Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Pambano Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 37—Maandiko ni Kinga

    “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi” (Isaya 8:20). Watu wa Mungu wameelekezwa kuyachukulia Maandiko kuwa kinga dhidi ya mvuto wa walimu wa uongo na nguvu ya udanganyifu ya roho wa giza. Shetani anatumia kila njia inayowezekana kuzuia watu wasipate ujuzi wa Biblia; kwa kuwa maneno yake ya wazi hufunua uongo wake. Katika kila uamsho wa kazi ya Mungu mfalme wa uovu anaamshwa na kujishughulisha zaidi; sasa anafanya kazi kwa juhudi zake zote kwa ajili ya pambano dhidi ya wafuasi Wake. Uongo mkuu wa mwisho karibu utafunuliwa mbele yetu. Mpinga Kristo atafanya kazi zake za maajabu mbele yetu. Vitu bandia vitafanana sana na vitu halisi kiasi kwamba haitawezekana kutofautisha kati ya kitu bandia na kitu halisi isipokuwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Kwa njia ya ushuhuda wa Maandiko kila kauli na kila muujiza lazima vipimwe.PKSw 453.1

    Wale watakaojitahidi kutii amri zote za Mungu watapingwa na kudhihakiwa. Wataweza kusimama kwa uwezo wa Mungu tu. Ili kustahimili jaribu lililoko mbele yao, inawapasa waelewe mapenzi ya Mungu kama yalivyofunuliwa katika neno Lake; wanaweza kumheshimu tu ikiwa wana uelewa sahihi wa tabia Yake, serikali, na makusudi Yake, na kutenda kulingana nayo. Ni wale tu ambao wameimarisha akili zao kwa ukweli wa Biblia watasimama na kushinda katika pambano kuu la mwisho. Kwa kila roho kutakuja mtihani wa kujihoji: Je, nimtii Mungu kuliko wanadamu? Saa ya uamuzi imewadia hata sasa. Je, miguu yetu imesimikwa juu ya mwamba wa neno la Mungu lisilobadilika? Je, tuko tayari kusimama imara kutetea amri kumi za Mungu na imani ya Yesu?PKSw 453.2

    Kabla ya kusulubiwa Kwake Mwokozi aliwaelezea wanafunzi Wake kuwa alikuwa anaelekea kuuawa na kufufuka tena kutoka kaburini, na malaika walikuwepo kunatisha maneno Yake katika akili na mioyo. Lakini wanafunzi walikuwa wakitarajia kupata ukombozi wa kidunia kutoka katika nira ya ukoloni wa Warumi, na wasingeweza kuvumilia wazo kuwa Yule ambaye matumaini yao yote yalikuwa yamekitwa kwake angekufa kifo cha aibu. Maneno waliyotakiwa kuyakumbuka yaliyeyuka na kuondoka katika akili zao; na wakati wa jaribu ulipofika, hawakuwa tayari. Kifo cha Yesu kiliharibu matumaini yao yote kiasi kwamba ni kana kwamba hakuwa amewapa tahadhari yo yote. Kwa hiyo, katika unabii, wakati ujao umefunuliwa mbele yetu kwa uwazi kama vile ulivyokuwa umefunuliwa kwa wanafunzi kwa njia ya maneno ya Kristo. Matukio ambayo yameshikamana na kufungwa kwa mlango wa rehema na kazi ya matayarisho kwa ajili ya wakati wa taabu, vyote vimeelezwa kwa uwazi kabisa. Lakini watu wengi hawana ufahamu wa ukweli huu muhimu kuliko kama ungekuwa haujafunuliwa. Shetani yuko macho akihakikisha kuwa anadaka na kufuta kila wazo ambalo lingeweza kuwafanya wawe na hekima ya kupata wokovu, na wakati wa taabu utawakuta wakiwa hawako.PKSw 453.3

