Nani Atasimama?
Nabii Malaki anasema: “Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki.” Malaki 3:2, 3. Wale watakaokuwa wanaishi duniani wakati huduma ya Kristo ya maombezi itakapokoma, watasimama mbele za Mungu bila mwombezi. Itapasa mavazi yao yawe safi bila mawaa, tabia zao zitakuwa zimetakaswa dhidi ya dhambi kwa kunyunyiziwa damu. Kwa neema ya Mungu na juhudi zao za dhati itawapasa kuwa washindi katika vita dhidi ya uovu. Wakati hukumu ya upelelezi inaendelea huko mbinguni, kutakuwa na kazi maalum ya kuondoa dhambi miongoni mwa watu wa Mungu hapa duniani. Kazi hii inaelezewa katika ujumbe wa Ufunuo 14. Kazi hii itakapokamilika, wafuasi Wakristo watakuwa tayari kwa Ujio wake. Wakati huo kanisa ambalo Bwana atalipokea wakati wa kuja kwake litakuwa “kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali ... takatifu lisilo na mawaa.” Waefeso 5:27.TK 266.1