi la wapinzani dhidi ya misa. Lakini gwaride hilo lilificha kusudio la mauaji. Baada ya kufika karibu na nyumba ya mfuasi wa Luther, msaliti alionesha ishara, lakini bila kutamka neno lo lote. Msafara ulisimama, nyumba iliingiwa, wanafamilia waliburuzwa nje na kufungwa minyororo, na kikundi cha kutisha kiliendelea mbele kutafuta wahanga wapya. Msafara huu “haukuacha nyumba yo yote, iwe kubwa au ndogo, hata vyuo vilivyokuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Paris.... Morin alitetemesha jiji lote.... Ulikuwa utawala wa hofu.”—Ibid., b. 4, ch. 10.PKSw 169.2

    Wahanga waliuawa kwa maumivu ya kutisha, hususan kwa kuwa iliamuriwa kuwa moto upunguzwe ili kurefusha muda wa uchungu wao. Lakini walikuwa kama washindi. Msimamo wao haukuyumba, amani yao haikuwa na mashaka. Watesi wao, kwa kukosa nguvu ya kuyumbisha uthabiti wao usiobadilika, walijisikia kushindwa. “Vitanda vya kuchomea watu moto vilitawanywa katika mitaa yote ya Paris, na uchomaji watu ulifanywa kwa siku zilizofuata mfululizo, lengo likiwa kueneza hofu ya uzushi kwa kueneza mauaji. Faida, hata hivyo, hatimaye, ilibaki upande wa injili. Paris yote iliwezeshwa kuona aina ya watu ambao mawazo mapya yaliweza kuzalisha. Hakukuwa na mimbari bora zaidi kuzidi ile ya rundo la maiti za wafia dini. Furaha yenye amani iliyoangaza katika nyuso za hawa watu walipokuwa wakipita ... wakielekea mahali pa kunyongewa, ushujaa wao waliposimama katikati ya ndimi za moto zenye uchungu, msamaha wao wa unyenyekevu kwa maumivu waliyoyapata, vilibadilisha, siyo mara chache, hasira kuwa huruma, chuki kuwa upendo, na kuunga mkono kazi ya injili kwa ufasaha usiopingika.”—Wylie, b. 13, ch. 20.PKSw 169.3

    Makasisi, wakiwa wamejielekeza kudumisha hasira katika viwango vyake vya juu kama ilivyozoeleka, walisambaza mashtaka ya kutisha dhidi ya Waprotestanti. Waprotestanti walishitakiwa kwa kupanga njama za kuangamiza Wakatoliki, kupindua serikali, na kumwua mfalme. Hakuna hata kivuli cha ushahidi walichoweza kutoa ili kuthibitisha madai hayo. Hata hivyo utabiri huu wa matukio mabaya ulipaswa kufikia utimilifu; licha ya kwamba ilikuwa katika mazingira tofauti kabisa, , na kutokana na sababu zilizo kinyume kabisa katika namna yake. Mambo ya kikatili ambayo Wakatoliki waliwafanyia Waprotestanti wasiokuwa na hatia yalirundikana na kuwa mzigo wa kisasi, na baada ya karne nyingi yaliwaletea majanga yale yale ambayo walikuwa wameyatabiri kuwa yangekuja, juu ya mfalme, serikali yake, na raia wake; lakini yaliletwa na watu wasiomjua Mungu na wafuasi wa upapa wenyewe. Ilikuwa siyo ustawishaji, bali ukandamizaji wa Uprotestanti, ambao, miaka mia tatu baadaye, ulileta juu ya Ufaransa majanga haya.PKSw 170.1

    Mashaka, kutoaminiana, na hofu sasa vilienea katika matabaka yote ya jamii. Katikati ya taharuki ya jumla ya watu ilionekana jinsi ambavyo mafundisho ya Luther yalivyokuwa yameshika akili za watu waliokuwa na kiwango cha juu cha elimu, mvuto, na uzuri wa tabia. Nafasi za amana na heshima kwa ghafla zikawa tupu. Mafundi, wachapishaji, wasomi, maprofesa katika vyuo vikuu, waandishi, na hata watu wa mitaani, walitoweka. Mamia ya watu walilikimbia jiji la Paris, wakiwa wakimbizi kutoka katika nchi yao walikozaliwa, katika matukio mengi jambo lililoonesha kwa mara ya kwanza kuwa waliipenda imani ya matengenezo. Viongozi wa upapa waliwatazama watu hao kwa mshangao wakipata wazo la uwepo wa wazushi walioishi nao bila kujua. Hasira yao iliwaka juu ya makundi ya watu maskini waliokuwa ndani ya uwezo wao. Magereza yalijaa wafungwa, na hewa iligeuka kuwa na utusitusi kwa sababu ya wingi wa watu waliochomwa moto-watu waliounguzwa kwa kuikiri injili.PKSw 170.2

    Fransis I alikuwa ametukuka kwa kuwa kiongozi katika vuguvugu kubwa la elimu lililoashiria ufunguzi wa karne ya kumi na sita. Alifurahia kukusanya katika ikulu yake wasomi kutoka kila nchi. Kupenda kwake elimu na dharau yake dhidi ya ujinga na ushirikina wa watawa vilikuwa, kwa kiasi fulani, sababu ya uvumilivu aliouonesha kwa matengenezo. Lakini, kwa kuchochewa na juhudi ya kukomesha uzushi, mlezi huyu wa elimu alitoa amri iliyopiga marufuku uchapishaji wa vitabu katika nchi yote ya Ufaransa! Fransis I anawasilisha mmoja miongoni mwa mifano mingi iliyopo katika kumbukumbu kuwa makuzi ya kiakili siyo tiba dhidi ya chuki za kidini na mateso.PKSw 171.1

    Kwa njia ya sherehe kubwa na ya hadhara Ufaransa ilijiweka kikamilifu katika kuangamiza Uprotestanti. Makasisi walidai kuwa dharau ambayo ilikuwa imetendeka dhidi ya Mbingu za Juu kwa kupiga marufuku misa ilipaswa kupatanishwa kwa njia ya damu, na kwamba mfalme, kwa niaba ya watu wake, alitakiwa atoe tamko lake hadharani kubariki kazi hiyo ya kutisha.PKSw 171.2

    Tarehe 21 ya Januari, 1535, ilipangwa kwa ajili ya sherehe hiyo ya kutisha. Hofu za kishirikina na chuki isiyokuwa na msingi ya taifa zima viliamshwa. Jiji la Paris lilifurika umati mkubwa wa watu kutoka katika nchi jirani kiasi kwamba mitaa yote ilijaa watu. Siku ilikaribishwa kwa maandamo makubwa yanayoduwaza. “Nyumba zilizokuwa kandokando ya njia maandamano yalikopita vilining'inizwa vitambaa vya maombolezo, madhabahu zilijengwa kila baada ya umbali fulani.” Mbele ya kila mlango uliwashwa mwenge kuheshimu “sakramenti takatifu.” Kabla ya mapambazuko waandamanaji walijipanga katika viwanja vya ikulu ya mfalme. “Mbele kulikuwepo bendera na misalaba kutoka kila parokia; halafu walifuata raia, wakitembea wawili wawili, na wakibeba mienge.” Mashirika manne ya watawa yalifuata, kila shirika likiwa na mavazi yao tofauti na ya kipekee. Halafu lilikuja kundi la watu waliobeba mifupa mingi ya watakatifu. Baada ya watu hawa walifuata waheshimiwa viongozi wa kanisa katika mavazi yao ya zambarau na majoho mekundu na mapambo ya vito vya thamani, wakiwa na mwonekano wa kifahari na unaomeremeta.PKSw 171.3

    “Hostia ilibebwa na askofu wa Paris chini ya mwavuli,... akisaidiwa na mapadri wanne wa damu.... Baada ya Hostia alifuata mfalme.... Fransis I siku hiyo hakuvaa taji, wala joho la dola.” Akiwa na “kichwa wazi, macho yake yakiangalia chini, na katika mkono wake akishikilia mshumaa unaowaka moto,” mfalme wa Ufaransa alionekana “katika hali ya kutubu.”—Ibid., b. 13, ch. 21. Kwenye kila madhabahu aliinama chini kwa kujidhili, siyo kwa sababu maovu ya nafsi yake, wala kwa sababu isiyo na hatia iliyochafua mikono yake, bali kwa sababu ya watu wake waliothubutu kukataa misaa. Baada ya mfalme alifuata malkia na waheshimiwa wa dola, nao wakitembea wawili wawili, kila mmoja akiwa na mwenge uliowashwa moto.PKSw 171.4