    Mungu anapowatumia watu maonyo yaliyo muhimu kiasi kwamba yanawakilishwa kana kwamba yanahubiriwa na malaika watakatifu wanaoruka katikati ya mbingu, anataka kila mtu mwenye ufahamu asikie ujumbe. Hukumu za kutisha zinazotangazwa dhidi ya ibada ya mnyama na sanamu yake (Ufunuo 14:9-11), zinapaswa kuwaongoza wote katika kujifunza kwa bidii unabii na kuelewa ni nini alama ya mnyama, na jinsi wanavyoweza kuepuka kuipokea. Lakini watu walio wengi wanageuza masikio yao wasisikie ukweli na wanageukia hadithi za kubuni. Mtume Paulo alitangaza, akizitazama siku za mwisho: “Utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima” (2 Timotheo 4:3). Wakati umeshafika tayari. Watu walio wengi hawataki ukweli wa Biblia, kwa sababu unaingilia tamaa za moyo wenye dhambi, unaopenda ulimwengu; na Shetani anawapa uongo wanaoupenda.PKSw 454.1

    Lakini Mungu atakuwa na watu duniani watakaodumisha Biblia, na Biblia pekee, kama kiwango cha mafundisho yote na msingi wa matengenezo yote. Maoni ya wasomi, mahitimisho ya sayansi, imani na maamuzi ya mabaraza ya makanisa, yakiwa mengi na yanayohitilafiana kama makanisa yenyewe yanayoyawakilisha yalivyo, sauti ya walio wengi—hakuna moja wala yote yanapaswa kuchukuliwa kama ushahidi unaounga mkono au unaopinga wazo lo lote la imani ya kidini. Kabla ya kukubali fundisho lo lote au kanuni yo yote, inatupasa kudai tamko la wazi la “Hivi ndivyo Bwana asemavyo” kuunga mkono fundisho hilo au kanuni hiyo.PKSw 454.2

    Shetani anajitahidi daima kuvuta usikivu uelekezwe kwa watu badala ya kuelekezwa kwa Mungu. Anawaongoza watu wawatazame maaskofu, wachungaji, maprofesa wa theolojia, kama viongozi wao, badala ya kuchunguza Maandiko ili wajifunze wajibu wao wenyewe moja kwa moja. Ndipo, kwa kutawala na kuongoza akili za hawa viongozi, anaweza kutawala watu wengi kulingana na matakwa yake mwenyewe.PKSw 454.3

    Kristo alipokuja kutangaza maneno ya uzima, watu wa kawaida walimsikiliza kwa furaha; na wengi, hata miongoni mwa makuhani na watawala, walimwamini. Lakini wakuu wa makuhani na viongozi wa ngazi ya juu wa kitaifa walidhamiria kupinga na kukosoa mafundisho Yake. Ingawa walishindwa katika juhudi zao zote kupata mashitaka dhidi Yake, ingawa hata wao walihisi mvuto wa nguvu na hekima ya Mungu katika maneno Yake, bado walijifungia katika chuki isiyo na sababu; walikataa ushahidi wa wazi kabisa wa Umasihi Wake, ili wasije wakajikuta wamelazimika kuwa wanafunzi Wake. Hawa wapinzani wa Yesu walikuwa watu ambao watu wote walikuwa wamefundishwa tangu utotoni kuwaheshimu sana, watu ambao mamlaka yao watu wote walikuwa wamezoea kuyatii bila maswali. “Inawezekanaje,” waliuliza, “viongozi wetu na waandishi wasomi wasimwamini Yesu? Hawa watu watakatifu si wangempokea kama kweli angekuwa Kristo?” Ilikuwa kwa sababu ya mvuto wa hawa viongozi taifa la Kiyahudi lilimkataa Mkombozi wao.PKSw 454.4

    Roho iliyowaendesha makuhani na viongozi wale ingali ikidhihirishwa na watu wote wanaodai kuwa watakatifu sana. Wanakataa kuchunguza ushuhuda wa Maandiko kuhusu ukweli maalumu kwa ajili ya wakati huu. Wanaonesha idadi yao, utajiri wao, na umaarufu wao, na wanawatazama kwa dharau watetezi wa ukweli kama watu wachache, maskini, na wasiopendwa na watu, walio na imani inayowatenga na ulimwengu.PKSw 455.1

