Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents

Tumaini Kuu

 - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Luther Alikata Rufaa kwenye Biblia Pekee

    Wakati maadui walipotegemea mila na desturi, Luther alikutana nao akiwa na Biblia pekee, hoja ambazo hawakuweza kujibu. Kutoka katika hotuba na maandishi ya Luther ilikuwa inatoka mionzi ya nuru iliyowaamsha na kuwaangazia maelfu. Neno la Mungu lilikuwa kama upanga ukatao kuwili, likikata ndani ya mioyo ya watu. Macho ya watu ambayo kwa muda mrefu yalielekezwa kwenye ibada za wanadamu na wapatanishi wa kidunia, sasa, kwa imani, yalikuwa yakimgeukia Kristo na Yeye aliYesulubiwa.TK 86.2

    Shauku hii iliyosambaa kote iliamsha hofu za mamlaka ya Papa. Luther alipokea hati ya kuitwa Roma. Rafiki zake waliijua wazi hatari iliyomkabili katika ule mji uliokuwa umeharibika, ambao tayari ulikuwa umelewa kwa damu ya wafia-dini wa Yesu. Waliomba kwamba afanyiwe mahojiano yake huko Ujerumani.TK 86.3

    Hilo lilifanyika, na balozi wa Papa aliteuliwa ili kulisikiliza shauri hilo. Katika maelekezo yaliyotolewa kwa balozi huyo, ilitamkwa kuwa Luther, tayari alikuwa ametangazwa kuwa ni mwasi. Balozi alipaswa tu “kutoa hukumu na kuitekeleza bila kuchelewa.” Balozi alipewa mamlaka ya “kumpiga marufuku katika kila sehemu ya Ujerumani; kuwakataza, kuwalaani, na kuwatenga wale wote waliokuwa wamefungamana naye,” kuwatenga wote, wenye vyeo vyovyote kanisani au serikalini, isipokuwa mfalme, ambaye atapuuzia kumkamata Luther na wafuasi wake na kuwapeleka Roma wakaadhibiwe. 50Ibid., bk. 4, ch. 2.TK 86.4

    Hakuna hata dalili ya kanuni za Kikristo au hata haki ya msingi zilizoonekana kwenye waraka huo. Luther hakupata fursa ya kujieleza au kuutetea msimamo wake; na bado alitangazwa kuwa ni mwasi na siku ile ile alisumbuliwa, akashitakiwa, akahukumiwa na kushutumiwa.TK 87.1

    Luther alipohitaji ushauri wa rafiki wa kweli, Mungu alimtuma Melanchthon kwenda Wittenberg. Maamuzi ya hekima aliyokuwa nayo Melanchthon, yakijumuishwa na usafi na msimamo mzuri wa tabia, vilistaajabiwa mahali pote. Mara, akawa ni rafiki aliyetumainiwa zaidi na Luther-upole wake, tahadhari, na umakini vilikuwa msaada, na kumpa Luther nguvu na ujasiri.TK 87.2

    Mji wa Augsburg ulitengwa kuwa eneo la kufanyia mashauri hayo na Mwanamatengenezo alisaflri kwa miguu. Vitisho vilitolewa kwamba angeuawa njiani, na rafiki zake walimwomba asijihatarishe. Lakini mzigo wake ulikuwa, “Mimi ni kama Yeremia, mtu wa migongano, na mashindano; lakini kadiri wanavyoongeza vitisho vyao, ndivyo furaha yangu inavyozidi...Tayari wameiharibu heshima yangu na sifa yangu...lakini roho yangu hawawezi kuiondoa. Yeyote mwenye shauku ya kulitangaza Neno la Mungu ulimwenguni, ni lazima atarajie kifo kila wakati.” 51Ibid., ch. 4.TK 87.3

    Habari za kuwasili kwa Luther katika mji la Augsburg zilimfurahisha sana balozi wa Papa. Mwasi mwenye usumbufu aliyekuwa amevuta usikivu wa ulimwengu, sasa alionekana yupo chini ya mamlaka ya Kanisa la Roma; hangeweza kuponyoka. Balozi wa Papa alipanga kumlazimisha Luther ayakanushe mafundisho yake, au akishindwa kufanya hilo, kumsafirisha hadi Roma ili akayashiriki yale yaliyowapata Huss na Jarome. Kwa hiyo kwa njia ya mawakala wake alijitahidi kushawishi Luther asipewe ulinzi, akijiamini mwenyewe kwa rehema yake. Hilo Mwanamatengenezo alikataa kulifanya. Baada ya kupewa waraka wenye ahadi ya ulinzi kutoka kwa mfalme, alikwenda kukutana na balozi wa Papa.TK 87.4

    Kwa ajili ya kufuata sera zao, watawala Kanisa la Roma, waliamua kumshinda Luther kwa mwonekano wa kiungwana. Balozi wa Papa alijifanya raflki mkubwa wa Luther, lakini alikuwa anamhitaji ajisalimishe kikamilifu kwa kanisa na kukikubali kila kipengele pasipo hoja ama swali. Katika jibu lake, Luther, alieleza anavyoliheshimu kanisa, shauku yake ya kujua ukweli, utayari wake kuzijibu hoja zote juu ya kile alichokuwa amefundisha, na kuyasalimisha mafundisho yake kwenye vyuo vikuu maarufu ili yachunguzwe. Lakini alikataa matakwa ya yule Kadinali kumtaka ayafute maoni yake pasipo kuthibitishiwa makosa yake.TK 88.1

    Jibu pekee lilikuwa, “Futa, futa!” Mwanamatengenezo alionesha kwamba msimamo wake ulijengwa juu ya Maandiko. Hangeweza kukanusha ukweli. Balozi wa Papa hakuweza kujibu hoja za Luther, alimshambulia kwa dhoruba ya shutuma, kebehi, sifa za uongo, nukuu kutoka kwenye mapokeo, na misemo ya mababa, akamnyima Mwanamatengenezo fursa ya kuzungumza. Hatimaye Luther alipewa ruhusa, japo kwa kinyongo, kutoa jibu lake kwa njia ya maandishi.TK 88.2

    Alimwandikia rafiki yake akisema, “Kitu kilichoandikwa kinaweza kupelekwa kwa wengine ili wakitolee uamuzi; pili, kuna uwezekano mkubwa kwa mtu mmoja kufanya kazi akiongozwa na hofu, kama siyo upande wa dhamiri, ya mtu mwenye majivuno na mdhalimu anayeropoka, ambaye, vinginevyo, anaweza kushinda kwa lugha yake ya kulazimisha.” 52Martyn, The Life and Times of Luther, pp. 271, 272.TK 88.3

    Kwenye mahojiano yake yaliyofuata, Luther, alileta ufafanuzi wa maoni yake kwa usahihi, habari nyingi katika maelezo mafupi, na yenye nguvu, yakijengwa juu ya Maandiko Matakatifu. Baada ya kuyasoma yale maandishi kwa sauti, alimpa yule Kadinali, ambaye aliyatupa pembeni bila kujali, akisema kuwa ni lundo la maneno yasiyo na maana na nukuu zilizowekwa mahali pasipozofaa. Sasa Luther alikutana na balozi wa Papa mwenye kiburi kwenye uwanja wake-na kuzipindua kabisa dhana zake.TK 88.4

    Balozi alishindwa kujidhibiti na kwa ghadhabu alipiga kelele akisema, “Futa! vinginevyo nitakupeleka Roma.” Na hatimaye alitamka kwa sauti ya kiburi na hasira kwamba, “Futa, ama usirudi tena.” 53D’Aubigne, London ed., bk. 4, ch. 8.TK 89.1

    Mwanamatengenezo pamoja na rafiki zake waliondoka haraka, kwa namna hiyo alitangaza wazi kuwa hakutegemea kamwe kufuta maoni yake. Hii ilikuwa kinyume na makusudio ya Kadinali. Sasa, akiwa ameachwa yeye na waliokuwa wanamwunga mkono, akamtazama mmoja baada ya mwingine akiwa amekata tamaa baada ya kushindwa kwa mbinu zake kinyume na matarajio.TK 89.2

    Kusanyiko kubwa lililokuwepo lilipata fursa ya kuwalinganisha hawa watu wawili na kuamua wenyewe juu ya roho walioionesha, na pia uwezo na ukweli wa misimamo yao. Mwanamatengenezo, ni wa kawaida, mnyenyekevu, jasiri, akiwa na ukweli upande wake; mwakilishi wa Papa, anajiona wa muhimu, mwenye kiburi, asiye na mantiki, asiye na hoja hata moja kutoka kwenye Maandiko, lakini kwa hasira alikuwa akipaza sauti yake, “Futa, ama upelekwe Roma.”TK 89.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents