Jinsi Sabato “Ilivyobadilishwa”
Unabii ulisema kuwa utawala wa Papa ungeazimu “kubadili majira na sheria.” Dan. 7:25. Ili kupata kitu badala ya ibada ya sanamu, ibada ya vinyago na vitu vya kale iliingizwa taratibu kwenye ibada ya Kikristo. Hatimaye, tamko la baraza kuu likaidhinisha ibada hiyo ya sanamu. Kanisa la Roma lilidiriki kufuta amri ya pili inayokataza ibada ya sanamu, kutoka kwenye sheria ya Mungu, kisha likagawa amri ya kumi ili kudumisha idadi ya amri kumi.TK 36.3
Viongozi wa kanisa wasiotakaswa walibadilisha amri ya nne pia, ili kuiondoa Sabato ya zamani, siku ambayo Mungu alikuwa ameibariki na kuitakasa (Mwa. 2:2, 3) na badala yake wakaitukuza sikukuu iliyokuwa ikiadhimishwa na wapagani kama “siku tukufu ya jua.” Katika kame za awali Sabato ya kweli ilikuwa ikishikwa na Wakristo wote, lakini Shetani alijitahidi kutimiza kusudi lake. Jumapili ikafanywa kuwa siku kuu ya kuadhimisha kufufukwa kwa Kristo. Huduma za kidini zikawa zinafanyika katika siku hii na ikawa inachukuliwa kama siku ya burudani, huku Sabato ikiendelea kushikwa kama takatifu.TK 36.4
Kabla Kristo hajaja, Shetani alikuwa amewafanya Wayahudi waiwekee Sabato masharti magumu. Sasa, kwa kutumia udhaifu wa mwonekano wa bandia ambao alikuwa ameifanya Sabato iwe nao, aliidhalilisha kwa kuifanya ionekane kama jambo la “Kiyahudi.” Wakati Wakristo wakiendelea kuiadhimisha Jumapili kama sikukuu ya furaha, aliwafanya waigeuze Sabato kuwa siku ya huzuni na masikitiko ili kuonesha chuki dhidi ya dini ya Kiyahudi.TK 37.1
Mfalme Konstantino alitoa tamko la kuifanya Jumapili kuwa sikukuu ya serikali katika dola yote wa Kirumi. (Angalia Kiambatisho.) Siku ya jua ilikuwa inatukuzwa na raia wake wa kipagani na kuheshimiwa na Wakristo. Alihimizwa kufanya hivyo na maaskofu wa kanisa. Wakiongozwa na uchu wa madaraka, waliona kuwa kama siku hii ingeshikwa na Wakristo na wapagani, ingekuza mamlaka na utukufu wa kanisa. Lakini wakati Wakristo wengi wacha Mungu walipokuwa wanaongozwa hatua kwa hatua kuichukulia Jumapili kana kwamba ina kiasi fulani cha utakatifu, waliendelea kuishika na kuiadhimisha Sabato ya kweli wakiitii amri ya nne.TK 37.2
Yule mdanganyifu mkuu hakuishia hapo. Aliazimu kutumia uwezo wake kupitia kwa mwakilishi wake, yaani askofu mwenye kiburi wa Kanisa la Roma ambaye alikuwa anadai kuwa ni mwakilishi Wakristo. Mabaraza makubwa yalikaa ambapo wakuu kutoka duniani kote walikutana. Karibu katika kila baraza Sabato ilishushwa chini kidogo, na Jumapili ikainuliwa. Kwa njia hiyo, hatimaye siku kuu ya kipagani ikawa inaheshimiwa kama siku ya Mungu, huku Sabato ya Biblia ikitangazwa kuwa ni jambo la Kiyahudi na ushikaji wake ukatangazwa kuwa umelaaniwa.TK 37.3
Yule mwasi alikuwa amefaulu kujiinua mwenyewe “juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa.” 2 Thes. 2:4. Alikuwa amediriki kubadili kanuni pekee katika sheria ya Mungu inayoelezea Mungu wa kweli aliye hai. Katika amri ya nne, Mungu anaelezewa kama Mwumbaji. Kama kumbukumbu ya kazi ya uumbaji, siku ya saba ilitakaswa kama siku ya kupumzika kwa wanadamu, ikiwa imekusudiwa kumfanya Mungu aliye hai akumbukwe kila wakati kuwa ndiye anayestahili kuabudiwa. Shetani anajitahidi kufanya watu wasitii sheria ya Mungu; kwa hiyo, jitihada zake anazielekeza hasa kwenye ile amri inayomwelezea Mungu kama Mwumbaji.TK 37.4
Sasa hivi Waprotestanti wanadai kwamba kufufuka kwa Kristo siku ya Jumapili kuliifanya Jumapili iwe Sabato ya Kikristo. Lakini Kristo wala mitume walikuwa hawajaipa Jumapili heshima kama hiyo. Chanzo cha kushika Jumapili ni ile “siri ya kuasi” (2 Thes. 2:7) ambayo hata wakati wa Paulo, ilikuwa imeanza kazi yake. Je, sababu gani inaweza kutolewa kwa ajili ya badiliko lisiloungwa mkono na Maandiko?TK 38.1
Katika kame ya sita, askofu wa Kanisa la Roma alitangazwa kuwa kichwa cha kanisa lote. Upagani ulikuwa umeupisha utawala wa Papa. Joka akawa amempa mnyama “nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.” Ufu. 13:2.TK 38.2
Sasa ikaanza ile miaka 1260 ya ukandamizaji wa utawala wa Papa uliotabiriwa katika unabii wa Danieli na Ufunuo. Danieli 7:25; Ufunuo 13:5-7. (Angalia Kiambatisho.) Wakristo walilazimishwa kuchagua ama kuacha unyoofu wao na kukubaliana na sherehe na ibada za utawala wa Papa, au kumalizia maisha yao katika magereza yaliyokuwa chini ya ardhi, au kufa. Sasa maneno ya Yesu yalikuwa yametimia: “Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu.” Lk. 21:16, 17.TK 38.3
Ulimwengu ukawa uwanja mpana wa mapambano. Kwa mamia ya miaka kanisa la Kristo lilitafuta usalama katika maeneo pweke na yaliyofichika. “Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini.” Ufu. 12:6.TK 38.4
Mwanzo wa zama za giza ulikuwa ni pale Kanisa Katoliki lilipopata nafasi ya kutawala. Imani ilihamishwa kutoka kwa Kristo kwenda kwa Papa wa Roma. Badala ya kumtegemea Mwana wa Mungu kwa ajili ya msamaha wa dhambi na uzima wa milele, watu walimwangalia Papa na mapadri aliokuwa amewakasimisha mamlaka. Papa akawa mpatanishi wao duniani. Kwao, alikuwa badala ya Mungu. Kukiuka matakwa yake kulikuwa sababu ya kutosha kupata adhabu kali. Kwa namna hiyo, mawazo ya watu yakageuzwa kutoka kwa Mungu kwenda kwa watu wenye kukosea na wakatili, na zaidi, kwa mkuu wa giza mwenyewe, aliyekuwa anaonesha uwezo wake kupitia kwao. Maandiko yanapopingwa, na mwanadamu kujichukulia kwamba yeye ndiye mwenye mamlaka yote, matokeo yake ni ulaghai, udanganyifu, na uovu wa kudhalilisha.TK 38.5