    Kristo aliona tangu mwanzo kuwa kujichukulia mamlaka kusikostahili kwa waandishi na Mafarisayo kusingekomeshwa na kusambaa kwa Wayahudi katika mataifa mbalimbali. Aliona kwa macho ya kinabii kazi ya kuinua mamlaka ya wanadamu na kutawala dhamiri, ambako kumekuwa laana ya kutisha kwa kanisa katika zama zote. Na maonyo ya kutisha kwa waandishi na Mafarisayo, na maonyo Yake kwa watu ili wasifuate viongozi hawa vipofu, yaliwekwa katika kumbukumbu kama maonyo kwa vizazi vya baadaye.PKSw 455.2

    Kanisa la Rumi, ni viongozi wa dini tu ambao wana haki ya kutafsiri Maandiko. Kwa misingi kuwa viongozi wa dini peke yao ndio wenye uwezo wa kufafanua neno la Mungu, Biblia imeondolewa kwa watu wa kawaida. [Tazama Kiambatanisho kwa ajili ya maelezo ukurasa wa 340.] Ingawa Matengenezo yalitoa Maandiko kwa wote, lakini kanuni ile ile iliyoshikiliwa na Rumi inawazuia watu wengi katika makanisa ya Kiprotestanti wengi kusoma Biblia wenyewe. Wanafundishwa kupokea mafundisho ya Biblia kama yanavyotafsiriwa na kanisa; na kuna maelfu ya watu wasiopokea cho chote, hata kama kimefunuliwa kwa uwazi katika Maandiko, kilicho tofauti na imani au fundisho lililokwishawekwa na kanisa lao.PKSw 455.3

    Licha ya Biblia kujaa maonyo dhidi ya walimu wa uongo, watu wengi wako tayari kusalimisha amana ya roho zao kwa viongozi wa kanisa. Wapo watu maelfu leo wanaodai kuwa wafuasi wa dini wasioweza kutoa sababu ya imani yao zaidi ya kusema tu kuwa wao wamefundishwa hivyo na viongozi wa dini. Wanapita bila kuyaona mafundisho ya Mwokozi, na wanaweka imani yao isiyo na swali kwa maneno ya wachungaji wao. Lakini, je, wachungaji hawakosei? Tunawezaje kuweka amana roho zetu kwa uongozi wao tusipojua kwa njia ya neno la Mungu kuwa ni wabeba nuru? Ukosefu wa ujasiri wa kimaadili wa kwenda kando ya njia iliyozoeleka ya ulimwengu huwafanya wengi wafuate nyayo za wasomi; na kwa sababu ya uzembe wa kuchunguza wenyewe, wanajikuta wamenaswa katika minyororo ya makosa bila matumaini. Wanaona kuwa ukweli kwa ajili ya wakati huu umefunuliwa katika Biblia; na wanahisi nguvu ya Roho Mtakatifu katika utangazaji wake; lakini bado wanaruhusu upinzani wa viongozi wa dini kuwageuza na kuwapeleka mbali na nuru. Ingawa busara na dhamiri vimeshawishika, roho hizi zilizodanganyika haziwezi kuthubutu kufikiri tofauti na mchungaji wao; na uamuzi wao binafsi, maslahi yao ya umilele, vinatolewa kafara kweye madhabahu ya mashaka, kiburi, na chuki, ya mtu mwingine.PKSw 455.4

    Kuna njia nyingi ambazo Shetani anazitumia kufanya kazi kupitia mvuto wa kibinadamu kuwafunga mateka wake. Anajipatia wafuasi kwa kuwashikamanisha, kwa njia ya kamba za hariri ya upendo, na wale ambao ni adui za msalaba wa Kristo. Mshikamano huu waweza kuwa wa wazazi, ndugu, ndoa, au kijamii, madhara ni yale yale; wapinzani wa ukweli wanatumia nguvu kutawala dhamiri, na roho zilizo chini ya utawala wao hazina ujasiri au uhuru wa kutosha kufuata kile wanachokiamini kuwa ndiyo wajibu wao.PKSw 456.1

    Ukweli na utukufu wa Mungu havitenganishwi; haiwezekani kwetu sisi, ambao tuna uwezo wa kupata Biblia kirahisi, tumheshimu Mungu kwa maoni yenye makosa. Wengi hudai kuwa siyo jambo muhimu kuwa mtu anaamini nini, ikiwa maisha yake ni mazuri. Lakini maisha huendeshwa na imani. Ikiwa nuru ya ukweli iko ndani ya uwezo wetu wa kuipata, na tunazembea kutumia fursa tulizonazo za kuusikia ukweli na kuiona nuru, ina maana kuwa tumeukataa ukweli kwa makusudi; tumechagua giza kuliko nuru.PKSw 456.2

    “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti” (Mithali 16:25). Kutokujua siyo udhuru wa makosa au dhambi, kunapokuwepo kila fursa ya kuyajua mapenzi ya Mungu. Mtu anatembea barabarani na anafika mahali ambapo kuna barabara kadhaa na kuna ubao unaoeleza kila barabara inakokwenda. Ikiwa mtu huyu atapuuza huo ubao wenye maelezo, na anaamua kupita katika barabara yo yote anayoiona sawa machoni pake, anaweza kuwa na nia nzuri kabisa, lakini kwa namna yo yote ile atajikuta akiwa katika barabara isiyokuwa sahihi.PKSw 456.3

    Mungu ametupatia neno Lake ili tuyajue mafundisho yake na tujue kile ambacho Mungu anakitaka kwetu. Wakati mwanasheria alipokuja kwa Yesu akiwa na swali, “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Mwokozi alimpeleka katika Maandiko, akisema: “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Kutokujua hakutakuwa udhuru kwa vijana au wazee, wala kuwaokoa wasipate adhabu kwa kuvunja sheria ya Mungu; kwa sababu katika mikono yao wanalo wasilisho kamili la sheria ya Mungu na la kanuni zake na madai yake. Haitoshi kuwa na nia nzuri peke yake; haitoshi mtu kufanya kile anachodhani kuwa ni sahihi au kile ambacho mchungaji wake anamwambia kuwa ni sahihi. Wokovu wa roho yake uko hatarini, na anapaswa kuchunguza Maandiko kwa ajili yake mwenyewe. Haidhuru ameshawishika kiasi gani, haidhuru anamwamini mchungaji wake kuwa anaujua ukweli kiasi gani, huu sio msingi wake. Anao mwongozo unaomwonesha kila alama ya njia katika safari ya kwenda mbinguni, na hapaswi kubahatisha katika jambo lo lote.PKSw 456.4

    Ni wajibu wetu wa kwanza na wa juu kabisa wa kila mtu mwenye akili kujifunza kutoka katika Maandiko kile ambacho ni ukweli, na halafu kutembea katika nuru na kuwatia moyo wengine wafuate mfano wake. Inatupasa siku kwa siku kujifunza Biblia kwa bidii, tukipima kila wazo kwa kulinganisha andiko kwa andiko. Kwa msaada wa Mungu inatupasa kujenga maoni yetu kwa ajili yetu sisi wenyewe kwa kuwa itatupasa kujibu wenyewe mbele ya Mungu.PKSw 457.1

    Ukweli ambao umefunuliwa kwa uwazi katika Biblia umetiliwa mashaka na kuwekwa giza na wasomi, ambao, kwa kujifanya kuwa wana hekima kubwa, hufundisha kuwa Maandiko yana maana yenye fumbo, ya siri, na ya kiroho isiyoonekana katika lugha iliyotumiwa. Watu hawa ni walimu wa uongo. Ilikuwa tabaka kama hili ambalo Yesu aliliambia: “Hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Marko 12:24). Lugha ya Biblia inapaswa kueleweka kulingana na maana yake ya wazi, isipokuwa pale ambapo ishara imetumiwa au kielelezo kimetumiwa. Kristo ametoa ahadi: “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo” (Yohana 7:17). Ikiwa watu wangeielewa kama inavyosomeka, ikiwa wasingekuwepo walimu wa uongo wanaopotosha na wanaochanganya akili za watu, kazi ingefanyika ambayo ingewafurahisha malaika na ambayo ingeleta maelfu kwa maelfu kundini ambao kwa sasa wanatangatanga katika makosa.PKSw 457.2

