Maandiko Matakatifu Ndiyo Kinga Yetu
Naliona ya kwamba jeshi la mbinguni walighadhabika sana kwa ajili ya huu ukavu wa macho wa Shetani. Nalitaka kujua kwa sababu gani madanganyifu haya yaliruhusiwa kuwa na nguvu katika fikara za wanadamu hali malaika za Mungu ni wenye nguvu, na wakitumwa, wangeweza kumshinda adui kwa urahisi. Ndipo nikaona ya kwamba Mungu alijua ya kwamba Shetani angeitumia kila njia ambayo kwayo angeweza kumharibu mwanadamu; ndiyo maana Mungu aliamuru Neno lake liandikwe, na kuyafanya makusudi yake juu ya wanadamu kuwa dhahiri, hata mtu mdhaifu wa namna gani asikose kwa ajili ya kutojua. Mungu alipokwisha kumpa mwanadamu Neno lake, alililinda kwa uangalifu lisije likaharibiwe na Shetani na malaika zake, wala na ye yote katika wajumbe wake. Ingawa vitabu vingine vitaharibika, Biblia ilikusudiwa kudumu milele. Na katika siku za mwisho. madanganyifu ya Shetani yanapoongezeka, nakili za Biblia zingezidishwa kuwa nyingi hata mtu ye yote angeweza kupata nakili yake mwenyewe; na hivyo wangeweza kujivika silaha za Neno la Mungu wakajilinda na madanganyifu na ajabu za uongo wa Shetani.VK 95.1
Naliona ya kwamba Mungu alihifadhi Biblia kwa namna ya ajabu; na pengine nakili za Biblia zilipokuwa chache, watu wengine waliokuwa wameelimika waliyageuza maneno yaliyoandikwa humo, wakidhani ya kuwa waliidhihirisha maana yake zaidi, lakini kwa kweli wakayafumba mambo yaliyokuwa dhahiri tayari, kwa sababu waliyafanya maneno yale yafuatane na maoni yao wenyewe ambayo yaliongozwa na mapokeo ya kibinadamu. Lakini naliona ya kwamba Neno la Mungu ni kama mnyororo uliokamilika, kiungo kimoja kikiungana na kiungo kingine na kuieleza maana yake. Watu wanaotafuta ukweli kwa makini hawana haja ya kukisia, kwa kuwa Neno la Mungu ni dhahiri na wazi kwa kumwonyesha mtu njia ya uzima. pia Roho Mtakatifu ametumwa kama mwongozi kwa kuwasaidia watu wapate kuifahamu njia ya uzima inavofunuliwa katika Biblia.VK 95.2
Naliona ya kwamba malaika za Mungu hawana ruhusa kutawala fikara za watu. Mungu ameweka mbele za mwanadamu uzima na kifo. Mwanadamu aweza kuchagua njia yake. Watu wengi wana hamu ya kuupata uzima, lakini wangali wakiendelea kuifuata njia iliyo pana. Wanachagua kuiasi mamlaka ya Mungu, ijapokuwa alionyesha upendo na rehema kuu kwa vile alivyomtoa Mwana wake wa pekee apate kufa kwa ajili yao. Wale wasiokubali kuuchagua wokovu ulionunuliwa na damu yenye thamani kuu, ni lazima wahukumiwe. Lakini naliona ya kwamba Mungu hatafunga mahali pa kutaabika milele, wala hatawachukua mbinguni; kwa kuwa kama wangepelekwa huko kuwa pamoja na watakatifu. wangetaabika zaidi. Lakini atawaharibu kabisa, na kuwafanya wawe kana kwamba hawakuwako; ndipo haki ya Mungu itatimizua. Alimwumba mwanadamu kwa mavumbi ya nchi. na wakaidi na watu wasio safi wataieketezwa kwa moto na kurudi mavumbini tena. Naliona ya kwamba kwa ajili ya ukarimu na huruma ya Mungu katika jambo hili, inawapasa wote kumpenda na kulitukuza jina lake takatifu. Baada ya kuharibiwa kwa waovu duniani, ndipo jeshi zima la mbinguni watasema, “Amina!”VK 96.1
Shetani hupendezwa kabisa na wale wanaojiita na jina la Kristo, na huku wanashikamana na madanganyifu yaliyoanzishwa naye Shetani. Kazi yake ingali ya kuyavumbua madanganyifu mapya, na uwezo wake na akili yake kwa kufanya hivi huongezeka kila mara. Aliwatilia mapapa na makasisi fikara ya kujivuna wakawataharakisha watu ili wawatese na kuwaangamiza wale waliokataa kuyafuata madanganyifu yake. Lo! maumivu na huzuni ya ajabu ambayo wafuasi wateule wa Kristo, walilazimishwa kuyavumilia! Malaika wameyaandika mambo hayo yote yaliyotendeka. Shetani na malaika zake waovu wakasimanga wakiwaambia malaika wa Mungu waliowahudumia watu wale wa Mungu walioteswa ya kwamba watauawa wote, asipatikane Mkristo wa kweli hata mmoja duniani. Naliona ya kwamba kanisa la Mungu lilikuwa safi kabisa katika siku zile. Hakukuwako na hatari ya, watu wenye mioyo michafu kuingia katika kanisa, kwa kuwa Mkristo wa kweli aliyethubutu kuisimamia imani yake alikuwa katika hatari ya kuteswa vikali, kuteketezwa moto, na kuadhibiwa kwa namna yo yote ambayo Shetani na malaika zake waliweza kutia katika fikara za wanadamu.VK 97.1