    Kama sehemu ya huduma za siku ile mfalme mwenyewe alihutubia maofisa wa ngazi za juu wa ufalme katika ukumbi mkubwa wa ikulu ya askofu. Kwa uso wenye huzuni alitokea mbele yao na kwa maneno yenye ufasaha na mguso aliomboleza “uhalifu, kufuru, siku ya huzuni na aibu,” vimekuja juu ya taifa. Ndipo alitoa wito kwa kila raia mwema kusaidia katika kuondoa gonjwa la uzushi lililotishia kuangamiza Ufaransa. “Kwa hakika, ndugu waheshimiwa, mimi hapa mfalme wenu,” alisema, “ikiwa ningejua kuwa mkono wangu mmojawapo ulikuwa na doa au umeugua uozo huu unaokera, ningeweza kuwapa muukate.... Na zaidi ya hapo, ikiwa ningeona mmojawapo wa watoto wangu amechafuliwa nao, nisingemwacha hai.... na ningemtoa kafara kwa Mungu.” Machozi yalikatiza hotuba yake, na mkutano wote ulilia na kutoa machozi, na kwa sauti moja walipiga kelele wakisema: “Tutaishi na kufa kwa ajili ya dini ya Kikatoliki!”—D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 4, ch. 12.PKSw 172.1

    Giza nene la kutisha lilikuwa limekuja katika taifa lililokataa nuru ya ukweli. Neema “iletayo wokovu” ilikuwa imeonekana; lakini Ufaransa, baada ya kuangalia nguvu na utakatifu wake, baada ya maelfu kuvutwa na uzuri wake wa Kimbingu, baada ya majiji na vitongoji kuangaziwa nuru yake, ilikuwa imegeuka na kuipa nuru kisogo, na kuchagua giza kuliko nuru. Walitupilia mbali zawadi ya mbinguni ambayo ilikuwa imetolewa kwao. Waliuita uovu wema, na wema uovu, mpaka wakawa wahanga wa kujitakia wa kujidanganya wao wenyewe. Sasa, ingawa kimsingi waliamini kuwa walikuwa wakimfanyia Mungu huduma kwa kuwatesa watu Wake, bado udhati wao haukuwafanya wasiwe na hatia. Nuru ile ambayo ingewaokoa kutoka katika udanganyifu, kutoka katika kuchafua roho zao kwa hatia ya kumwaga damu, walikuwa wameikataa kwa uchaguzi wao wenyewe.PKSw 172.2

    Kiapo kikuu cha kukomesha uzushi kilifanyiwa katika kanisa kubwa ambapo, takribani karne tatu baadaye, Mungu Mke wa Mantiki alitawazwa na taifa lililokuwa limemsahau Mungu aliye hai. Kwa mara nyingine tena maandamano yalipangwa, na wawakilishi wa Ufaransa walijipanga kuanza kazi ambayo walikuwa wameapa kuifanya. “Katika umbali wa karibu karibu majukwaa yalikuwa yamejengwa, ambapo Wakristo Waprotestanti fulani walipaswa kuchomwa moto wakiwa hai, na ilipangwa kuwa kuni ziwashwe wakati mfalme anapokaribia, na kwamba msafara usimame na kushuhudia mhanga akifa.”—Wylie, b. 13, ch. 21. Maelezo ya kina ya maumivu waliyopitia hawa mashahidi wa Kristo yanatisha mno kiasi kwamba hayafai kusemwa; bali hakukuwa na kutetereka kwa aina yo yote kwa upande wa wahanga. Alipolazimishwa akane, mmoja alijibu: “Ninaamini tu kile ambacho manabii na mitume walihubiri awali, na kile ambacho kundi lote la watakatifu walikiamini. Imani yangu ina uhakika kwa Mungu ambaye atazipinga nguvu zote za kuzimu.”—D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 4, ch. 12.PKSw 172.3