    Inatupasa kuelekeza nguvu zetu zote za akili katika kusoma Maandiko na inatupasa tujipe kazi ya kufahamu na kuelewa, kwa kadiri inavyowezekana kwa watu wenye hali ya kufa, mambo ya kina ya Mungu; lakini hatupaswi kusahau kuwa utiifu na ujisalimishaji wa mtoto ndiyo roho ya kweli ya mwanafunzi wa Biblia kwa sababu matatizo ya kuielewa Biblia hayawezi kutanzuliwa kwa mbinu zinazotumiwa katika kuchambua matatizo ya kifalsafa. Hatupaswi kuingia katika kujifunza Biblia na ile hali ya kujitegemea ambayo wengi wanaingia nayo katika uwanja wa sayansi, bali kwa maombi na kumtegemea Mungu na shauku ya dhati ya kujifunza mapenzi Yake. Inatupasa kuja kwa unyenyekevu na roho ya kufundishika ili kupata maarifa kutoka kwa Yeye ambaye ni MIMI NIKO. Vinginevyo, malaika waovu watapofusha akili zetu na kuifanya mioyo yetu kuwa migumu ili tusiweze kuupokea ukweli.PKSw 457.3

    Sehemu nyingi za Maandiko ambazo wasomi wanazitangaza kuwa zina mafumbo, au wanaziruka kwa kigezo kuwa siyo za muhimu, zimejaa faraja na mafundisho kwa mtu ambaye amepata mafunzo katika shule ya Kristo. Sababu moja ambayo inawafanya wanatheolojia wasiwe na uelewa sahihi wa neno la Mungu ni, wanafumba macho yao wasiuone ukweli ambao hawako tayari kuuishi. Ufahamu wa ukweli wa Biblia hautegemei sana nguvu ya akili iliyoingizwa katika utafiti; bali hutegemea zaidi udhati wa kusudi, shauku ya dhati ya kuwa mtakatifu.PKSw 457.4

    Kamwe Biblia isijifunzwe bila maombi. Roho Mtakatifu pekee Ndiye anaweza kutufanya tuhisi umuhimu wa mambo yale ambayo ni rahisi kueleweka, au kutuzuia tusianze kupotosha ukweli ambao ni mgumu kwetu kuuelewa. Ni kazi ya malaika wa mbinguni kuuandaa moyo kuelewa neno la Mungu kiasi cha kuweza kufurahia uzuri wake, kubadilishwa na maonyo yake, au kuchangamshwa na kuimarishwa na ahadi zake. Inatupasa kulifanya ombi la mtunga Zaburi kuwa ombi letu: “Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako” (Zaburi 119:18). Majaribu yanaonekana kuwa yasiyozuilika kwa sababu, kwa kuzembea maombi na kujifunza Biblia, mtu anayejaribiwa hawezi kukumbuka kirahisi ahadi za Mungu na kumkabili Shetani kwa silaha za Maandiko. Lakini malaika wanawazunguka wale walio tayari kufundishwa mambo ya Mungu; na katika wakati wa mahitaji makubwa watakumbuka ukweli ambao unahitajika kwa wakati huo. Kwa hiyo “wakati adui atakapokuja kama mkondo wa mto wa mafuriko; Roho wa Bwana atainua bendera dhidi yake” (Isaya 59:19).PKSw 458.1

    Yesu aliwaahidi wanafunzi Wake: “Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohana 14:26). Lakini mafundisho ya Kristo yanatakiwa kuhifadhiwa mapema akilini ili Roho wa Mungu aweze kutukumbusha wakati wa hatari. “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako” Daudi alisema, “Nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11).PKSw 458.2

    Wote wanaothamini maslahi yao ya milele inawapasa kuwa macho dhidi ya kuvamiwa na kutokuamini. Nguzo muhimu za ukweli zitashambuliwa. Haiwezekani kutokufikiwa na dhihaka na falsafa za uongo, mafundisho nyemelezi na hatarishi, ya ukafiri wa kisasa. Shetani anabuni majaribu yanayolingana na hali ya matabaka yote ya watu. Anawashambulia wasio na elimu kwa kejeli na dharau, wakati anawakabili wenye elimu kwa vipingamizi vya kisayansi na hoja za kifalsafa, njia zote zikilenga kuchochea mashaka au kudharau kwa Maandiko. Hata vijana wenye uzoefu mdogo wanapenyeza mashaka kuhusiana na kanuni za msingi za Ukristo. Na huu ukafiri wa vijana, ingawa ni wa juu juu, bado una mvuto mbaya. Wengi wanaongozwa kukejeli imani ya baba zao na kumdhihaki Roho wa neema (Waebrania 10:29). Maisha ya watu wengi yaliyokuwa na mwelekeo wa kumheshimu Mungu na kuwa baraka kwa ulimwengu yamechafuliwa na pumzi chafu ya ukafiri. Wote wanaotumainia maamuzi yenye majivuno ya hoja za kibinadamu na kudhani kuwa wanaweza kueleza siri za Kimungu na kufikia ukweli bila msaada wa hekima ya Mungu wananaswa katika mtego wa Shetani.PKSw 458.3

    Tunaishi katika kipindi muhimu sana cha historia ya ulimwengu. Hatima ya umati mkubwa wa wakazi wa dunia inakaribia kuamriwa. Hali yetu njema ya baadaye na pia wokovu wa roho zingine hutegemea njia ambayo tunaifuata sasa. Tunahitaji kuongozwa na Roho wa ukweli. Kila mfuasi wa Kristo inampasa kuuliza kwa: “Bwana, inanipasa nifanye nini?” Inatupasa kujinyenyekesha mbele ya Bwana, kwa kufunga na kuomba, na kutafakari zaidi juu ya neno la Mungu, hususani juu ya matukio ya hukumu. Inatupasa sasa kutafuta uzoefu wa kina na hai katika mambo ya Mungu. Hatuna wakati wa kupoteza. Matukio muhimu yanatokea mbele yetu; tupo katika eneo ambalo limerogwa na Shetani. Msisinzie, askari wa Mungu; adui anavizia karibu, akiwa tayari wakati wowote, ikiwa mtazembea na kulala, kuwarukia na kuwafanya mawindo yake.PKSw 458.4

    Wengi wamedanganyika kuhusiana na hali yao ya kweli mbele za Mungu. Wanajipongeza kwa matendo mabaya ambayo hawayafanyi, na wanasahau kuorodhesha matendo mema na yanayofaa ambayo Mungu anataka wayafanye, lakini ambayo wamezembea kuyafanya. Haitoshi kuwa wao ni miti katika bustani ya Mungu. Inawapasa kukidhi matarajio Yake kwa kuzaa matunda. Anawawajibisha kwa kushindwa kutekeleza mambo yote mema ambayo walipaswa kuyafanya, akiwaimarisha kwa njia ya neema Yake. Katika vitabu vya mbinguni wameandikwa kama wataabishaji wa ardhi. Lakini hata tabaka hili sio kuwa halina tumaini kabisa. Hawa ambao wamedhihaki rehema ya Mungu na kudharau neema Yake, moyo wenye upendo na uvumilivu ungali unasihi. “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; ... mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu” (Waefeso 5:14-16).PKSw 459.1

    Wakati wa kujaribiwa utakapofika, wale ambao wamelifanya neno la Mungu kuwa kanuni ya maisha yao watafunuliwa. Wakati wa kiangazi hakuna tofauti kati ya miti ya kijani na miti mingine; lakini wakati pepo za wakati wa baridi zinapokuja, miti ya kijani hubaki bila kubadilika, wakati miti mingine ikivuliwa majani yote. Kwa hiyo mtu anayejifanya kuwa Mkristo hawezi kutofautishwa na Mkristo wa kweli, lakini wakati umekaribia ambapo tofauti itaonekana. Acha upinzani utokee, acha ubaguzi wenye chuki na kukosa uvumilivu vishike hatamu, acha mateso yawashwe, ndipo wenye mioyo isiyojitoa kikamilifu na wanafiki watakapoyumba na kuiacha imani; lakini Mkristo wa kweli atasimama kama mwamba, imani yake itakuwa na nguvu zaidi, tumaini lake litang'ara zaidi, kuliko katika siku za mafanikio.PKSw 459.2

    Anasema mtunga Zaburi: “Shuhuda zako ndizo nizifikirizo. Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo” (Zaburi 119:99, 104).PKSw 459.3

    “Heri mtu yule aonaye hekima.” “Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda” (Mithali 3:13; Yeremia 17:8).PKSw 459.4

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents