Sura Ya Kumi Na Nane - Kuokolewa Kwa Watakatifu
*****
USIKU wa manane ndio wakati ambao Mungu aliu chagua kwa kuwaokoa watu wake. Waovu walipokuwa wakidhihaki, mara jua likaonekana, liking’aa kwa nguvu nyingi, na mwezi ulitulia. Waovu walishangaa walipokiona kioja kile. lakini watakatifu walifurahi walipoona dalili za kuokolewa kwao. Ishara na maajabu yakafuatana kwa upesi. Kila kitu kilionekana ya kwamba kimegeuzwa hali yake ya kawaida. Mito ilikoma. Mbingu zikatanda mawingu mazito na meusi yaliyogongana. Lakini kulikuwapo na mahali pamoja palipokuwa na utukufu na utulivu, mahali sauti ya Mungu ilipotokea kama sauti ya maji mengi, ikitikisa mbingu na nchi. Kulikuwako na tetemeko kuu la nchi. Makaburi yalifunguliwa, na wale waliokufa katika imani ya ujumbe wa malaika wa tatu, wakiitunza Sabato, waliondoka mavumbini wakiwa na utukufu, wapate kulisikia agano la amani ambalo Mungu alitaka kufanya na wale walkmshika amri zake.VK 117.1
Mbingu ilifunguliwa na kufungwa, na kulikuwako msukosuko. Milima ilitikisika kama mainzi inavyopeperushwa na upepo, na ikatupatupa miamba huko na huko. Bahari ilichemka kama mtungi, na ikayatupa mawe juu ya nchi kavu. Mungu alipokuwa akiitangaza siku na saa ya kuja kwa Yesu, na kutoa agano lake la milele kwa watu wake, aliyatamka maneno machache, akanyamaza kidogo maneno yake yalipokuwa yakienea duniani pote. Watu wa Mungu walisimama na macho yao wameyakaza juu, wakiyasikiliza maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa Mungu, yakisikika duniani kama sauti kuu ya ngurumo. Ulikuwa wakati wa kutisha kabisa. Baada ya kila fungu la maneno ya Mungu, watakatifu walipaaza sauti zao wakisema, “Utukufu!” Halleluya!” nyuso zao ziliangazwa na utukufu wa Mungu, ziking’aa na utukufu kama uso wa Musa ulivyong’aa aliposhuka kutoka katika mlima wa Sinai. Waovu hawakuweza kuwatazama kwa ajili ya utukufu ule. Na wale waliomheshimu Mungu kwa kuitunza Sabato yake takatifu walipobarikiwa na mbaraka usio na mwisho, kukawa na shangwe kuu ya ushindi juu ya mnyama na sanamu yake.VK 117.2
Ndipo miaka ya furaha ikaanza, yaani miaka ya kupumzika kwa nchi.VK 118.1
Naliwaona watumwa waliomcha Mungu wakiondoka katika ushindi wakishangilia, wakiiondoa minyororo iliyowashika, na huku mabwana wao waovu walitatanishwa wasijue la kufanya, kwa maana waovu hawakuweza kuyafahamu maneno yaliyotoka kinywani mwa Mungu.VK 118.2