    Tena na tena msafara ulisimamishwa mahali pa mateso. Baada ya kufika mahali walipoanzia katika ikulu ya mfalme, watu walitawanyika, na mfalme na maaskofu waliondoka, wakiwa wameridhika na mwenendo wa shughuli ya siku ile huku wakijipongeza kuwa kazi ambayo ilikuwa imeanza ingeendelea hadi kukomesha kabisa uzushi.PKSw 173.1

    Injili ya amani ambayo Ufaransa ilikuwa imeikataa hakika iling'olewa kabisa nchini, lakini matokeo yake yalikuwa ya kutisha. Tarehe 21 ya Mwezi Januari, 1793, miaka mia mbili hamsini na nane tangu siku ile ambayo Ufaransa ilianza rasmi kuwatesa Wanamatengenezo, maandamano mengine, yenye kusudi tofauti, yalipita katika mitaa ya Paris. “Safari hii tena mfalme ndiye alikuwa mhusika mkuu; safari hii tena kulikuwepo vurugu na makelele; safari hii tena zilikuwepo kelele kwa ajili ya wahanga wengine; safari hii tena yalikuwepo majukwaa meusi ya kuulia wahalifu; na safari hii tena mandhari ya siku hiyo ilifungwa kwa mauaji ya kikatili sana; Louis XVI, akipambana mkono kwa mkono na askari waliokuwa wakienda kumnyonga, alikokotwa kuelekea jukwaani, mahali pa kunyongea, na akiwa ameshikiliwa pale kwa nguvu shoka lilipigwa na kukata shingo na kichwa kilichotenganishwa na kiwiliwili kilibiringika jukwani.”—Wylie, b. 13, ch. 21. Wala siyo mfalme peke yake aliyekuwa mhanga; jirani na hapo aliponyongewa mfalme watu elfu mbili na mia nane waliuawa kwa kunyongwa katika siku za umwagaji damu za Utawala wa Hofu.PKSw 173.2

    Matengenezo yalikuwa yamewasilisha kwa ulimwengu Biblia iliyo wazi, yakifunua kanuni za sheria ya Mungu na kuhimiza madai yake katika dhamiri za watu. Upendo usio na kikomo ulikuwa umewafunulia watu amri na kanuni za mbinguni. Mungu alisema: “Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili” (Kumbukumbu 4:6). Wakati Ufaransa ilipotupilia mbali zawadi ya mbinguni, Ufaransa ilipanda mbegu ya uasi na uharibifu; na utendaji kazi usioepukika wa asili na athari ulizalisha Mapinduzi na Utawala wa Hofu.PKSw 173.3

    Muda mrefu kabla ya mateso yaliyochochewa na mabango, Farel jasiri na makini alilazimika kuikimbia nchi alipozaliwa. Alihamia Uswisi, na kwa kazi zake, akijenga juu ya ile ya Zwingli, alisaidia katika kuyafanya Matengenezo yapokelewe zaidi. Miaka yake ya baadaye ilitumiwa hapa, lakini bado aliendelea kuchochea matengenezo katika nchi ya Ufaransa. Katika miaka yake ya kwanza ya ukimbizi, juhudi zake zilielekezwa hasa katika kupeleka injili katika nchi yake alikozaliwa. Alitumia muda mwingi akihubiri miongoni mwa raia wa nchi yake karibu na mpakani, ambapo kwa juhudi zisizochoshwa alifuatilia mgogoro na kusaidia kwa maneno yake ya kutia shime na ushauri. Kwa msaada wa wakimbizi wengine, vitabu vya Wanamatengenezo wa Kijerumani vilitafsiriwa katika lugha ya Kifaransa na, pamoja na Biblia ya Kifaransa, vilichapishwa kwa wingi. Kwa njia ya wainjilisti wa vitabu vitabu hivi viliuzwa kwa wingi katika nchi ya Ufaransa. Viligawiwa kwa wainjilisti wa vitabu kwa bei ndogo, ili faida inayopatikana iwawezeshe kuendeleza kazi hiyo.PKSw 173.4

    Farel alianza kazi yake katika nchi ya Uswisi katika vazi la unyenyekevu la ualimu. Akiwa katika Parokia isiyofikika kirahisi, alitumia muda mwingi kufundisha watoto. Kando ya kufundisha masomo ya kawaida ya mtaala husika, kwa tahadhari alianzisha kufundisha kweli za Biblia, akitumaini kuwa kwa kupitia watoto angeweza kuwafikia wazazi. Walikuwepo baadhi walioamini, lakini mapadri walikuja na kuzuia kazi hiyo, na wananchi washirikina waliamshwa na kuleta upinzani dhidi yake. “Hiyo haiwezi kuwa injili ya Kristo,” mapadri walidai, “hususan kwa kuwa kuhubiri injili hiyo hakuleti amani, bali vita.”—Wylie, b. 14, ch. 3. Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa kwanza, alipoteswa katika jiji moja alikimbilia jiji lingine. Kutoka kijiji hadi kijiji, kutoka jiji hadi jiji, alikwenda, akisafiri kwa mguu, akistahimili njaa, baridi, na uchovu, na kila mahali akiwa katika hatari ya kuuawa. Alihubiri katika masoko, katika makanisa, nyakati zingine katika mimbari za makanisa makubwa. Nyakati zingine alikuta makanisa hayana wasikilizaji; nyakati zingine mahubiri yake yalikatizwa kwa makelele na kuzomewa; hali kadhalika aliwahi kuburuzwa kikatili kutoka katika mimbari. Zaidi ya mara moja aliwahi kukamatwa na kundi la watu na kupigwa hadi karibu ya kufa. Lakini alisonga mbele. Ingawa mara nyingi alikataliwa, bila kukata tamaa alirudi tena katika shambulizi; na, moja baada ya mwingine, alishuhudia miji na majiji ambayo yalikuwa ngome za upapa, zikifungua malango yake na kuipokea injili. Parokia ndogo ambayo hapo awali iliwahi kutumika muda si mrefu ilipokea imani ya matengenezo. Miji ya Morat na Neuchatel nayo pia ilikataa kaida za Kiroma na kuondoa sanamu zilizoabudiwa kutoka katika makanisa yao.PKSw 174.1

    Farel alitamani kwa muda mrefu kusimika bendera ya Uprotestanti katika jiji la Geneva. Ikiwa jiji hili lingeongolewa, lingekuwa kitovu cha Matengenezo katika nchi za Ufaransa, Uswisi, na Italia. Akiwa na lengo hili kichwani mwake, aliendeleza kazi zake hadi miji mingi na vitongoji vingi vya karibu vilipoongolewa. Ndipo akiwa na rafiki yake mmoja waliingia katika jiji la Geneva. Lakini aliruhusiwa kuhubiri mahubiri mawili tu. Makasisi, baada ya kushindwa kupata hukumu ya kumnyonga kutoka kwa mamlaka za kiraia, walimwita mbele ya baraza la kikanisa, ambapo walikuja wakiwa na silaha zilizofichwa ndani ya majoho yao, wakiwa wamedhamiria kumwua. Nje ya ukumbi, kundi la watu wenye hasira, wakiwa na marungu na mapanga, lilikusanyika kuhakikisha kuwa anauawa ikiwa atafanikiwa kupona katika baraza. Uwepo wa mahakimu na maaskari wenye silaha, hata hivyo, ulimwokoa. Mapema asubuhi ya siku iliyofuata alipelekwa, na rafiki yake, ng'ambo ya ziwa hadi mahali palipo salama. Hivyo ndivyo juhudi zake za kwanza za kuihubiri Geneva zilivyoishia.PKSw 174.2

    Kwa ajili ya jaribio la pili mtu wa hali ya chini zaidi alichaguliwa—mtu kijana, aliye mnyenyekevu katika mwonekano kiasi kwamba alidharauliwa hata na watu waliodai kuwa marafiki wa matengenezo. Lakini mtu kama huyo angefanya nini mahali ambapo Farel alikuwa amekataliwa? Ingewezekanaje mtu ambaye ana ujasiri na uzoefu mdogo astahimili dhoruba ambayo watu wenye nguvu na ujasiri zaidi walikuwa wamelazimika kuikimbia? “Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi” (Zakaria 4:6). “Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu.” “Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu” (1 Wakorintho 1:27, 25).PKSw 175.1

    Froment alianza kazi kama mkuu wa shule. Ukweli alioufundisha kwa watoto shuleni, watoto nao waliwafundisha watu wa nyumbani kwao. Muda si mrefu wazazi walisikiliza Biblia ikifafanuliwa; darasa lilizidi kujazwa na wasikilizaji makini. Nakala za Agano Jipya na vijizuu vilisambazwa kwa wingi, na viliwafikia watu ambao wasingethubutu kuja wazi wazi kusikiliza mafundisho mapya. Baada ya muda mfupi huyu mtendakazi naye alilazimishwa kukimbia; lakini ukweli alioufundisha ulikuwa umeota katika akili za watu. Mbegu ya matengenezo ilikuwa imepandwa, na iliendelea kukua, kupata nguvu, na kuenea. Wahubiri walirudi, na kwa njia ya kazi zao ibada ya Kiprotestanti ilianzishwa katika jiji la Geneva hatimaye.PKSw 175.2

    Jiji lilikuwa tayari limeshatangaza kuunga mkono Matengenezo wakati, baada ya mizunguko na mabadiliko mbalimbali, Calvin aliingia malangoni mwake. Akirudi kutoka ziara yake ya mwisho ya mahali alipozaliwa, alikuwa njiani kuelekea Basel, ambapo, baada ya kugundua kuwa barabara ya moja kwa moja ilikuwa inatumiwa na majeshi ya Charles V, alilazimika kupita katika njia ya mzunguko ya Geneva.PKSw 175.3

    Katika ziara hii Farel aliuona mkono wa Mungu. Japokuwa Geneva ilikuwa imepokea imani ya matengenezo, bado kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya hapo. Ni mtu mmoja mmoja na wala siyo kundi la watu wanaoongoka kumfuata Mungu; kazi ya kuzaliwa upya lazima ifanyike katika moyo na dhamiri kwa nguvu ya Roho Mtaktifu, siyo kwa amri za mabaraza. Wakati watu wa Geneva walipokuwa wametupilia mbali mamlaka ya Roma, hawakuwa tayari sana kuachana na uovu ambao ulishamiri chini ya utawala wa Roma. Kujenga kanuni safi za injili na kuandaa watu hawa kujaza kikamilifu nafasi ambazo Mungu alikuwa anawaita wazijaze haikuwa kazi ndogo.PKSw 175.4

    Farel alikuwa na uhakika kuwa kwa kumpata Calvin alikuwa amepata mtu ambaye angeshirikiana naye katika kazi hii. Katika jina la Mungu alimwapisha mwinjilisti kwa kiapo kikuu abaki na kufanya kazi pale. Calvin alirudi nyuma kwa tahadhari. Akiwa mtu mwoga na mpenda amani, alisita kushikamana na roho jasiri, huru, na hata iliyo na fujo ya mtu wa Geneva. Udhaifu wa afya yake, pamoja na tabia yake ya kupenda kusoma, vilimsukuma kutafuta mahali pa kupumzika. Akiamini kuwa kwa njia ya kalamu yake angeweza kuchangia zaidi katika kazi ya matengenezo, alitamani apate mahali patulivu kwa ajili ya kusoma, na akiwa pale, kwa njia ya uandishi, afundishe na ajenge makanisa. Lakini wito wenye nguvu wa Farel ulimjia kama wito kutoka Mbinguni, na hakuthubutu kuukataa. Ilionekana kwake, alisema, “kana kwamba mkono wa Mungu ulikuwa umenyoshwa kutoka mbinguni, kana kwamba ulimshika, na kumweka daima mahali ambapo hakuwa na uvumilivu wa kupaacha.”— D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 9, ch. 17.PKSw 176.1

    Wakati huu hatari kubwa iliikabili kazi ya Uprotestanti. Laana za papa ziliunguruma dhidi ya Geneva, na mataifa makubwa yalitishia kuiangamiza. Ni kwa jinsi gani jiji hili dogo lingeweza kupinga mamlaka hii kubwa ambayo mara nyingi iliweza kulazimisha wafalme na wafalme wakuu kujisalimisha? Ni kwa jinsi gani Geneva ingeweza kusimama dhidi ya majeshi ya washindi wakuu wa dunia?PKSw 176.2

    Katika ulimwengu wote wa Ukristo, Uprotestanti ulihatarishwa na maadui wa kutisha. Ushindi wa kwanza ulipita, Roma ilikusanya nguvu mpya, ikitumaini kuangamiza Uprotestanti. Wakati huu shirika la Majesuti liliundwa, shirika katili, fidhuli, na lenye nguvu zaidi kuliko mashirika mengine yote ya kipapa. Wakiwa wamejitenga na mshikamano wowote wa kidunia na maslahi ya wanadamu, wakiwa hawana urafiki na mtu, akili na dhamiri vikiwa vimenyamazishwa kabisa, hawakujua kanuni nyingine, hawakuwa na mahusiano na mtu, isipokuwa uhusiano na shirika lao, na hawakuwa na wajibu mwingine zaidi ya kupanua mamlaka yake. (Tazama Kiambatisho.) Injili ya Kristo iliwawezesha wafuasi wake kukutana na hatari na kustahimili mateso, bila kukatishwa tamaa na baridi, njaa, suluba, na umaskini, kushikilia bendera ya ukweli mbele ya kitanda cha kutesea, gereza, na nguzo ya kuchomea watu moto. Kushinda nguvu hizi, Ujesuiti ulihamasisha wafuasi wake kwa ushikiliaji sana mambo bila kutumia akili uliowawezesha PKSw 176.3

    kustahimili hatari kama hizo, na kupinga nguvu ya ukweli kwa kutumia sila za uongo. Hakukuwa na uhalifu mkubwa wowote ambao wasingeweza kuufanya, hakuna uongo wowote mbaya ambao wasingeweza kuusema, wala uigizaji wowote ambao wasingeweza kuufanya. Wakiwa wameapa kuishi maisha ya kimaskini na ya chini daima, ilikuwa ni kusudi lao la msingi kupata utajiri na madaraka, kujitolea kuangusha Uprotestanti, na kuanzisha upya ukuu wa upapa.PKSw 177.1

    Walipoonekana kama wanachama wa shirika hilo la Ujesuti, walivaa vazi la utakatifu, wakitembelea magereza na hospitali, wakiwahudumia wagonjwa na maskini, wakitangaza kwa ulimwengu kuwa wameuacha ulimwengu, na kulibeba jina la Yesu, ambaye alikwenda kila mahali akitenda wema. Lakini makusudi ya kiuhalifu na kimauaji yalikuwa yamefichwa chini ya mwonekano huu mzuri wa nje. Ilikuwa kanuni ya msingi ya shirika hilo kuwa mwisho huhalalisha njia. Kwa kanuni hii, matendo ya uongo, wizi, udanganyifu, mauaji, siyo tu kuwa yalisameheka bali pia yalisifiwa, ikiwa yalilinda maslahi ya kanisa. Kwa kofia mbalimbali Majesuiti walipenya na kufanya kazi katika ofisi za serikali, wakipanda vyeo hadi kuwa washauri wa wafalme, wakipanga sera za mataifa. Walifanya kazi ya utumishi ili wawapeleleze mabwana zao. Walianzisha vyuo kwa ajili ya watoto wa kiume wa wana wafalme na malodi, na shule kwa ajili ya watu wa kawaida; na watoto wa wazazi wa Kiprotestanti walilazimishwa kushika kaida za kipapa. Utukufu wote wa nje na kujionesha kwa ibada za Kiroma ulitumiwa kuchanganya, kuduwaza na kushika akili, na hivyo uhuru ambao baba zao waliutaabikia ulisalitiwa na watoto wao. Majesuiti kwa muda mfupi walijieneza katika Bara zima la Ulaya, na kokote walikokwenda, uamsho wa upapa ulitokea.PKSw 177.2

    Ili kuwapa nguvu kubwa zaidi, amri ilitolewa kurudisha mahakama za uchunguzi. (Tazama Kiambatisho.) Licha ya chuki ya jumla ambayo watu walikuwa nayo dhidi ya mahakama hiyo, hata katika nchi za Kikatoliki, mahakama hii ya kutisha ilianzishwa tena na watawala wa kipapa, na ukatili wa kutisha kiasi cha kutoweza kuoneshwa wakati wa mchana ulirudiwa katika magereza ya siri. Katika nchi nyingi, maelfu kwa maelfu ya maua ya taifa, watu safi na waungwana, watu wenye akili na wenye elimu ya juu sana, wachungaji wacha Mungu na waliojiweka wakfu, watu wenye bidii na wazalendo, wasomi wenye uwezo mkubwa wa akili, wanasanaa wenye talanta, mafundi wenye stadi za juu kabisa, walichinjwa au walilazimishwa kukimbilia nchi zingine.PKSw 177.3

    Hizo ndizo njia ambazo Roma ilizitumia kuzima nuru ya Matengenezo, kuwatenganisha watu na Biblia, na kurudisha ujinga na ushirikina wa Zama za Giza. Lakini chini ya mbaraka wa Mungu na kazi za watu waaminifu ambao Mungu aliwainua kumfuata Luther, Uprotestanti haukuangushwa. Nguvu yake haikutokana na upendeleo au silaha za wafalme. Nchi ndogo kabisa, mataifa maskini na dhaifu kabisa, zilitokea kuwa ngome ya Uprotestanti. Ilikuwa jiji la Geneva katikati ya maadui wenye nguvu wakipanga maangamizi yake; ilikuwa nchi ndogo ya Uholanzi kwenye pwani ya mchanga ya bahari ya kaskazini, iliyopambana dhidi ya ukatili wa Uhispania, ambayo wakati ule ulikuwa ufalme tajiri sana; ilikuwa nchi ndogo ya Swideni isiyo na rutuba, isiyovutia, ambayo ilipata ushindi kwa ajili ya Matengenezo.PKSw 177.4

    Kwa karibu miaka thelathini Calvin alifanya kazi katika jiji la Geneva, kwanza kuanzisha kanisa pale linalosimamia maadili ya Biblia, na halafu kwa ajili ya kueneza Matengenezo katika Bara zima la Ulaya. Siyo kweli kuwa kazi yake kama kiongozi wa umma haikuwa na dosari, na siyo kweli pia kuwa mafundisho yake hayakuwa na makosa kabisa. Lakini alikuwa chombo kilichotumika kutangazia ukweli ambao ulikuwa na umuhimu wa pekee katika wakati wake, katika kudumisha kanuni za Uprotestanti dhidi ya wimbi la upapa lililokuwa linarudi kwa kasi, na katika kuhamasisha makanisa yaliyofanya matengenezo katika usahili na usafi wa maisha, badala ya kiburi na ufisadi vilivyojengwa na mafundisho ya Kiroma.PKSw 178.1

    Kutoka Geneva, machapisho na walimu walitoka na kwenda kueneza mafundisho ya matengenezo. Mahali hapa ndipo palikuwa mahali ambapo watu wote walioteswa katika nchi zote walikuja kupata mafundisho, ushauri, na kutiwa moyo. Jiji la Calvin lilitokea kuwa makimbilio ya Wanamatengenezo waliowindwa katika nchi za Ulaya Magharibi. Wakikimbia dhoruba kali zilizoendelea kwa karne nyingi, wakimbizi walikuja kwenye malango ya Geneva. Wakiwa na njaa, wakiwa na majeraha, wakiwa hawana nyumba wala ndugu, walikaribishwa kwa furaha na walitunzwa kwa upendo; na baada ya kupata makazi hapa, walilibariki jiji kwa ujuzi wao, elimu yao, na uchaji wao. Wengi waliopata hifadhi hapa walirudi katika nchi zao kupinga ukatili wa Roma. John Knox, Mwanamatengenezo jasiri wa Kiskochi, Wapuritani wa Kiingereza ambao hawakuwa wachache, Waprotestanti wa Uholanzi na Uhispania, na Hugenoti wa Ufaransa walichukua kutoka Geneva mwenge wa ukweli kuangaza giza la nchi zao walikozaliwa.PKSw 178.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents