Sura Ya Ishirini Na Moja - Ufufuo Wa Pili
*****
BAADAYE Yesu na mafuatano ya malaika watakatifu, na watakatifu wote waliookolewa, waliondoka katika mji. Malaika walimzunguka Amiri Mkuu wao, wakamwandama alikokwenda, na mafuatano ya watakatifu waliookolewa nyuma. Ndipo kwa utukufu wa ajabu na wa kuogofya, Yesu aliwaita waovu waliokufa; waliondoka katika makaburi wakiwa na miili yenye hali ile ya unyonge na ugonjwa jinsi walivyokwenda makaburini. Jambo la kutisha! Jambo la ajabu kweli! Katika ufufuo wa kwanza wote waliondoka katika hali ya kutokufa, lakini katika ufufuo wa pili alama za laana zinaonekana kwa wote. Wafalme na wakuu wa dunia, wanyonge na watu duni, watu walioelimika na wasioelimika, wote huondoka pamoja. Wote humwona Mwana wa Adamu; na wale hasa ambao walimdharau na kumdhihaki, waliomwekea taji ya miiba kichwani na kumpiga na mwanzi, wote humwona katika utukufu wake wa kifalme. Wale waliomtemea mate wakati wa hukumu yake sasa hugeuka wasione macho yake na utukufu wa uso wake ambao unawapenyeza moyo. Wale waliomchoma mikono na miguu kwa misumari sasa huzitazama alama za kusulibishwa kwake. Wale waliomchoma ubavu kwa mkuki huona alama za ukali wao mwilini mwake. Watajua ya kwamba yeye ndiye yule ambaye walimsulibisha na kumdhihaki katika maumivu yake ya kukata roho. Hapo ndipo kutakuwa kilio cha huzuni kuu, wakikimbia na kujificha kutoka mbele za Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.VK 126.1
Wote wanataka kujificha chini ya miamba, hutaka kujificha wasiuone utukufu wa kuogofya wa Yeye ambaye zamani walimdharau. Na wakishindwa na kuchomwa moyo na utukufu wake mkuu walipaaza sauti zao kwa moyo mmoja, na kwa sauti inayosikika wazi wakisema, “Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.”VK 127.1
Ndipo Yesu na malaika watakatifu. wakifuatana na watakatifu wote, wakaingia tena mjini, na maombolezo makuu na vilio vya waovu vikasikiwa pote. Ndipo nikamwona Shetani akianzisha kazi yake tena. Alipita huko na huko kati ya watu wake, akawafanya walegevu na wanyonge wawe na nguvu, akawaambia ya kwamba yeye na malaika zake ndio wana uwezo. Aliwaonyesha watu milioni nyingi sana waliofufuliwa. Palikuwa na askari waliokuwa hodari na wafalme wenye akili katika kufanya vita, na ambao walikuwa wamezishinda falme kuu za dunia. Palikuwa na majitu hodari na mashujaa ambao tangu awali walikuwa hawajashindwa katika vita vyo vyote. Nalimwona Napoleon, yule jemadari hodari na mwenye kiburi, ambaye mashambulio yake yaliwatetemesha wafalme wa dunia. Naliwaona watu warefu na wenye kuadhimishwa, ambao walishindwa katika vita wakiwa na hamu ya kushinda Walipoondoka katika makaburi yao, walianza kuwaza mambo jinsi walivyokuwa wakiwaza wakati wa kufa kwao. Walikuwa na hamu ile ile ya kushinda waliyokuwa nayo moyoni walipokufa. Shetani alishauriana na malaika zake, halafu akashauriana na wafalme na majemadari wakuu na watu walio hodari. Ndipo akalitazama lile jeshi kubwa, akawaambia ya kwamba kundi la watu walioko pale mjini ni wachache tena ni wanyonge, tena wanaweza kupanda na kuuteka mji, na kuwafukuza watu wakaao ndani yake, na kuzitwaa mali zote zilizomo ndani na kuupata ule utukufu.VK 127.2
Shetani hufaulu kwa kuwadanganya, na ndipo wote wakajikusanya mara wajitayarishe kwenda vitani. Katika jeshi lile kubwa wako watu wengi walio stadi na wenye akili kwa vita, hao nao wakaunda aina zote za vifaa vya vita. Ndipo jeshi lile likaanza mwendo wao na Shetani akawaongoza, Wafalme na askari za vita vya zamani walitembea karibu na Shetani, na makutano walifuata nyuma makundi makundi. Kila kundi lilikuwa na mtangulizi, na walitembea kwa utaratibu juu ya nchi iliyobomoka wakielekea ule Mji Mtakatifu. Yesu akaifunga milango ya mji, na jeshi hili kubwa likazunguka mji, wakajipanga safu safu, wakiyatazamia mapigano makali.VK 128.1